Jumatatu, 15 Mei 2017

YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU KWA MUNGU YANAWEZEKANA.

Mwalimu Oscar Samba
Uhali gani mpenwa mwenzangu katika Bwana? Natumai u buheri wa afya.

Leo nimekuandalia ujumbe mahususi kwa ajili ya kukujuza ukubwa na Uweza wa Yesu Kristo katika mambo yaliyoonekana ni magumu kama mlima ama bahari katika maisha yako.

Ni kweli hitaji ama jambo lilopo mbele yako ni kubwa kuliko wewe na hata mimi mwenyewe ni kweli siliwezi, ila Yesu tunayemuamini analiweza. Amini tuu kama alivyomwambia dada yake na Lazaro rafiki yake kuwa anapaswa kuamini tu.


Wana wa Iziraeli walikutana na mambo kadha wa kadhaa katika maisha yao ya kisafari na  kimakazi ila walimtazama Yesu aliye Bingwa wa mambo yaliyoshindikana na alifanya njia katika hayo yote.
1.     Bahari ya Shamu, Hili lilikuwa ni jaribu kubwa sana kwa Wana wa Iziraeli ila Mungu hakuwaacha maana Mungu wetu huwa na sifa ya kutupigania kila uchwao.
Kutoka 14:13 Musa akawaambia watu, “Msiogope! Simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakao wafanyia leo; kwa maana hao Wamisiri mliowaona leo hamtawaona tena milele.14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimiya”
 Nami kwa imani iliyo kuu ninakwambia ya kwamba usikate tama wala usirudi nyuma bali simama kwa imani iliyo kuu nawe itauona mkono wa Bwana katika hilo jambo lako kwani Mungu huyu aliyetajwa na Musa hapa ndiye tunayemwabudu na kulitaja jina lake.

Tuangaliye kilichotokea, Kutoka 14:21 Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari. Bwana akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. 22 Wana wa Iziraeli wakaenda ndani ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto.

Huyu Mungu wetu sio wa kawaida wala uweza wake haufananishwi na jambo lolote lile maishani kwani ni Mungu muweza na mwenye mamlaka ya hali ya juu iwezayo kuigawa bahari na kuiamisha milima. Na katika uweza huwo, huweza kuligawa jaribu lako lililo bahari nawe ukavuka salama huku adui zako wakimezwa na bahari hiyo ama kuiamisha hiyo milima iliyo mbele yako.

Wewe usiwatazame wanadamu bali mtazame Yesu aliyemgawa bahari, Ni kweli madakitari wamesema hutapona ila YESU anasema hakuna lisilowezekana kwake.
 Ni kweli kwenu hakuna aliyesoma hadi kidato cha nne na wewe unataka kuchukuwa Dikrii, (Shahada). Sika Neno la BWANA kwa kinywa changu, “Nitafanya njia pasipokuwa na njia, na mito ya maji huko jangwai na nyikani”

Ni kweli ndoa yako haina amani, huyu YESU aliyetuliza dhoruba baharini na kukawa shwari kuu, anaweza kutuliza hiyo migogoro kwenye ndoa yako, Mathayo 8:23-27, 26 Akawaammbia “mbona mmekuwa waoga, enyi wa Imani haba? Mara akaondoka akazikemea pepo na bahari, kukawa  shwari kuu.”
Na wewe usiwe Muoga, Omba kwa Imani na muite Yesu kama mtuliza bahari ili atulize hayo mawimbi kwenye ndoa yako. Kwake Yeye hakuna Neno la kumshinda maana jina lake ni Alufa na Omega, yaani mwanzo na mwisho kwa kifupi ni bingwa wa yaliyoshindikana.

2. Kukosa maji pale Masa, Tutazame tukio jingine la kukusosa maji, na yamkini shida yako ni kukosa Chakula ama Mavazi au Ada ya shule, wewe mtazame Yesu aliye wapa Mana wanaye na maji kule jangwani atatenda na kwako pia.
Kutoka 17:1-7, Utaona jinsi Bwana alivyo watendea watu wake kwa kuwapa maji mara baada ya Musa kupiga mwamba wa Horebu na mara maji yakatoka na wana wa Mungu wakanywa, kumbuka walikuwa jangwani na wewe hayo maisha magumu ni taswira ya jangwa rohoni.
Ni maombi yangu kwa Mungu ayafanye hayo kwako halisi leo na afunguwe madirisha ya mbinguni kwa ajili yako kama alivyofanya huko jangwani, (Zaburi 78:23 Lakini aliyaamuru mawingu juu, akaifungua milango ya mbinguni; 24 akawanyeshea mana ili wale, akawapa nafaka ya mbinguni. 25Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.)
3.     Goliati, Mfano mwingine ni ule wa Goliati, kumbuka kuwa huyu alikuwa ni shujaa wa jeshi hasimu la Wafilisti na alikuwa tishio kimwili na kiroho pia, ila Mungu alimuinua Daudi kwa ajili ya kusudi hili takatifu nyakati zile. 1Samweli 17:40-50. Ukipata muda soma sura yote.
Mungu huyu aliyefanya haya kwa wanae kipindi hicho atafanya na kwako leo kwani yakupasa kumtazama Bwana ili akuinuliye Daudi wako atakayemsambaratisha Goliati aliye mbele yako. Yamkini Goliati wako ni hilo jaribu la kukosa kodi, ama biashara kuwa ngumu, punguza kuwaza bali inua macho msalabani na hapo utapa nguvu kama Daudi za kuchukuwa kombeo na jiwe kisha utamuangamiza huyu adui na kwa jiwe la kombeo utashinda.
Tuone haya maandiko kwenye 1Samweli 17:50, “Basi hivyo Daudi akamshinda yule Mfiliti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamua, ..”
Na wewe katika hilo hitaji lako ni hakika Mungu atakupigania ila lilo la msingi ni wewe kumtazama Yeye na kuweka imani yako kwake na ukishaomba amini tayari amekwisha kutenda.
Marko 11:24 Kwa sababu hiyo nawaambia: Myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”
Anza sasa kuingia kwenye maombi ya kumpiga Goliati wako, ama kumuomba Mungu akuinuliye Daudi wako, ama ya kuigawa bahari iliyombele yako au kumuita Yesu kama mtuliza bahari. Au anza yale ya kuamisha milima iliyo mbele yako; na yaombe kwa Imani.
Marko 11: 23 Amin,nawaambia: Yeyote atakayeuambia mlima huu,
Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.  


Na Huduma ya UKOMBOZI GOSPLE, Arusha Tanzania, Kwa maombi, Ushauri, Maswali au Sadaka wasiliana nasi, Barua pepe: ukombozigosple@gmail.com Simu: +255 759 859 287 pia waweza itumia kwa M-PESA. Zaidi www.ukombozigosple.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni