Ijumaa, 9 Juni 2017

NGUVU YA AGANO Sehemu ya 1.

Na Mwalimu Oscar Samba wa Ug Ministry.
Hakika ni jambo la kushangaza kwani siku chache zilizopita nilikuaidi kukuandikia kitabu hiki cha Nguvu ya Agano kama Mungu atanipa kibali na siku ile alinipa, leo amenitaka kuanza kukumegea baadhi ya vitu vilivyomo kwenye hicho kitabu na nilikuaidia kuwa katika kitabu hiki nitazungumzia kiundani aina yote ya maagano ikiwemo yale ya Mungu na yakipepo.

Atukuzuzwe Mungu juu mbinguni na duniani ilipo sehemu ya kuweka miguu yake, leo nitakujuza kiundani kuhusu maagano ama Nguvu iliyopo kwenye maagano ambayo tunaingia na Mungu. Pia jambo hili likupe kiu yakuingi agano ama maagano binafsi na Mungu ili kuwa katika uwakika mkubwa wakutembea na Mungu, kwani kama kuna kitu Mungu hukiheshimu ni Agano.


Agano ni mapano baina ya pande kuu mbili au zaidi dhidi ya jambo fulani. Katika maagano ama Agano kuna mambo kadha wa kadha kama nilivyokujuza huku nyuma, ikiwemo, Ishara, Mapatano, ama makubaliano, Kiapo cha uamainifu na kadhalika. Huko mbeleni katika kitabu hiki nitakujuza kwa undani zaidi kuhusu mambo hayo.

Leo nataka tuione hiyo Nguvu iliyopo katika maagano ya kimungu ikiwa ni baada ya kuiona iliyopo kwenye maagano ya kipepo siku kadhaa zilizopita kwenye makala ya Msaada kwa wanaoota ndoto wakiwa wanakula vyakula.Pamoja na zile za Namna ya kujinasua kwenye vifungo vya pepo mahaba.
Kumbuka pia Bibilia ni Agano au ni mkusanyiko wa maagano makuu mawili, yaani lile la Kale na Jipya, ndio maana hutaacha kumuona Mungu kama utasoma Bbilia kwa Sura ya Kiagano, na ufahamu ni kati ya Mwanadamu na Mungu. Na Agano ni mapatano. Ukisoma kwa mtazamo huo wa kuona kilichopo ndani yake kuwa ni mapatano baina yako na Mungu hutatoka kama ulivyo mara baada ya kusoma maandiko na hutakubali kusoma kwa sura ya kawaida ama mazoea.

1. AGANO LA IBRAHIMU: (Hapa ninajibu lile swali ama ninatimiza ile ahadi niliyokuadia hapo nyuma ya kukupa sababu za watu wanaoomba kwa jina la Mungu, wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, nikiyaita ni maombi ya kiagano).
Kuna Agano Mungu alifunga na Ibrahimu aliye baba yetu wa imani na Agano hili limekuwa na Nguvu kubwa sana  na Nguvu moja wapo ni hii. Tulione hilo Agano, Agano hili limetiwa nguvu katika sura kadha wa kadha za kitabu hiki cha Mwanzo kwa hiyo tutatazama kila kipengele kilichopo miongoni mwa Agano hili kulingana na uhitaji wa hoja nitakayo ijenga katika mada ama pwenti husika,ila nataka kukudokezea kipengele kimoja kabla ya kusonga mbele zaidi.
Ni Mwanzo 15: 18 Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati,
19 Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni,
20 na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai,
21 na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.

Umeliona hilo jambo hapo? Tutalichambua huko mbeleni.
(a) Lili husika katika kumbariki Kiuzao Ibrahimu, Kikawaida Ibrahimu umri wake wa kupata mtoto ulikuwa umepita, ila kwa sababu ya Agano hili la Mungu kumpa uzao na ambao utakuwa kama Mchanga wa Bahari na kuwa tajiri Mungu alilazimika kutimiza jambo hilo bila kuangalia kikwazo cha Umri wake ama ule wa mkewe.
Tuone hiyo ahadi ya uzao kiagano, Mwanzo 17: 7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.
8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.
9 Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.

10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa.

Katika hilo hakuna namna Mungu angeweza kuacha kumpa Isaka, maana tayari ameshajifunga na kiapo, na makubaliano yaliyopo kwenye Agano hilo.
Kumbuka Lengo kuu la kitabu ama mafundisho haya ni kukupa mwanga wa kuyatumia maagano haya yaliyopo kweye bibilia ili kujinasua mahali ulipo ama kunufaika na Baraka zilizomo ndani ya Bibilia maana bibilia ni mkusanyiko wa maagano makuu mawili yaani lile la Kale na Jipya ambalo maandiko huliita kuwa ni bora zaidi.
Wakati tunasonga mbele  nataka kukupa uwakika wa kwamba Baraka hizi ni matokeo ya Agano hilo, ndiposa Ibrahimu akampata huyo mwana bila kuangalia umri wake ama kigezo chochote kile cha kibaolojia ili na wewe kama mwana wa Agano hili uwe na ujasiri wakumuomba Mungu bila kuangalia kizuizi chochote kile kilichopo mbele yako.
Tudhibitishe jambo hili kutoka kwenye kinywa cha Mungu mwenyewe, Ni Mwanzo 17: 21 Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao.
22 Mungu akaacha kusema naye, akapanda kutoka kwa Ibrahimu.
Hapo Ni Mungu anayanena hayo wala Sio Jirani yake na Mungu.
(b) Lilimpa Baraka za Mali, Kumbuka Agano hufanywa Imara kwa sadaka, maombi na kadhalika, ndio maana wale wanaofanya maagano na mapepo hupaswa kutoa kafara za damu za wanyama, ndege, hata watu. Na kanuni hiyo Shetani ameiiga kwa Mungu.
Mara baada ya Ibrahimu kukubali kumtoa Mwanaye Mungu alinena naye kuhusu kumbariki kiuchumi ikiwa ni sehemu ya kiagano. Mwanzo 22: 15 Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni
16 akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,
17 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;
18 na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.
Hapo panatajwa kumiliki malango ya Adui, maana yake ni kuwa na uwezo wa ulimwengu wa roho wakuteka na kutaifisha mali ama utajiri wa adui zako kisha kuugeuza kuwa wako, kwa kifupi ni kuwafanya mateka wa uchumi. Tulihakiki jambo hilo kwenye kitabu hiki hapa:
Isaya 60: 11 Malango yako nayo yatakuwa wazi daima; Hayatafungwa mchana wala usiku; Ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa, Na wafalme wao wakiongozwa pamoja nao.

Pia sentesi inayofunga mazungumzo hayo ipo katika mstari wa 18, hapo kwenye kitabu cha Mwanzo, ambayo inadhiirisha dhairi kuwa Agano hili ndilo lililopenyeza Baraka kwa kila taifa duniani, ndio maana mataifa yakitaka kubarikiwa ni vyema kujiunganisha ama kujiambatanisha kiroho na Taifa la Iziraeli. Nataka kukuonyesha sentensi hiyo; “na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia
Najua unatamani kuendelea nami ila kwa kweli muda sio rafiki yangu, ila kabla sijakutaka tuonane kesho, ambapo nitaendelea na Agano hili kabla ya kuchambua lile la Nuhu, na mengineyo, ninataka kukupa uwakika kwamba wewe ni sehemu ya Agano hili la Ibrahimu ili kukujengea Imani dhabiti itakayokusaidia kupata uwalali wa kuingia kwenye maombi leo ili kudai Baraka zako za kiagano kama mwana wa Mungu.

Kabla ya andiko hilo kumbuka Yesu alikuwa akiwaponya watu wengi ila alitia mkaza sana kwa watu wa Uzao wa Ibrahimu, ndio maana alipomuona yule mama mgonjwa alimuhurumia na kusema kuwa imekuaje hivi kwa mtu wa uzao wa Ibrahmu, alikadhalika kwa mama mkaninayo yule aliyebembeleza na kusema kuwa hata mbwa hula makombo ya bwana zao na kisha kutendewa mujuza. Pale unamuona Yesu akisema kuwa alitumwa kwa ajili ya watu wa Uzao wa Ibrahimu, ukiona Uzao wa Ibrahmu kama wewe uliyepita darasa hili langu picha unayoipata pale ni kwamba hii ilikuwa ni kauli ya KIAGANO.

Maana yake ni kwamba Yesu alipaswa kutilia mkazo kwa watu hawa kwa sababu ya Nguvu ya kiagano. Kwa mantiki hiyo Mungu hapendezwi na mateso ama taabu kwa mtu wa Uzao wa Ibrahimu. Yaani wewe uliyeokoka na mimi pia. Maana wapo wa uzao huo kibaolojia ambao ni Wayahudi na wapo wa Uzao huo ambao ni wale wa Imani yaani waliokoka. Na jambo hili limetiwa muhuri na Mungu mwenyewe kimaandiko.

Kwa ujasiri fungua nami maandiko haya hapa: Ni WAGALATIA 3.29 Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
Neno ahadi hapo linawakilisha AGANO, Maana kama umekuwa mwanafunzi wangu Mwaminifu na Makini utakumbuka vipengele vyote tulivyo visoma vimesheheni ahadi za Ibrahimu kubarikiwa.
Tukutane kesho, ila kama huja Okoka fahamu kuwa hutaweza kuridhi Baraka hizi na maombi utakayoomba hayatakuwa na Nguvu ya kiagano. Na kwa aliyeokoka hivi sasa ninamtaka kuingia kwenye hayo maombi ya kiagano ili kufungua milango iliyofungwa nakudai baraka zako za Watoto, Utajiri na kadhalika.

Kama hujaokoka na unataka kuokoka ama ulirudi nyuma kiroho na unataka kutengeneza na BWANA kwa upya leo, tafadhali fwatisha nami maneno haya kwa Imani, Sema: BWANA YESU, NINAKUPENDA, NINAKIRI NA KUAMINI MOYONI MWANGU KUWA WEWE NI MUNGU, ULIKUFA NA KUFUFUKA KWA AJILI YANGU, INGIA NDANI YANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU LEO, AMENI.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo.

Na Huduma ya UKOMBOZI GOSPLE, Arusha Tanzania, Kwa Maombi, Ushauri, Maswali au Sadaka wasiliana nasi, Barua pepe: ukombozigosple@gmail.com  Simu: +255 759 859 287 pia waweza itumia kwa M-PESA. Zaidi www.ukombozigospel.blogspot.com   #UkomboziGosple  #MwalimuOscarSamba
Pia #Like #Penda Page/Ukurasa wetu au kundi la Fb, ili kupata habari hizi kwa haraka, zaidi. Ug Ukombozi Gosple,                                                                                       PAGE: https://www.facebook.com/Ug-Ukombozi-Gosple                                              
Kikundi: https://www.facebook.com/groups/2268418230050621/
Pia kwenye mtando Mpya wakitanzania wa

2 DAY SKY: https://www.2daysky.com/home

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni