Jumanne, 27 Juni 2017

NGUVU YA AGANO, Sehemu ya 7.

Na Mwalimu Oscar Samba wa Ug Ministry.
Ni mwingi wa furaha kwa Mungu kutuwezesha tena kukutana siku ya leo maana sio kwa uweza wetu wala fikra zetu bali ni kwa kudra zake Yeye liyemneemeshaji wa Neema na Baraka zote, Ameni.

Leo ni siku ya saba katika mfululizo wa hii makala yetu ya Agano na tunaendelea kumtazama Yakobo na Uzao wake, kwa sasa tumuone Yusufu Mwana wa Mzee Yakobo.
(k) Kupitia Yusufu walimiliki Malango ya Misiri, Natumai unakumbuka kuwa katika hili Agano pale Mwanzo 22 mara baada ya Ibrahimu kufaulu ule mtihani wa kumtoa Isaka sadaka Mungu alimuaidia kummilikisha Malango ya adui zake kupitia Uzao wake.
Tafadahali naomba tuhakiki jambo hilo ilituweze kwenda sawia ama sanjari. Ni Mwanzo 22: 17 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;


Mungu alianza kulidhibitisha jambo hilo kupitia kijana Yusufu aliyekuwa utumwani ama gerezani katika hiyo nchi. Kijana huyu alijipatia kibali kikubwa sana kwa Mfalume wa hiyo nchi, kibali kilichompa nafasi ya utawala ama ya uongozi na heshima ya hali ya juu. Sio hayo tu bali alipewa jukumu adimu na adhimu la kugawa pamoja na kusimamia chakula kwa nchi nzima. Hili lilikuwa ni Lango kubwa sana.

Kisha uzao wa babaye ukaamia katika hilo taifa na kuruhusiwa kuishi humo na kufanya shuhuli zao za ufugaji hapo.
Tuanze kutizama jinsi Yusufu alivyofanyika baraka katika kumiliki Malango haya ya wa Misiri.
Mwanzo 41: 38 Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?
39 Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.
40 Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.
41 Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.
42 Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
43 Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri.
44 Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.
45 Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri.
46 Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi yote ya Misri.
47 Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi.
48 Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake.
49 Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu.

Turuke hadi mistari ya chini yake na ujione hapo hili jambo;
55 Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni.
56 Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri.
57 Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.

Kija wakiebrania anamiliki Lango kubwa namna hii! Tena ugenini! Haya ni matokeo ya hili Agano, na kwako pia inawezekana kupata kibali mahali ambapo kila mtu alidhania haiwezekani, na sio kibali tu bali nakuwa mtu mkuu sana, sio mkuu tu bali na kuwawezesha ndugu zako walio wapendwa katika Kristo Yesu kunufaika na baraka hizo pia.
Na kuna tatizo kubwa sana kwa wapendwa wa leo kwamba wakinufaika hawakumbuki watu wenzao wa uzao wa Ibrahimu, bali hujinufaisha wao tu ama na wengineo. Maandiko yanatutaka tutendeane mema tena hasa sisi wa njia moja.
Ila haikuwa hivyo kwa Yusufu, kwani alipofanikiwa aliwataka nduguze kuja kushiriki hizo baraka na wala hakukumbuka waliyomtenda hapo awali, jambo hili na wewe likae moyoni mwako; Ili kutuza mujiza ambao Mungu amekupatia ni vyema kujifunza kuachilia kwa kusamehe, wasamehe wale wote waliokuwa kikwazo kwenye safari yako, na kwa sasa wakumbuke na uwatendee mema na ikiwezekana nena kama Yusufu maneno haya:
Mwanzo 50: 17 Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye.
18 Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako.
19 Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu?

Jibu ninalotaka ulione ni hili hapa, ila huo Utangulizi nilikusudia ukupe kuelewa taswira sahihi ya mazingira ya hili jibu ili punde utakapokuja kuinuliwa usijikute unawatenda mabaya waliokuwekea miiba, mawe na misumari barabarani. Ona Jibu hilo Mubashara sasa:
Ni Mwanzo 50: 20 Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.

Kuna Ushuhuda mmoja wa Mtumishi fulani aliyekuwa ni Mchungaji na mara Mungu kumuinua na kumpa Uasikofu kwenye Dhehebu lake, kilichofwata kilikuwa ni kuwaamisha wale waliokuwa wakimpa upinzani kwenye safari yake ya uasikofu ama kitumishi. Aliwatoa kwenye mazingira ya mjini na kuwapeleka vijijini ama kwenye mazingira magumu kiuchumi, kijamii, kijografia alikadhalika yaliyo makame kiroho.

Natumai kwa mtaji huo umenielewa. Na jambo pekee litakalo kusaidia nikujiwekea akiba ya mema badala ya ile ya hila kama Mithali inenavyo.
Ni Mithali 26: 25 Anenapo maneno mazuri usimsadiki; Kwa maana ana machukizo saba moyoni mwake.
26 Ingawa chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko.


Maneno hayo ni mazito wala sio mepesi hata kidogo, kwani unaposema moyoni mwako hivi: Mimi nitajilipizia kisasa ni hakika jambo hilo huumbika na kuna siku litakuwa dhairi ama bayana katika uso wa nchi huku maandiko yakipinga jambo hilo
Ni Mithali 24: 29 Usiseme, Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; Nitamlipa mtu huyo sawasawa na tendo lake.

Atukuzwe Mungu kwa kipengele hicho kizuri na hakika ni kusudio lake maana hakikwepo kwenye notisi yangu, turejee sasa kwenye hili Agano.
Ukisoma sura ile ya 42, utauona ukarimu wa Yusufu kwa ndugu zake, na tunakaribia kabisa kugusa jambo ambalo nilikuaidia toka hapo awali kukujuza nalo ni hili.

Ukisoma Mwanzo 15, utaona Mungu anamjuza Ibrahimu kuhusu uzao wake kuelekea Misiri ikiwa ni taarifa ya kiagano, kwani mbele yake tunamuona akifunga naye Agano hili tunalolidodosa leo kimapana zaidi. Nami kwa taarifa hiyo kiduchu sinabudi kukuaga kutoka kwenye uandishi huu kwa siku ya leo ila ni hakika kuwa kesho tutatizama jambo hilo katika uwanda mpana na mororo zaidi.

Kama hujaokoka na unataka kuokoka ama ulirudi nyuma kiroho na unataka kutengeneza na BWANA kwa upya leo, tafadhali fwatisha nami maneno haya kwa Imani, Sema: BWANA YESU, NINAKUPENDA, NINAKIRI NA KUAMINI MOYONI MWANGU KUWA WEWE NI MUNGU, ULIKUFA NA KUFUFUKA KWA AJILI YANGU, INGIA NDANI YANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU LEO, AMENI.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo.

Na Huduma ya UKOMBOZI GOSPEL, Arusha Tanzania, Kwa Maombi, Ushauri, Maswali au Sadaka wasiliana nasi, Barua pepe: ukombozigospel@gmail.com  Simu: +255 759 859 287 pia waweza itumia kwa M-PESA. Zaidi www.ukombozigospel.blogspot.com   #UkomboziGospel  #MwalimuOscarSamba
Pia #Like #Penda Page/Ukurasa wetu au kundi la Fb, ili kupata habari hizi kwa haraka, zaidi. @ugukombozi Gospel 
 PAGE: https://www.facebook.com/ugukombozigospel/
Pia kwenye mtando Mpya wakitanzania wa

 Pia TAZAMA VIDEO ZETU HAPA  https://www.youtube.com/channel/UCv1tghnugOSpbmb5h6ebJtA  (Ukombozi Gospel)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni