Ujumbe huu ni sehemu ya kitabu chetu cha Mungu yu Pamoja Nawe, pwenti ya nne, karibu: Na Mwalimu Oscar Samba.
4. Uwe na Utulivu Nafsini Mwako, kukosa utulivu maana yake ni kuwa na mahangaiko moyoni, ni kuwa na wasiwasi au mashaka, ni hali ya kujisumbukia au kuhaha.
Hali hii ni mlango wa dhambi, maana ni adui wa imani, humuondolea mtu uwezo wa kumtegemea Bwana, maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari liwezalo kupelekwa huku na kule na upepo !
Kukosa utulivu ni kukosa raha, ni kupungukiwa kwa kiasi kikubwa na amani, ambayo hiyo amani ni njia ya Mungu kuongea, maana maandiko husema kuwa na amani ya Kristo iamuwe mioyoni mwenu, kwa hiyo hayo mazingira humzuilia Mungu kuamua ndani yako, lakini pia amani ni njia ya Mungu kukuongoza, sasa ikipotea maana yake hutaiona njia, ndio maana dalili kubwa ya mtu aliyekosa utulivu na matokeo yake ni kuwa kama mtu aliyeko njia panda asiyejua njia ya kuiendea !
Mtu huyu atahaha ajui afanye nini, maamuzi haya atayaafiki asubuhi na adhuuri anayapangua, baadae anakuwa na wazo hili kisha baada ya muda kitambo ameshabatilisha, jioni anapangua la alasiri na usiku ana kazi ya kuondoa wazo la jioni !
Asipojituliza atashangaa hadi kichwa kinamuuma, na kufadhaika huja kwani na Roho naye anaugua ! Utulivu ni zao la amani na amani ni dalili ya utulivu, na hiyo amani ndio njia; Isaya 59:8 Njia ya amani hawaijui; wala hapana hukumu ya haki katika miendo yao; wamejifanyizia njia zilizopotoka; kila apitaye katika njia hizo hajui amani.
Andiko nikupalo linaonyesha kuwa watu hawa wataongozwa kwa amani, ikiwa na maana kuwa amani ni kiongozi, sasa hapa amani inamuwakilisha Roho Mtakatifu, maana nasi tu twajua kuwa waongozwao na Roho ndio wana wa Mungu, pia Yesu alisema kuwa atatuongoza na kutitia katika hiyo kweli yote !
Jambo jingine anataja hali ya kuimba, na kupiga makofi, japo inatajwa miti na milima, lakini nawiwa kukwambia kuwa hii ni aina ya mioyo ya wanadamu, sasa ina maana kuwa amani na furaha vikikosekana ndani ni dhairi kuwa swala la kuimba au la ibada huwa mahali pa gumu, kwa hiyo aliyekosa utulivu hata ibada yake huwa ngumu pia !
Jionee; Isaya 55:12 Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi.
Hata wana saikolojia huwa wanasema kuwa ukiwa mahali pa gumu epuka kufanya maamuzi ya haraka, mfano ukiwa na uchungu, hasira, huzuni au ukijeruhiwa nafsi, wao husema ukiadhirika kisaikolojia, maana maaamuzi hayo huja kuwa na majuto baadae, wapo waliovunja ndoa, uchumba na kadhalika kutokana na kuamua walipokuwa hawana utulivu, wapo walioacha kazi, au kuacha biashara ama kuamua vibaya na baadae walipokuja kupata utulivu waligundua kuwa wamekosea kuamua vile !
Na katika hali ya hamaki kama hiyo hata Roho Mtakatifu akiongea ni vigumu sana kumuelewa, maana Yeye ni Amani na kwa amani hukuongoza, kwa amani hukuzuilia jambo na kwa amani hukuonya, maana akikukosesha amani yaani akiugua ndani unaelewa hiki ni kiashiria cha Roho Mtakatifu ama anaipa ishara fulani, sasa kama amani haiwezi kukaa maana yake unapoteza kitu kikubwa sana.
Dhoruba ilipowapiga wanafunzi wa Yesu pale ziwani walikosa utulivu, na kujikuta wanahaha na kutaharuki,ila Yesu katikati ya dhoruba aliweza kupata usingizi, alafu angalia walipomuasha, utaona aliamua maamuzi mema na makubwa sana, na dhoruba kutulia, ila waliohaha waliishilia kuchota maji tu !
Wakati wa bahari kuchafuka kipindi cha Yona, Yona alikuwa na utulivu, alilala, japo ilikuwa ni ghadhabu ya Mungu maana alimjua Mungu wake, na sifa moja wapo aliyoijua sana kwake ni rehema, sasa ambao hawakumjua walijikuta wanatupa baharini shehena zao, mizigo yao ya dhamani ilitupwa baharini, ila aliyekuwa na utulivu aliweza kuwapa suluhu moja zuri na la kudumu, kuwa wamfunge na wamtupe baharini, na hapo kukawa shwari kuu !
Nataka kukufundisha nini hapa ! Nawiwa kukujuza kuwa katikati ya shida hakikisha moyo wako unakuwa na utulivu, hata kama umekosea kama Yona, maana utaweza kupata majibu na suluhisho la Kiungu, Yuda hakupata utulivu wa ndani na aliishilia kujinyonga, ila Petro aliupata ndio maana aliweza kutubu na kuendelea na safari !
Wakina Meshaki na Shedraka na Abrinego waliweza kuwa na utulivu katikati ya hofu ya mauti, na hata waliotupwa motoni waliweza kutulia, na humo waliuona wokovu wa Bwana, ukiwa na hofu hutaacha kuisujudia sanamu ya mfalme, Danieli alivuka salama katika pito lile la tanuru la simba maana alimjua Mungu wake, naye hakika alimsaidia, angekuwa na hofu na mashaka asingekuwa na huo ujasiri wa kuwa tayari kutupwa humo !
Jionee hili andiko, ambapo linabeba msisitizo wangu mkubwa kuhusu uhusiano ulipo kati ya amani na utulivu; Isaya 32:17 Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima. 18 Na watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama, na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu.
Kwa hiyo kuwa na utulivu moyoni ni kuwa na usalama ! Ni kweli nami ninalisadiki hili, kuna kisa kimoja nilikisikia nami nawiwa kukudokezea, kwamba simba akitaka kuchukuwa ng'ombe kwenye boma, huwa haingii ndani, anakaa nje karibu na boma na kunguruma, ananguruma kwa muda, alafu anavizia yule ng'ombe muoga atakayeruka, na kweli yule atakaye ruka huyo ndie anayekuwa kitoweo chake !
Sasa kukosa utulivu, kutakufanya kukosa usalama wako, maana utajikuta unamrukia/mkimbilia, ukiona binti kaamua kuolewa kienyeji na anajaribu kutoa sababu isizo za msingi kuwa ameona Mungu amechelewa uwe na hakika kuwa alikosa utulivu, ukiona mshirika amejeruhiwa kanisani na mkuu wake kidini na kuchukuwa maamuzi magumu uwe na hakika alikosa utulivu na kumrukia simba kisha kuraruliwa nae !
Uliwahi kusikia kisa cha panzi liyeko kwenye chupa iliyopo mbele ya kuku ! Huyu panzi asipojua uwezo wa chupa kuwa hata kuku afanyeje hawezi kumdhuru basi hawezi kuwa na utulivu, ndio maana panzi wengi na kama sio karibia wote huamu kuruka ruka pale kuku anapojaribu kuwadonoa akizania anadonolewa na asijuwe chupa inamlinda !
Sasa panzi muoga zaidi huruka zaidi, ndipo huweza kujikuta ameruka na kuufikilia mdomo wa chuma na kisha kutoka nje, hapo ndipo umezwa ! Nawe majaribu yakikujia ni sawa na panzi kwenye chupa, kuku hawezi kukudhuru, ila ukitoka nje atakumaliza,elewa sana kuwa Shetani ni kama simba angurumae akizunguka-zukunga huku na huku akitafuta mtu ammeze kama 1 Petro 5:8 isemavyo, sasa anayezunguka zunguka maana yake yupo nje ya boma, anavizia aliyetoka nje ya boma ili aweze kummeza, ngurumo zake zisikufanye uone kuwa adui yumo ndani ya boma la ! Ni kuku nje ya chupa, ile una muona au kusikia ngurumo haina maana anao uwezo wa kukudhuru la ! Tena ni la hasha !
Na kukosa utulivu ndiko kunakoweza kukupelekea kuruka nje ya neema, kutoka kwenye chupa au kwenye boma, usidhubutu kuacha wokovu, kisa hujaolewa, kuacha neema kisa uchumi ni mgumu, ama kuachana na wokovu kisa maisha ya ndoa ni magumu, au kuvunja ndoa kisa mwenzako haeleweki, bali moja kwa moja hakikisha unaendelea kutulia kwenye neema, na ukiona inakuwia vigumu geuza jambo hili kuwa "ajenda" yako ya maombi, yaani msihi Mungu ukimwambia kuwa akupe neema, akupe utulivu ! ( Katika majira magumu sana utulivu unageuka kuwa neema, maana akili zetu huwa na mipaka. )
Sasa katika mifano hiyo miwili utaelewa ni kwa nini wale waliotupwa kwenye moto na Danieli kwenye tundu lenye simba hawakuwa na hofu, bali walitulia, ni kwamba walijua ni simba aliye nje ya boma,ni panzi ndani ya chupa hakuna haja ya kurukaruka maana jogoo hawezi kumdhuru ! Ndiposa Yesu katikati ya dhoruba aliendelea kuuvuta usingizi hadi wanafunzi wake kushangaa, sasa kuikemea dhoruba ni muhimu maana inaweza kukuchelewesha, nikiwa na maana kwamba usije kuacha kumfukuza simba nje ya boma, kwa madai kuwa hawezi kukudhuru ni kweli ila kumfukuza ni muhimu maana kila jambo linalonuia kukuondolea utulivu ni la kukemea,lakini mengine ni ya muda tu, na njia kuu, ni wewe kutulia, yaani kusalia na amani, maana utulivu utakupa kufikiri kabla ya kutenda, kuwa simba yumo nje, sasa nikirukia nje ndo nitakuwa nimemalizika kabisa, kwamba huyu jogoo au kuku yumo nje ya chupa sasa nikimfuata huko ndo nitamalizika moja kwa moja !
Ila ukikosa utulivu huwezi kuyafikiri hayo ! Maana kama shida ni mume, utagundua nikitoka kwa Yesu hakika ndipo nitajiharibia zaidi ! Maana maandiko husema huko nje kuna mbwa !
Kama hujaokoka na unataka kuokoka tafadhali fuatisha nami kwa imani sala hii ya toba, Sema: Mungu Baba, nisamehe, nimetambua ya kuwa ni mwenye dhambi, sasa ninatubu, ninakuamini na kukupokea moyoni mwangu kama Bwana na mwokozi wa maisha yangu, nakuomba ufute jina langu kwenye kitabu cha huku na uliandike sasa kwenye kitabu cha uzima wa milele, Ameni.
Hongera kwa kuokoka, na tafuta sasa kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, na ujitambulishe kuwa umeoka hivi karibuni ili wakulee zaidi kiroho, kwa mawasiliano au sadaka M-PESA, maombi na ushauri, ni +255759859287, E-Mail: ukombozigospel@gmail.com, Tupo Arusha Tanzania. Na Mwalimu Oscar Samba. Zaidi tembelea, www.ukombozigospel.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni