Na Mwalimu
Oscar Samba:
“Akawaambia
mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.” Luka
18:1.
Nina
kusalimu ndugu yangu kupitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo! Ni yangu matumaini
ya kuwa u mzima tena buheri wa afya tele, na kama sivyo basi Bwana wetu Yesu
Kristo aipatie nafsi yako amani, na faraja tele. Na kama ni uponyaji au haja fulani,
ipokee kwa imani sasa!
Siku ya leo
hapa mtandaoni nimekuandalia ujumbe huu muhimu sana, wenye mukutadha ama sura
ya kukutaka kuona umuhimu wa maombi ya nayoombwa bila kukoma, au kukata tamaa!
Kuomba sio
msisitizo wangu mkubwa sana hapa, bali ulio mkubwa ni kuomba bila kukuta tamaa,
ni maombi yenye kukaza na yasiyo na hali ya kulega, au muombaji asiye zimia
njiani, ni mwenye kumngoja Bwana, kama vile Zaburi isemavyo kuwa amemngoja kama
vile mlinzi aingojavyo asubuhi, au Ayubu kama vile muajiriwa anavyosubiria mshahara
wake wa mwisho wa mwenzi!
Huku siko
kungoja kwa kawaida, bali ni kungoja kulikojawa na matumaini ndani yake wapo
wanaongoja ila mioyoni mwao walishazimia, maana kitendo cha Zakaria kushindwa
kumuamini moja kwa moja malaika Gabrieli aliyemletea taarifa za majibu ya
maombi yao kiliashiria hali fulani ya kuchoka au kuvunjia moyo ndani!
Mpendwa!
Kisa kifuatacho ni muhimu sana kwenye maisha yako ya wokovu ! ni habari za mtu
ambaye Yesu anatufunza kuhusu jambo hili kwamba alikuwa na rafiki yake, na
alipatwa na mgeni, na kwenda kuhitaji msaada kwake maana mgeni huyu alikuja
usiku na hakukuwa na bajeti yake, naye moja kwa moja kufikiri kwenda kwa rafiki
yake ili amsadie!
Alipomuendea
haikuwa jambo jepesi kwake kupata msaada, bali moja kwa moja alikabiliaana na
upinzani, lakini hakukata tamaa, alizidi kukaza, na hatimae rafiki yake aliamua
kumpatia hitaji lake!
Ona:
Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki,
akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate
mitatu,
kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka
safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema,
Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto
wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia
ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile
asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.
Yesu
anunganisha kisa hiki na somo la kujibiwa kwa maombi yetu, jambo linalotupa
hakikisho la kujibiwa ila changamoto inasalia kuwa ni kuwa na aina hii ya moyo
au tabia ya kutokukata tama kabla ya kupokea majibu yetu!
Endelea
kusoma: Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni,
nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye
abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba
mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai,
atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa
vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao
wamwombao? Luka 11:5-13.
Ni kwambie
wazi kuwa sio kila mahitaji utayapata kwa wakati ambao wewe unautaka, na ni
kawaida kabisa ya moyo wa mwanadamu kuumia pale mahitaji yanaposhindwa
kupatikana au kupatiwa ufumbuzi kama muhusika alivyohitaji, maana Mithali
husema bayana kuwa hiyo haja ikipatikana ni kama mti wa uzima ila ikikosekana
moyo huugua, 13:12, lakini nakuimiza sana kufahamu kuwa sio kila hitaji uombalo
utajibiwa kiwepesi, na kimya cha Mungu haimaanishi kuwa amekusahau, au amepuzia
hitaji lako! Hili lishike sana.
Sasa leo
sitakujuza sababu za Mungu kutokufanya hivyo, ila tambua kwamba zipo kadha wa
kadha ikiwemo za Mungu kukuimarisha kiroho, akihitaji kukujengea saburi, na kisha
udhabiti wa moyo kama vile Warumi 5:1-5 inavyodhibitisha, lakini usisahau
kwamba upinzani pia upo, majibu ya muombaji Danieli yalichelewa na ni shauri ya
upinzani, nawe yamkini siku uliyoanza kuomba tu ulikwisha kujibiwa ila adui
ameweka upinzani, sasa usife moyo bali endelea kuomba yamkini upo siku ya 20 au
ya 17, na bado masaa au siku chache tu ili upokee mujiza wako!
Najifunza
nguvu hii ya maombi ya kutokukata tamaa sio kwa Danieli tu ambaye licha baada
ya kumaliza siku zake 21 alikuja kutokewa kiupya na Mungu siku ya 4 baada ya
kumaliza hiyo vita, lakini pia ninaipata nguvu na ujasiri mwingine ninao uchukuwa
kutokana na mafunzo ya Yesu katika kitabu kile cha Luka 18, pale tunajifunza
funzo muhimu sana, ambalo linatutaka sio kusalia na matumaini tu, bali
tuendelee kumkumbusha Mungu, japo haina maana kuwa huwa anafika pahali na
kusahau, ila kumkumbusha kwetu ni sawa na kumsonga, kama huyu mjane kwa hakimu,
ama kama vile huyu aliyemwendea rafiki yake na kuzidi sana kumsonga, kisha
alipokea haja yake!
Ni kweli
Mungu huweza kusema nitakujibu, nitakupa, ila kwa kumsonga kwako akalifanikisha
kwa haraka, na ipo hatari kwamba kwa kunyamaza kwako huwenda usilipate kabisa
jambo hilo, maaana jaribu kufikiri kama huyu angeishilia hatua ya kwanza mara
baada ya jibu la rafiki yake kuwa tumekwisha kulala na hakuhitaji huo usumbufu
ama jibu la awali la hakimu kama lingefanyika kikwazo kwa mama mjane! Sidhani
kama hitaji lao lingalikuwa na majibu!
Jionee:
Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa
kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika
mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na
mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui
wangu.
Naye kwa
muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali
watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije
akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi
dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na
usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini,
atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?
Jambo hili
na aina hii ya tabia ni muhimu sana katika maisha ya muamini! Usikubali kuwa
mtu mwepesi wa kukata tamaa, maisha ya wokovu yanawahitaji mashujaa wa imani,
watu ambao wanaona majibu hata katika mazingira ambayo sio rahisi kuonekana,
uwe kama Daudi, wakati wengine wamekata tamaa, na hawauoni msaada wa Mungu
maana adui yao amewatukana kwa muda wa siku 40, yeye aliuona, na kusema kuwa
asizimie mtu moyo, tena amwambia mfalme Sauli, ikiwa na maana kwamba alimjua anayemtegemea
na kumuamini.
Uwe shujaa
wa imani, usikubali kuchoka kiwepesi, macho yako yamtazame yeye, mkumbuke
mwanamke aliyeshika pindo la Yesu, na kupokea uponyaji wake ni kwamba aliteseka
na jambo hilo kwa muda wa miaka 12, na baadae Mungu alikuja na kumtokea, lakini
hakumtokea akiwa amechoka, bali alichukuwa hatua ya kushika ule upindo, aliungangania
na kisha kuondoka na mujiza wake.
Mpedwa
kuchoka kiroho hukuondolea imani, kwa hiyo siku ya kushika pindo itakupita
maana imani yako haipo tena, na utakuwa ukibishana na msukumo wa Roho Mtakatifu
unapokutaka kuingia kwenye maombi, kama walio wengi hivi leo wanavyobishana
maana wamechoka, na wanapoimizwa kufunga na kuomba, wanaanza kuwaza na kukubali
kuhubiriwa na Shetani kuwa mbona Mungu hakuwatokea siku zote hizo! Huo ni moyo
ulioinama na kwa bahati mbaya sana unashindwa kushika pindo la Yesu!
Mpendwa ni
kweli swala la kuomba bila kukoma halipo tu katika mukutadha wa muda, (ikiwa na
maana ya muhusika kuona majibu yake yamekawia tu la!) Bali hata vikwazo!
Kuna watu
wanapanga maombi ya kufunga na kuomba na kukitokea vita wanajikuta wanahairisha,
huko ni kushindwa kushinda vizuizi vya maombi, wengine huishilia kufadhaika na
kumia kissha kujikuta wakiomba kiulegevu au hawaombi kabisa, na wapo ambao huomba
maombi ya manunguniko; mtu mmoja akaniambia kuwa anajikuta kila akitaka kuomba
au akimtafakari Mungu anamtukana tu! Ni baada ya kumuona Mungu kama
aliyechelewa kumponya dada yake!
Mtu mmoja
alisema kuwa Mungu ni Mungu hata kama hajajibu maombi yake, na hata kama
amechelewa huwa anasalia kuwa Mungu, amejibu au hajajibu, hiyo haibadilishi Uungu
wake! Wala msingi wa Uungu na wokovu haupatikani katika kuomba na kujibiwa!
Hapa ni
muhimu sana kupajua maana nimeona watu walioomba ndugu zao wapone na wanapokuja
kufariki au kuteseka kwa muda mrefu, hujikuta wanashindwa kumuelewa Mungu hata
wengine kufikia hatua kabisa ya kutaka kuacha wokovu, na wengine hawaombi tena,
ama hujawa na manunguniko!
Sasa kitabu
chetu cha USIFIE JANGWANI kina mada ya namna ya kufanya unapomuona Mungu
amechelewa au kukawia kujibu maombi yako, pia kipo kitabu cha NGUVU YA MAOMBI
YA MUDA MREFU, lakini fahamu sana kuwa Mungu ni Mungu hata kama amekujibu au
hajakujibu!
Daudi
alikuwa ni mfalme, lakini aliomba na mwanae hakupona, Yesu aliwahi kuomba
maombi ambayo hayakujibuwa, yale ya kikombe kimuepuke, aliwahi kuumia na
kufikia hatua ya kusema Mungu wangu mbona umeniacha! Hapo napo pana funzo
kubwa!
Lakini
tukiendelea ni kwamba, ni muhimu kujifunza kushinda vikwavyo, na vipo vingi,
mumeo, au mke, watoto, na afya, mchungaji kwa watumishi, au washirika na wakuu
wako kikazi wanaweza kufanyika kikwazo, lakini wewe usife moyo na kuamua
kuhairisha maombi yako, au kujikuta ukiomba kwa ulegevu ama kuacha kuomba
kabisa!
Jionee kwa
huyu mtu! Alikuwa ni kipofu, napo alihitaji kumuendea Yesu. Lakini watu wake
Yesu waliokuwa nae, ambao tulitegemea ndio ambao walipaswa kuwa msaada wa
kwanza kwake, walimvunja moyo, walijaribu kumzuia!
Wakafika
Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake,
na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa
ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza
sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, Na wengi wakamkemea ili anyamaze,
lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu.
Tazama zuio
hilo lakini mara baada ya amri ya Yesu iliyowataka kumuita, hao hao ndio
waliokuja kufanyika watiaji moyo wake, na hatimae kwa kukaza kwake, alipokea msaada
au majibu yake! Jifunze sana kuwa, alipozuiliwa, hakuvunjika moyo, bali alizidi
kuita!
Katika Mathayo
tunauona mukutadha huu vyema, japo kuna kuonekana kuwa walikuwa wawili, ila
nataka uuone huu mukutadha wa kutokukatishwa tamaa kiupana zaidi; “Mkutano
wakawakaripia, wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema,
Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi.” 20:31 .
Tuendelee;
Yesu
akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo;
inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu,
akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu,
nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara
akapata kuona; akamfuata njiani.
Mwanamke
huyu ni kielelezo kikubwa sana cha kujifunza kwetu! Yesu alimpitisha katika
vipimo kadha wa kadha na hatimae alishinda na yeye kuondoka na majibu yake! Kwa
hiyo hupaswi kuvunjika moyo, uwe shujaa, maana tabia hiyo ndio ambayo Yesu anahiitaji
kwako;
Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile
akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti
yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake
wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele
nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya
Israeli.
Naye akaja
akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa
chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa
hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia,
Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu
saa ile.
Licha ya kujifunza
swala la umuhimu wa kuwa na moyo usiokata tamaa kiwepesi na hata kukwazika kwa
haraka, lakini pia lipo somo la kujifunza jingine, ambalo ni umuhimu au dhamani
ama nguvu ya maombi ya hoja, kila hoja aliyoletewa kama kikwazo, aliipangua kwa
maumakini!
Tunamuona Yesu
akiisifia imani yake, ikiwa na maana kwamba pia unatakiwa kuhakikisha kiwango
chako cha imani hakiyumbi pindi unapokuwa katika hali kama hii ya majibu yako
kuonekana kana kwamba yamekawia mbele za Mungu!
Yapo mengi ndugu
yangu ambayo ningeweza kuyanena ili kuzidi kukutia moyo, ila kwa hayo, nawiwa kukukumbusha
kuhakikisha kwamba unazidi kukaza katika kumtazama Yeye, ambaye ndiye mwenye
kukupatia majibu yako, haijalishi ni mwenzi wako au mwanandoa mwenzako amekuwa
mwiba, ni mwenye hitaji la kuoa au kuolewa, uchumi ni mgumu, huduma haina
mpenyo, yote katika yote fahamu sana kuwa utavuna kwa wakati ila kama hutazimia
moyo, kwa hiyo usikubali kuzimia moyo.
Lakini pia
kama hujaokoka, na unataka kuokoka, tafadhali fuatisha nami maneno haya ya sala
ya toba, na fahamu sana kuwa wokovu sio dini mpya, bali ni kutengeneza na
Bwana, ni kuishi maisha mapya yanayompendeza Mungu, ili hata ukifa leo uende mbinguni,
na kumbuka nje ya wokovu hakuna kumuona Mungu, bali kuna adhabu ya moto wa
jehanam wa milele, ni yangu rai kukuepushia adhabu hiyo, na kukusaidia kuingia
katika Paradiso nchi au eneo lenye raha ya milele, ili umiliki, kufurahi, na
kuishi pamoja na Mungu, tuwaone watakatifu huko kama wakina Ibrahimu, na
Lazaro, na mitume, na manabii kama wakina Elian pia Heneko, Musa na wengine ambao
yamkini walifanikiwa kuingia, kumbuka tena kuwa, nje ya hapo utaishi na Shetani
milele, sasa epuka hili!
Sema; MUNGU
BABA, NINAKUPENDA, ASANTE KWA KUNIPENDA KWANZA, LEO NIMETAMBUA KUWA MIMI NI
MWENYE DHAMBI, NA NIPO TAYARI KUOKOOKA, TAFADHALI INGIA NDANI YANGU, SAMEHE
DHAMBI ZANGU, NA FUTA JINA LANGU KATIKA KITABU CHA HUKU, NA ULIANDIKE SASA KATIKA
KITABU CHA UZIMA WA MILELE, Ameni.
Kwa kufanya
hiyo umekwisha kuokoka sasa, na tafadhali tafuta kanisa la watu waliokoka lililopo
karibu nawe ukasali, hapo, waambie kuwa umeokoa hivi karibuni, ili wakulee
vyema kiroho.
Mawasiliano
yetu, kwa M-Pesa au Simu: +255 759 859 287, barua pepe: ukombozigospel@gmail.com
pia temnbelea:
www.ukombozigospel.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni