Alhamisi, 25 Juni 2020

UWE HODARI, SHUJAA NA MOYO MKUU.



Na Mwalimu Osacar Samba
Kuna kipindi nilipitia mahali pa gumu sana, na kutamani kufa, ama kujiua, ilifika mahali nikiwa napita mjini nilitamani kujirusha mbele ya gari ili nife! Moyo wangu ulipoteza matumaini kwa kiwango kikubwa sana! Ila kila nikitaka kufanya hivyo mbele yangu kwenye ulimwengu wa roho na kwenye mawazo yangu au nafsini mwangu nilikuwa nikiletewa picha ya watu ambao wamekwama mahali na kisha sauti kuniambia kuwa hao watu wananitegemea au wananingojea mimi! Nikikwama na wao watakwama!

Wakati namsimulia mshirika au kijana wangu mmoja aliniambia kuwa, “sasa mchungaji hauoni kuwa hao watu ndio mimi! Kama ungejiua leo ningepata wapi huu msaada!” nilifikiri kwa kina na kulitia jambo lile moyoni mwangu!


Sasa leo asubuhi (siku ya mwanzo ya uandishi) nikiwa hapa darasani, wakati naongoza maombi nilisukumwa kusoma andiko la kitabu cha Yoshua, 1:6-8; ambapo Roho alinifunza kitu kigumu kiidogo, kwamba ni Yoshua ndiye aliyepewa jukumu la kuhakikisha wana wa Israeli wanavuka salama!

Ikiwa na mjaaana kwamba kukwama kwa Yoshua kunatazamwa kama kukwama kwa wana wa Israeli! Maaana Mungu yu akisema kuwa, “.. maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.

Ni “wewe, utakaye warithisha!” kuna kanuni kadhaa alimpatia, ikiwemo ya ujasiri, au ushujaa, ila nataka tu kwanza uone uzito wa jambo hili, kwamba kufika Kanani kwa wana wa Israeli ni kwa kiasi gani kulimtegemea Yoshua! Na sasa uje katika uhalisia, ujione ni kwa jinsi gani watu ambao Mungu amewaweka mbele yako wanavyokutegemea wewe! Kama hujijui wewe ni nani uwe na hakika Mungu anakujua, na Shetani analifahamu hilo pia ndio maana aachi kukuletea vita ili usiwafikishe watu wako katika urithi wao!

Labla nikuulize jambo hili muhimu sana! Je, uliwahi kufikiri kuwa ni watu wangapi wanategemea kusimama kwako? Ni watu wangapi wanategemea kusoma kwako? Ni watu wangapi wanategemea kuinuka kwako kiuchumi? Bidhaa zako unajua zinatakiwa kuwanufaisha watu wangapi? Au ni wangapi wanategemea ajira kutoka kwako?

Na kama ukikwama leo kiutumishi kwa kukata tamaa ni watu wangapi wataenda jehanum ya moto kutokana na kushindwa kwako kihuduma!
Kama hujawahi kuwaza hilo twende moja kwa moja kwa Yesu pale Gethisismane, ambapo alifikia mahali pa gumu sana na kuomba ikiwezekana kikombe kile kimuepuke! Jaribu kuwaza kama angekwamia pale, ni nini kingetokea? Ni hasara kubwa kiasi gani ingetokea kama Paulo mtume angeshindwa kuvuka vikwazo vya kihuduma! Hapana shaka nyaraka kama za Wathesalonike, Wakorintho, Timotheo, Tito na Wagalia, bila kusahau Warumi na sehemu kubwa ya Matendo ya Mitume tusingekuwa navyo leo! Natumai ni bila shaka!

Nawe unajua moyoni mwako kuna nyaraka ngapi za Matendo ya Mitume, kuna wakina Timotheo, na Tito wangapi wanaokusubiria ili wao wasimame! Je, uliwahi kufikiri kuna Wagalatia wangapi na watu wa kanisa la Rumi ambao kwa kweli wewe ndie wanaokutazama maana injili uliyopewa ni kwa ajili yao, ni kweli wapo wakina Petro ila wao wameitiwa kwa Wayahudi!

Jaribu kufikiri waliobuni umeme, au tekinolojia ya “komputa” au mtandao wa “intaneti,” simu na kadhalika kama wangekwamia njia ni nini kingetokea? Leo unasafiri kwa ndege na magari ila fahamu kuna watu walilipa gharama, kuna waliobuni madawa na vifaa vya mahosipitalini ambao waligharimika hata uhai wao ila leo ukienda hosipitalini unapata huduma kiurahisi! Fikiri kama wao wangekwama je!

Yamkini umeajiriwa, na unaona kuna ugumu kupambana ili nawe siku moja uwe na kampuni yako ambayo itaajiri watu wengi, na msukumo huo unao, lakini umechoka kiwango cha kukata tamaa, fikiri kama aliyekuajiri naye angekwamia mahali je! Au unafikiri naye hakupitia changamoto! Hapana! Tena kwa ujarsiri kabisa ninamsema kuwa ni hapa!  Alijipa moyo, na kushinda vikwazo, uamini kamulize au tafuta ushuhuda wake!

Kuna watu wanategemea hilo wazo lako, ambalo Mungu ameliweka moyoni mwako, na kukwama kwako ni kukwama kwao pia! Hakuna mabadiliko yanayoletwa na watu wawili, au watano, wazo huanza na mtu mmoja, wengine ni waunga mkono wa ndoto hizo au hiyo.

Karibu sana kwenye kitabu hiki, ambacho kinalenga kukutazamanisha umuhimu wa kilichopo moyoni mwako, ili uweze kushinda vikwazo ambavyo vinakukabili leo, kwani Mungu alimbwambia “Yoshua” awe hodari, na moyo wa ushujaa mkuu, maana ni yeye ndiye mwenye kurithisha, na wewe ndie mwenye kurithisha watu uliopewa, wewe ndie mwenye majibu yao, kwa hiyo usije kufikiri kukwama hapo, katika kitabu hiki utajionea pia jinsi Musa na wengineo walivyokwama na watu kukwa, Musa alipokimbia Midiani, wana wa Israeli walichelewa kutoka utumwani kwa muda wa miaka 30, na walitoka Musa alipokaa kwenye nafasi yake, wasomaji wa kitabu cha waamuzi watakubaliana na mimi kiurahisis sana! Na wewe ni jibu kwa watu! Ukikwama watakawama na wao pia, Daudi alifanyika jibu kwa watu waliotukanwa siku 40, jaribu kufikiri kama naye angekwama je! Sasa mbona wewe unataka kuacha masomo! Mbona unafikiria kuacha huduma, mbona unataka kuacha imani! Inuka, uwe hodari, na moyo wa ushujaa mkuu maana ni wewe, wala sio jirani yako atakayewafikisha watu uliopewa na Mungu katika hatima yao njema!

Wala usiseme tena kuwa wapo wengine! Ni kweli wakina Petro na Yohana walikwepo, ila wao waliitiwa kwa Wayahudi, kuna watu wa Galatia, Krete, na Hispania, na Rumi na Wathesalonike wanao subiria kuinuka kwako, kama umepigwa kama Paulo na kuburutwa hata nje ya mji wewe inuka tena, na songa mbele, melikebu ikivunjika,na huko katika mji huo wa Malta, wewe hubiri, mseme Yesu hapo, maana hapo napo kuna watu ambao wanakutegemea;
Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakapozwa;  nao wakatuheshimu kwa heshima nyingi; basi tulipoabiri wakatupakilia vitu vile tulivyokuwa na haja navyo. Matendo ya Mitume 28:9 -29.

Tuna kitabu kinachoitwa, KATIKATI YA SHIMO MKUMBUKE MUNGU, unajua kina semaje? Kauli kuu ya kitabu hiki au nia yake, ni kumtia moyo na kumtaka mtu ambaye yupo mahali pa gumu kuendelea na kusudi la Mungu!
Wanakina Meshaki, Shedraki na Aberinego walikuwa katika shimo la moto, lakini huko nako waliendelea kumtukuza, hata walipotishiwa kutupwa huko bado walitaja ukuu wa Mungu wao!

Danieli alipokuwa kwenye tanuru lile la simba, bado alitaja ukuu wa Mungu, maana mfalme alipomuliza,hakuwa na maneno ya kukata tamaa, bali alimtukuza Mungu wake; Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Danieli 6: 22. Hayo ni maneno ya mtu ambaye amezingirwa na simba! Tena yupo kwenye shimo ambalo hawezi kutoka! Na anayemjibu ndiye aliyemtupa kwenye hilo shimo! Kikawaida angeweza kumkasirikia na kumtamkia maneno magumu na kumuona kama mtesi wake! Angeweza kumkasirikia pia na Mungu wake!

Ila alijua kuwa leo kuna wakina Mwalimu Oscar na wewe ambao watahitaji kusoma hiki kitabu cha Danieli ili watiwe moyo, nao wajuwe uweza wa Kiungu jinsi ulivyo! Na wewe mbele yako au miaka ijayo, wapo ambao watasimama na kuinuka kutokana na utendaji wako wa leo!

Kwa hiyo, ukiwa kwenye shimo lako, usife moyo, wewe endelea kusonga mbele,Yusufu alipokuwa kwenye lile shimo walilomtupa, waliendelea na imani, wala hakuwakasirikia ndugu zake!

Hata gerezani cha ajabu aliendelea kumsema Mungu na kumtaja Yeye! Wengine wakipita kwenye shida kidogo tu hata kabla haijakolea vizuri tayari wameshanungunika maneno yote! …Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu?...Mwanzo 40:8.

Nakukumbusha tena na tena kuwa, mbele yako kuna watu, na hao watu wanakutegema wewe! Ukikwama sio kwamba umekwama wewe mwenyewe, bali ni umewakwamisha wengine! Kama Yesu angekwama siku ile ya usiku mmoja, fikiri ni wangapi waliotegema ukombozi wake ambao wangekwama pamoja naye!

Ni rahisi sana kusema kuwa Mungu ana watu wengi! Sio kweli, mwenyewe husema haya maneno!
 Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.  Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU. Ezekia 22: 30-31.

Ni muhimu sana kuijua hii kanuni, kuwa Mungu hawezi kushuka katika ulimwengu huu na kupita mitaani akihubiri injili, au akifanya biashara ama kufungua kampuni itakayo ajiri watu kadhaa, ama akipita na kuimba, au akifanya shughuli za kilimo jibu ni la! Ndio maana hata alipohitaji ukombozi, wa ulimwengu ilimlazimu kufwata kanuni za kuishi katika ulimwengu huu, akamtoa mwanaye kisha akampatia mwili ambao ndio ungemuwezesha kuishi humu dunini!

Pili jambo la kufanya kitu fulani ni kipawa, maana yake kuna mtu ameandaliwa maalumu kwa ajili ya kitu hicho! Na mahali fulani, au watu fulani, ama kusudi fulani, hukuitiwa kufanya kila kitu, na hutakaa uweze kufanya kila kitu!

Hapo tunaambiwa kuwa Mungu alitafuta mtu! Kisha alimkosa huyo mtu ambaye alikuwa akimtafuta! Na kilichotokea ni Mungu kuangamiza! Kwa hiyo kuna watu waliangamia kwa sababu ya kukosekana mtu! Na wewe kuna watu wataangamia sio kwa sababu watu hawapo ambao wangetenda hayo, ila kwa sababu wewe hukukaa kwenye nafasi yako kwa kukosekana wewe mtu! Wao wanaangamia! Mimi ni mtu! Ninayekuletea kitabu hiki, na usifikiri kuwa safari yangu ya kiroho imekuwa nyepesi! La! Leo nina vitabu zaidi ya mia moja, haikuwa jambo rahisi, ila ukweli ni kwamba! Nimejitahidi kushinda vikwazo, nabado nazidi kuvishinda maana mimi mi ktu ambaye Mungu anamuhitaji au anamtaka akae kwenye nafasi yake! Najua nyuma yangu wapo wengi wanaotarajia kuvuka kwa huduma yangu! Na kwako pia wapo! Hata kama ni muuza karanga, wapo ambao wanakutegemea !

Unajua wazo hili la kusema wapo wengine ni wazo dhaifu sana! Ndio, wala usipigwe na butwaa, maana jaribu kujiuliza ni kwa nini Mungu aliamua kumfuata Yona baharini alipokimbia! Ni kwa sababau hakuna mwingine aliyekuwa ameandaliwa kwa ajili ya jukumu lile!
Mungu wetu ni mwekezaji, kama mwalimu mmoja wa neno la Mungu anavyopenda kusisitiza hili jambo! Mungu aliwekeza kwa Yona, na Mungu amewekeza kwako pia! Anataka faida, anataka umtumikie!

Nakumbuka kisa kimoja cha mwalimu wetu wa chuo cha Biblia, Dr. Immaculate Nighula, alitumbia kuwa alipokuwa nahitimu masomo yake ya chuo katika nchi fulani, aliamua kuingia kwenye pango au msitu wa maombi, na kuomba kwa muda wa siku saba, Mungu alimtokea maana alikuwa na hitajio la kutaka kujua ni eneo gani ambalo Mungu anamtaka aende kuhudumu! Anasema kuwa cha ajabu kilichotokea ni hiki! Aliota au aliona katika maono akiwa anahesabu fedha nyingi sana, alizihesabu hadi alipozimaliza!

Alishituka na kuanza kujiuliza maana yake ni nini! Katika fahamu zake, alidhania kuwa Mungu atampatia fedha nyingi sana! Ila alisikia sauti ikimwambia kuwa, “sadaka zangu,” ikiwa na ufafanuzi kwamba nimewekeza kwako, na anahitaji yeye alipe uwekezaji huo kwa kumtumikia!
Unajua kikawaida sio rahisis sana kwa yeye kukubali kuja kufundisha chuo cha biblia maana wengi tukiitwa mbio zetu ni kwenye utumishi wa madhabahuni na hii huwa na sababu zake kadha wa kadha!

Ila Mungu anajaribu kumwambia kuwa mimi ni mwekezaji, nimetumia gharama zangu, umesoma kwa sadaka zangu, sasa nataka faida! Unafikiria Mungu hana watu, ni kweli ana watu ila hana kila mtu!

Inawezekana na wewe hujalipiwa ada kwa jinsi ya mwilini, ila kuna shule ya kiroho uliyopitishwa, jifunze sana kwa Yoshua, ambapo Mungu alimwagiza Musa amlee, amfundishe, amtie moyo, ili baadae aje kuwa kiuongozi.
 Lakini mwagize Yoshua umtie moyo mkuu, umtie na nguvu; kwani ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, na nchi utakayoiona atawarithisha yeye. Kumbukumbu 3:28.

Twende kwa wanfunzi wa Yesu, ambao walikaa mjiguuni pa Yesu kwa muda wa miaka kadhaa, wakifundishwa, na kulelewa, kuna muda Yesu alikuwa anawatuma kufanya mazoezi, kisha itokee wakujaribu kukataa wito! Au kazi! Uwe na hakika ni hasara kwenye ufalme wa mbinguni, maana ni gharama kubwa imetumika kumuandaa muhusika!

Lakini licha ya maandalizi kama hayo yapo mengine pia ya ulinzi! Kwani hukuwahi kusikia kuwa kulikuwa na majambazi sita, watano wameuawa ila mmoja tu ndiye aliyepona! Na alipopona alikuja kuokoka, na sasa ni mtumishi! Unajua maana yake ni nini! Ni kwamba kuna ulinzi fulani wa ziada ulisalia, na sio kwamba ulikuwa na kazi nyingne tu, wala haina maana kuwa huyu ni mwema sana la! Ila ni kwa sababu ya kilichokwepo ndani yake ambacho kinasubiriwa na watu wengi!
Kiongozi wetu au katibu wetu wa seriali ya wanafunzi hapa chuoni aitwae Chai, anasema kuwa siku moja walikuwa wakisafiri na gari lao kuharibikia njia, walipokuwa wakipakuwa mizigo ili waamishie gari jingine, ghafula alisikia sauti ikimwambia kuwa “toka hapo na uingie kwenye gari,” na alipotoka mara baada ya kuingia, lilitokea gari jingine na kuwagonga watu waliosalia kwenye ule mstari na hapo kwa papo walifariki watu kama watano!

Huyu kapona! Ila wengine hawapo! Ni kwa sababu mbele yake kuna watu wanaomsubiria, japo na waliokufa nao walikuwa na watu ila neema yake Mungu haichunguziki!

Watoto walipotakiwa uuawa, Musa aliokolewa, kimujiza, Yesu alitoroshwa, na watoto wengi sana kuawa katika nchi ile, sio kwamba Mungu hakuwapenda hao wengine, na wazazi wao mbona hawakuambiwa nao wakimbie, ila ukweli ni kwamba Mungu amelinda kilichopo ndani yako!

Kuna muhubiri mmoja mkubwa na mwalimu wa neno la Mungu hapa nchini, anasema kuwa kipindi anazaliwa kila aliyeenda kwenye ile hosipitali aliyejifungua kwa njia ya upasuaji alikuwa anakufa yeye na mtoto, yaani mama na mwanaye, kuna ndugu wa mama yake ambaye ni dakitari aliamua kumwambia mamaye kuwa angojee kidogo maana dakitari husika atarudi nchini kwao likizo, akitaka kumuokoa na hali husika, na kweli ikawa hivyo, naye alizaliwa salama na kuishi hadi leo japo mamaye naye alifanyiwa upasuaji!

Jambo jingine la kufahamu ni kwamba, Mungu amewekeza ndani yetu hata kabla hatujazaliwa, kabla ya kutoka tumboni tayari uwekezaji ulikwepo, kipaji cha uimbaji, ufahamu wa kitekinolojia, utumishi na kadhalika husimikwa tumboni, au kabla ya mimba kutungwa, uongozi pia kama kipaji, sasa unapokuja duniani tayari wewe ni mbeba maono, jifunze kwa Yohana mbatizaji, Samsoni na Isaka, utajionea jambo hili, pia habari za kuzaliwa kwa Yesu.

Lakini pia Yeremia moja, inasema hili wa kina sana, jionee hapa ambapo Paulo mtume anapolilisisitiza jambo hili;
Wagalatia 1:15  Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake.

Ni muhimu sana kutambua kuwa, Mungu hajakuleta duniani kwa mbaya! Lipo kusudi, ama lipo jambo ambalo unapaswa kulifanya! Pia hakuna jambo linaloweza kufanikiwa kirahisis! Inakuhitaji kuwa na moyo mkuu, inakuhitaji kuwa shujaa, na hodari! Ile maandiko yanakutaka kuwa hodari, kisha ushujaa uzaliwe, uwe na hakika kwamba vipo vita, ama zipo changamoto!

Safari ya kubeba maono sio nyepesi, sio jambo lenye kuhitaji ulegevu, bali linahitaji moyo mkuu, tunatazama jinsi wabeba maono walivyopitia misukosuko, na ujiulize sana kwamba kama wangekwama nini kingalitokea! Na majibu yake yaweke kwako!

Sijui kama unajiuliza hili swali! Kwamba kama Elia angekwama pale, (katika 1 Wafalme 19) alipojiombea nafsi yake afe, ni kwamba tusingempata Elisha, wala Yehu, lakini pia Elisha baadae upako aliokuwa nao, ulitegemea uwepo wa Elia maana ndie aliyemrithisha kijiti!

Elisha alipokea ujumbe wa wito kutoka kwa Elia, Yehu ni matokeo ya Elia, lakini pia mwishoni Elisha alipokea upako mara dufu! Sasa ingalikuaje kama Elia angekatisha safari yake!

Ni kweli mazingira yalikuwa magumu, ndio! Ila hupaswi kuishia njiani! Yupo Elisha wako, wapo wakina Yehu, ambao wanakusubiria wewe! Ukikwama na wao pia wamekwama!

Fahamu sana, tena mno, kuwa hakuna “kopi” yako huku duniani! Wewe ni wewe, kuna vitu vya kipekee vimo ndani yako, ambavyo hata kwa Paulo mtume havikwepo!
                                Kitabu kikitoka kitafute!
Hongera kwa kusoma ujumbe huu, nakutia moyo kuzidi kumtazama Mungu, na pia uwenda hujaokoka, yaani Yesu sio Bwana na mwokozi wa maisha yako! Nakutia moyo pia kuokoka sasa! Yamkini ni uchumi, fedha, hazipatikani, unazingirwa na nuksi na mikosi, kila unalofanya haliendi, unakabwa na mapepo, ! Wewe njoo kwa Yesu na hayo yote yatapita kabisa ! Sasa natumi u tayari!
Sema; MUNGU BABA, NINAKUPENDA, ASANTE KWA KUNIPENDA KWANZA, LEO NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NA NIPO TAYARI KUOKOOKA, TAFADHALI INGIA NDANI YANGU, SAMEHE DHAMBI ZANGU, NA FUTA JINA LANGU KATIKA KITABU CHA HUKU, NA ULIANDIKE SASA KATIKA KITABU CHA UZIMA WA MILELE, Ameni.

Kwa kufanya hiyo umekwisha kuokoka sasa, na tafadhali tafuta kanisa la watu waliokoka lililopo karibu nawe ukasali, hapo, waambie kuwa umeokoa hivi karibuni, ili wakulee vyema kiroho.
Mawasiliano yetu, kwa M-Pesa au Simu: +255 759 859 287, barua pepe: ukombozigospel@gmail.com


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni