Ijumaa, 9 Juni 2017

MSAADA WA KIROHO KWA WANAOOTA NDOTO WANAKULA VYAKULA, NYAMA, DAMU ,IKIWA NI SEHEMU YA MAAGANO YA KIPEPO. Sehemu ya 1

Na Mwalimu Oscar Samba wa Ug Ministry.
Kuna watu wamekuwa wakisumbuliwa na ndoto mbali mbali ikiwemo wanazoota wakiwa wanakula vyakula, baathi yavyo ikiwa ni nyama, na mbaya zaidi hula nyama za watu, wengine ni damu na nyingine ni damu za watu.

Na baada ya ndoto hizo hujikuta wakiwa na hali mbaya sana kiroho, huku nafsi zao zikigubikwa na huzuni, mafadhaiko yasiyo na uvumilivu, masononeko moyoni, na hata wapo wanaotamani kujiuwa ikiwa ni matokeo ya jambo hilo.

Wapo wanaoishilia kujikwamua katika hilo kwa kujikaza kwa aina ambayo waswahili huiita kujikaza kisabuni lakini adhari zake bado hazikwepeki kwani kama wameokoka hujikuta wakiwa wazito kwenda kanisani, kusoma Neno, kufanya Maombi, na kama walikuwa ni wahuduma kama waimbaji na kadhalika hujikuta wakiwa na uzito wa kuhudumu bila kuwa na sababu za msingi.


Ikifika muda wa ibada gafula hujikuta na uzito ndani mwake usioelezeka wa kwenda kanisani na wengine huwa hivo pia kwa siku ama majira ya kusoma Neno, Maombi au kwenda kwenye huduma ikiwemo mazoezi ya kwaya kwa waimbaji. Ukimuliza sababu huweza kuokoteza yoyote ile ila kwa aliyekuwa wazi huishilia kukwambia ni Shetani tu, au niombee Mtumishi ninamashambulizi au kuna hali nisiyo ielewa.

Ndiposa ninakuwa makini ninapomuona mtu ambae alikuwa ni muudhuriaji mkubwa sana wa ibada na gafula amerudi nyuma ama Mtumishi kushindwa au kulega kufanya huduma. Pia ni mwepesi wakupima au kuchuja kiroho pale mtu anapotoa sababu zilizokufa ili kuuhisha hoja yake ya kutokuja kanisani ama kuacha huduma.
Kwa utangulizi huo sasa twende sanjari katika hoja ninayokusudia kuileta mezani pako majira haya; Awali ya yoto fahamu kuwa sio kila ndoto unayoota unakula ama kunywa maji, soda, juisi ni ya kipepo. La! Bali zipo pia za kimungu, katika kitabu changu cha NGUVU YA NDOTO KWENY ULIMWENGU WA RHO, nimelielezea jambo hili bayana, na nimesema kuwa inamaana pia ya Vita, Kuishi, ikiwa na tafsiri yakwamba kama muhusika amemaliza chakula basi siku zake za kuishi kibibilia zimemalizika maana maadiko husema kuwa mtu atashibishwa siku zake. Ila leo ninazungumzia upande wa tafsiri ya maagano ya kipepo.

Katika makala yangu ya jana nilikupa tafsiri ya maagano ama Agano na kukujuza kuwa ni mapatano baina ya pande kuu mbili. Na kwenye maagano nika kwambia kuwa kuna vitu wa kadaha wa kadha ikiwemo , Mapatano, Mashariti, Ishara ama Alama na kiapo Cha Uaminifu.

Mambo hayo niombee kwa Mungu yamkini tukapata siku ya kuyachambubua ila kwa Ishara nilikwambi kuwa lile Agano la Mungu na Nuhu lilikuwa na Ishara ya upinde wa Mvua na alikadhalika kwa Shetani huwa hivyo ndio maana jamiii nyingine mapaka yakilia usiku ama bundi kwa aina fulani ya sauti ama jambo fulani kutokea wazee wa maeneo hayo hujua hili ni ishara fulani ndiposa hufanya mila ili kutimiza mapatano au mashariti yaliyopo kwenye agano.
Fahamu kuwa maagano tunayoyazungumzia leo ni yale yaliyofanywa na wazazi, mababu zako, viongozi wako wa kisiasa ama kiserikali, wakaya, kabila ama waazilishi wa jambo fulani ambalo wewe ni mhusika aidha kiroho ama kimwili, na yaweze kuwa hata kampuni unayofanyia kazi, shirika au taasisi fulani.
Pia yawezekana ni yale ambayo wewe uliyaingia bila kujua. Haijalishi umeokoka ama huja okoka maswala haya yanahitaji kuyashuhulikia kiundani ili kukufanya kuwa huru. Kumbuka leo ninazungumzia kipengele tu cha chakula ingawaje mbinu hizi pia huweza kuwanasua wale wanaoakumbwa na matatizo ya kuridhi kama magonjwa; unakuta baba au bibi ama mama aliugua ugonjwa huo na kisha mtoto kuugua pia. Somo hilo yamkini likawa ni baada ya hili na litaitwa; NAMNA YA KUJINASUA  KWENYE MATATIZO YA KURDHI KIROHO. Niombee akipenda Mola nikujuze.
Chakula kinasimama kama sehemu ya Agano, kwa hiyo unapoota ndoto za kipepo kama hizo ni fika kuwa ni Ishara ya kwamba upo kwenye Agano ambalo yamkini hata wewe hulijui.
Na unapooteshwa hivyo fahamu kuwa Shetani anakutumikisha, au kuna jambo anataka kuliadhiri kwenye maisha yako.
Upo uhusiano wakaribu sana kati ya chakula na nafsi, ndio maana kwenye kitabu changu kimoja wapo nimeonya sana kula chakua kila mahali kiolela.
TUONE UHUSIANO HUO: Yesu alisema ya kwamba aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino, maana yake aliyeungana nami, au aliyekuwa shirika nami amenisaliti. Yohana 13:18.
Kitabu kile cha Mithali kinasadifu jambo hili na kinaonyesha hayo mahusiano ya nafsi na chakula.
Mithali 23: 6 Usile mkate wa mtu mwenye husuda; Wala usivitamani vyakula vyake vya anasa; 7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe.
AwazavyoNafsini mwake, kwa hiyo muda unakula au kabla yeye huwana na mawazo mabay ama ya hila dhidi yako na hukudhuru. Nimetumia neno kukuwazia maana bibilia ya kingereza haijatumia aonavyo bali imetumia neno afikirivyo ama awazavyo;
(7 For as he thinketh in his heart, so is he: Eat and drink, saith he to thee; but his heart is not with thee. ) Hiyo ni ya King James Version,
Tuone ya Basic English; (Proverbs 23:7 For as the thoughts of his heart are, so is he: Take food and drink, he says to you;but his heart is not with you.{Ni kama yalivyo mawazo ya moyo wake}

Mathara hayo tunayaona kwenye msatari wa 8 ambapo hudhiirika mwilini pia; (8 Tonge lile ulilokula utalitapika, Na maneno yako matamu yatakupotea. )
Mstari wa 6, anataja chakula cha mtu huyu mwenye husuda, kisha msitari wa 7, Tunayaona mahusiano hayo, kwani mtu huyu anakupa chakula kwenye mstari wa 6, ila wa saba, anakinenea ama anakiwazia nafsini mwake na jambo hilo huwa na mathara kwako.

Ninachotaka ukione hapa ni kwamba, mtu huweza kukupa chakula na moyoni ama nafsini mwake akakuwazia vibaya ama anakunenea vibaya na chakula hicho kukudhuru ndiposa mstari wa 8 ukasema utakitapika, na hautaishilia tu hapo bali na maneno matamu yatakutoka. Ikiwa na maana pia mapepo yanapokuotesha hiyo ndoto, hali yako ya kiroho inadhurika kwani maneno matamu huwakilisha pia Uzuri wa Kristo maana Yesu ni Neno. Ndio maana baada ya kuota hivyo, huwa na masoneno huku hali yako ya kiroho ikidumaa. Somo hili lizingatiye maana kwenye kitabu cha Ndoto  kipengele hiki sijakichambua kwa kiwango hiki maaana kitabu kile pia kina lenga sana kutoa tafsiri ya ndoto na kinatafsiri zaidi ya 120 ya ndoto. Tuendelee;
Kabla ya kukujuza namna ya kujinasua ngoja nikupe udhibitisho wa kimaandiko kuhusu uhusiano kati ya maagano na chakula, mana kila mafunuo ya kimungu ni lazima ya bebwe na maandiko.
Tuanze kwenye Agano la Kale, Yule Mtumishi wa Ibrahimu alipotumwa kwenda kumtafutia Isaka Mke, alipofika kwa wakina Labani, alikataa kula chakula hadi kwanza apate majibu ya ombi lake. Maana yake kitendo cha yeye kula chakula kiliashiria mapatano ama makubaliano juu ya jambo fulani baina yake na upande mwingine na jambo hilo huitwa Agano.

Tujiridhishe kimaandiko, Ni Kitabu cha Mwanzo 24: 33 Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema.
Baada ya hapo alisema yaliyompeleka hapo na alipokwisha kufanikiwa ndiposa alikula chakula. Tuone kwenye mstari ule wa Hamsini na nne;  54 Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.
 

Umeona jambo hilo?
 Jana nilikujuza kuhusu alama kwenye Agano, niruhusu kidogo na hapa nitoke nje ya somo kwa kukuonyesha alama ambayo huyu mtumishi aliiweka kwenye hili agano ama patano la kuchumbia ama Ndoa. Mstari wa 22 Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu.
Vitu hivyo alimvika huyu binti, ndio maana ni jambo la hatari sana kwa vijana wanaokubaliana kuoana na kufikia hatua ya kuvikana pete bubu ama vikuku, kumbuka vikuku ni aina fulani ya bangili za shanga ama za asili ambazo huvaliwa miguuni na wengine huvaa kama bangii mikonni. Jambo hili ni hatari sana na mapepo huweza kukaa hapo na kisha kukudhuru. Na kwa wale waliovunja uchumba madhabauni ama kwa njia bubu kwa uchumba bubu kunahitaji kushuhulikia jambo hilo kiroho kwani maagano haya huweza kukuzuilia wewe kuoa ama kuolewa na hata ukifanya hivyo kujikuta una ndoa ngumu isiyoisha migogoo kila siku.
Ndiyo maana baada ya kukubalia ama mtumishi huyu alifanya hivi: 53 Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia.  Tukutane kwenye somo husika.
Tuendelee na chakula kama sehemu ya Agano,ila katika kipengele hicho hapo juu pia ni vyema kuepuka kupokea zawadi ama vitu kwa mtu ambaye baado haujamridhia kuwa naye kimahusiano kwa ajili ya kuingia kwenye Ndoa maana pia ni hatari kama atavinenea au kuviambatanisha na agano. (yaweza kuwa hivi.. “Kama kweli umenipenda, pokea zawadi hii na kila uitumiapo, uiangaliapo ukumbuke pendo letu”). Ukipokea hata kama huja sema ndio maana yake umeingia kwenye Agano. Maana agano ni mapatano.
Ndio maana Msichana anayekula hipsi kuku za mvulana fulani ni vigumu kukwepa ama kuponyoka kwenye mtego wa ajenda ya huyo mwanaume, maana chakula kile huambatana na nafsi yake, na fahamu kwenye nafsi ndiko kwenye maamuzi, akili na hata nia.
Ni hatari kula cha mtu alafu ukijifanya eti utakula kisha utamkwepa, rohoni anakubalidisha, utashangaa, huyo ni kama vile umemkwepa ila baada ya miaka au miezi kadhaa umenaswa kwenye mtego wa mwingine mwenye ajenda kama ile bila kujua chanzo ni yule wa awali na aliadhiri Nia yako. Waliosoma makala moja wapo iliyotangulia hivi majuzi nilizungumzia habari ya Nia, makala iliyokuwa ya mwisho ya Namna ya kujinasua kwenye vifungo vya pepo mahaba, Sehmu ya 5. Na hapa wataniaelewa kiurahisi kuhusu Nia. Siku zijazo nitazungumizi athari za watu waliookoka kula vyakula vya Kufuru vya mifungo vya dini nyingine pamoja na vyakula vya kafara ama sherehe za kipepo.Tuendelee kwani niligusa kumnasua mtu hapo.

Katika kitabu hicho cha Mwanzo kunaandiko ambalo linadhibitisha jambo hili pia, Isaka aliishi katika nchi ambayo ilikuwa chini ya ufalume wa Abimeleki na ilifika mahali mahusiano yao yakaingiwa na mashaka, na mfalume na watu wake wakaitaji matengenezo ambayo yalipaswa kukaa kiagano, na katika hili hawakukubali kula hadi kwanza walipo patana. Maana yake chakula kilikuwa ni ishara ya kupatana kwao au la. Wakila tumepata, wasipokula hatuja patana.
Fungua nami sura ile ya 26. Nitakupa maandiko mengi kidogo ili kukuonyesha ninalotaka kukuonyesha hapo pamoja na udhibitish wa somo langu la jana ya kwamba kwenye Agano kunakiapo.
Pia kumbuka Agano ni mapato baina ya Pande mbili au zaidi. Tusome maandiko hayo: Mwanzo26:26 Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake.
27 Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu?
28 Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba Bwana alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe.
Mstari wa 28, umefungwa na maneno, Mapatano, kisha Tuapiane, kwa hiyo ni dhairi kwamba Maagano hubeba mambo hayo, Shika haya sana maana tunapokwenda ni muhimu mno.
Tusonge mbele na maandiko. Sasa mstari unaofwata ndio unaonyesha Agano hilo, 29 ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa Bwana. Baada ya makubaliano hao ndiposa wanakubali kula, Mstri uofwata; 30 Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa.
Tuone tena udhibitishwa wa chakula kama sehemu ya Agano kwenye Agano Jipya, Fahamu kwanza sababu zinazotufanya kushiriki meza ya Bwana! Na ni kwa nini yatupasa kula mkate na maji ya zabibu. Ukiyatafakari mambo hayo kiroho ni hakika hutakubali kushiriki meza ya Bwana kwa njia ya mazoea bali ukiona kile alichokimaanisha Yesu wakati angali hapa Duniani.

Tuanze na kitabu kile cha Yohana. Fungua sura ile ya 6 ili kuona mambo haya kiundani, ipo mistari mingi hapa inayozungumzia habari ya kula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake na maswala haya huwakilisha Agano, ila mimi nitachunguza nawe mistari michache na kwa muda wako tafuta kujua zaidi.
Yohana 6: 54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.
57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.
58 Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.
59 Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.

 Katika kila Neno Chakula na Damu ama Mwili wa Kristo wewe weka Agano, utafahamu ya kwamba chakula kinachonenwa hapa ni Agano Jipya na tutalidhibitisha hilo punde.
Hayo maandiko yanazungumzia jambo la ajabu sana ya kwamba aulaye mwili wa Yesu na kuinywa damu yake huwa na uzima wa milele. Sasa kwa upande wa maagano ya kipepo unaweza kupata picha ya kwamba aulaye mwili wa maagano ya kipepoo huwa na uharibifu kiasi gani.
Mstari wa 56, anasema mtu kama huyu hukaa ndani ya Yesu na Yeye Yesu hukaa ndani yake, na kwa upande wa Shetani ama maagano ya kipepo, ni dhairi kwamba aulaye mwili wa maagano hayo Setani hukaa ndani yake ama madhara ya Shetani hukaa ndani yake na yeye hukaa ndani ya Shetani.
Najua yamkini unasuasua katika kulinganisha chakula ama damu ya Yesu au Mwili wa Yesu na Agano, nilikuaidi kulidhibitisha au kuliweka bayana pasina shaka wala woga jambo hili mbele yako; nami ninalileta dhairi shairi bila mashairi mbele zako.

Kwa mwendo wa upole na utulivu kifikra fungua nami kitabu kile cha Luka 22, na hapo utamsikia Yesu mwenyewe akinena haya wala sio jirani yake ama mtu kwa niaba yake.
Luka 22: 19 Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
20 Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]

Umeona kitu hapo? Embu rejea tena kusoma mistari hiyo…. Kwa hiyo ni fika kwamba chakula ama damu huwakilisha Agano.
Ilinipasa kuchukuwa nguvu na muda wote huo kukujuza mambo hayo ili kukufikisha hapa. Na wakati huu kama mkao wakufunguliwa kutoka kwenye adha ama kadhia hiyo.
NAMNA WATU WANAVYOINGIA MAAGANO HAYA YA KIPEPO. …Kwa kweli ni kiu yangu kuendelea na ujumbe huu ila muda umeanza kunivuta shati toka muda mrefu uliopita nami kujikakamua ila nilipofikia sina uwezo wakuendelea kushindana nao tena, tafadhali tukutane kesho na ni ahadi yangu kuwa tutaendelea na sehemu hiyo na kisha kukufikisha kwenye kipengele cha namna ya kujinasua.

Kama hujaokoka na unataka kuokoka ama ulirudi nyuma kiroho na unataka kutengeneza na BWANA kwa upya leo, tafadhali fwatisha nami maneno haya kwa Imani, Sema: BWANA YESU, NINAKUPENDA, NINAKIRI NA KUAMINI MOYONI MWANGU KUWA WEWE NI MUNGU, ULIKUFA NA KUFUFUKA KWA AJILI YANGU, INGIA NDANI YANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU LEO, AMENI.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo.

Na Huduma ya UKOMBOZI GOSPLE, Arusha Tanzania, Kwa Maombi, Ushauri, Maswali au Sadaka wasiliana nasi, Barua pepe: ukombozigosple@gmail.com  Simu: +255 759 859 287 pia waweza itumia kwa M-PESA. Zaidi www.ukombozigospel.blogspot.com   #UkomboziGosple  #MwalimuOscarSamba
Pia #Like #Penda Page/Ukurasa wetu au kundi la Fb, ili kupata habari hizi kwa haraka, zaidi. Ug Ukombozi Gosple,                                                                                       PAGE: https://www.facebook.com/Ug-Ukombozi-Gosple                                              
Pia kwenye mtando Mpya wakitanzania wa

2 DAY SKY: https://www.2daysky.com/home

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni