Ijumaa, 28 Agosti 2020

YESU ANAKUPENDA!

 Na Mwalimu Oscar Samba

Sijui kama unajua kuwa Yesu anakupenda! Ni hatari kujaribu kusema kuwa mbona ninateseka, mbona maisha ni magumu, sasa inawezekanaje Yesu anipende wakati huu ni mwaka wa .. sijapona?

Ukweli ni kwamba Yesu anakupenda, na kuteseka kwako ni wewe tu bado hujatambua unachotakiwa kufanya ili kukubaliana na pendo hili! Unajua ndugu yangu acha nikwambie ukweli huu, nikuweke wazi katika viwango hivi vya uwazi! Mungu ili afanye kazi kwenye maisha yako ni lazima wewe umpe nafasi!

 

Mungu ni tofauti sana na Shetani, Shetani huweza kulazimisha, anaweza kutumia hila na mbinu batili ili kufanya jambo kwenye maisha yako, ila ili Mungu akusaidie wewe unapaswa kumruhusu!

 

Mfano, kuna mama mmoja alitokwa na damu kwa muda wa miaka 12; kwenye biblia tunajuzwa hili jambo, muda wote huo alikuwa akiwaendea waganga wa kienyeji na matatibu wa dunia hii! Ila siku alipoamua na kudhamiria moyoni mwake kwa kulishika pindo la vazi la Yesu hapo hapo alipokea uponyaji, wake!

Sasa jionee! Ni kwamba kupona kwake, kulitokea pale ambapo aliamua, alidhamiria kumuendea Yesu; Luka 8:43  Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote, 44  alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma.

 

Hapo pendo la Kristo linadhibitika ndani yake! Uponyaji unatokea, lakini sio kwamba Yesu alianza kumpenda alipomponya la! Upendo ulikwepo ila huyu mama alipoamua kukubaliana na pendo hilo ndipo alipopona!

 

Yesu alitupenda na alimpenda huyu mama hata kabla hajavaa mwili yaani hajaja humu ulimwenguni, na pendo hili linadhibitishwa na Uungu wote; Yohana 3:16  Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

 

Dhambi ilipoingia ulimwenguni pendo la namna hii ililijidhiirisha mara! Halikuanzia katika kuzaliwa kwa Yesu, bali hata Agano la mlima Sinai ni ishara ya hili pendo, Mungu alipochinja mnyama na kuwavika wakina Adamu nguo ilikuwa ni sehemu ya utendaji wa hili pendo! Mahali pengine kwenye biblia hujulikana kama neema, unapoona neema, uwe na hakika huwakilisha pendo la Kristo, tumeokolewa kwa neema tu, ama tumeitwa kwa neema tu, uwe na uhakika ni pendo lake!

 

Pendo hili haliwezi kujifunua kwako wakati ukiwa na shida unaenda kwa waganga wa kienyeji, ukiwa na mahitaji humulezi Yesu unawaeleza watu tu na kuishia hapo! Hutaki kwenda kanisani, maana huyu mama alimfuata Yesu kwenye kusanyiko, na penye kusanyiko maana yake ni penye uwepo wa Mungu, sasa kwenye ibada ndipo alipo Kristo!

 

Usiende kanisa ni kanisa, usiende kusanyiko ni kusanyiko, maana siku hizi watumishi wengi wa uongo wameibuka, tafuta kanisa la watu walio hai kiroho, mahali ambapo kiukweli hata akili na ufahamu wako wa kawaida unatambua hapo Mungu yupo, epuka mbwe mbwe za Shetani, na misisimko isiyo na Mungu ndani yake.

 

Yawe ni maombi yako na ni maombi yangu pia kuwa Mungu afunguwe macho yako ya ndani ili uweze kujua sehemu sahihi itakayokuwezesha kukutana na Yesu wa kweli, maana siku hizi kuna ma-yesu wengi wa uongo, hawamuhubiri Yesu mwenye kukemea dhambi, kwao dhambi ni sehemu ya ibada, hapo kimbia!

 

Ukiona huduma isiyokemea dhambi, hiyo imepotoka, ukiona huduma ambayo wazinzi na walevi wamo humo humo na ni watumishi, hapo kimbia wala usiage! Ukiona mtumishi anawataka washirika wake kimapenzi ujue huyo ni “ajenti” ama wakala wa kuzimu, na ukimkubalia atakuunganisha na kuzimu moja kwa moja, kwani mashariti yao moja wapo ya kuwaunganisha ni kulala na watu! Hususani wenye nyota ambazo zitawasaidia kuvuta watu makanisani! Epuka na kimbia hili!

 

Unajua kuna watu wanaenda kanisani ili kuirithisha nafsi yao kuwa nao wapo kanisani! Hii ni hatari sana, ni sawa na kunywa maji machafu ili tu uwe umekunywa maji! Ni sawa na kula mkapi au vyakula vibovu ili tu kukidhi hitajio la kula! Ukifikia hapo upo mahali pagumu sana!

 

Maana baada ya muda afya yako itakongoroka tu! Wengine huabudu kwa kufuata mkumbo! Yaani ni mtumishi yupi anawika sana mjini siku za leo, akipoa au akiona ushabiki umempungua basi hufikiri kuhama hapo! Akiibuka mwingine mjini, humfuata!

 

Watoto hata! Shetani huwa naye anahubiri, tena ni muhubiri mzuri tu! Ukipinga muendee Yesu kwenye Mathayo na Luka 4, utamuona Yesu akihubiriwa na Shetani pale, na maandiko anamsomea, kuwa akiwa ndie Mwana w aAdamu ageuze jiwe kuwa mkate, na alimuonyesha hata utajiri alionao akimpa na kanuni kuwa akimsujudia atampatia!

 

Sasa usitishike na injili za mafanikio, maana hawakuanza wao alianza Shetani, na kupata fedha au mafanikio kutoka kwao sio jambo la kigeni, maana hata Yesu angemsujudia hakika angepewa, maana ni muhimu kujua nao huwa wanamsujudia nani!

Kusoma maandiko na kuyafafanua siyo kipimo, kwani hata Shetani alimsomea Yesu, maana ni kweli yapo kwenye biblia! La muhimu na jambo zuri kuliko yote ni wewe kuhakikisha kuwa ndani yako unapata amani ya Kristo, maana wapo ambao Mungu anawakosesha amani na mtu husika ila kwa ushabiki huzidi kugandamana naye! Huku ni kupotea!

 

Injili ambazo jina la Yesu limewekwa kando, msisitizo wa maombezi sio katika jina la Yesu na Damu yake kwenye uhalisia, ama nguvu za Roho Mtakatifu, bali ni katika viambatanishi, au visaidizi, kama mafuta ambayo yamesingiziwa kuwa ya upako, na wengi hawataki kujua kama ni upako upi unaotajwa hapo, maji ya upako au maji ya baraka, wengine wanagawa hadi bangili za upako, pete za upako, nasikia siku hizi kuna keki za upako,  hii ni hatari sana!

 

Najua wana wa upotevuni ni wepesi sana kukinzana na ukweli huu, na wana hoja nyingi sana wakitumia maanadiko, ila mioyoni mwao wanaujua ukweli, maana sifa zipo kwenye mafuta na maji yakaniponya, Yesu amekuwa kama ni msaidizi!

 

Nisikilize, ukitaka kuliona pendo la Kristo likikusaidia maishani mwako ni muhimu sana kuhakisha kuwa unaambatana na Yesu kama alivyo, waepuke wanaokupa maji machafu, katika Yohana 7:38-39 Yesu anaita akiwataka wale wenye kiu waje au waende kwake ili awape maji!

 

Maji yake ni safi, alimwambia yule mama kwenye kisima cha Yakobo katika Yohana 4 kuwa kiyanywa hayo maji ya Yesu hataona kiu tena! Sasa wamekupa Yesu na bado kiu ya ulevi ipo, wamekupa Yesu na bado una kiu ya kuiba waume za watu! Ukimuona mume wa mtu mate yanakutoka kama fisi na mfupa! Wamekupa Yesu angali bado una kiu ya dogo-dogo, ukimuona kijana “handsame” ama binti mrembo, hata kama ni umri wa mwanao jicho linakutoka kama vile fundi simu aliyedondosha nati, maana nati zake ni ndogo kwa hiyo asipotoa macho hawezi kuziona kirahisi, huu akiwa na hofu usikute imepotea!

Unasema eti umeokoka, au unamependa na una Yesu, sawa sikataii! Lakini mbona hajaondoa kiu ya dhambi nadani yako! Bado ni mwizi, unazini kwa siri, nyumba ndogo kuacha umeshindwa! Hakika huna Yesu aliyehai una yesu marehemu! Wala usinikunjie ndita, ila ukweli ndio huo!

 

Anasema hivi; Yohana 4:13  Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena.

Yesu akiingia nadani yako, na kiu ya mambo ya dunia ispoondoka, uwe makini, rejea msalabani upya!

Neno la Mungu ni maji, sasa injili kama inahubiriwa haibadilishi maisha yako, kuna mambo mawili hapo makuu, wewe mwenyewe u na moyo mbovu, ama injili unayopewa ni maji machafu, ni maji yasiyo na uwezo wa kukausha kiu ya dhambi, na tamaa zake, swala la upinzani wa Shetani hili ni la maombi tu! Ila hatuwezi au maombi hayawezi kukusaidia sana kama wewe mwenyewe hujakaa eneo salama, maana pepo mchafu amtokapo mtu na akipata mwanya mwingine hurejea, maandiko husema mmekuwa safi kwa lile neno, neno hukuweka kuwa safi, na mapepo hayakai maeneo ambayo yamesafishwa kwa Damu ya Yesu!

Huwa nasema kuna yesu aliyekufa, na kuna Yesu aliye hai, unaposema nataka kumuona Yesu, nina haja na Yesu, uwe makini maana wakina Pilato wapo hapo kukupa yesu aliyekufa kama Yusufu wa arimathayo, huyu alipewa Yesu/yesu ila mfu, aliyempatia alihakikisha kuwa amekwisha kufa! Na aina hii ya Yesu hawezi kuleta mabadiliko kwenye maisha yako!

 

Unasema una Yesu lakini hatuoni badiliko la ndani; ndani yako, una sema una Yesu lakini hatuoni matokeo ya wewe kuhuishwa hata kidogo! Yesu aliye hai, hukushindia dhambi, huhuisha utu mpya na kuua ule utu wa kale, hawezi kuchangamana na dhambi! Ukiona unajiita una Yesu lakini hakuna badiliko la dhambi au la kiroho ndani yako uwe na hakika kuwa kuna shida ipo mahali, utakuwa wamekupa yesu aliyekufa siyo Yesu aliye hai kama Yule aliyefufuka siku ya tatu, maana kuna dini zina yesu sawa, ila ni yesu marehemu!  

Wanahubiri habari za Yesu, Lakini wao wenyewe ni wazinzi, ni walevi, hawawezi kusimama madhabahuni bila kunywa pombe kidogo, hawawezi kukaa bila kutongoza washirika! Ni mzee wa kanisa ila sigara anavutia chooni!

 

Ona hapa; Marko 15:44  Lakini Pilato akastaajabu, kwamba amekwisha kufa. Akamwita yule akida, akamwuliza kwamba amekufa kitambo. 45  Hata alipokwisha kupata hakika kwa yule akida, alimpa Yusufu yule maiti.

Kuna dini, zimehakikisha kuwa yesu waliye naye amekwisha kufa, ndio maana wamekupa wewe! Maji yao siyo yale halisi yenye uwezo wa kuondoa kiu ya dhambi, ndio maana wamekupa wewe!

 

Huwa ninaweka sana angalizo hili, kuwa unapokuwa na kiu ya kutaka kumjua Yesu, unapokuwa na kiu ya kutaka kukoka, unapaswa kuwa makini tena mno, maana ukisema nina kiu, moja kwa moja uwe na hakika kuwa wapo watu ambao hawaachi kukuletea maji, ambayo kwa kweli siyo sahihi, ndio maanaYesu kwenye ile Yohana akapaza sauti aksema kila mwene kiu na aje kwangu, aje anywe, hakusema na aje achote maji ila alisema na aje kwangu, kwa hiyo jifunze kumtafuta Yesu kwanza, na sio maji kwanza , kama wengi wafanyanvyo! (Maana ukiwa na Yesu, atakwambia haya maji uliyopewa siyo yangu.)

Najifunza sana kwa Yesu mwenyewe, alipokuwa pale msalabani na alipopatwa na kiu, alisema naona kiu, na badala ya kumletea maji walimletea siki! Uwe na hakika na wewe ukisema nina kiu, wapo na watu ambao nao watakuletea siki ama maji machafu!

 

Ukisema nataka kuokoka, ninamtaka Yesu watakwambia usiondoke kwenye dini yetu maana na huku pia watu wanaokoka, kuna vikundi huku nako vya uaomsho, uwe na hakika ni uamsho bandia, maana kuna na moto bandia, ambao hufananishwa na ule wa Roho Mtakatifu!

 

Namtaka Yesu, wanakuletea Yesu ambaye amekufa, hawezi kuondoa dhambi! Ndio maana adui ameweka utitiri wa madhehebu na makanisa mapya na watumishi wengi, ni ili kuwapoteza watu, maana ma-yesu wafu wamejaa sana humu duniani! Umakini unahitajika sana!

Asante kwa kunisikiliza (nafsini mwako), ama kunifuatilia kwa njia ya usomaji huu wa hii makala, nina amini kuwa kuna kitu umekipata hapa, Yesu anakupenda, ila kama hujakutana na pendo lake uwe na hakika kuna dosari ipo mahali, chukua hatua mapema mnoo!

Pia anasema kwamba mtu akimpenda atazishia amri zake, kwa hiyo kama kweli umedhamiria, mpende kwa kuzishika amri zake, epuka michanganyo, epuka kuuzoelea wokovu, asante na Mungu akubariki mno; Yohana 14:23  Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. 24 Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka.

Hongera kwa kusoma ujumbe huu, nakutia moyo kuzidi kumtazama Mungu, na pia uwenda hujaokoka, yaani Yesu sio Bwana na mwokozi wa maisha yako! Nakutia moyo tena kuokoka sasa! Yamkini ni uchumi, fedha, hazipatikani, unazingirwa na nuksi na mikosi, kila unalofanya haliendi, unakabwa na mapepo, ! Wewe njoo kwa Yesu na hayo yote yatapita kabisa ! Sasa natumi u tayari!

Sema; MUNGU BABA, NINAKUPENDA, ASANTE KWA KUNIPENDA KWANZA, LEO NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NA NIPO TAYARI KUOKOOKA, TAFADHALI INGIA NDANI YANGU, SAMEHE DHAMBI ZANGU, NA FUTA JINA LANGU KATIKA KITABU CHA HUKU, NA ULIANDIKE SASA KATIKA KITABU CHA UZIMA WA MILELE, Ameni.

 

Kwa kufanya hiyo umekwisha kuokoka sasa, na tafadhali tafuta kanisa la watu waliokoka lililopo karibu nawe ukasali, hapo, waambie kuwa umeokoa hivi karibuni, ili wakulee vyema kiroho.

Mawasiliano yetu, kwa M-Pesa au Simu: +255 759 859 287, barua pepe: ukombozigospel@gmail.com

pia temnbelea: www.ukombozigospel.blogspot.com .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni