Ijumaa, 5 Juni 2026

MTAZAMO WA MUNGU/KIBIBLIA DHIDI YA ADUI AU WATESI WAKO.

Na Mwl Oscar Samba Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu cha KWA NINI MUNGU ANATUTAKA TUSIJILIPIZIE KISASI? Nia kuu ya mada au kipengele hiki ni kukuwezesha ama kukujengea aina sahihi ya fikra dhidi ya aina ya watu wanaokutesa kutoka katika kona ya mbingu. Kwa nini? Itakusaidia kutokupambambana nao, kutokuwawekea kisasi wewe na kumuachia Mungu; lakini pia hutateseka kwa nini Mungu bado anawapenda (angali kwako ni mwiba). Ama kwa nini Mungu anakawia kuwaadhibu. Sababu za kukawia kwake zitakuwa wazi mbele ya fikra zako. Na hata sababu za Yeye kuwaruhusu kukutesa. Nakumbuka mie mwenyewe binafsi nilikuwa sijalielewa sana hili andiko la Yesu, lakini ipo siku nilikuja kulifahamu. Kuna jambo nililipitia kutoka kwa mkuu wangu la kuzuiliwa kuhudumu (kwa miezi kadhaa); na siku hiyo kuna namna nilipaswa kuchangia katika muda fulani kanisani: kumbe tayari barua ya kufurumushwa kazini ilishaandikwa: sikupata hiyo nafasi kabisa. Nikiwa nimekaa pale kwenye eneo letu maalumu: ndipo Roho Mtakatifu akanisemesha haya maneno. Ni andiko la Yesu dhidi ya mtu aliyepaswa kuitumia mamlaka yake kipindi cha kuteswa kwake. Lilinipanua kufikiri sana andiko hili; Yohana 19:10 Basi Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha? Yohana 19:11 Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi. Nikajifunza kuyaona mapenzi ya Mungu katika ukatili ule. Ama nikajifunza kuuona mkono wa Bwana dhidi yangu au ukiwa upande wangu katika kipindi cha mateso ama moto ule. Kwa kifupi nilipata fikra pana zaidi kuanzia pale. Na ndipo nilipoelewa alipokuwa anapitia Yesu, na kitu ambacho Yesu alikuwa akikimaanisha. (Maandiko yanaposema mamlaka hutoka kwa Mungu, haina maana ya moja kwa moja kwa kila aliyeteuliwa au kuchaguliwa hutokakwa Mungu. Bali maana yake kubwa ni kwamba Mungu ndiye mwanzilishi wa mfumo wa uongozi na utawala. Swala la kiongozi kutoka wapi, na anamtumikia nani ni jambo jingine). Na Mungu huweza aidha kukuondoa katika mamlaka zao, au kuiondoa/kumuondoa mtumiaji wa mamlakanasiyeitumia kwa haki. Ile amekuacha hapo bado, endelea kumshukuru; maana pia angeweza kuhakikisha huo mfumo unapokea mtu ambaye angeendana na kusudi hilo japo maombi hayo ni muhimu sana kwa kanisa siku za leo: Asante. 1. Biblia Husema Yesu Aliteswa na Mungu. Kati ya jambo la ajabu na lenye maajabu yake lililowahi kunishangaza ni hili; eti maandiko hukiri wazi ya kwamba Yesu hakuteswa na waliomsulubisha! Hakika ilinishangaza sana hii. Tunafahamu waliopanga njama za kumkamata na kisha askari waliotumwa walitoka upande gani, waliomsulubisha na kupiga kelele asulubiwe, asukubiwe. Lakini katika mateso hatimaye kifo cha msalaba mbingu zinajinadi hizo ndizo zilizohusika na sio Wayahudi kadhaa na Shetani nyuma yao! Tazama; Isaya 53:4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Kwa wasomaji wa hicho kifungu wanafahamu kinazungumza habari za mateso ya Yesu Kristo. Maandiko yako wazi hapo kabisa ya kwamba ni Mungu. Sasa basi, kama mbingu zinajitwika tukio la wewe kuteswa, uwe na hakika hazina haraka kukuondoa kwenye mateso. Kama zinasema huo moto ni wangu; usijaribu kwenda kuita zima moto waje, (jeshi la zima moto na uokoaji). Maana watagoma na kusema tunaona mkuu wetu ndiye anayesimamia tukio la nyumba yako kuungua moto. Wanaishilia kukupa ile Isaya 43 ya kwamba maji mengi hayatakugarakiisha wala mwali wa moto hautakuunguza. Watakwambia ni moto kweli, ila hautakuteketeza; maana hata tofali la kuchoma lazima lipitie moto ili liimarishwe. Sasa yamkini unajiuliza ni kwa nini mbingu zinakuwa na lugha ya namna hii? Mosi ni kwamba, ndizo zilizoruhusu tukio hilo. Mungu asingeruhusu lisingekujilia. Kivipi? Nami nakuuliza kama unajua maana ya andiko hili? Soma;1 Wakorintho 10:13 Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. (Ukiwa katika jaribu zito; hilo neno Mungu ni Mwaminifu unaweza lisoma mara mbili mbili....) #IngawaNiKweliNiMwaminifu Nataka ujikite katika A, jaribu lililo ndani ya uwezo wako, B; kujaribiwa kwa kiasi au kipimo utakachoweza kustaimili na kisha C, Mungu ndiye mfanyaji wa huo mlanago au mratiibu wa namna ya wewe kutoka. (Nakupa "Home Work" ya kutafiti kwa nini neno uwezo na kiasi vimetumika pamoja, tafuta sababu...ukiweza nenda hadi katika lugha ya asili, pia soma tafsiri mbalimbali za Biblia.) Tuendelee: Hapo sasa, unijubu...je, huyu anayeweza kupima kiwango cha moto unaoweza kuivisha vizuri tofali anashindwa kuuzima huo moto? Uliwahi kupika chapati au wali katika jiko la gesi au umeme? Si kuna kiwango cha moto huwa unapima? Je, unayeweza kufanya hivyo unashindwa kuuzima huo moto kweli? Jibu ni kwamba Mungu angeweza kuzuia jaribu hilo. Anayeweza kufanya mlango au kuratibu namna ya wewe kutoka katika pito hilo unathani angeshindwa kukuzuilia usiingie katika hilo jaribu? Yaani aweze kuwa na mipango ya kukutoa, alafu akose mipango ya kukuzuilia usiingie! Laiti kama ungejua ni majaribu mangapi yanaandaliwa kwa ajili yako lakini BWANA Mungu huwa anayazuilia! Maana anajua hayana utukufu kwake, ama huyawezi au muda wake bado. Pili, Hataki Utukufu Umuendee Shetani ama Washirika Wake. Kati ya kitu muhimu katika Biblia ni kuhakikisha utukufu wote ni wa Mungu. Mbingu haziwezi kushiriki utukufu na Shetani hata siku moja. Kwa hiyo, hauwezi zisikia zikimsifia Shetani kwa kumpiga Yesu. Au kwa kukupitisha wewe, badala yake zitautaja mkono wa Bwana. Naye Shetani huwa mkimya maana anajua kama sio Bwana usingaliweza kutoka katika mikono yake salama. 2. Kinachokufanya Wakutese ni Kusudi Ulilobeba. Hii nayo ni ajabu nyingine. Ndio maana mtazamo wa mbingu ni tofauti kabisa na wawalio wengi inapofika eneo la namna hii. Mungu hawatazami sana watesi wako, badala yake hujikita katika kulitazama kusudi ulilobeba. Na anachokiona ni wewe kupitishwa kwa ajili ya aidha kuandaliwa kuwa mtu sahihi katika kuweza kuubeba huo mpango wa Mungu; ama kupitia huko kuna mchango gani katika kukamilishwa kwa kusudi. Yesu aliteswa kwa ajili ya kuzalisha ukombozi wa wanadamu. Kupigwa kwake kulifanya damu kuvuja. Damu ilipomwagika ndipo kusudio lilipotimia. (Umejionea hiyo siri hapo?) Ndio maana maandiko hayakumuona Shetani wala kikundi kile cha Wayahudi wakorofi kilichomkamata na kumsulubisha. Bali kiliona kusudi la ukombozi ndani ya yale mateso. Na kwako, mbingu haziwaoni watesi wako, bali zinaliona lile kusudi lilokufanya kupita hapo. Soma Tena Andiko Hili Katika Sura Hii na Mtazamo Huu; Isaya 53:5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. 6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. (Ukiijua siri hii, kuna aina tofauti sana za fikra zitakufunika...utajifunza kulinda heshima ya mbingu pamoja na kusudio linalokupitisha hapo. Heshima ya mbingu kwa maana kwamba, kuna namna utamzuilia Shetani kupata utukufu. Kuvuka kwako kutakuwa kipaumbele kikubwa ili mbingu zipate heshima yake. Kisasi hakiwezi kuwa sehemu ya kipaumbele chako hata kidogo. Na badala yake utakiacha kwa Bwana Yesu Kristo mwenyewe...Amina) NB: Katika kuunganisha pointi iliyopita na hii, mistari hii ijayo, inatuambia mambo muhimu sana. Anasema Bwana aliridhia...umeliona hilo neno hapo? Ni kwamba mbingu zilikubali...kukubali ni ni? Yaani kuteswa kwa Yesu hakukuwa kwa bahati mbaya...kuna kikao kilikaa na kupitisha ajenda hiyo. Kama una Biblia yako hapo tafadhali pigia mstari hayo maneno Bwana aliridhia. Na mstari huo upige moyoni mwako ya kwamba Bwana ameridhia pia wewe kupita hapo unapopita... Tazama; Isaya 53:10 Lakini BWANA aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake; 11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. (Swala la ukombozi lilikuwa na thamani kuliko mateso ya msalaba kwa Yesu. Na kwako ndivyo ilivyo...ya kwamba kesho ya utumishi wako ina thamani kubwa kuliko leo unayoitesekea....niamini mimi...kama tu kitabu hiki kinakusaidia...uwe na hakika nisingepita utukufu huo usingalikuwa juu yako.) Kumbuka tena...Mungu aliridhia....Kati ya kitu Shetani angetamani usione, ni wewe kumuona Mungu katika kupitishwa kwako. Huwa anatamani umuone yeye Shetani katika pito hilo ili azidi kujitutumua zaidi.....ila fahamu Mbingu Zimeridhia kupita kwako hapo....na ni jambo la muda kitambo tu. 3. Wanaokutesa Hawakutesi Wewe, ni Wanamtesa Yesu Mwenyewe. Kati ya maajabu niliyoyagundua katika Biblia kipindi cha somo hili; basi pointi hii nayo ilinishangaza mno. Yesu anamwambia Paulo Mtume mbona unaniudhi...Biblia ya Kingereza ikatumia neno mbona unanitesa...Paulo akauliza u nani wewe Bwana...Yesu akamwambia ni mimi Yesu unayenitesa...! Maajabu na kweli, tukitazama tunamuona Paulo akilitesa kanisa, akiwatesa watakatifu wa Yerusalemu na hata hapo alikuwa akiwafuata walipotawanyikia...lakini Yesu haoni hivyo. Anamuona Paulo aliyekuwa Sauli akimtesa...kumbe wanapokufanyia mabaya hawakufanyii wewe, bali humfanyia Mungu mwenyewe aliye mbinguni! Hii ni ajabu kabisa, kabisa. Tazama; Matendo ya Mitume 9:4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? And he fell to the earth, and heard a voice saying unto him, Saul, Saul, why persecutest thou me? In simple terms we cana say, why do you perscute me? Kwa nini unanitesa...Kwa kiswahili neno linalotumika ni kuniudhi...kingereza ni kunitesa. Matendo ya Mitume 9:5 Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Umeuona huo mtazamao? Ndiposa kisasi unapaswa kukiruhusu kuwa cha Bwana, maana mateso hayo ni ya Bwana na sio yako wewe hapo. Mwewe anaponyemelea banda la vifaranga, pigo hilo ni lako wewe, ingawaje kinachowindwa ni kifaranga; na ingawaje kifaranga na mama yake na kuku wengine utawasikia wakipiga kelele. Fisi anapowinda kondoo au mbuzi wako, pigo hilo ni lako wewe; ingawaje anayekuwa hatarini ni huyo mfugo wako. Na ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu, alivyo dhidi ya pigo au teso lolote juu y tu. (Kumbuka tusingekuwa wake, tusingeteswa...kwa hiyo tunateswa kwa ajili yake na kwa sababu sisi ni wake Yeye.) Soma Hapa; Luka 10:16 Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma. Unaniambia Mwalimu Oscar lakini adui hawa wamenitenda moja mbili tatu..! Ni kweli, maana hata Sauli alilitawanya kanisa kule Yerusalemu, aliwaua wateule wengi na kuwatesa kabisa kabisa....na hata Stefano alikufa mikoni mwake...lakini kwa kazi hiyo injili ilienea zaidi.(Vua mtazamo wako na utazame kimbingu zaidi...) 4. Anayepigana na Kusudi la Mungu Ndani Yako, Ni Anajaribu Kuupiga Mwiba au Kitu Chenye Ncha Kali Mateke. Yesu anamwambia Paulo (Sauli) neno gumu kabisa, ya kwamba hawezi kufanikiwa kuendelea kulitesa kanisa. Na anachokifanya ni anajiumiza yeye mwenyewe. Anamwambia ni sawa na kujaribu kuupiga mchokoo teke. Wengine husema ni mti wenye miiba mikali sana, ukija katika lugha kadhaa utaambiwa pia ni kitu chenye ncha kali kama sindano, na kwa wengine ni kifaa cha kulimia au kuchimbua aridhini ambacho hukokotwa aidha na wanyama au gari maalumu ambacho huwa na ncha kali sana....sasa ndicho ambacho Sauli anajaribu kukipiga mateke. Kikawaida kabisa ni nani anayeweza kupiga mateke au kupigana na mti wenye miiba? Haiwezekani hata kidogo, kabisa kabisa. Mungu ndivyo anavyowaona adui zako. Ndio maana kila mara wanakuchukia tu! Hata wakikutesa mara baada ya hapo unafikiria wataridhika kumbe badala yake chuki ndo inazidi kuendelea...! Ni kwa nini? Kwa sababu walipokupiga, kuna kitu kimewachoma...walipokurushia teke wamekutana na mchokoo ukawadunga...sasa maumivu yake yanawapa hasira....(Ni ukweli nakueleza...hili ndilo jibu lake.) Tazama; Matendo ya Mitume 26:14 Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. 15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. 5. Wapende Adui Zako, Waombee na Uwatendee Yaliyo Mema. Biblia inatutaka kuwapenda adui na wale wanaotutesa au kutuudhi. Hili nalo ni jambo la kushangaza katika hali ya kawaida. Lakini ndivyo ilivyo na inavyopaswa kuwa. Mosi kisaikolojia itakusaidia kuepukana na makosa ya hasira na hamaki. Mtu anapokuwa mtesi, kuna hatari ya kukufanya kukosea. Majibizano ya maneno, kinyongo na hata kujikuta umeingia mwilini na kupigana au kutumia upanga kama Petro wakati wa kukamatwa kwa YESU. Lakini Biblia pia inatoa sababu zake muhimu...kwanza tulione andiko na kisha sababu zake.. Andiko; Mathayo 5:44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, Anaendelea n kutoa Sababu; 45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. A. Tupate kuwa wana wa Mungu wetu aliye mbinguni. Kwa hiyo, ukiwatendea hivyo adui zako, ni unakuwa mtoto wa Mungu. Kwa maana kwamba, kama ukitenda kinyume chake kwa kuwachukia, kuwawekea kinyongo na hata kunilipizia kisasi ni unakuwa mtoto wa nani vile...? Ni mtoto wa Shetani aliye wapi...? Aliye kuzimu...na ukiwa mtoto wa huyo jamaa uwe na hakika utatenda yampendezayo huyo baba yako wa kambo..ambapo ni husuda, chuki, kulipiza kisasi na kadhalika... B. Anatuambia ili Tuweze Kumfanania Mungu Kitabia...anasema ya kwamba Yeye huwanyeshea mvua wema na wabaya...jua lake huwaangazia watu wote. Sijui kama unajua maana yake hii? Kuna viongozi ambao huwapandisha vyeo watu ambao wanawataka wao, watu ambao ni marafiki zao...ila wale ambao huwapinga na kuwakosoa hawawezi kupata kibali kwao hata kidogo. Wale wanao wasifia hata katika makosa yao, hao ndio ambao zikija nafasi za marupurupu hutumwa...kazi za sulubu hupewa wale ambao hunyoosha sentensi, ambao nyeupe ni nyeupe na nyeusi ni nyeusi huwa katika kundi la kifo...kundi la mateso na upinzani mkali...kundi la sulubu. Ila Yesu kwake sivyo, watu wote ni sawa. Hata ambao ni watenda dhambi...ndio maana tunapaswa kuwa na mtazamo sahihi sio dhidi ya adui zetu tu, bali hata maasimu wetu. Hili ni swala muhimu sana kulifahamu. Tabia ya namna hii ingekwepo kwa viongozi wetu wa kisiasa leo, makanisani, makazini na kadhalika; kuna aiana ya mateso ambayo watu hupitia wasingeyapitia kabisa, kabisa. C. Ni ili tuweze kujipatia thawabu. Tuzo au kutuzwa na Mungu. Kuna aina ya neema au baraka kutoka kwa Bwana inakuwa juu yetu. Kwa maana kwamba kama hutendi hivyo, kuna aiana fulani ya hii neema utaikosa. Soma;Mathayo 5:46 Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? D. Sehemu B ya hilo andiko hutujuza kuwa ni ili Tusifanane na Watu Wasio Mjua Mungu. Yakwamba wapagani hutenda kama hayo. Sasa nasi tunapaswa kufanana na kundi la Mungu. Hii nayo ni siri muhimu sana katika kanisa la leo. Na kiukweli ni kwamba viongozi wengi wa kiroho wamekuwa na kasumba za namna hii. Kanisa lina hali mbaya sana... Mathayo 5:47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? F. Inatupatia Ukamilifu wa Kiungu. Sijui kama unaelewa fundisho la ukamilifu wa Kristo? (The Doctrine of Perfecion in Jesus Christ or Doctine of Christ Likeness). Waefeso ile 4 ndiyo inayotupatia mtaji wa namna hii muhimu. Ya kwamba tukue katika kimo na cheo cha kumfahamu Yesu Kristo, ili tuweze kumfikia Yeye. Kila mkristo kipimo chake muhimu ni kumfikia Kristo Yesu. Hapo ndipo tunapotaka kufika. Sasa maandiko hutuambia ya kwamba, kama tukimjua Yesu kwa "staili" ya namna hii katika kuchukuliana na adui zetu, basi tutafanikiwa kukua kiroho. Kumbe maisha ya kinyongo, kisasi na hata husuda ni matokeo ya uchanga kiroho! Hii ni siri kubwa sana ambayo huachi kuijua. Tazama Andiko; Mathayo 5:48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. 6. Ni Mtumishi Wake Mteule. Wakati wewe unamuona ni mtesi, (kweli ni adui sikatai) muda huo, huo mbingu zinatazama kilichomo ndani yake. Wanadamu tuna tabia ya kutazama sana madhaifu ya watu, mapungufu na hayo maudhi kutoka kwa mtu hufanyika zuio kwetu. Tunamuweka mtu katika kundi la kukataliwa moja kwa moja. Lakini Mungu hutazama mambo yote mawili. Sura zote mbili ni muhimu sana kwa Mungu. Na hiki ndicho kinachomfanya kuwavumilia watu, na kuzidi kuwavuta na neema yake iokoayo. Kuna watumishi wa Mungu hivi leo, lakini hapo awali walikuwa wauaji, watesaji,.majambazi na wengine ni wachawi ama waganga walioua na kutesa watu wengi sana. Sasa unaonaje katika nyakati kama hizo kama Mungu angewafutilia mbali! Yamkini hata wewe kabla ya neema uliwahi kuwa mtu wa hivyo. Na inawezekana hata baada ya neema kuna maisha ya kikatili uliwahi kuishi; ulikuwa mtu wa ovyo kabisa. Aidha kwa mkeo, mumeo, watoto, ndugu, mshirika, mpendwa; na yamkini ni mfanyakazi wako na kadhalika. Lakini leo Bwana amekubadilisha, nikuombe kuwapa muda wa kubadilika na hao watesi wako. (Swala la kutokubadilika liweke kwa Mungu; ndio maana tukaimizwa sana ya kwamba kisasi kisiwe juu yetu...maana Yeye ndiye ajuaye ya kwamba huyu ni sikio la kufa ama huyu ni wa kupona.) Sauli aliyekuja kuitwa Paulo alikuwa mtu wa ovyo na hatari sana kwa kanisa la Mungu kwa wakati ule. Lakini neema ya Bwana iokoayo haikuwahi kumkatia tamaa. Mungu alimbadilisha na hatimaye kuwa mtu anayefaa. Unaposoma Warumi, Wagalatia, Wakolosai na Wathesaloni...jaribu kujiuliza kama tungalimosa mtu huyu! Kuna adui ukonao leo, lakini ndani yao kuna nyaraka muhimu kwa kanisa; Waefeso, Barua kwa Filomoni, Timotheo na hata Tito vimo ndani yao. Unapojaribu kumlipizia kisasi uwe na hakika ni unapigana na Bwana mwenyewe, maana kwa Mungu mtu huyo ni chombo kiteule chake. Na unapojaribu kumpinga, na kumfanyia fitina mbingu zinakuona na wewe ni sehemu ya adui wa mapenzi makamilifu ya Mungu. (Kumbuka jicho la Kiungu linatofauti sana na letu. Sisi hutazama mtu wa leo, mbingu zinamjua huyo mtu miaka kadhaa ijayo ni nani?) Nikwambie ukweli kwenye madanguro kuna wahubiri wengi wakubwa! Je, madanguro yote ya chomwe moto! Katikati ya wachawi walioua watoto wako kuna watumishi muhimu sana humo! Je, wachawi wote wafe leo, leo? Jibu ni la! Na utaelewa sasa ni kwa nini mbingu sii nyepesi kujibu maombi unayomuomba Mungu usiku na mchana ya kuwa huyo adui yako anapaswa kufa. Kwa sababu jicho la Kiungu lipo tofauti sana, sana. Anania alimtazama Paulo kama muuaji na mtesi wa kanisa (ni kweli kabisa) lakini Mungu wakati huu alimtazama kama chombo chake kiteule. Mungu alishampa mashitaka yake ya kwamba mbona unaniudhi Sauli! Na wakamalizana hapo, hapo. Anania anajaribu kumtaja Sauli muuaji, Mungu anamuona Sauli muhubiri wa injili. Hiki kwa Mungu ni cha thamani kubwa sana...maandiko husema ya kwamba hatamani watu waangamie, ila wote waifikiliye toba kwanza...nalicha ya kuifikilia toba, bali hutamani tena ya kwamba kile kilichowekezwa ndani yao kitumike kuujenga ufalme wa mbinguni. Huyo adui yako, yamkini ni chombo kiteule cha Bwana...(Sikuzuilia kuendelea kumsihi Mungu kuhusu watesi wako, la hasha! Silo lengo langu...ila nanjia kukupa taadhari na kukupanua uelewa wako kuhusu mtu huyo na kukutaka kuona yamkini kama Mungu anavyomuona...ili kukuzuilia kutoka katika masumbufu ya kwamba mbona adui wanachanua angali ni adui wako na mbingu...) Soma kisa hili; Matendo ya Mitume 9:13 Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; 14 hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. 15 Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. 7.