Jumapili, 28 Mei 2017

MAJIRA YA FARAO ASIYEMJUA YUSUFU.

Na Mwalimu Oscar Samba #Ug Ministry
Yapo majira ya Kuingia, kuishi na hatimaye kutoka Misiri huku ukiyakabili majira mapya ya Jangwani ama nyika isiyopandwa kitu kwani haina umande, pia yapo majira ya kuingia ama kuishi Kanani.

Na majira hayo yote yamegawanyika katika majira kadhaa, na leo ninakujuza kuhusu Majira ya Farao Asiyemjua Yusufu. Ni kweli wana wa Iziraeli waliingia Misiri na Mungu alihaidi kuwabariki ama kuwazidisha huko kupitia ahadi ya Ibrahimu; Mwanzo 15:13. Andiko hilo pia lilitaja muda wa kuishi huko ikiwa ni miaka 400.

Na kipindi cha Mzee Yakobo jambo hili lilitimia pale Mungu alipomtaka kushuka huko Misiri na ajenda iliyowasukuma ilikuwa ni njaa; Mwanzo 46. Baada ya hapo maisha yalikuwa mazuri mno kwani Kijana wake Yusufu alipata kibali na kibali hicho kikawa juu ya Iziraeli yote.

Lakini ili ahadi ya Mungu ya kuwatoa Misiri itimiye ni lazima wapitiye Jangwani, na maisha ya jangwa ni magumu mno, na Mungu alilazimika kuhakikisha ya kwamba anatengeneza mazingira yakuwafanya wayaone walau maisha ya jangwani ni bora kuliko ya utumwani. Kwani lazima wapitiye shule iitwayo jangwa ili kuweza kuishi vyema katika jiji la raha liitwalo Kanani.

Ndiposa Mungu akaruhusu majira mazuri mno kiroho ila magumu sana kimwili ya itwayo; “MAJIRA YA FARAO ASIYEMJUA YUSUFU.” Kwani Mungu alitazama jinsi walivyoyafuraia yale maisha ya masufuria ya nyama na matango na matikiti ukizingatia walikimbia njaa kule Kanani.

Tuyadodose hayo majira kwa mapana zaidi: Kutoka 1:8 Basi akainuka mfalume mpya kutawala Misiri, asiyemjua Yusufu.
Huyu ndiye Huyo Farao, Tutizame atakayotenda.
9 Akawaambia watu wake, “Angalieni watu wa wana wa Iziraeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. 10 Haya! na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, kukitokea vita wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii.” 11 Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji yakuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi.
 Mstari wa kumi na mbili unadhibitisha faida yangu moja wapo ya majira haya kwani unasema ya kwamba; “Lakini kwa kadri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Iziraeli.”  Na wewe kadri wanavyokutesa ndivyo unavyozidi kuongezeka kiroho na upako unajaa huku mafuta ya Mungu yakikutiririkia mara dufu huku ukaribu wako na Mungu ukipanuka kila Uchwao.

Natumai umeanza kujionea kuhusu ugumu au majira haya, ila sio huo tuu bali tujionee zaidi.
13 Wamisiri wakawatumikisha wana wa Iziraeli kwa ukali; 14 wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa  kazi ngumu; kazi za chokaa na matofali, na kila namna ya kazi za mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.
Mateso hayakuishia hapo bali yalizidishwa makali kama ule moto wa mfalume Nebkadreza kwa wakina Azaria ulivyochochewa mara 7 zaidi, tumulike mstari wa 15.
15 Kisha mfalume wa Misiri akasema na wazalishaji wa waebrania, … 16 akasema, “Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamuke basi na aishi.”

Hakika hayakuwa majira mepesi kwao lakini Mungu aliyaachia kwa makusudi na hili ndilo kusudi lake: Alitaka kuwatengenezea msuli wa kuweza kuimili mikikimiki ya jangwani, pili alilenga kuwafanya watambuwe kuwa hiyo sio nchi yao kwani hatuwaoni mahali wakiwa na kiu yakurejea kama ilivyokuwa kwa Yusufu ambaye alitamani kurejea kiasi chakuwataka kutokuacha hata mifupa yake huko.

Tatu, alilenga kutengeneza hoja itakayowafanya wana wa Iziraeli kuishikilia na kuisimamia ili kuwa na umoja wakutoka katika nchi hiyo na itamfanya Farao na taifa lake kutamani ama kutaka kuwaachiilia huku ikikumbwa kwamba wamisiri walishaonyesha chuki juu yao. Na fahamu kuwa mtu unayempenda kumuachuilia ni ngumu hata kama ni hatari kwako ila ukisha mchukia waweza muachilia ingawaje bado unamuitaji.
Nne, alitafuta namna yakuwatoa ambayo itamfanya akumbuke Agano lake na awatowe kiagano maana aliwapeleka kiagano.

Katika njia hii Mungu alifanikiwa mno, Wana wa Iziraeli walilia kwa sauti iliyo kuu katika majira haya, na kumlilia Mungu. Maombi yaliyomfanya Mungu kutokutulia na hatimaye kumtuma Musa huku akilikumbuka Agano. Kwa moyo mkunjufu ninakufunulia maandiko hayo.

Kutoka 6:2-8, 4 Tena nimelidhibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanani, nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. 5 Na zaidi ya hayo nimesikia kuugua kwao wana wa Iziraeli, ambao wa misiri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu.

Musa anatumwa kwa ajili ya ukombozi, Na fahamu anatumwa katika majira ya FARAO ASIYEMJUA YUSUFU, kwa hiyo Mpendwa mwenzangu yamkini unapita katika mazingira magumu sana kimaisha na hali hiyo inakupa kusononeka sana ila fahamu ya kwamba hayo ni majira ya Frao asiyemjua Yusufu na Mungu amesikia kilio chako ndiposa mimi nikatumwa kama Musa ili kukutangazia ukombozi wako hivi leo.

Yamkini hapo awali ulikuwa na kibali sana kwa Mchungaji wako, Shemasi ama kiongozi fulani kanisani na uwenda ikawa ni kwenye kwaya ila hivi sasa kimetoweka. Ulipendwa na kukubalika mno kazini ila kwa sasa ni kama umepoteza mvuto.

Mume ama mke alikupenda na kukudhamini, wazazi na hata wakwe walikuona ni mwenye dhamani ila muda huu wamekunyanyapaa.

Nisikilize, hayo ni majira mapya kwako kwani ilikuwa hivyo hata kwa wana wa Waebrania kwani kiti ama cheo au nafasi ile ile ya Farao iliyompa kibali ama kumpongeza Yusufu kipindi kile ndiyo iliyokuja kugeuka na kuwa adui ama sehemu ya utumwa kwa wanae na nduguze.
Tazama Farao aliyemjua namna alivyomkubali na kumpa Heshima hii sanjari na sifa kemukemu ama kedekede;
Mwanzo 41:38 Farao akawaambia watumwa wake, “Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?” 41 Farao akamwambia Yusufu, “Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misiri.” 42 Farao akavua pete yake ya mhuri mkononi mwake, akaitiya mikononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani kizuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.

Yamkini na wewe hapo awali walikuona hivyo, kwani walisema; “Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake” Ila kibao kwa sasa kimegeuka na kuwa hivi:
Haya! na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka” ama “Wamisiri wakawatumikisha wana wa Iziraeli kwa ukali.” Walikuona mtumishi mzuri tena mwenye heshima, muimbaji bora, kijana mcha Mungu. Walikushirikisha kila jambo kipindi cha majira ya Farao aliyekujua ila majira yamebadilika.

Wewe mtazame Yesu kwani kubadilika kwa majira hayo ni kwa ajili ya kukutoa katika nchi ya utumwa, na ninakuhakikishia ya kwamba muda wa ukombozi wako umekaribia. Wewe mliliye Mungu na punde mambo yako yatakaa sawa kwani ninakwambia hili kama Musa aliyekwisha kukutana na Mungu  pale kijiti kilipokuwa kikiwaka moto na ujumbe wangu ni huu.
“Kwa sasa lia mbele za Mungu ili alikumbuke agano lake ulilofunga na Ibrahimu kwani wewe ni sehemu ya hilo agano tangu pale ulipoamua kuokoka. (Mwanzo 15:16 Siku ile Bwana akafanya agano na Abrahamu, akasema, “Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misiri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati.”)
Pili hakikisha haupambani na huyo Farao bali wewe muachiliye kwa Bwana naye atashuhulika naye kwa maana yapo mapigo kumi kwa ajili yake na wewe bahari ya Shamu itafunguka kwa ajili yako.”

Hongera kwa kuwa pamoja na mimi na ni yangu imani ya kwamba wakati wako wakutoka hapo utumwani umefika na hautatoka kwa kutoroka bali mpaka umempata Musa wako maana ukifika Masa yeye ndiye atakayeupiga mwamba wa Horebu ili ukupatiye maji na pale Shamu fimbo yake ndiyo itakayo ugawa mwamba. Ukimpata Musa basi na Yoshua unaye maana ndiye atakayekurithisa Kanani yako.

Kama hujaokoka na unataka kuokoka ama ulirudi nyuma kiroho na unataka kutengeneza na BWANA kwa upya leo, tafadhali fwatisha nami maneno haya kwa Imani, Sema: BWANA YESU, NINAKUPENDA, NINAKIRI NA KUAMINI MOYONI MWANGU KUWA WEWE NI MUNGU, ULIKUFA NA KUFUFUKA KWA AJILI YANGU, INGIA NDANI YANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU LEO, AMENI.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo.

Na Huduma ya UKOMBOZI GOSPLE, Arusha Tanzania, Kwa Maombi, Ushauri, Maswali au Sadaka wasiliana nasi, Barua pepe: ukombozigosple@gmail.com  Simu: +255 759 859 287 pia waweza itumia kwa M-PESA. Zaidi www.ukombozigosple.blogspot.com   #UkomboziGosple  #MwalimuOscarSamba
Pia #Like #Penda Page/Ukurasa wetu au kundila Fb, ili kuupta habari hizi kwa haraka, zaidi. Ug Ukombozi Gosple,                                                                                       PAGE: https://www.facebook.com/Ug-Ukombozi-Gosple                                              






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni