Jumamosi, 21 Novemba 2026
KUSHINDA NI LAZIMA
Na Mwl Oscar Samba
Kati ya Jambo Muhimu na la Ulazima Kufahamika Katika Fikra za Kanisa; ni Swala la Wao Kuwa Washindi.
Mfumo wa Shetani hufanya kazi kwa lengo kuu la kupigana na utendaji wa Mungu ndani yetu. Shetani adui yake mkubwa ni kanisa.
Wakati nafundisha chuo fulani cha Kithiolojia hapa nchini, kuna somo moja lilibeba pointi hii muhimu: ya kwamba Shetani anapigana na sisi kwa sababu hapendezwi na taswira ya Mungu ndani yetu. Anapigana na sisi kwa sababu ya wivu, alitamani kuwa kama Mungu akashindwa...
Uadui wote huo ni kwa sababu sisi tumeamua kumchagua Mungu na kumkataa yeye mwana wa kuasi.
Lakini ishukuriwe Biblia inayotuhakikishia ushindi kila mara, na kila wakati.
Tazama Hili Andiko: 1 Wakorintho 15:57 Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Ukisoma mazingira ya hilo andiko, utagundua kitu Paulo Mtume anachokifafanua. Ni mazingira ya hali ya mapambano makali kati ya kanisa ama Kristo dhidi ya Shetani.
Lakini katika yote hayo ashukuriwe Mungu anayetupa kushinda na zaidi ya kushinda.
Kwa hiyo, haijalishi unapita mahali pagumu kiasi gani, unakutana na milima mingapi; maadamu tu umeokoka, basi fahamu ya kwamba ushindi kwako ni lazima. Mimi na wewe tumekwisha kuahidiwa ushindi, mbingu zimekwisha kushinda tayari. Hata Shetani analijua hilo, ndio maana anasubiria tu hatima yake ya kutupwa katika moto wa milele mara baada ya kanisa kunyakuliwa na hukumu ile ya mwisho.
Ugumu unaoupitia leo, usikupe tafsiri ya kwamba wewe ni wakushindwa, badala yake uruhusu ufanyike kuwa chachu ya kumtukuza Mungu. Katika ugumu huo, taja ukuu wa Mungu wako. Ndicho ambacho Paulo mtume alikifanya katika kanisa lile la Warumi.
Warumi 8:33 Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. (Kwa hiyo usisumbuliwe moyo na wanadamu na maneno yao)
34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. (Mkono wa kuume maana yake mamlaka...ushindi, utukufu na kadhalika...na kwa mujibu wa Biblia sisi tuliookoka tumepewa kuketi pamoja naye; kwa hiyo umekaa upande wa walio/wanaoshinda ....ni upande wenye nguvu na mamlaka...)
35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? (Hata hatari, au upanga yaani vita haviwezi kututenga)
36 Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. (Mama mmoja aliye okoka muda mrefu, aliwahi kuniambia siku moja.."kama tunauwawa kila majira, na hatufi...maana yake tunafufuka kila mara"..)
37 Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. (Jipige kifua mara tatu huku ukijitaja na jina ukijiambia ambia ya kwamba...MIMI NI MSHINDI,.. MIMI NI MSHINDI,... Mimi ni Mshindiii!)
38 Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
(awe rafiki, "bosi" kazini, mfanyakazi mwenzako, mwenza wako, mzazi ama ndugu...wala kiongozi yoyote yule...)
39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Hakika hakuna kinachoweza kututenga sisi na upendo wa Kristo Yesu, hakika hakipo....ni wazi na bayana kabisa ya kwamba hakipo....maana tunashunda na zaidi ya kushinda. Kukosa fedha, mavazi wala kukosa mtoto ama ndoa ngumu na hata kutokuolewa, bado hakujafikia kuwa na sifa ya kututenga na huu upendo wa ajabu wa Yesu Kristo.
Nikutakie Maisha ya Fikra za Ushindi Hivi Sasa, Na Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja Nawe..Amina
Tafadhali Endelea Kutufuatilia
Follow the Mwalimu Oscar Samba Mafundisho Ya Neno La Mungu channel on WhatsApp: https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni