Jumatano, 18 Novemba 2026
UKIKIRI, Utashinda
Na Mwl Oscar Samba
Ipo nguvu kubwa sana katika Ukiri. Mithali hutuambia ya kwamba, tutakula matunda ya vinywa au maneno yetu.
Ushindi ni kitu kinachoundwa, kutengenezwa au kupaliliwa. Kuna mahusiano makubwa kati ya maneno yanayotoka kinywani mwako, na yale yanayoingia masikioni mwako yakiwa yanatoka au ni sauti za wengine.
Nafsi huwa inasikia, maneno yanaweza kuwa silaha ya kivita katika pande zote mbele, upande wako kupigana ili ushinde na upande wa adui kukudhuru au kukudhoofisha ili ukwame.
Kuna mahali Paulo Mtume alikuwa akipitia, palikuwa pazito na penye kuogofya sana, hakukubali kukwamia hapo, na badala yake alikiri ushindi.
Kiri ya kwamba mambo yote unayaweza sii kwa nguvu zako, bali katika Yeye Yesu akutiaye nguvu. Adui wakijaribu kuonyesha jinsi ulivyo dhaifu, usikubali kushindana nao, jiambie moyoni yamkini ni kweli mimi ni dhaifu, ila nitashinda katika nguvu za Bwana.
Tazama; Wafilipi 4:13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
Kuna mahali pia Paulo alipitia, na alifahamu wazi ya kwamba yeye ni dhaifu, lakini hali hiyo haikuwa kikwazo kwake, na badala yake alitanguliza ukuu wa Mungu wake. Alitambua katika udhaifu wake ndipo uweza wa Mungu hujitukuza. Acha waseme huyu si ndo yule aliyekuwa "kilaza" shuleni! Sasa amewezaje kufika hapo?
Watu wengi hawajui katika neema ipo nguvu za Mungu za kuwawawezesha kukabiliana ama kuufunika udhaifu husika! Ukilijua hili, hutakubali kuutazama udhaifu kama kikwazo, na badala yake utaufanya kuwa fursa. Fursa ipi? Ya Mungu kuingilia kati na kukupigania. Ya Mungu kupenyeza utukufu wake.
Tazama; 2 Wakorintho 12:9 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.
10 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
Udhaifu wa kukosa mtaji wa biashara, ugeuze kuwa fursa ya Mungu kujitwalia utukufu. Muujiza wa yule mama mjane wa Sarepta usingekuwa na nguvu, kama ukame usingetawala. Pili, kama kisingekuwa chakula chake cha mwisho. Tatu kama angekuwa na mume ukubwa wa muujiza usingevuma hivyo.
Maana tunafahamu wajane, na yatima ni miongoni mwa makundi maalumu. Ambayo yanahitaji msaada, sasa hapa badala ya mjane kupokea msaada, yeye ndiye anayetakiwa kumtunza Mtumishi wa Mungu Elia. Na sio mara moja tu, bali ni muendelezo maana Elia kaagizwa ahamie kwake kabisa!
Kuna watu Mungu anawapa maagizo ya namna hii katika nyakati ngumu kama hizi; na tazama maneno ya kwanza yanatoka vinywani mwao! Siwezi, mimi ni masikini, kipato changu ni kidogo. Mchungaji kwani hajui hali yangu...!
Maamuzi yanakuwa ni kuhama kanisa, au kuacha kabisa wokovu. Akisema sababu ni kwamba kanisa lilizidi michango! Unajua maana yake ni nini? Ni sawa na kusema kanisa lilizidi fursa ya kuinuliwa au kubarikiwa kwangu. (Nikazikimbia!)
Ujapojiona u dhaifu, udhaifu wa mtu wa ndani, basi msihi Mungu akutie nguvu ili ikusaidie kuepukana na kutokunufaika na neema ya namna hii...macho yako ya kiimani yakitiwa nuru basi moja kwa moja utaweza kuiona hii neema; na utajikuta ukikiri ya kwamba unayaweza mambo yote katika Yeye Mungu akutiaye nguvu.
Waefeso 3:16 awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. (Utu wa ndani ni mtu wa ndani, yaani nafsi yako na roho yako...tuseme pia moyo wako).
18 ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina;
20 Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu (Lazima nguvu itende kazi ndani ya mtu huyo wa ndani, na ukiri wako utaiwezesha kufanya hivyo).
Nikuage kwa kukupatia andiko hili hapa;
Waefeso 6:10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
Kwa Sadaka, Shuhuda; Wasiliana Nasi, +255759859287 M-pesa Jina ni Oscar Samba
Tafadhali Usiache Kutufuatilia
Follow the Mwalimu Oscar Samba Mafundisho Ya Neno La Mungu channel on WhatsApp: https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni