Alhamisi, 19 Novemba 2026
USIWE NA MASHAKA
Na Mwl Oscar Samba
Yesu Anauliza, Ewe wa Imani Haba, [imani chache) chache ni isiyotosheleza hitajio] mbona uliona shaka?
Mathayo 14:31 Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?
Hii ni hali ya mtu kuwa au kutokuwa na imani vya kutosha kutokana na njia au jambo alilonuia kulifanya. Petro alitamani kweli kutembea juu ya uso wa maji kama ilivyokuwa kwa BWANA wake Yesu Kristo, na alianza tayari kufanya hivyo, lakini mara wimbi lilipokuja, moyo wake ulianza kukosa imani na njia, au tendo ama tukio au tuseme maamuzi yale!
Yesu akagundua tatizo sio wimbi, kama wengi tuonavyo; ila ama bali tatizo lilikuwa ni imani ndani ya Petro.
Na ndivyo ilivyo kwako wewe hivi leo, Yesu alikupa kibali cha kuanza ujenzi wa nyumba, ujenzi wa hema ya kumuabudu Mungu, lakini ghafula umeingiwa na wasiwasi mara baada ya kazi yako kusumbua, mara baada ya kukutwa na changamoto kwenye maisha yako, na kujikuta unakata tamaa. Alipohama mshirika fulani tu, basi moyo wako ukafa; ukajikuta unarudi nyuma na mipango yako ya ujenzi inakufa nafsini mwako! Yesu anakuuliza mbona umeona shaka? We wa imani chache, ewe wa imani isiyotosheleza au iliyopungua kipimo mbona umekuwa muoga!
Katika tukio la kukutwa na dhoruba kule ziwani, Yesu alinena na wanafunzi wake na kushangaa, jinsi walivyokuwa na imani, ndogo, chache, ama iliyopungua!
Maandiko yanasema Yesu alistaajabu, yaani alikasirika na kuwa mkali mbele yao. Kisha anawauliza, mbona mmekuwa waoga enyi wa imani haba? Anauliza swali jingine, gumu akisema nitachukuliana nanyi hadi lini? (Hapo ni katika tukio lile la kushindwa kumuombea yule mtoto bubu na mwenye kifafa). Yesu anauliza, kwa kumaka ya kwamba ataendelea kukuvumilia, yaani kuchukuliana nawe hadi lini? Unamchosha kwa kuendelea kuwa muoga.
Mathayo 8:25 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. 26 Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu.
Epuka sana hofu, uwoga ama wasiwasi; vitakuondolea imani, na kuifanya kutokutosheleza kiwango kinachohitajika. Hali itakayoishilia kukuacha na imani haba. Yaani imani isiyotosheleza kiwango. Utapwaya..
Mathayo 8:25 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia.
26 Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu.
Tazama tena kwa makini katika tukio lile la kumuombea yule mtoto na wao kukwama; Mathayo 17:16 Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. 17 Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu.
Hapo awali, jumlisha na andiko hili, utafahamu ya kwamba kuna nguvu inapaswa kuzalishwa ndani yetu dhidi ya kupambana na upinzani au kuifanya kazi fulani. Sasa, kama ukishindwa, tatizo halipo kwa Mungu; lipo kwako wewe. Na Yesu jibu lake kwake huja ya kwamba, umepungukiwa na imani. Tatizo sio kwake, ila lipo kwako wewe. Kizalishaji cha nguvu ambacho ni imani kimepunguka.
Ukifuatilia andiko hili, utakutana na jambo muhimu sana, ngoja tusome muendelezo wake na kisha nitakujulisha
18 Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.
Hapa tunajifunza swala muhimu, soma mstari huu kisha nitakumegea tena:
Mathayo 17:19 Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa?
20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.
Haiwezekani bila kufunga na kuomba!
Sio dhambi kuondoka na fundisho la kukutaka kuwa na utamaduni wa kufunga na kuomba ili kupambana na milima au vikwazo vinavyosimama mbele yako.
Ila somo kubwa la Yesu hapa ni kwamba, ushindi wowote ule hususani wa kiroho unahitaji mkakati . Lazima kuwa na mpango mkakati.
Mungu akikwambia nenda, jenga, azisha mradi, fanya biashara , fungua huduma ama fanya hiki na kile; usiishilie kwenda moja kwa moja kwa kukurupuka. Bali jikite kwenye swala la kujenga mpango mkakati. (Petro hakuwa na makakati: maana mkakati utakupa kugundua au kujiandaa na vikwazo, ama changamoto za kutembea juu ya maji...yaani utajiandaa na dhoruba; likija inajikuta ulishajiimarisha...sio swala la njoo tu...bali la ninakujaje! )
Yeriko haikuanguka tu kwa sababu Mungu alitaka ianguke. Bali ilianguka kwa sababu ya pili, ambayo ni wahusika kushika maelekezo ya Mungu. Maelezo yalikuwa mpango makakati wa vita kwao. Wewe sababu ya kwanza ni kibali cha Mungu, ushiishilie hapo, bali nenda hadi kwa ya pili ambayo ni ya mpango mkakati.
Yesu, anakuuliza mbona umeona shaka? Ana wasiwasi na imani yako.
Inuka tena sasa, mwambie imani yangu ni kweli imekuwa haba. Lakini niongezee imani. Nipe imani inayokuwa kama mbegu ya haradani.
Ambayo huanza ikiwa chembe ndogo sana kama ya mchicha, lakini hukua na hatimaye kuwa mti mkubwa sana.
Haijalishi mwanzo wangu, utakuwa mdogo kiasi gani, nipe imani ya kuona mwisho jinsi ulivyo.
Mungu akubariki.
Follow the Mwalimu Oscar Samba Mafundisho Ya Neno La Mungu channel on WhatsApp: https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni