Jumatano, 26 Agosti 2026

#UMUHIMU WA KUFANYIKA KWA TENDO LA NDOA (Kibiblia)

Na _Mwl Oscar Samba_ . Ningepewa nafasi ya kuandika au kuandikwa kwa amri kumi za ndoa, ningeanza na Mosi, #Msinyimane ; 1 Kor. 7: 5. Pili Na Malazi Yawe #Safi; Waebrania 13:4..(Usafi wa Uaminifu Katika Ndoa). Tatu #Hakikisha Mwenzi Wako #Ametosheka, Ukiwiwa kuniongezea basi shiriki nami katika eneo la maoni au "comment". Kwa moyo mkunjifu kabisa ninawiwa kukaribisha katika makala hii fupi *(eBook)* inayozungumzia umuhimu na thamani pamoja na sababu za tendo la ndoa. Imizo kubwa lipo kwa wanandoa kukutana; nje ya wanandoa ni chukizo na uovu mkubwa mbele za Mungu. Katika somo hili au makala hii, jiandae kufahamu kiupana zaidi kuhusu vita, au ni kwa nini Shetani hufanya vita katika tendo hili la ndoa. Lakini utafahamu kiupana na kiunaga ubaga nini huwa kinatokea kipindi cha tendo la ndoa! Hali itakayokuimarisha zaidi katika kufahamu kiundani sasa ni kwa nini Shetani analipinga au anapiga vita sana jambo hili la tendo la ndoa. Kiroho tendo hili lina maana gani? Hakika jiandae kutokuwa mtu wa kawaida mara baada ya kulifahamu hili jambo. Maarifa ambayo yatakuongezea thamani katika tendo hili. Ufanisi wake ni dawa, ni tiba, ni kiungo katika kuleta umoja; linatimiza dhima ya mwili mmoja. Naungana na wanasaikolojia kadhaa kuhusu mitazamo yao katika thamani ya tendo hili. Mmoja aliwahi kusema ya kwamba, tendo hili likifanywa kwa ufanisi, huijenga ndoa kwa asilimia 15 na likikosekana au ufanisi ukipungua huwezakuibomoa ndoa kwa asilimia 85. Kwa hayo na mengine mengi nikukaribishe. Lakini pia, ukitulia katika ujumbe huu; utaweza kufahamu japo kwa sehemu ni kwa nini majini mahaba au mapepo mahaba hupenda kuzini au kufunga ndoa za kiroho na wanadamu! Kuna jambo gani wananufaika nalo? Hata vita vingi vya kiutumishi, huhusisha maswala ya kuota au kuzini katika ndoto. Ambapo kama kesho mhusika ana hudumu mahali, basi akiota hivyo anajikuta nguvu katika ile huduma hazipo kabisa. Kwa nini? Kuna jambo lipo katika maingiliano ya namna hii. Na sababu za watu baadhi wanapotaka kumuadhiri mtu, au kuiba mafanikio yake kwa jinsi ya kishirikina; kupewa masharti ya namna hii..ikiwemo kuzini na mtu husika, na hata kuwatumia mapepo ya kuzini nayo! Na hii ndiyo inayompa au inayowapa mapepo mahaba kuwa vinganganizi sana katika maisha ya mtu. Maana wanajua siku akifunguliwa hapa, na mipaka yake ya kiutumishi, kiuchumi au kibiashara ama katika mahusiano itafunguka. Ipo siri kubwa tu hapa. Karibu Tujifunze; #Muktadha wa Tendo la Ndoa na Tendo Lenyewe Kiroho. 1. Huijenga Nafsi. Kama Biblia inalitaja kama tendo linaloweza kubomoa nafsi, kuijerui au kuweza kuifikia nafsi na kuidhuru: endapo litafanyika katika mazingira ya nje ya ndoa; basi uwe na hakika likifanyika katika mazingira sahihi, huijenga nafsi. Huwa na dhima ya kuiimarisha hiyo nafsi. Tujione katika mazingira ya tendo hili pale linapofanywa katika njia haramu, au njia isiyokuwa sahihi. Mithali 6:32 Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. 33 Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima! Kinyume chake ni kwamba, tendo hili huleta uponyaji wa moyo au ndani, na kujenga heshima. Sasa heshima hii huweza kuwa katika ndoa, yaani baina ya mume na mke, lakini pia huwa miongoni mwa jamii. Hutumia neno kibali katika maana ya namna hii. Mke akimheshimu mumewe, kiroho ni anamtengenezea kibali. Tukio la malikia Vashtii kumdharau mfalme, sio kwamba lilikuwa linawafanya wanaume wengine kudharauliwa tu, bali lilikuwa na lengo pia la kuivunja au kuishusha heshima ya mfalme kwa watu wake wa karibu na jamii pia. #Tendo la ndoa limewekwa ili kujenga na kudumisha heshima. Sijasema wale wanawake wanodharau waume zao sabau ni kukosekana au kuzorota kwa tendo hili. Na wala sijasema ya kwamba likikosekana au kukiwa na udhaifu basi heshima lazima ipotee. Ila hii haiwezi pia kuondoa ukweli ya kwamba jambo hili likifanyika katika ufanisi wake; heshima haikosekani. Hali inayozaa kibali. Katika mke kuna kibali, ambapo huchipuza kutoka kwake na kuonekana kwa jamii. Adui akitaka mara nyingi kukukosesha kibali kwa watu, huanzia ndani. Na kutoka ndani, huweza kukikuza kwa nje, yaani kwa jamii. #Tazama Hapa; Mithali 18:22 Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA. Hapa anasema kwa Bwana, uwe na hakika hata kwa wanadamu pia. Mke si mtu, ingawaje anyeolewa ni mtu wa jinsia ya kike yaani mwanamke. Ila anapokuwa mke, sio swala la mtu. Bali ni swala la nafasi. Ndoa ndiyo inayozaa nafasi itwayo mke (wife). Kwa hiyo, swala la heshima ya tendo la ndoa ni muhimu katika nafasi ya mke (ambayo amepewa mwanamke). Nakufundisha hili, ili uwe mwepesi wa kuelewa ni kwa nini adui Shetani anapotaka kupigana na kibali kilichopo juu yako mara kwa mara hukimbilia kwanza kwenye ndoa. Na akikwama hapo ni amekosa kitu kikubwa sana. #Muhimu : Ni muhimu kufahamu ya kuwa sii kila heshima inazalishwa na tendo la ndoa. Maana heshima ni heshima kwa sababu ni heshima. Lakini ukweli ni kwamba, kuna aina ya heshima inayozalishwa katika tendo la ndoa. Sio swala la kumridhisha au kumfikisha tu mwenza wako kileleni; (japo ni muhimu sana) bali ni swala la yeye kulifurahia tendo hilo na kuridhika. Kwa maana kwamba, jambo la uaminifu ni muhimu. Maana nafsi ikigundua mwenzake sio mwaminifu; hujeruhiwa. Na heshima ya namna hii haiwezi kuzalishwa kutoka katika nafsi ya mwenzako (iliyoumia) wala nafsi yako (ambayo pia dhambi hii imeijerui). Lakini pia, kwa wale wanandoa ambao wameoa au kuolewa ama wenye vifungo vya mapepo mahaba, ni vigumu kufikia aina hii ya utoshelevu. Kileleni anaweza kufika, ila ile hali ya kuridhika ndani yake isifanikiwe kufikika. Nawiwa pia ujifunze, Shetani anapoleta upinzani au pingamizi katika tendo la ndoa, ni kitu gani anakiwinda! Ili ikupe kujifunza kupambana naye, usiuchukuli udhaifu wowote kama sehemu au jambo la kawaida. Badala yake ujifunze kuukabili kiroho. #Atapata #Jeraha! Tumeangazia eneo la heshima, sasa tuangalie eneo la jeraha. Kinyume chake ni uponyaji. Wanandoa watakubaliana na mimi kabisa ya kwamba kati ya eneo ambalo huwaunganisha watu vizuri na kuwafanya warudi katika upendo wa awali, ni suluhisho linaloletwa au kuzalishwa kitandani. Tendo la ndoa, hujenga ndoa, huunganisha wanandoa. Huponya ndoa. Ndio maana mtu anapozini, yaani anapotoka nje ya ndoa, inafananishwa na kujaribu kuziachanisha karatasi mbili zilizounganishwa au kuambatanishwa pamoja kwa kupitia gundi. Hali ambayo huzifanya kuraruka na kuzalisha jeraha. Ndoa huunganisha nafsi, unapotoka nje ya ndoa ni unajaribu kuzitenganisha. Agano la ndoa ni kama gundi. Kwa hiyo, kunapotokea mikwaruzano midogo midogo na hata ile mikubwa mikubwa; tendo hili hutumika katika kuleta suluhisho. Kwa hiyo, likikosekana au likikosa ufanisi; uwe na hakika ni mnapokonywa mahakama ya amani ndani ya nyumba. Mungu ametupa hakimu mwema, ambaye hukumu yake ni mapatano bila adhabu. Ndio maana wanandoa wanashauriwa hata wakikwazana haipaswi kunyimana. Maana katika kupeana ndiko kunakozalisha hali ya kuelewana au kupatana. Adui Shetani asingetamani kuiona mahakama hii huru ikiendesha kazi zake vizuri. Maana anajua tu itakwamisha mipango yake. Ndio maana wanandoa wengi, husani mama zetu, wakikwazika hawataki hata kusogelewa! Hili ni tatizo. Ananuna katika kuongea hadi kufungua duka. Duka linafungwa na huduma hakuna. Inakulazimu mwanaume ubadilishe mboga ya dagaa na kuleta nyama, uvunje bajeti na kuja na zawadi ya kitenge au wigi jipya! Hapo ndipo duka litafunguliwa. Zawadi haipaswi kuwa kipatanishi! Kitanda kina nafasi hiyo. Wenye akili, wakiona tu siku haijashinda vizuri, basi wanaimalizia ishee salama na kwa wema kabisa. Siri ni matumizi mazuri ya sita kwa sita. Hakimu huyu hana hukumu ya hila. Ukiona unategemea zawadi, basi umekuwa hakimu mla rushwa. (Sipingi zawadi, ila zawadi sio mbadala). 2. Huimarisha Akili. Kumbuka katika andiko lile, husema aziniye na mwanamke hana akili kabisa. Kwa hiyo jambo la kuzini, linaadhiri akili. Kwa lugha nyingine ni kwamba, tendo la nje ya ndoa au tendo haramu huhusisha akili au ni tatizo la kiakili. Na kwa lugha sahihi ni kwamba tendo la ndoa hujenga akili, ama ni matokeo ya akili njema. Ninachotaka kusema ni kwamba, tendo la ndoa huchangia kujenga afya ya akili. Sio katika eneo la kumuondolea mtu tu msongo wa mawazo, bali ni katika kumjengea pia uwezo wa kufikiri, na kupanga mipango yake vizuri. Ukimnyima, usilalamike uchumi ndani kuwa mgumu au usijilaumu kwa mwenzio kuwa na matumizi mabaya ya fedha. Kwa maana kisababishi ni wewe. Uchoyo wako ndio uliompelekea ashindwe kufikiri vizuri. Kile ni sawa na kiburudisho au tukio la utalii, mandhari nzuri hujenga afya ya akili. Ni sawa na kumtoa mtu "out" ni unajenga saikolojia njema. Ukitaka mwenza wako afikiri vizuri, wewe zidisha tu dozi ya sita kwa sita. Hakikisha inafanyika kiufanisi. Utashangaa hata uso wake umeanza kuondoa mikunjo. Wewe ndie uliyeshikilia funguo za kutokuzeeka kwake kabla ya wakati. Mahasira ya mara kwa mara, majibu ya mkato kwako na kazini ama jaziba za ovyo kwa watoto; ni matokeo ya afya mbaya ya akili. Dakitari ni wewe. Tendo hili sio mahakama huru tu; bali ni dakitari mzuri na mwenye tiba ya akili njema. Mpe bila kumbania bania. Utaona matokeo tu. Jambo hili linaiokoa pia nafsi; Mithali 6:32 Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Kuiangamiza nafsi ni nje ya tendo halali. Maana yake lililo halali huwa na dhima ya kuiponya nafsi. Lazima kutaka sana kujua kwenye nafsi kuna nini na nini? (Kitabu chetu cha SABABU ZA MUNGU KUTUTAKA TUSIJILIPIZIE KISASI na kile cha IMANI INAPOJARIBIWA), vitakusaidia kuifahamu nafsi kiundani. Mosi kwenye nafsi kuna akili, pili kuna hisia, ambapo ni hisia kama za kimapenzi, hasira, furaha, chuki na hata hisia za tamanio la tendo la ndoa. Maana kuna mahusiano ya karibu sana kati ya mfumo wa fahamu na nafsi. Akili ni kiungo muhimu katika mfumo wa fahamu na kipo katika nafsi. Ubongo upo katika mwili, viungo vya uzazi vina mishipa au upo mshipa wenye mawasiliano ya moja kwa moja na uti wa mngonau ubongo. Pia katika nafsi kuna maamuzi au utashi. Katika nafsi pia kuna fikra. Uwezo wa kufikiri. Lakini neno fikra lina upana kuliko neno mawazo, maoni au kufikiri. Fikra kwa kingereza hutumika neno "mindset" lenye maana ya kwamba mtu jinsi alivyo ni matokeo ya fikra zake. Hutengeneza mfumo wa maisha kwa mtu. Ukisikia kufikiri ni kuishi; basi kufikiri au mkusanyiko wa mawazo ambayo yanafanyika kama mfumo; ndio huitwa fikra. Kwa hiyo, tendo hili la ndoa salama huijenga nafsi. Sasa unaweza kuelewa ni vitu gani humo huweza kujengeka. Ndio maana mchungaji akinyimwa, usishangae na jumapili upako unakuwa mzito! Kwa nini? Katika nafsi kuna kiunganishi cha mbingu. Nafsi ni daraja la ulimwengu wa roho. Mambo ya Walawi hutuambia ya kuwa huo upatanishi kwa njia ya damu hunuia kuhuisha uhai katika nafsi. Uhai wa ndoa pia upo katika nafsi. Nafsi ni pumzi ya Mungu. Alipotuumba akatupulizia pumzi yake ndipo tulipokuwa nafsi hai. Sasa basi, kama ni daraja kati ya Mungu na sisi, uwe na hakika nafsi ikiwa vizuri, na daraja litafanya kazi vizuri. (Ndio maana Shetani katika ndoa za watu waliokoka hufanya vita sana katika tendo hili..ni ili nini? Avunje au adhoofishe kufikiri kwetu, akili ibada au avunje daraja kati yetu na Mungu). Na utaelewa sasa ni nini kinatokeaga, adui au mapepo mahaba yanapozini na mtu? Hususani aliyeokoka..kuna kitu kinapandwa, kuna daraja linanajisiwa...kuna roho ya mauti inapandwa ili kupingana na uhai wa ndoa, uhai wa mahusiano yetu na Mungu...ama uhai wa ustawi wa kimaisha.... Uchumi au utajiri ni nguvu...ndivyo Kumbukumbu la Torati 8, inatuambia. Inasema ya kwamba Mungu ndie anayetupa hizo nguvu za kupata la utajiri. Kwa hiyo, utajiri ni nguvu. Na nguvu hizi hazikai katika mwili, maana sio nguvu za kula ugali hizi. Kibali, heshima...fikra nyepesi kiuchummi (ni sehemu ya nguvu hizi) uwezo wa kuteka, kutawala na kumiliki katika ulimwengu wa roho ni sehemu pia. Kwa maana kwamba, sehemu zinapokaa ni katika eneo la nafsi. Ukitaka kujua ni kweli, tazama kipindi ambacho mhusika anaota ndoto za namna hii. Lazima mbele kuna jambo..ndipo utakapogundua ya kwamba sio ndoto au kuzini kwa kawaida, bali ni zinaa kama vita. Shetani hupigana na wewe kwa lengo la kukudhoofisha ili akushinde. Ananua fika ya kuwa, ukiwa dhaifu humuwezi. 3. Ni Tendo Linalofanyika au Kufanywa na Mtu wa Ndani na Mtu wa Nje. Wasomaji wazuri wa Biblia watakubaliana nami ya kwamba, zinaa ni miongoni mwa dhambi mbaya sana; maana hufanywa nje na ndani ya mwanadamu. Kati ya mafundisho mengi, hili ni moja wapo linalodhibitisha jambo hili; 1 Wakorintho 6:18 Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Mtu amegawanyika katika sehemu kuu mbili, mtu wa nje, ambaye ni huu mwili wa damu na nyama au huu unaoonekana. Yupo pia mtu wa ndani. Ambaye huhusisha nafsi na roho. Sasa ukizini ni umefanya kosa dhidi ya mwili wako wa ndani na wa nje. Dhidi ya mtu wa ndani na mtu wa nje. Nikikupa zawadi, nikakupiga kibao, au fimbo ni matendo dhidi ya mtu wa nje. Lakini zinaa huhusisha maeno yote mawili. Je, nataka kukwambia nini hapo? Kama zinaa hufanywa nje na ndani. Basi uwe na hakika na ndivyo ilivyo katika tendo la ndoa. Mtu wa ndani na mtu wa nje wote wawili hushiriki jambo hili. Hii ni faida kubwa sana na dhima muhimu katika musudio la Mungu kuliweka tendo la ndoa. Na laiti kama kanisa lingelijua jambo hili. Upande wa pili wanalijua sana, ndio maana hujigeuza na kulala na watu kwa njia za kimapepo mahaba. Wanajua wanachopanda ndani ya nafsi zao na jinsi silaha hii ilivyo sehemu kubwa ya mafanikio yao sio katika kuharibu tu maisha ya watu, ama kuitawala dunia; bali katika kulidhoofisha kanisa pia. Nasema kulidhoofisha kanisa maana kati ya keshi nyingi na za kisiri sana ni watu wa kanisani kusumbuliwa na zinaa katika ndoto. Na wengi wamedumbukia na kuzama kabisa, katika wimbi kubwa la kutazama picha za utupu; pamoja na kupiga punyeto. [Punyeto ni hali ya mtu kujichua au kujitosheleza mwenyewe kimapenzi aidha kwa kutumia vifaa au vidole vyake mwenyewe au mikono]. (Adui ana mhadhiri mtu nje na ndani.) Ndani kuna nafsi na roho yake. Unapolala na mwenzi wako, ni unafanya tendo ndani ya mwili na nje ya mwili wako. Viungo hivi ama tendo hili limepewa hiyo nafsi. Nasikitika kanisa linajua sana hatari ya dhambi ya uzinzi ama uasherati. Mtu kuanguka kiroho tunajua ni kosa kubwa sana. Lakini naumia kwa kanisa hili, hili kutokujua umuhimu wa tendo la ndoa linapopatikana katika usahihi wake kwa wanandoa na jamii. Pamoja na athari zake kunapokuwa na mushkeli dhidi yake. Mimi huwa nikiletewa malalamiko yoyote kuhusu ndoa, mara kadhaa sehemu yangu ya kuanzia utafiti wangu ni kutaka kujua kama tendo hili linafanyika katika hali ya ufanisi! Maana mtu wa ndani akipokea chakula hiki, kuna baadhi ya matatizo yatajitatua juu kwa juu. Mtu mwenyewe minyoo akiwa na njaa, anasumbua sana; lakini mtu huyu huyu mwenye minyoo akishiba; hutaona usumbufu. 4. Unafanyika Kuwa Mwili Mmoja na Mmke au Mume Wako. Maandiko yapo wazi kabisa ya kwamba, unapolala na kahaba unakuwa mwili mmoja pamoja naye. Kumbe tendo lililo haramu huweza kumuuunganisha mtu na kahaba. Basi ndivyo ilivyo kwa tendo sahihi, huweza pia kumuunganisha mtu na mwenza wake. Nao wakawa mwili mmoja. Wengi wanafikiri hii ni dhana ya kiapo cha kiagano cha ndoa tu. Mimi sikatai hilo, ila kuna maana pana zaidi ya hapo. Ambapo utimilifu wake upo katika tendo hili. Sheria za ndoa haitambui ndoa bila tendo la ndoa. Ndoa ni tendo la ndoa, (hiyo ni lugha ya kisheria). Sasa utaelewa ni nini huwa kinatokea kama Shetani akifanikiwa kuwafarakanisha wana ndoa katika hili tendo la ndoa? Hapana Shaka ni anafanikiwa kuwanyima umoja. Mshikamano, wnasalia kuwa wawili na sio mwili mmoja tena! Kwa hiyo, kuna hatari ya kuwa na ndoa ambazo ni wawili na sio wamoja. Nataka pia nikudokezee na swala ambataniahi hapa katika muktadha wa haya maandiko. *Tazama* ; 1 Wakorintho 6:15 Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Jambo lenyewe ni hili hapa, adui akifanikiwa kukuingiza katika wimbi la dhambi hii ya zinaa, uwe na hakika ni anamnyima Kristo Yesu kuwa na utawala katika mwili wako! Maana ndicho Paulo Mtume anajaribu kutudokesea hapa...na kwa wale wanaoota hizo ndoto, maana yake moja wapo ni kwamba; adui anapingana na umiliki wa Kristo katika miili yetu. Ukisoma maandiko yote utatambua anazungumzia kuhusu sisi kununuliwa na kuwa mali ya Kristo. Unajisi huu unanuia kuadhiri jambo la namna hii. Kwa lugha nyingine ni kwamba, Shetani anapigania umiliki wa mwili wako. Ili nini? Ni ili afanikiwe lile analolikusudia! Anauliza bapo katika huo mstari ya kwamba, je, avitwae viungo vya Kristo na kuwa viungo vya kahaba? Ufafanuzi ni kwamba, je atwae viungo hivyo ya Kristo na kuvifanya vimikiwe na roho iliyopo ndani ya kahaba! Sasa inategemea ni roho gani, kuna wengine wamebeba roho za kuua huduma au kipawa chako. Wapo waliobeba roho ya madeni. Wengine wananuia kukuibia kibali au kudhuru mbaraka wako (wanaita nyota). Wapo waliobeba magonjwa na kadhalika. _Tuendelee_ ; 1 Wakorintho 6:16 Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Hapa ndipo pale penye kiini chetu; natamani sana uelewe na unufaike na thana hii ya kukufanya kuwa mwili mmoja na mkeo au mwenza wako. Ukikwama hapa ni umekwama eneo kubwa sana, sana. 17 Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. Katika sura ile nyingine, ni kwamba wale wanaozini, wanaungwa na kuwa roho moja na Shetani. Hili ni agano au patano katika uharibifu. Kwa hiyo, unapoota unazini katika ndoto ni muhimu kutaka kujua unaungwa na roho gani. Mfano, wapo wanaoota wanazini na baba, bibi au babu. Mama, mzazi shangazi na hata mjomba au mama mdogo na kadhalika. Wengine ni binamu, dada ama kaka na hata mpwa. Fahamu wazi ya kwamba kuna aina ya roho ya kifamilia au kutoka sio kwa mwanafamilia bali ni kutoka katika nafasi husika ya kifamilia unaunganishwa nayo. Kama ni roho ya kutokupata mtoto sawa, ni roho ya umaskini au kutokuolewa pia ipo. La muhimu ni kutaka kufahamu ni roho gani unaunganishwa nayo. (Roho Mtakatifu atakusaidia kuijua.) 1 Wakorintho 6:18 Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Maandiko yanapotoa agizo la wewe kuikimbia, ujue na kwenye ndoto akili zako zinatakiwa kufanya hivyo. Ukiona katika ndoto unaridhia kiwepesi, au ni hata ni wewe ndie unayetaka au kufurahia; uwe na hakika ya kwamba kiwango chako cha kuwa mateka au cha kukamtwa na hii roho ni kikubwa zaidi. (Mtu anapolala akili zake hazilali, maana nafsi pamoja na roho ndivyo huota ndoto; na akili zipo katika nafsi. Sasa nafsi iliyo mateka na fahamu za mhusika huwa mateka pia.) Ulimwengu wa roho ni wa kiroho, lakini nafsi yako ina nafsi ya kimaamuzi kama ingali huru.) Ndoto za kuota unakula vyakula zinahusika sana katika kubana akili au kuifanya nafsi iwe mateka. 19 Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe. Roho Mtakatifu anadhima ama jukumu la kuifanya miili yetu isiwe mali yetu wenyewe (maana ndio chapa au harabuni ya rohoni yaani anatupiga mhuri na kuwa hakikisho la Kristo katika kutumiliki). Kwa upande mwingine, ile roho inayokumiliki au uliyounganishwa nayo ina nafsi ya kukufanya kuwa mali ya roho husika. Ndio maana tuna wakristo wanaofanana na sanamu ya mfalme Nebukadreza. Huku shaba, kule udongo, huku chuma na kule dhahabu. Ibada wanapenda, uongo wanao. Kanisani wapo, usiku wanatazama picha za ngono. Uasherati haachi, na kushuhudia wanafanya. Uwe na hakika, wana wamiliki wengi. Na ishara wana wamiliki wengi, tazama aina ya ndoto wanazoota! Kama sio za kuzini basi ni za vyakula. Kuota unakula katika ndoto, ni unaunganishwa na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu au mashetani. Kwa lugha nyingine ni vyakula ambavyo ndani yake vina roho nyingine. Ni meza ya mashetani. Vyakula vya kichawi. Kama meza ya Bwana ni chakula chema cha uzima, ndivyo ilivyo na meza ya mashetani. (Ndoto ni mlango wa kiroho). Na huwa mbaya zaidi kama utakula vyakula vya matambiko, vyakiganga au vya futari ya dini fulani. Hivyo huwa na nguvu zaidi. 20 maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu. Kati ya kitu anachonyimwa mtu wa namna hii, ni Mungu kutukuzwa katika mwili wake. Usishangae hata uvaaji na unyoaji wake au mtindo wake wa nywele, na mavazi havimpi Mungu utukufu. (Usininukuu vibaya, sijasema kuvaa nguo fulani ni dhambi, wala kugusia unyoaji fulani...nimesema havimpi Mungu utukufu. Mimi kulala na nguo ya ndani chumbani kwangu sio dhambi...ila nikitoka nayo nje na kwenda nayo sokoni nina mnyima Mungu utukufu. Japo pia sio dhambi, ila ninamnyima Mungu utukufu. Maana halina heshima jambo hilo mbele za jamii, watu watajikwaa...na watu wakijikwaa Mungu hana utukufu. ) Mungu akikosa utukufu, na wewe utakosa utukufu. Hilo lishike daima. Ili ujue adhari za kuvaa na kunyoa kiholela holela. Nimesema Mungu akikosa utukufu na wewe utakosa utukufu...na utukufu wa Mungu ukipungua katikati yako...(Simalizii)... Watu wengi fundisho la mavazi wamekuwa wakilihukumu kiutofauti sana. Lakini nikufikirishe tu, kama katika dunia hii ungekuwa upo mwenyewe; kwani kutembea na nguo moja ingekuwa ni dhambi au tatizo? Naamini hata kutembea uchi kusingekuwa ni tagizo! Lakini kwa sababu ya watu wengine, tunalazimika kuishi katika namna fulani. Ukipuzia hapo; sawa: ila nakushauri sasa ungetafuta sayari yako mwenyewe ukaishi huko ili sasa uwe na uhuru wako binafsi. Mtu mmoja akasema nanyoa au navaa hivi kwa sababu mume au mke wangu anapenda. Mie namshauri, mvaliye mkeo au mmeo mkiwa wawili. Nyoa ukiwa naye, ukitoka mbele yetu hivyo, ujue sisi tutakwazika...na huo utukufu utakuondokea...(Sijaweka fundisho la mavazi hapa...na wala sio kusudio langu hata kidogo....nimeguswa tu kulichomekea hilo na wala lisikukwaze tafadhali maana nami sio wale wa misimamo mikali..... 5. Humnyima Adui Shetani Nafasi...andiko la kututaka tusinyimane...linakamilisha dhima na thana muhimu ya kwamba, kama hatutanyimana...Shetani anakosa nafsi ya kuipiga au kuivamia ama kuijaribu ndoa na hata familia. ...(Inaendelea..) 6. 7. 8. KITABU KINAENDELEA: Nikushukuru kwa Kuungana Nami Hadi Wasaa Huu... Kitabu Hiki Hakijafikia Tamati...Bado Kinaendelea...Ukikihitaji Utalazimika Kulipia Fedha za Kitanzania Shilingi Elfu 5....Nawe Utatumiwa kwa njia ya PDF kikiwa Kamili na Kikiprintiwa Tutawajulisha Pia... Àsante: Namba ya Mawasiliano: +255759859287 Oscar Samba Kama Bado Hujaokoka na unaguswa kufanya hivyo, Fuatisha Pamoja Nami Sala Hii ya Toba. #Sema; MUNGU BABA, NINAKUJA MBELE ZAKO, MIMI NI MWENYE DHAMBI, NAKUOMBA UNISAMEHE: AMENI. Hakikisha unatafuta kanisa la Watu Waliokoka Ukaabudu Hapo. Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h Kwa Maombi: +255759859287 http://www.ukombozigospel.blogspot.com Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv Kwa Maombi +255759859287 Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL UWE NA AMANI