Jumatatu, 3 Juni 2019

Mtumaini Bwana Bila Wasiwasi !

Zaburi 26:1.
Na Mwalimu Oscar Samba.       Najua kuna mambo mengi kadha wa kadha umeyaombea ila bado hujaona majibu yake ! Yangu rai ni kukusihi kuwa Bwana yu malangoni, na ana heri yule amngojae hapo, ikiwa na maana kuwa amebarikiwa aliyeweka tumaini lake kwa Bwana.

Ni muhimu sana kufahamu sana kuwa imetupasa kumuomba Mungu bila kukata tamaa, hii iwe ndio dira yetu peke maana Mungu hujibu kwa wakati wake, na inatupasa kumuomba siku zote bila kuvunjika moyo, maana sisi wenye kumkumbusha Bwana twaambiwa tusiwe na kimya, anasema ameweka walinzi juu ya kuta zako, ambao hawatanyamaza usiku wala mchana , walinzi mpendwa ni aina ya waombaji !

Kwa hiyo Bwana amekusimamishia watu
ambao yamkini huwajui, ama unao wajua lakini huwadhani nao wanakuombea, na wengine hawajijui maana hunena kwa lugha ila wanashangaa tu siku hizi wanakuota sana, au hukuona roho, ama kila wakikukumbuka wanasikia mzigo rohoni, hiyo ni dalili kuwa Mungu amekusimamishia waombaji, ambao anasema hawatanyamaza.

Sasa wewe ukikata tamaa maana yake unawafukuza, au unamwambia Mungu sihitaji tena msaada wako, la muhimu wewe endelea kumtazama nyoka wa shaba, maana hapo ndipo yalipo majibu yako, msalaba ni ishara ya ukombozi, usiupe kisogo bali ukodolee macho, usikodolee jeraha ama adha yako bali inua macho yako mtini.

Usikubali kutishwa na kelele za adui zako, bali mtazame Bwana, naye atakujibu tu !

Kama alimjibu Ayubu baada ya siku nyingi, wadhani kwako  hatakuja !

Hapana, usikubali kuyafikiri hayo, bali mtazame Kristo, maana ni jambo, au neno gani ambalo kwake ni gumu ! Hakika halipo .

Aliigawa bahari, alilisimamisha jua na mwezi, aliukausha mto Yordani, alimuokoa muaji Sauli na kumfanya chombo chake, wathania atashindwa kumuokoa au kumkomboa huyo mumeo na ulevi, la ! Hasha ! Maana mkono wake sio mfupi kiasi hicho !

Sara aliyekuwa tasa alizaa, na kusema Bwana amemfanyia kicheko, na kila atakayesikia atacheka pamoja naye !

Unathani umri wako umefikia ule wa Sara ! Jibu  natumai ni la Mwalimu Oscar Samba , sasa kama ndivyo, huna budi kukaza katika kumngoja Yeye.

Ni kwa nini umekubali kuishiwa nguvu za maombi ? Ni kwa sababu umemuona Bwana amekawia kukujibu !

Hapana mpendwa ! Kwa kuwaza hivyo naona humtendei haki huyu Mungu wetu !

Maana Yeye ni mwaminifu, hasemi uongo, wala hakawi, sio mtu ama mwandamu ajute, akihaidi atatenda uwe na imani naye !

Kama yuke hakimu dhalimu, leo tungalimuita hakimu fisadi au fethuli, aliweza kutoa haki kwa mama mjane, wathania Mungu aliyemwenye haki kwako hatatenda ?

Hapana, Yeye ni mwaminifu yu asema kwenye Hesabu kuwa akisema atatendanda basi atalifanya !

Alimwambia Habakuki, katika ile Habakuki 2 kuwa hutenda kwa wakati wake ! Wala hakawii pia hawai !

Sasa wewe unayejiuliza unapaswa kungojea hadi lini ! Jibu lake ni hadi wakati wa Bwana ufike !

Yamkini unaniuliza sababu za Mungu kutokukujibu leo !
Mie ninakujibu kama baada ya mfano wenye agizo la kuomba bila kukata tamaa au kukoma unavyoitimishwa kwenye ile Luka 18, "kuwa ajapo Mwana wa adamu je ataikuta ama ataiona imani duniani' !

Imani yako ipo kwenye kipimo, sasa ukiacha wokovu, ukiamua kuolewa kiholela au kuoa mtu ni mtu kisa majibu yamechelewa, au ukiamua kwenda kwa waganga kisa biashara ni ngumu au umeomba bila majibu, maana yaje imani yako itakuwa imepimwa na kukutwa imepunguka ! Mungu anapima yako imani !

Yakobo hutuambia kuwa twawaita heri yaani wabarikiwa kwa sababu ya uvumilivu wao, na kipimo cha uvumilivu ni muda ! Jifunze kwa Ayubu, Mungu anaonekana mwishoni, sasa ukiniambia Mwalimu Oscar Samba nimeomba ila Mungu hanijibu, ni kama vile anisikii mimi nitakwambia kuwa hata Yesu pale msalabani aliwahi kutuambia " Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha," sasa hii haikuwa na maana ya kukatakiwa, maana alipofufuka alisema nimekabithiwa vyote !

Sasa na wewe ukitaka kukabithiwa vyote unavyovihitaji, ukitaka kurejeshewa kama Ayubu ambaye tunauona ukimya wa Mungu katika sura kadha wa kadha hadi anakuja kujitokeza mwishoni ni lazima uhakikishe unapita salama, yamkini unapita na kufikia hatua ya kumuona Mungu kuwa yu kimya !

Fahamu sana kuwa: Yeye sio kiziwi, wala hasinzii useme labla leo kapitiwa na usingizi, Kwenye Yeremia 23 anasema ni Mungu aliye karibu !

Siku moja nilikuwa mahali pagumu sana na kumsikia muhubiri moja akisema kuwa Mungu yu karibu kuliko pumzi yangu, na kuendelea tena kusema yu karibu kuliko mavazi au nguo zangu !

Moyoni niliguna, maana nalikuwa kama Gideoni alipoambiwa na malaika kuwa "Bwana yu pamoja nawe ewe shujaa" !

Kilimsumbua maana hali yao ni ngumu, sasa anajiuliza Bwana anawezaje kuwa pamoja naye angali wanapitia mahali pagumu kiasi hicho !

Ila ukweli ni kwamba alikwepo ! Ukitaka kuamini kasome Maombolezo ndipo utagundua kuwa anaposema ni rehema za Mungu ndio maana hatukuangamia ! Kuna namna walikuwa wakimaanisha.

Nawe kufika ulipofika ni rehema zake, sasa usiisukumie mbali hiyo neema uliyo nayo kwa kunungunika, ama kuyanena yasiyofaa badala yake, Jipe Moyo na Usonge Mbele tena !

Endelea kuomba, kama uliacha anza tena kuomba, ukijua ndio maana ya swali lake la ya kwamba ajapo Mwana wa Adamu je ataikuta imani ulimwenguni !
Sasa  akija leo kukupa majibu yako je ataikuta imani moyoni mwako !

Zakaria alipokea majibu yake lakini katika adhabu !
Sasa angalia na wewe usije kupokea majibu na adhabu juu maana imani itakuwa ilishapotea !

Na epuka sana kutoka nje ya wokovu, nimeandika kitabu kiitwacho, MUNGU NI KIMBILIO NA MSAADA, nikiwa na mantiki kuwa uwapo taabuni jifunze kumkimbilia Mungu, na sio kumkimbia, kama wengine wafanyavyo maana kwake kuna msaada, na nguvu tena tele !
Asante !

Na kama hujaokoka na unataka kufanya hivyo sasa tafadhli kwa imani kubwa nakuu kabisa fuatisha pamoja nami maneno haya, au sala hii ya toba ili uweze kuokoka, Sema;

BWANA YESU, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NATUBU MBELE ZAKO LEO, NISAMEHE NA NINAKUOMBA UFUTE JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, TAFADHALI LIANDDIKE KWENYE KITABU CHA UZIMA, NINAKUKIRII NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU, HAKIKA WEWE NI MUNGU NA ULIFUFUKA KATIKA WAFU, Amen.

Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, kwa maombi, sadaka kwa njia ya M-Pesa, kupiga simu au Wasats App, ni +25559859287. Tupo Arusha Tanzania.

Kwa undani wa Mafundisho au Habari zetu tembelea; www.ukombozigospel.blogspot.com .
#MwalimuOscarSamba #UgMinistry #UkomboziGospel #MwalimuOscarVitabu #Neno #Biblia #Zaburi #Pic #Picha #Tanzania #Afrika

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni