Alhamisi, 13 Juni 2019

Mngoje Bwana


Mngoje Bwana, Jipe moyo, Usife Moyo
"Yeye aliyeahidi ni mwaminifu", kwa hiyo; hiyo ni sababu moja kubwa muhimu sana inayokupasa kumngoja !
Unajua mwanadamu haaminiki kwa asilimia zote, huweza kukwambia ningoje hapa, nisubirie hapa, na kisha asije kutokea, au akakwambia nilikwama, nilipitiwa, ila sio Mungu wetu, huyu Mungu ni mwaminifu, ni wa dhati na kweli.

Kuna heri, au ipo baraka kwa wanaomngoja Bwana ! Mithali 8:34 Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu.
Hasemi siku moja, mbili, au tatu ! Hasemi mwezi mmoja, wala miaka miwili, bali husema siku zote !

Hili ni jibu kwa wenye swali la ningoje hadi lini ? Na kufuatiwa na maelezo kama kungoja kwa kweli nimengoja sana, nimesubiri sana, ila sijibiwi ! Ni hadi haki yako ichomoze kama mwangaza, na kufanywa sifa, na unapaswa kufanya hivyo siku zote, na ungoje kwenye vizingiti vya milango yake !


Kumbuka kwa mujibu wa Yohana 10 Yesu ndio huo mlango ! Sasa anaposema akingoja katika vizingiti vya mlango wake maana yake uzidi kudumu katika wokovu ! Na katika saburi, maana hapo husema akisubiri, na kazi ya saburi ni kukupa ustaimilivu, au uwezo wa kungoja bila kuchoka.

Zaburi anatuambia kuwa kitu kimoja wapo kinachomfanya kumngoja Bwana ni kwa kuwa yeye ndie msaada wao, mbele yake baada ya kumngoja tunapata dhima ya kujawa na tumaini kisha furaha, sasa hii ikupe sana kufahamu kuwa ungojaji wenye saburi, humfanya muhusika kuwa na hali ya furaha kana kwamba amekwisha kukipata kile anachokihitaji, kwa hiyo, ukiona huzuni, fadhaa, uchungu, na masononeko ni ishara ya saburi kupungua, au kutoweka kwa amngojaye Bwana;

Zaburi 33:20 Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.21 Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu. 22 Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.

Kumngoja Bwana kuna kupa kuirithi nchi, yaani kukutana na mujiza wako, maana unamsubiria aliyekwambia naja, sasa akija na kukuta eneo la tukio ni fika na bayana kuwa utakutana na mujiza wako; Zaburi 37:9 Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao Bwana ndio watakaoirithi nchi.
 Kifungu kifuatacho kinaonyesha mazingira ya Mwana Zaburi huyu, ambapo ni ya kuugua, na maumivu, ikimanisha kuna majibu anayongoja kwa Bwana, utahakiki asemapo haja zake zi mbele yake, ila nataka ujione aitumiapo kanuni hii ya kumngoja Bwana, katikati ya adha, anaitaka iingie kazini !
Zaburi 38:8 Nimedhoofika na kuchubuka sana, Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu. 9 Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako, Kuugua kwangu hakukusitirika kwako.
10 Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha; Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka.

15 Kwa kuwa nakungoja Wewe, Bwana, Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu. ( Ana uhakika kwa kuwa anamngoja Bwana, basi kujibiwa ni lazima,nawe hii ikae moyoni mwako !)
Anatuambia tena kuwa kilio chake kilisikika katika kumngoja, nawe ukitaka kujibiwa, mngoje, tena kwa saburi, nikimaanisha huku imani ikiwa ndani mwako, matumaini, na mwenye uvumilivu katika Yeye; Zaburi 40:1 Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.

Zaburi Anamtaja Mungu kama nguvu zake, hii ikupe kuitumia sana hii kanuni ili uzidi kudumisha nguvu zako za maombi, mana kungoja ndiko hukupa kuwa na Bwana kama nguvu za kufikilia mujiza wako ! 59:9 Ee nguvu zangu, nitakungoja Wewe, Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu
Kumngoja kwake kulijawa na fikra yakinifu na pevu kabisa kuwa kwake Yeye ndimo mlimo wokovu, kwa hiyo na tumaini akaliweka kwa huyo aliye na majibu yake, na ukiendelea katika hiyo sura utamuona akiitia moyo mioyo ya wengine kuhusu huyu Bwana, ukimuona mtu aliyeanza kupoteza uwezo wa kufariji wengine uwe na hakika kuna namna naye amechoka kumngoja Bwana;

Zaburi 62:1 Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake.
5 Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake. 6 Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.

Ungojaji wenye saburi, kumbuka daima umebeba tumaini mbele zake; Zaburi 130:5 Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja, Na neno lake nimelitumainia. 6 Nafsi yangu inamngoja Bwana, Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi, Naam, walinzi waingojao asubuhi.
Enzi za Biblia kulikuwa na kisima ama biraka ambalo malaika hushuka na kuyatibua maji kisha wahusika hupokea uponyaji hapo !
Lakini, tunaambiwa walikuwa wakingoja ! Na palikuwa na mmoja wao ambaye maandiko kwenye Agano Jipya yanamtaja, ambaye kungoja kulimpatia mujiza wake, Yesu alitokea hapo na kumponya ! Hii ikupe kujifunza kungoja, maana huyu haikuwa ndani ya mwaka mmoja wala wiki, ni miaka mingi tena sana, kila mara alipitwa, ila ilifika siku yake, nawe yamkini wengi wamekupita, wengine ni wadogo zako unawaona wakioa au kuolewa, wakiwa na maisha mazuri, ila wewe bado hayajawa halisi kwako, la muhimu ni kungoja, maana siku yako yaja, Yesu yu na ratiba ya kukujilia, usife moyo ngoja kwa saburi, jifunze sana kwa huyu mlemavu, maana alipitwa kila uchwao, ila yake siku ilimdia, na yako siku i malangoni;

Yohana 5:3 Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke. 4 Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.]

8 Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. 9 Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.
Ni kweli wamekupita,ila siku yako yaja; (Yohana 5:6 Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? 7 Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.)

Ombi Langu kwa Bwana: Ee, Bwana, Mungu wa Israeli, Isaka na Yakobo mjoli wako, ninakuomba kila akungojae asiaibike, kaka au dada huyu, kijana ama mzee huyu akungojae, umtokee sawasawa na haja ya moyo wake, na mapenzi yako ee Bwana unisikie kuomba na kuugua kwangu katika Roho wako; Zaburi 69:6 Wanaokungoja Wewe wasiaibishwe, Kwa ajili yangu, Bwana, MUNGU wa majeshi. Wanaokutafuta Wewe wasifedheheshwe, Kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.

Bwana, kila akungojaye, umpe chakula, umpatie upesi haja yake, fadhili zako ziwe naye Ee Bwana wangu, na Mungu wangu; Zaburi 104:27 Hao wote wanakungoja Wewe, Uwape chakula chao kwa wakati wake.
Asiabike yeye bali waabike walio adui zake wao wafedheheshwe na kusononeshwa nawe, ila yeye afurahi kwa kuona wokovu wako. ( Amen.)

Mpendwa , kama hujaokoka na unataka kufanya hivyo sasa tafadhli kwa imani kubwa nakuu kabisa fuatisha pamoja nami maneno haya, au sala hii ya toba ili uweze kuokoka, Sema;

BWANA YESU, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NATUBU MBELE ZAKO LEO, NISAMEHE NA NINAKUOMBA UFUTE JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, TAFADHALI LIANDDIKE KWENYE KITABU CHA UZIMA, NINAKUKIRII NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU, HAKIKA WEWE NI MUNGU NA ULIFUFUKA KATIKA WAFU, Amen.

Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, kwa maombi, sadaka kwa njia ya M-Pesa, kupiga simu au Wasats App, ni +25559859287. Tupo Arusha Tanzania.

Kwa undani wa Mafundisho au Habari zetu tembelea; www.ukombozigospel.blogspot.com .
#MwalimuOscarSamba #UgMinistry #UkomboziGospel #MwalimuOscarVitabu #Neno #Biblia #Zaburi #Pic #Picha #Tanzania #Afrika

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni