Na Mwl Oscar Samba
1. Cha Kufanya Unapotupwa Kwenye Shimo.
1. Uwe Utayari na Ufahamu ama Akili ya Kukubali Kuishi Katika Shimo. Lugha ya kutupwa katika shimo ina maana ya kushushwa au adui kunuia kukuua. Ni aina ya pigo la kukung'oa au kukuangamiza kabisa kabisa. Mfano vijana wale wa tatu wa Yuda alipotupwa katika tanuru la moto; Meshack, Shedraka na Aberinego. Danieli katika shimo lenye simba wakali. Alikadhalika Yusufu gerezani, maana alitolewa katika maisha ya utukufu, na kisha kushushwa chini ghafla. Alikadhalika pia alipotupwa katika shimo na nduguze, na kisha kuuzwa utumwani. Maisha ya utumwa kwake bado yalikuwa ni kama shimo, maana anatolewa katika familia ya
kiagano, na kwenda kuishi kwa mataifa. Kwa Myahudi kuishi katika maisha ya wasiotahiriwa bado ni jambo gumu.Ni hatari ukaishi na fikra za nyumbani kwa mzee Yakobo, ukiwa kwa Potifa. Wasije wakakutupa kwenye shimo ukataka kujitetea na kudeka kama ulivyokuwa ukidekezwa maana ni mtoto upendwaye na baba yako. Ni hatari ukajibizana na kaka zako kama ilivyokuwa ukiwa nyumbani! Kwa ujumla kuna aina ya akili inahitajika ili uweze kufauli mazingira ya namna hii.
Ukiwa gerezani, usitake kuishi kama ukiwa kwa Potifa, huko hakuna uhuru. Unakula kwa kipimo, unalala kwa amri. Kengele ndiyo kiongozi wako. Ni hatari ukakosa maarifa haya. Usikubali kupoteza utayari wowote ule. Mimi katika kipindi hiki nimekuwa tayari kuhamia kwenye nyumba yangu hata kama haijakamilika, hapa nilipo kwa muda wananiuliza siogopi fisi (maana ninapohamia ama nilipojenga ni mashambani, na wanapajua maana waliwahi kuvuna mpunga wangu huko... usiku walijikuta wakisikia vinanda vya fisi vikiwahimiza kutoka na kwenda walipokuwa wamepanga kulala usiku huo). Mie nimewajibu ya kwamba, mimi nami ni fisi wa kiroho. Nikawakumbusha jinsi Daudi alivyopambana na Simba na Dubu porini! Nikawaambia aliyekuwa ndani ya Daudi ndiye aliyendani yangu hivi sasa.
Kwa kweli maji ya kuogea na kufulia na hata kutumia, usishangae tukanganyana na ng'ombe. Wenyeji wa mazingira kama haya wanafahamu kitu kinachoitwa "rambo", hili ni bwawa la maji, linalotumika kuifadhi maji, kwa ajili ya mifugo na matumizi ya nyumbani. Lakini hili halinipi hofu, maana hata leo nimetokeo huko ili kukamilisha ujezi wangu katika hatua za mwishoni sasa, lakini maji niliyokunywa leo nasikia kwenye koo huku kwa ndani kuna kata-kata. Na nina mpango wa kuanza kulibandika mikono ili liwe radhi kuishi hapo, likubaliane na kila hali.
Sikuwahi kuogea maji ya bwawa kama hili, maana yana rangi ya tope, lakini naogea bila shaka. Chura akizama kwenye ndoo, unamchukuwa na kumuweka pembeni. Sera yangu imekuwa ya kwamba; "kama watu wanaishi, basi na mimi nitaishi. Kama wanatumia maji kama haya na hawafi, basi na mimi sitakufa." Nikikosa akili kama hizi, nitakwama. Kinachosababisha sonona ama msongo wa mawazo kwa watu wengi wanapofukuzwa kazi; ni kushindwa kukubaliana na mazingira mapya. (Roho Mtakatifu Hutuwezesha...jukumu letu ni utayari tu).
Dada mmoja aliyeachika kwenye ndoa, akataka kujiua! Mtaalamu mmoja wa saikolojia na ushauri na shaha; akamuuliza kwani kabla hujawa na huyu mwanaume hukuwa unaishi! Akajibu nilikuwa naishi! Akamwambia sasa mbona unataka kujidhuru!
Kuna maisha nje ya kazi uliyopoteza. Kuna maisha nje ya ndoa yako iliyokufa. Kwa kifupi kuna maisha nje ya uchumba wako ulioharibika. Nasema, maisha hayajaishia hapo...Shetani asikudanganye. Mwalimu Mwakasege aliwahi kusema ya kuwa; kwanza wengine ni wakina Kaini, wakienda waache waende.
Siku moja Mwalimu huyu aliwahi kusema tena, ya kuwa tukiachwa hatupaswi kukata tamaa maana tupo ndani ya Kristo; na humu ndani tuna kwenda na kuwa na uhai wetu! Hatupaswi kukata tamaa kwa sababu tumeachika...hapana...maana huyo mchumba au mwenza...sio Mungu...hajashikilia uhai wako...bali uhai wako umeshikiliwa katika Kristo Yesu....sio kwa huyo aliyekuacha...na hatari ya kumng'amng'ania ni kumfanya Kristo Yesu aliyeamua kumuondoa kwenye maisha yako, au aliyeruhusu upite hapo ni kama vile amekosea sana...lazima ujue ya kwamba, hakuna vita mbaya kama kuweka tumaini lako kwa mwanadamu. Yesu anataka akaye moyoni mwako kama Mungu. Hataki nafasi yake ichukuliwe na yeyote au chochote. Labla kama Yesu hajakupenda...akikupenda atapiga kila kitu...ili nafasi yake ibaki palepale.
Kumbuka, uhai wetu u katika Kristo Yesu, tunaishi ndani yake. Tunakwenda na kuwa na uhai wetu sio kwa sababu tuna kazi. Sio kwa sababu tumeajiriwa, bali ni kwa sababu tumo ndani ya YESU Kristo.
Akigundua, umeegemea kazi, au kuna pahali pengine umetegemea, uwe na hakika atapagusa tu. Mashitaka ya Shetani kwa Ayubu yalilenga kumuaminisha Mungu au ni ushindani wa Shetani ya kwamba Ayubu anampenda Mungu kwa sababu tu amemtajirisha! Hapo Mungu akasema, sasa na tudhibitishe. Na wakafanya hivyo. Jaribu kufikiri, safari yote hiyo ama mapito, Mungu na Shetani wanashindania jambo moja tu! La je, Ayubu kweli kaweka tumaini lake kwa Yesu au Mali!
Naye Ayubu ni kama vile alikwepo, katika ushindani huo. Naamini Roho Mtakatifu alimsaidia kujua kinachoshindaniwa...maana hapa anajibu vyema kabisa;
Lazima ujue kinachotafuta katika ulimwengu wa roho unapokuwa katika shimo. Ili ikusaidie kuwa na matokeo mazuri. Ayubu 31:24 Ikiwa nimeifanya dhahabu kuwa tumaini langu, Na kuiambia dhahabu safi, Wewe u tegemeo langu;
25 Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi;
26 Kama nililitazama jua lilipoangaza, Au mwezi ukiendelea katika kung’aa;
28 Hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; Kwani ningemwambia uongo Mungu aliye juu.
Tumaini lake halikuwa katika mali. Imani inapopimwa katika mazingira kama haya, inamaanisha kinachotazamwa au kutafutwa ni moyo wako kama uliitegemea hiyo mali. Kwa hiyo, ukitaka kujua kinachotafutwa katika ulimwengu wa roho, tazama pepeto limepita wapi. Mali, kazi au mahusiano ya kindoa? Ama ni katika utumishi?
Nakukumbusha tena ya kuwa, uhai wetu umefungwa katika Kristo Yesu. Wana wa Agano, wanaishi kiagano. Kuishi kwetu hakutegemei mkate au ugali, yaani ajira au kipato. Hupaswa kumtegemea Yesu! Najua kuna gharama ya kulipa unapopitia katika mazingira kama haya, ila baada ya ushindi; utangara kama Ayubu au Yusufu wa Yakobo.
Ingekuwa rahisi kwa Daudi, kujibanza kwa Sauli, na kukubali kuzika ndoto zake hapo ili tu aishi kiusalama mbele ya mfalme Sauli. Wasaka Tonge wengi wapo hivyo. Wapo tayari kubana fikra zao, na kuishi na dhamiri zinazowahukumu kila siku ili tu walinde ugali wao wa kila siku. Watu kama hawa, hufa kibudu. Wanalazimika kuishi katika ndoto za watu wengine, huku ndoto zao zikiwa kaburini. Na kaburi hilo lina pingu zinazoitwa ugali ama mkate wa kila siku.
Uhai wetu ni katika Kristo Yesu, usikubali kukata tamaa mara adui anapokupokonya ugali. Mwambie, naishi katika Kristo, mimi ndani yake na Yeye ndani yangu.
Tahadhari: Sikutaki kuchezea kazi. Hilo ni kosa baya sana. Unatakiwa kuilinda Edeni yako. Walipokabidhiwa hiyo Busani, Mungu aliwaambia wailime na kuitunza. Na wewe kazi yako ilime yaani hakikisha inazalisha faida, isifanye kazi ya kuleta hasara. Wala isizae mapooza. Pia itunze ili maadui wasiiharibu. Gharama ya kuishi nje ya Edeni ni kubwa sana, ukibisha waulize wakina Adamu na Hawa ukifika mbinguni.
Lakini, adui akikutupa shimoni, mwambie hunisumbuia maana Bwana yu pamoja nami. Maandiko hutujulisha ya kuwa Yusufu kwa Potifa alifanikiwa kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, kwa mkuu wa gereza alijipatia kibali wala makosa yaliyokuwa juu yake hayakutazamwa kwa sababu Bwana alikuwa juu yake.
Mwambie, siishi kwa sababu nimechumbiwa ama nina kazi. Ninaishi kwa sababu nipo ndani ya Kristo Yesu. Paulo mtume alifikia hatua ya kusema ya kuwa, hata mwlli huu ukiharibika, tutapewa mwili usioharibika. Ni ushindi mkubwa sana huo katika kiwanda cha fikra zetu.
Mwambie hata nikifa bila mtoto naenda mbinguni, nikifa bila mume au mwenza siji uliko. Hata nikifa nikiwa sina fedha, na hata nikifa njaa kwako siji naenda zangu kwa Baba. Maana uhai wangu umo kwake Kristo Yesu. Naishi kwa kuwa Yeye alikufa na kufufuka. Mauti ya mwili hainisumbui, bali mauti ile ya Pili ndiyo niishindayo. Ila ninajua, hata mauti ya mwilini isiyokuwa na kibali cha Mungu hainiwezi. Maana Yesu ni uhai, na ndiye mtoa uzima. ...akiyasikia hayo utamsikia akijisemea...amenigundua..amenigundua...atayoyoma kama nyoka aliyesikia harufu ya mafuta ya taa ama takataka jamii ya plasitiki zikichomwa moto....na hutamuona tena...
Tazama Andiko: Matendo ya Mitume 17:28 Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.
"..kwenye maisha lazima ujifunze, na uwe tayari kuishi mazingira yoyote; unapotupwa chini ni muhimu kuwa na akili na utayari wa kuishi popote na kivyovyote...Daudi alikuwa ameshapakwa mafuta ya kifalme, lakini kuna majira alilazimika kuishi kama tahira. Alipogundua yupo chini ya himaya ya kifalme, na wasifu wake wa kumua Goliathi ni tishio mbele ya serikali na jeshi ama idara ya usalama wa nchi ile: basi alilazimika kujifanya chizi.
Maandiko yanasema akajipaka paka mate, na udenda mwingi na kadhalika...akawa kama kichaa...mfalme akawa mkali kwa wao kumleta kichaa Ikulu...akaamuru atolewe kwake mara moja...Kwa hiyo, kuna majira lazima ukubali kujifanya chizi ili uvuke. Usikubali kusumbuliwa na ukuu uliokuwa nao... lazima ujifunze kuishi kwenye shimo lenye tope kama Yusufu, uwe tayari kuishi na simba shimoni ingawaje jana ulikuwa mbele ya mfalme.
Ukikwama hapa ni umejiandaa kutokuingia katika msimu wako mpya....Katika nyakati kama hizi lazima uwe na akili ya ziada, usikubali kutazama wadhifa uliokuwa nao kabla ya kutupwa shimoni! Maana Daudi alikuwa na mafuta ya kifalme, Yusufu alikuwa na ndoto ya kukaa mahali pa utukufu, lakini waliishi kulingana na kila mazingira....kukubaliana na mazingira ya kuishi katika shimo haikuondolei wadhifa au kukuzuilia kuinuliwa...shika hili daima."
Huishi kwa sababu hayo ndiyo maisha yako. Bali unaishi kwa sababu hicho ndicho kivuko chako. Lifahamu hilo ili uwe salama kifikra. Haijalishi adui zako watacheka kiasi gani, moyoni waambie ninaisubiri siku yangu ya 3, maana leo ni kweli mmeniua na kunizika. Ila kuna siku ya utukufu wangu...nayo ni siku ya tatu...hapo mtakaposema hayupo tena kaburini. Amefufukaa.
Kama Bado Hujaokoka na unaguswa kufanya hivyo, Fuatisha Pamoja Nami Sala Hii ya Toba.
#Sema ; MUNGU BABA, NINAKUJA MBELE ZAKO, MIMI NI MWENYE DHAMBI, NAKUOMBA UNISAMEHE: AMENI.
Hakikisha unatafuta kanisa la Watu Waliokoka Ukaabudu Hapo.
Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Kwa Maombi: +255759859287
http://www.ukombozigospel.blogspot.com
Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD
Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk
Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv
Kwa Maombi +255759859287
Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL
UWE NA AMANI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni