Ijumaa, 13 Juni 2025

FIKRA SAHIHI KATIKA LANGO LAKO LA MSIMU MPYA.

Na Mwalimu Oscar Samba

Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya cha MOTO WA UAMSHO KATIKA BIBLIA

Tunachambua kila Tukio Muhimu Katika Biblia Nzima, hususani lile lenye Ujumbe wa Kiuamsho Ndani Yake.

Kitabu cha Kutoka, Sura ya 13 na 14

Somo la .... KUVUKA BAHARI YA SHAMU: Ushindi Katika Mlango wa Msimu Mpya Kihuduma au Kimaisha.

Msimu Mpya maana yake ni mabadiliko au hatua nyingine mpya ya kimaisha, na hata kihuduma yaani kiroho. Mabadiliko haya huanzia rohoni kweli, ila huwa na matokeo katika maisha ya uhalisia ya mwilini. Kabla ya kuingia msimu huo mpya, unahitaji kupita katika lango la msimu. Hapa ndipo huwa na upinzani mkubwa sana. Mwanafunzi yeyote lazima awe makini na kipindi chake cha mitihani. Na kuna wengine kipindi hicho huwa katika mashambulizi sana. Ni kwa nini? Ni kwa sababu kuingia kwake katika hatua nyingine, kunategemea kuvuka kwake katika mtihani huo.

Wana wa Israel walikuwa wanaingia katika msimu wa maisha mapya. Kiuchumi tungeuita sekta isiyo rasmi. Maana ile ya jangwani tunaiita ni sekta ya umma. Walilishwa na serikali, na kuhudumiwa na wao. Jangwani wanajiandaa kuishi maisha ya ndege wa angani, yaani sekta isiyo rasmi. Hapo wanalishwa na MUNGU mwenyewe kwa njia ya muujiza. 

 Ndiposa walipokosa chakula walilazimika kuomba kwa Mungu, wakapewa mana. Maji nayo walikuwa wakinyweshwa kwa njia ya kimiujiza vivyo. Lakini siku walipofika tu Kanani, yaani walipoonja zabibu za hapo, ile mana ilikoma. Ikiwa ni ishara ya kuiingia katika msimu mwingine uitwao Sekta rasmi. Huku mtu anakula kwa kulima, kwa jasho au kwa jitihada. Kazi ya maisha ya jangwani ni kukujengea imani katika msimu wako mpya.

Tatizo kubwa kwa wapendwa wa leo, aidha ni kuishi na fikra za Misri yaani za sekta ya uma kipindi wakiwa jangwani, au kuishi na fikra za jangwani yaani zile za sekta isiyo rasmi kipindi wakiwa Kanani.

Kwa sababu hapo awali alikuwa anaweza kukaa tu na mtu akamletea fedha ya ada za watoto, bila kulima akajikuta ndani ana chakula cha kula mwaka mzima; na sasa analazimisha kuishi hayo maisha, na anashangaa maisha ni magumu zaidi. 

Kipindi kile kila akifanya biashara inakufa, akilima hapati mazao, na wala akitafuta kazi hapati; analazimisha na sasa iwe hivyo. Amesahau ya kuwa, kipindi kile alikuwa jangwani, ambapo ni nchi isiyopandwa kitu. Ni nchi ya chumvi, na sasa yupo Kanani kwa jinsi ya rohoni, yaani katika nchi ilimwayo zabibu na ya ufugaji. Maana kama kuna maziwa, maana yake kuna kufuga, na kama kuna asali; ni dhairi maua yapo, yaani mazao na mimea: ni nchi ya kilimo pia.

Kama kuna vita muhimu tunayotakiwa kuishinda, ni ile ya kuwa na fikra sahihi katika kila nyakati. Mfano, ukilazimisha biashara au biashara kubwa na maisha mazuri jangwani, utakwama tu. Maana hiki ni kipindi chakulishwa kama ndege. Katika kipindi hiki kwangu hata nguo zilikuwa hazichakai haraka, ila kila miradi yangu ilikufa; hata kazi nilifukuzwa. 

Sikufa njaa, japo nilijifunza kulala bila kula au kushiba. Maana Mungu alikuwa akiniandaa katika maisha ya kushiba ninayoishi sasa, nilitamani kujenga na kununua viwanja au mashamba lakini ilishindikana kabisa. Lakini kwa sasa hayo yanawezekana. Utamuelewa Mungu sasa katika Kumbukumbu la Torati ni kwa nini anawahakikishia kujenga nyumba na kuishi ndani yake pamoja na kula na kushiba watakapoingia Kanani.

Lakini pia, ni hatari ukaingia Kanani, na ukaendelea kusalia na mawazo au fikra za jangwani! Fursa za kulima na mashamba au viwanja; zinakuja, unazisukumizia mbali kwa kujitetea ya kuwa; hatutakiwi kujisumbua kwa jambo lolote; maana Mungu atatulisha kama ndege wa angani. Uwe na hakika andiko la asiyefanya kazi na asile litakuhukumu tu.

Kwa kuwa wanaokutunza au namna ulivyotunzwa kama zamani imebadilika, watunzaji hawaji tena; unaona kama ni jaribu kwa hiyo unavumilia tu. Ama unakemea maana kwako ni upinzani wa adui Shetani. Unasalia kutaja shuhuda za jinsi Mungu alivyokupigania zamani, ukiamini na sasa ataendelea kufanya hivyo. Mungu mbinguni anajisemea huyu mtu wangu anaangamizwa kwa kukosa maarifa. Yaani anaangamizwa kutokana na kuwa na ujinga wa kushindwa kutambua nyakati. (Kilichowaponza wale wana Wali watano wapumbavu ni hiki; kwao majira ya kununua mafuta yalifungwa katika fahamu zao.)

Wana wa Israel walipofika Kanani, hawakuwa wakiamka tena asubuhi kwenda kuokota au kukusanya mana. Maana ilikoma punde walipoanza maisha ya Kanani. Wangekuwa ni watu wenye kasoro za kiufahamu kama wakiwa Kanani wangekuwa kila siku asubuhi "wanadamka" mapema na madishi au pishi kwa ajili ya kujiokotea mana. 

Sasa, leo kuna wapendwa Mungu ameshawafikisha Kanani, lakini kila siku asubuhi wanaamka mapema, wakiwa na mabeseni au vibeseni vya kuokotea mana! Nyumba kama hivi zimejaa maisha magumu sana. Maana Kanani hatuna muujiza wa mana, hakuna mvua wala umande wa mana: badala yake kuna mvua ya kupandia mazao, kukuzia na ile ya kuvunia. Huku kuna umande wa kulimia bustani, sio ule wa mana.

Huku ukikosa maji, unaenda idara ya maji wanakuja na kukuwekea miundombinu ya maji. Hakuna muujiza wa kuupiga mwamba ndipo upate maji. 

Kanani tunaishi kwa akili na nguvu yaani jasho. Jangwani tuliishi kwa muujiza. Japo imani inapaswa kutumika katika nyakati zote mbili. 

Upinzani wa Kuvuka Katika Lango la Msimu Mpya na Maelekezo Yake.

Mungu alionekana kuwa makini sana na aina ya fikra za namna hii, hofu yake kubwa ilikuwa ni wao wasije wakatamani au kufikiri kurudi Misri. Fikra za namna hii Mungu alijihami nazo mapema; Kutoka 13:17 Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri.

 Kwa hiyo, kuna aina ya fikra ambazo ni dhairi hufanyika kikwazo katika maisha ya msimu mpya, na Mungu hujitahidi kukabiliana nazo katika lango la huo msimu. Ndio maana, katika kipindi cha kuvuka, kuna weza kuja majaribu na mapito mengine magumu sana; ili kukutaadharisha ya kuwa, au kufanyika Ole kwako kama utajatamani au ungalitamani kurudi Misri.

Kwa wakati huu mimi ni Mwalimu katika idara ya Elimu Tag, siku chache kabla ya kuja huku niliugua ugonjwa wa TB. Na nilimsihi Bwana aniponye, kati ya himizo kubwa au lenye sababu ya kuponywa kwangu ni katika hali ile ya kukubali au kuridhia utumishi huu. Niliingia idarani nikiwa mgonjwa na mwenye kuendelea na matibabu. Ila mara baada ya muda mdogo tu, ama muda ule ule nilipokubali swali hili na kwenda kwenye usahili; uzima mkubwa ulijidhiirisha kwangu.

Sasa, wakati najiunga na idara nilikutana na vita na upinzani mkubwa sana. Akili ilipotaka kufikiri kurudi nyuma au hata tu wazo la kutoka Idarani mapema ile lilipotaka kubisha hidi; mwili wangu ulisisimka maana nilitoka katika ugonjwa wa mauti. Kwangu wakati naumwa hali ilikuwa ngumu sana, kiasi cha kushindwa kubeba au kuinua hata chupa ya chai ile ya vikombe 3! Nakumbuka mwili ulisisimka kila nilipokumbuka maisha ya awali ya ugonjwa!

Maana fahamu zangu zilijua fika nilipewa nafasi ya kuishi tena kwa ajili ya maisha haya ya ualimu idarani. Maana yamkini isingalikuwa rahisi kwa mimi kuitikia wito wa kuja huku.

Maandiko tuliyoyasoma, yanatuambia ya kuwa Mungu aliwapitisha katika njia ndefu, na tunafahamu ilikuwa ngumu ili wasije wakarudi watakapokutana na vita njiani! Kuna mambo Mungu anayaachilia unapokuwa katika nyakati kama hizi, na sio kwamba alishindwa kukuvusha kirahisi; la! Hasha. Bali kuna aina ya fikra alitaka kuzifungia mlango, ili hata zikibisha hodi, zikutane na komeo katika malango ya kujaribu kurudi.

Bahari ya Shamu ilifanyika komeo. Kwa maana kwamba, walivuka kwa muujiza, na wakitaka kurudi lazima muujiza kama ule utendeke; swali linakuja katika uasi huo muujiza utakwepo? Musa, naye je, atakubali kurudi pamoja nao?

Licha ya upinzani na vita kutoka katika nyumba ya utumwa ya Misri, lakini upinzani moja wapo ulikuwa ni katika fikra zao wenyewe. Hili likumbuke daima, ili ujifunze kujiombea pamoja na kujijenga katika fikra sahihi, maana ukivuka hapa hata Mungu utamrahisishia kazi. Hata lazimika kukupitisha katika njia ngumu tena. Kwa mfano, kama wana wa Israel wangekuwa hawampi Mungu mashaka kuhusu hatari ya wao kurudi Misri, kusingekuwa na haja ya wao kuipitia hiyo njia yenye mizunguko mingi! Kwa hiyo, maisha na njia waliyoipitia, sii kwamba Mungu alikusudia hivyo, bali ni hali ya moyo wao.

Hakiki Tena; Kutoka 13:17 Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; 

18 lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha. 

Na watu wengi hawajui ya kuwa, japo njia hii ni ya kuzunguka, lakini nayo hailingani na muda waliokaa Jangwani! Muda wa kukaa jangwani ulikuwa ni adhabu. Na adhabu hiyo ilitolewa siku za mwanzoni kabisa. 

Sijui unavuka msimu wako mpya ukiwa na fikra za namna gani? Unapaswa kuvuka ukiwa na fikra sahihi ili usije ukaishilia kutangatanga jangwani. Usije ukawa tu mzururaji katika nyika. 

Wana wa Israeli walijikuta kila mara wakitamani maisha ya jangwani, wakitamani kurudi Misri. Jambo lililofanyika hasira kwa Mungu. Njaa au kiu kidogo na hata ile habari mbele yao: hushilia katika malalamiko makubwa. Wanakumbuka matikiti maji na vitunguu ama nyama za Misri. Kwao jangwa lilikuwa ni sehemu ya kifo. Wanamuuliza Musa je, hakukuwa na makaburi kule Misri hata ukaonelea tuje tufie huku jangwani?

Haya ni madhara ya kukwama kifikra katika lango la huu msimu.

Kumbuka, toka Mungu alipomtokea Musa katika kile kilichoonekana jiti kule nyikani; lango lao la msimu lilikuwa limeanza kuwafungukia. Walipaswa kujiandaa kuyaishi maisha ya mpito. Maana jangwa ni maisha ya mpito, yanayokuelekezea katika maisha ya kudumu ya Kanani!

Wao wakaingia jangwani wakiwa na fikra za kupumzishwa nafsi. Hawakujiandaa kifkra kuandaliwa kwa upya kwa ajili ya Kanani!

Mabinti wengi hawajui ndoa au kuolewa ni kutoka katika sekta ya Umma na kuingia katika sekta rasmi. Lakini kabla ya kuyaishi maisha ya sekta rasmi, wana ndoa wengi wachanga japo sio wote; hupitia kipindi hiki cha mpito. Ambacho hunuia kukuandaa kwa ajili ya maziwa na asali. Na hapa ndipo wengi hufanya makosa, hususani kwa mabinti. Maana kuna namna alijiandaa kifkra huko aendako. Na wakiume asipokaa vizuri, anaweza kukoseshwa kuingia Kanani yake kama Musa alivyokoseshwa na wale ndugu!


Tafadhali Kitabu Kikitoka Kitafute 


Au Zaidi Endelea Kutembelea: https://ukombozigospel.blogspot.com/?m=1 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni