Jumatano, 18 Juni 2025

KUMSIFU NA KUMUABUDU MUNGU, KULIKO HALISI

  Na Mwl Oscar Samba

Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya cha MOTO WA UAMSHO KATIKA BIBLIA, Tunachambua kila Tukio Muhimu la Kiuamsho Katika Biblia.

Somo la .... SIFA NA KUABUDU KWA KWELI; Maneno Yenye Uhalisia Katika Kumuabudu au Kumsifu Mungu.

Licha ya umuhimu wa hali ya kiroho ya mtu anayemsifu au kumuabudu Mungu, ambapo tunaangizwa na lile andiko la Zaburi linalotutaka tuwe na moyo safi ( Zaburi 33:1 Mpigieni BWANA vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Rejoice in the LORD, O ye righteous: for praise is comely/inatoka for the upright.); lakini pia uteuzi wa maneno na muundo wa sentesi zetu katika kumuimbia Mungu: lazima visadifu uhalisia.

Lazima yataje aidha ukuu wa Mungu, uweza wake au utukufu na utakatifu wake. Tabia zake na utendaji wake uliotukuka vinapaswa kuwa ni sehemu ya maneno yaliyoteuliwa na mtunzi sanjari na muimbishaji wa wimbo.
Tuna nyimbo nyingi leo zinaitwa za kuabudu ni kwa sababu tu zinaimbaa katika hali ya utulivu. Na zile za kusifu ni kwa sababu zinaimbwa kanisani na katika hali ya kuchangamka. Hatusifu kwa kuwa wimbo unamsifu Mungu, bali ni kwa kuwa muimbishaji katuambia tusiamame tumsifu Mungu. Ni kwa kuwa mpigaji kapiga mapigo yakutuchangamsha.

Utukufu wa Mungu hauwezi kujidhiirisha katika uimbaji ili mradi uimbaji. Maneno yake ni lazima yawe na uwezo wa kupeleka sifa, au kumtukuza Yeye. Sifa lazima itaje sifa. Maabudu lazima yataje utukufu wake, lazima yaelezee yeye ni nani kwako. Wewe unampa nafasi gani maishani mwako. Usanii umekuwa mwingi sana katika ibada za siku hizi. Sikatai ubunifu na utaalamu, ila visiondoe kiini hiki ninachokifunza hapa. Tusijitete tu ya kuwa Zaburi imesema tuimbe kwa akili bila kulielewa hilo andiko vizuri.

Akili tajwa hapo sio za utaalamu wa kisanaa tu, bali pia ni akili katika kumjua Mungu. Ni akili katika kufahamu namna ya kuteua na kuchagua maneno mazuri ya kumfaa Mungu kwa watu wa wimbo huo. Ni akili pia za kuwa na mpangilio mzuri wa wimbo wako na ni akli za kuutafuta uwepo wa Mungu pia.

Katika Zaburi takribani mara mbili andiko hili lime kuwa likijirudia, rudia. Ya kuwa Mungu anachungulia duniani akimtafuta, mtu mwenye akili; amtafutaye; Zb. 14:2 na 53:2 . Kwa hiyo, kumtafuta Mungu ni aina ya akili. 1 Yohana 5:20, anasema ya kuwa Yesu amatupa akili ilintumjue.

Kwa hiyo, ni makosa kuzitazama akili katika andiko hili kama akili katika ubunifu wa nyimbo tu, sanjari na utaalamu wa kuimba.
Zaburi 47:7 Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa akili. For God is the King of all the earth: sing ye praises/kusifu with understanding/ufahamu. (Msifu ukiwa na Ufahamu).

Ukilitazama hilo andiko kwa umakini hapo, utagundua ya kuwa limeanza kwa kutaja nafasi ya Mungu katika dunia pamoja na kuuelezea ukuu wake kwetu. Baada ya hapo sasa, sehemu ya pili ndipo anapokuja kutupa agizo la kuzitumia akili. Na Biblia hiyo ya kingereza hapo, imejikita katika kuimba kwa namna ya kumsifu. Ambapo ufalme wake duniani unatajwa, na hata mstari unaofuatia ukiusoma utakutana na kitu cha namna hii.

Kinachonifanya nikulete huku kote ni tukio lile la wana wa Israeli kuivuka bahari ya Shamu, na namna walivyomuimbia Mungu mara baada ya ushindi ule.

Aina ya maneno waliyoyateua, ndiyo yanayonipa ujumbe huu pamoja na msukumo au imizo lake kuu.
Tutazame kwa Pamoja; Kutoka 15:1 Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. 

Anasema ametukuka sana, kisha anataja kilichotekea ambacho ni cha wale farasi wa jeshi la Farao kutupwa baharini pamoja na askari. 

Tazama kwa umakini maneno ya mstari wa pili yalivyojaa maabudu mazuri. Utagundua yanamtaja Mungu ni nani kwake (kwao)? Hali inayotengeneza sababu ya maneno ya sifa kinywani mwake!
          Ona; Kutoka 15:2 BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. (Maneno Mungu wangu na Mungu Wetu; huwa na nguvu tofauti inapofika swala la kumuabudu au kumuadhimisha Mungu).

Nyimbo Zetu Zinataja Matukio Mungu Aliyotutendea? Au Tunajitungia na Kujiimbia Tuu! Kutoka 15:3 BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. (Wasifu wake).

4 Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. (Udhiirisho wa utendaji wake au jambo alililowatendea, udhiirisho wa ukuu na uweza wake kwao.)
Kuna wingu, na mahusiano baina yetu na Mungu hayawezi kujengeka mpaka tumeling'amua hili swala vizuri. 

Tuna maneno mengi katika nyimbo zetu ya kutusisimua, na kutufanya turuke ruke, kuliko za kuelezea ukuu wa Mungu wetu dhidi ya miungu mingine, na namna anavyotupigania kinyume chao; Kutoka 15:11 Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? 

12 Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza.
13 Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.
Unapokuwa katika uimbaji wako binafsi, sifa binafsi au maabudu; jifunze kuweka maneno ya kumuelezea Mungu jinsi alivyo kwako, na wewe kwake: pamoja na matukio aliyokupigania. Hii ndiyo ibada ya kumuimbia ya kweli. Maana ni halisi, na inatoka moja kwa moja katika vilindi vya moyo wako. Sipingi uimbaji mwingine, wenye matukio mengine: ila hapa natilia mkazo katika wewe na Mungu kiupekee na kiubinafsi. Kama huwezi kuchomekea/kupenyeza hayo maneno katika nyimbo, basi yataje katika kumuadhimisha Bwana.

Ona mfano; Kutoka 15:19 Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, BWANA akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari. 

Waimbishaji mnapaswa kutuongoza katika ukuu, utakatifu, wema, fadhili na kila sifa ya Mungu. Sanjari na ule utendaji wake kwetu. Na sii vinginevyo; Kutoka 15:21 Miriamu akawaitikia, Mwimbieni BWANA kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. 

Tazama Andiko Hili; Zaburi 30:4 Mwimbieni BWANA zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake. 

Anasema utakatifu wake. Hapa hakuna imizo la utakatifu wako, bali ni wake Yeye Mungu. Unataja kumbukumbu lake. Kuna kumuimbia zaburi, alafu shukurani; alafu pia wanaotakiwa kufanya hivyo ni sisi tuliojitoa kwake katika kifungo cha usafi na utumishi yaani watauwa, Biblia moja ya kingereza ikasema watakatifu penye watauwa; yaani sisi tuliokoka. Kwa hiyo, wokovu ni muhimu, lakini pia ninayokuelekeza hapa ni ya msingi pia.
Kumsifu, Kumuabudu na Kumshukuru Kuliko Bora Mungu: Huwa Kunabeba Sababu za Kufanya Hivyo. Nje ya hapo na ni kukariri na kutimiza wajibu tu wa kiibada. Hapa wanafanya hivyo, kwa sababu fadhili zake wameziona, na wakagundua ni za milele. Kumbuka ni mazingira ya kulipokea sanduku la Bwana la Agano. Hali hiyo iliibua moyo wa ajabu wa ibada. Na ukiweza soma sura yote kwa utulivu. Utajifu za mambo muhimu sana hapa.

Hakiki; 1 Mambo ya Nyakati 16:34 Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Na kwamwe huwezi Kukosa sababu ya kumuabudu Mungu, kumbuka hata pumzi, uhai ama afya ulinayo (hata kama sii nzuri sana); bado ni sababu ya kumuabudu na kumsifu.

Kitabu kikitoka Tafadhali Kitafute
Mawasiliano: +25559859287

Zaidi Tembelea: https://ukombozigospel.blogspot.com/?m=1

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni