Shalom Mtu wa Mungu, Karibu katika Makala hii, ikiwa ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya cha JIFUNZE KUMUAMINI ROHO MTAKATIFU KATIKA HILO ENEO*..
Na Mwl Oscar Samba
Katika Badiliko la Tabia
. Unageuzwa/Hutugeuza Na Kutupa Maisha Mapya . Dhambi ilipoingia ulimwenguni ilitupatia mwili wenye tabia au vinasaba vya chembechembe za dhambi. Ile mauti iliyonenwa, iliua sehemu kubwa ya asili au ya tabia ama ya vinasaba vya Kiungu katika maisha yetu. Na badala yake, tukatwa asili ya Shetani. Ndiposa kuna kitu Paulo hukiita utu wa kale, pia tabia za mwilini ama mwili huu wa tamaa ama tamaa za mwili. Ndiposa suluhu hutajwa ni kuokoka, ili uwe au uusulubishe mwili wako pamoja na Kristo pale msalabani. Waruni 5-8, na Wagalatia 5 inatusaidia sana katika hili.
Paulo anatufundisha sana kuwa, Yesu alipokuwa anakufa, aliufia mwili wa dhambi. Yaani mauti yake, ilikuwa inauwa asili ya Shetani katika miili yetu; japo kwa lugha ya Kibiblia neno nguvu ya mauti, au utawala wa mauti katika miili yetu linaonekana kutumika zaidi. Kwa lugha nyingine tunasema mfumo wa dhambi. Lile andiko la tulio wa Kristo hatutendi dhambi (1 Yohana 3:6, 8, 9; "ukisoma utakuna na neno mbegu, tafakari kwa kina neno hilo" wa 10, 'unakupa matokeo:') maana yake, tuliookoka hatupo au hatutawaliwi na mfumo au utawala wa dhambi. Ikimaanisha nguvu ya mauti, au mauti twajua ni nguvu ya Shetani kupenyeza dhambi.
Soma; Waebrania 2:14 Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,
15 awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.
Oanisha Na..Warumi 5:14 walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja.
15 Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
17 Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo.
Unapoooka, unausulubisha mwili wa dhambi, na kuufanya mwili wa utakatifu kuhuiishwa kwako. Yesu alipokufa alikuwa akiusulubisha, na alipofufuka alikuwa akiufufua mwili wa utakatifu. (Uliuawa pale Edeni na mauti waliyoikaribisha).
Tazama; Warumi 6:1 Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?
2 Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?
3 Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
4 Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.
5 Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;
6 mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;
7 kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.
8 Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye; Zaidi soma kitabu chetu cha YESU KAMA NEEMA NA KWELI, na kile cha NAFASI YA MWILI AU VIUNGO VYA MWANADAMU KATIKA UFALME WA MBINGUNI sanjari na cha ZIJUE NA UZISHINDE ROHO ZA KABURI NA MAUTI.)
Kwa nini ninakujuza haya yote? Tena nikitokea katika kona ya Yesu wakati mada ni Roho Mtakatifu. Ukisoma kitabu chetu cha NAFASI YA ROHO MTAKATIFU KATIKA MAISHA YETU, utakutana na swali au mada ya Sababu za Yesu Kuja, Ndipo Roho Mtakatifu Aje.
Ni muhimu kufahamu ya kuwa, zipo sababu za msingi zilizomfanya Roho Mtakatifu asije, kabla ya Yesu kuja. Alikadhalika, zipo za msingi sana, ambazo zinakutaka wewe kuokoka kwanza, ndipo uweze kujazwa Roho Mtakatifu.
Kwa kifupi ni kwamba dhambi iliondoa makao ya Roho Mtakatifu, sii ndani yetu tu, au sii ulimwenguni tu; bali hata ndani yetu. Kabla ya dhambi, tuna muona huyu Roho akiwa duniani, akitajwa juu ya vilindi vya maji. Na kama dhambi ndiyo iliyomuondoa, sasa ili makao yake yajengwe au yawepo, ni lazima kuwe na ondoleo la dhambi. Damu ya Yesu hufanya hiyo kazi, ni Mathayo 26:28, Luka 22:20 na Waebrani 19:22-25.
Sasa, unapookoka, unajiweka safi, unasafishwa kwa ile Damu ya Yesu. Kuna kuwa na ondoleo la dhambi. Lakini pili, unakuwa umeusulubisha mwili wa dhambi, au mwili wenye vinasaba vya Shetani. Na kutwaa mwili wa utukufu, wenye vinasaba vya uzima wa milele; kwa maana ya kuachana na ule wenye vinasaba vya mauti. Maana ndivyo walivyoambiwa pale Edeni; ya kwamba mkila mtakufa hakika.
Mwili huo wa uzima, ndio unaokuwezesha sasa, kufanyika hekalu la Roho Mtakatifu. Kumbuka sana au fahamu sana ya kuwa, huyu Roho, makao yake ni katika miili yetu.
Na kama ndivyo basi, ni wazi kabisa hawezi kukaa kwenye mwili wenye kumilikiwa na Shetani. Mwili ambao bado unatawaliwa na mauti au nguvu za dhambi ambazo ni mauti. Yaani mwili ambao upo chini ya mfumo wa dhambi. Paulo hutuambia, mwili ambao ni utu wa kale. Moja, ni kwa sababu ni mchafu, pili ni miliki ya mungu aitwaye shetani, au wa dunia hii. Na tatu hakuna makao yake. Hana makaazi hapo. Maana dhambi imemuondoa.
Nikikuliza taja sababu tatu za Roho Mtakatifu kutokukaa kwenye mwili wa mtu ambaye hajaokoka; je, utaweza kuzitaja?
Kumbuka Yesu, ndiye aliyetujuza kanuni hii muhimu, na alituambia wazi ya kuwa: ukimkubali, ndipo wanakuja (Utatu Mtakatifu wa Mungu) na kisha kufanya makao kwako. Tazama, hii ni ili ikupe kuhakikisha: moja kama hujaokoka unaokoka, na aliyeokoka anatunza huo wokovu. Hakiki sasa; Yohana 14:23 Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. . (Katika mstari wa 25, anaanza mada ya Roho Mtakatifu).
Jibu moja muhimu la kufahamu hapa ni kwamba, kila aliyeokoka kujazwa Roho Mtakatifu ni haki yake ya msingi kabisa. Na pili yake, au upande mwingine wa shilingi, ni kwamba kama hujaokoka; huwezi kunufaika ipasavyo na Roho Mtakatifu. Maana hata nyumba, haijengwi hewani, lazima kuwe na mazingira sahihi kwanza. Na ndivyo ilivyo kwako wewe inapofika swala hili.
Sasa, ukija kwenye Wagalatia 5, utakutana na utendaji wa Roho Mtakatifu katika kukubadilisha kitabia. Awali yanatajwa matendo mabaya, matendo ya mwili wa dhambi. Matendo ya mtu anayetawaliwa na mfumo wa dhambi. Kisha mara baada ya hapo, ndipo yanakuja matendo mema. Tabia njema, ambapo kwa lugha nyingine huziita Tunda la Roho Mtakatifu. (Tuna kitabu cha TUNDA LA ROHO, kitafute.)
Mbele yake, anakuja kutukumbusha utendaji huu muhimu wa kuusulubisha mwili yaani kupambana na mfumo wa dhambi wa Shetani na utu wa kale, na kuweka makao ya Roho Mtakatifu ndani yetu. Kwa hiyo, wokovu na kubadilishwa kitabia huenda pamoja.
Tazama sasa hayo maandiko tajwa hapo, kumbuka yamegawanyika sehemu kuu tatu. Moja ni ya mtu anayetawaliwa na mfumo wa dhambi, yaani matendo ya mwilini. Pili ni mtu aliyeokoka na kupewa utu mpya anayestahili sasa kupewa tabia za Roho Mtakatifu, katika mwili wake. Na tatu tunakumbushwa umuhimu wa hayo matendo mema upo katika kuisulubisha miili yetu, yaani katika wokovu.
Soma sasa rasmi; Wagalatia 5:16 Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
18 Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,
21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
24 Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
25 Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
Sasa, ninakutia moyo kumuamini Roho Mtakatifu inapofika swala la kuhitaji badiliko la kitabia. Kama huna uvumilivu, huna upole wala kiasi, ama upendo na kadhalika: usife moyo. Wewe muombe naye atakupatia. Atakupa tu maana ni wajibu wake, ni sehemu ya majukumu au utendaji wake ndani yako.
Inawezekana sio kwako, ila ni kwa mume wako, au mke wako. Mtoto, ama kiongozi mwenzako. Nakutia moyo kuhakikisha ya kuwa, unamuombea, wala usikate tamaa. Wewe, muamini tu Roho Mtakatifu ya kuwa yupo kazini na Mungu atamponya, ama atakutana tu na hiyo haja ya moyo wako.
Kubwa zaidi usimkatie Roho Mtakatifu tamaa. Paulo mtume aliyekuwa muuaji, na mtesaji mkuu wa kanisa, kama iliwezekana kwake kubadilishwa, basi inawezekana na kwa huyo unayemuombea. Hata kama hajaokoka, bado kuna namna Roho Mtakatifu anaweza kung'oa baadhi ya tabia mbaya na za kikatili au za kidhalimu ndani yake.
Kitabu Kikitoka Tafadhali Kitafute.
Zaidi Endelea Kutembelea:
https://ukombozigospel.blogspot.com/?m=1
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni