Jumanne, 29 Aprili 2025

Pasaka ya Kweli: UKOMBOZI SAHIHI KATIKA MSAMAHA WA DHAMBI.

 Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya cha MOTO WA UAMSHO KATIKA BIBLIA. Ni kitabu kinachochambua kila Tukio la KiUamsho Ndani ya Biblia nzima.

Na Mwl Oscar Samba 

 Kitabu cha Kutoka. Sura ya 12 ...

Somo la...... UKOMBOZI KWA NJIA YA DAMU: Kristo Yesu Ndiye Pasaka.

1 Wakorintho 5:7 Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;

8 basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli. 

Tunajulishwa ya kuwa Kristo ndiye Pasaka wetu, na ili kumuenzi au kuyaishi maisha yake basi tunapaswa kuwa na mwenendo au moyo safi ama weupe wa moyo. Tuifanye karamu hii katika hali au kusudio lililokusudiwa pale msalabani ambalo ni la ukombozi wa kutoka dhambini. Tumaanishe katika wokovu, kwa lugha nyingine Ukristo sio dini tu, bali kunabeba maana pana ya kuyaishi yale aliyoyaishi Yesu Kristo. 

Kuyaacha mambo ya kale, maisha ya Misri yako, maisha yenye michanganyiko na chachu za dhambi, uzinzi, masengenyo, biashara za magendo na kadhalika. Ukristo ni Kuokoka, hakuna utofauti kati ya wokovu na Ukristo. Anayejiita Mkristo na hajaokoka huyo ni mpagani mwenye dini. Lazima uiondoe chachu inayokufanya kuwa donge lisilofaa, uwe na maisha safi, maisha bila chachu.

Miongoni mwa imizo kubwa la Mungu katika siku hii ya Pasaka kule Misri ilikuwa ni kula mikate isiyotiwa chachu kwa muda uliopangwa. Lengo lilikuwa ni mkazo wa kiroho katika picha ya maisha ya wokovu, ambapo ni maisha bila mawaa. Sijui unakisoma kitabu hiki ukiwa wapi, na ni lipi dhehebu lako; na inawezekana linasherekea na Pasaka, na yamkini huamini kuhusu wokovu! Pole ni nyingi kwako, maana karamu hiyo unaifanya kwa hasara. Paulo anatutaka kuifanya kwa faida. Bila chachu ndani yake; 1 Wakorintho 5:8 basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli. 

Kuokoka sio dini na makubaliano ya watu fulani, bali wokovu ndio ajenda na mpango mkuu wa Mungu kwa mwanadamu. 

Pasaka ya kwanza kule Misri ilibeba mantiki kamili ya wokovu. Sio tukio la siku ya siku kuu, inakuwa sherehe kwa sababu walikombolewa kutoka katika utumwa wa Wamisri. Na kwako au kwetu hivi leo, lazima iwe sherehe kwa sababu tumekombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi. Sasa kama bado ni mlevi, mshirikina, mchawi na mzinzi; huna haja ya kujiita Mkristo na wala sio kuisherekea tu Pasaka, bali hata kujivunia Yesu. Ni sawa na kukisifia chakula ambacho hata kukila huwezi kukila kutokana na kuzuiliwa na dakitari maana afya yako hairuhusu. (Utumwa wa dhambi, unakuzuilia kuufurahia uhuru wa kutoka Misri ya Shetani yaani Wokovu yaani Ukristo wa kweli.)

Ukristo ni wokovu, huwezi kuvitenganisha. Ni sawa na maji na damu, ukivitoa kwenye mwili; hakuna uhai tena. Ukombozi wa Yesu msalabani ndio huitwa Pasaka. Na alitukomboa ili tutoke dhambini. Sio ili tusalie dhambini, na tuendelee kukombolewa. Au tuendelee kusubiria kukamilishwa kwa ukombozi huo. La! Sivyo kabisa.

Maana kuna watu wapo kwenye dini kana kwamba ukombozi wa dhambi ni mchakato unaoendelea kwenye maisha yao. Uwokovu ni mara moja. Ukiwa ndani ya Kristo unatarajiwa kuwa kiumbe kipya, unageuzwa mara moja. Chachu haitakiwi kuonekana tena kwako.

Tazama; 2 Wakorintho 5:17 Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. 

Kwa nini hatuhitaji kukombolewa tena kwa jinsi ya msamaha wa dhambi, ni kwa sababu kuokoka ni kuhamishwa kutoka katika nguvu za giza na kuingizwa katika Ufalme wa Mungu. Aliyehamishwa, hayupo tena katika ng'ambo ya kale. Wana wa Israeli walipotoka Misri, hakuna namna wangeweza kutolewa tena Misri, maana hawapo huko. Kwa hiyo, wanaosubiria ukombozi au ambao kwao ukombozi wa dhambi unaendelea, ni wazi kuwa bado hawajakombolewa.

Tazama hapa, ili uone kile ambacho hutokea mtu anapookoka; Wakolosai 1:13 Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; 

14 ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; 

15 naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 

19 Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; (For it pleased the Father that in him should all fulness dwell).

Ukiweza unaweza kutwaa muda wako na kukisoma kifungu hiki kwa upana na uwazi zaidi. Lakini nilitaka ujionee hapo hii dhima ya ukombozi wa milele au wakudumu katika eneo la msamaha wa dhambi. ( Najua baada ya kuokoka, kuna weza kukawa na changamoto kama za kiafya na baadhi ya shida kama za uchumi kusalia katika maisha, hizi tunazidi kuomba na kumshinda adui. Maswala ya kuendelea kupambana na baadhi ya changamoto hayo ni muendelezo wa mapambano ya vita vya kiroho. Sisemei hayo.) Badala yake ninanena ukombozi kutoka katika vifungo na minyororo au utumwa wa dhambi, hususani katika eneo la msamaha wa dhambi. 

Unapookoka, unasamehewa vyote, Mungu anakusamehe na hakumbuki tena. Ndicho kinachonenwa katika hayo maandiko niliyokupa hapo juu. Kuna maneno msamaha wa dhambi hapo. 

Ngoja nikufafanuliye ni kwa nini ninayasema haya; kuna watu wa dini fulani, wanaamini maombi baada ya kufa. Kwao, ukristo sio ukamilifu. Bali ukifa, kuna mahali unaenda, na kuna maombi unaweza kuombewa, ili utakaswe utoke katika eneo hilo la mateso na kuingia paradiso au mbinguni. Ukifa na ukazikwa na misa au ibada takatifu; unaenda mbinguni. Waliopo duniani wanaweza kutoa sadaka, na maombi na wewe ukabadilishiwa adhabu (toharani) na kupokea msamaha wa dhambi.

Kwa watu kama hawa, ukombozi haufanywi au haukamiliki; wanapoamini. Bali ni mchakato unaendelea baada ya kuamini kwao. Kitu ambacho sii kibiblia, ni kinyume kabisa na fundisho la kweli kuhusu Ukristo na msamaha wa dhambi. Ndio maana wakajikuta wakilazimika kuutofautisha Ukristo na Uwokovu. Vitu ambavyo haviwezi kutofautishwa. Ni kitu kimoja, maana uwokovu ndio mlango unaokuingiza kwenye Ukristo. Huwezi kuwa mfuasi wa Kristo kama hujakombolewa kutoka katika dhambi.

Watu ambao hawakukombolewa na damu ya Pasaka kule Misri, hawakuweza kuianza safari ya kuelekea Kanani. Badala yake waliishi kwenye nyumba zenye misiba ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama, hadi binadamu.

 Nakutaka kuwa makini usikute nawe ni miongoni mwa wale waliopo kwenye nyumba za Kimisri na zenye misiba mbalimbali; alafu umejipa jina la Ukristo. Kisa tu, dini yako inamtaja Yesu, na umetwishwa fikra zisizo sahihi za kuendelea kukombolewa, au kuutazamia ukombozi. Waliosamehewa na Yesu, wamesamehewa. Hawahitaji kusamehewa tena, hakuna ukombozi juu ya ukombozi. 

Fundisho la ukombozi juu ya ukombozi, linawafanya wadhambi (wanaoishi katika mfumo wa dhambi) kuendelea kujipa moyo na maisha ya dhambi, na kutokuyachukia maana fikra zao zimepumbazika ya kwamba, bado wanalotumaini la kutubu au kusafishwa. Wamesahau ya kuwa wakati wa uwokovu ni sasa. Na Waebrani 9:27 inatuambia mara baada ya kifo ni hukumu. Wala sio sala za marehemu tena. 

Na ukitaka kuamini, hakuna mahali kwenye Biblia mtu yeyote anakufa, alafu anaenda kuombewa ili asamehewe dhambi zake. Hakuna! Sasa kama Biblia haina hicho kielelezo, wewe unakubalije uongo wa namna hii ukutawale? 

Wanaosingizia tukio la wale wakina Mariamu kuliendea kaburi la Yesu mara baada ya kifo na maziko, hawaelewi sana wanachokisema. Kama ni msomaji wa Biblia mzuri, utaelewa ya kuwa lile lilikuwa ni tukio la utamaduni wa Kiyahudi, ya kwamba mtu akishakufa, kuna namna wanaenda kuupaka mwili wake marashi/mariamu au mafuta ama viungo vya kimarashi. 

Sio ibada, haikuwa ibada ile. Ndiposa, hakuna swala lolote la kiibada likitajwa. Ni makosa kuhusianisha tukio hilo kama la kiibada. Mfano maziko ya Yesu na Lazaro katika kaburi lisilofukiwa na udongo, yaani lenye kufunikwa na mfuniko wa jiwe kama pango; ilivyokuwa ni utamaduni na sio kwamba ndivyo maziko ya Kibiblia yanapaswa kuwa. Ni makosa akatokea mtu na fundisho la kuzika kwa namna ile. Atakuwa anapotoka na anafundisha imani isiyo sahihi.

Imizo kubwa katika somo hili ni ukombozi wa kweli, yaani Wokovu. Katika maisha safi yasiyo na chachu. 

Musa anatujuza jambo muhimu hapa, nasi tunazidi kupata ufunuo ya kuwa, watu walio okoka; malango yao ya maisha yanalindwa kwa Damu ya Yesu ya Pasaka. Damu hiyo imo malangoni hata sasa. Ndio maana wachawi na waganga hawawezi waliokoka.

Tazama; Kutoka 12:21 Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka. 

22 Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi.

23 Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi.

24 Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele.

Kwa hiyo, ukimuona mtu anajiita Mkristo; huku akiwa na njia nyingine, uwe na hakika ya kwamba huyo Wokovu haupo kwake. Hawezi kuwa Mkristo mwenye hirizi kiunoni, ambaye juu ya mlango wake kuna kasha la konokono, kwenye "geti" lake au lango lake la nyumba kuna pembe ya mnyama imening'inizwa au kuna dawa ya mganga iliyochimbiwa shambani kwake ama chini ya mlango. Walio kwa Yesu, wanalindwa na Damu ya Mwanakondoo iliyomwagika msalabani. Hawategemei damu za kafara za mbuzi na zenye maelekezo ya kishirikina. 

Ndio maana nikakufunulia kweli yote na kile kinachomaanishwa kuhusu Pasaka ya kweli kibiblia ili uweze kujifanyia tadhimini mwenyewe. 

Yamkini umeusikia ujumbe huu, na unataka kuokoka sasa. Unahitaji ukombozi wa kweli, nikutie moyo na kukupongeza ya kuwa; umefikiri na kuamua vyema kabisa. Nenda miongoni mwa kurasa za nyuma ya kitabu hiki uifuatishe Sala ya Toba hapo, nawe utaokoka. Kisha uanze sasa kuishi maisha ya wokovu, ili uweze kunufaika na Pasaka ya Kweli Maishani Mwako. (Yaani, Masamaha ya Dhambi.)

Sala ya Toba

Sema; MUNGU BABA, MIMI NI MWENYE DHAMBI, NINAKUJA MBELE ZAKO. NIKIKUOMBA UNISAMEHE DHAMBI ZOTE, NISAFISHE KWA DAMU YAKO YA PASAKA: Amen.

Hongera kwa kuokoka, tafuta kanisa la watu walio okoka ukasali hapo. Wokovu sio dini mpya, wala usiogope kubadili dhehebu, bali wokovu ni kuanza maisha mapya na Yesu. Ni vyema ukaamua kuishi na watu waliokwisha amua kuishi na Yesu Kiusahihi Zaidi Toka Zamani. 

Asante na ujitambulishe hapo ya kuwa umeokoka hivi karibuni ili wakusaidie zaidi.

Tafadhali Kitabu Kikitoka Kisome

Zaidi Endelea Kutembelea: https://ukombozigospel.blogspot.com/?m=1

Fuata pia Channel Yetu ya WhatsApp 

https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni