Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya cha MOTO WA UAMSHO KATIKA BIBLIA. Katika Pointi ya Pambano la Nguvu (Ni kitabu kinachogusa Matukio na Mambo Muhimu Katika, Biblia Nzuma.)
Na Mwl Oscar Samba
Kitabu cha Kutoka. Sura ya 7:..
Somo la .... : PAMBANO LA NGUVU; Pigano la Ushindi Dhidi ya Wakala au Mwakilishi ama Mjumbe wa Ibilisi yaani mfalme wa Ufalme wa Giza.
Ni wasaa mwingine mzuri, tunaendelea kujifunza kuhusu Moto wa Uamsho Ndani ya Biblia. Kama nilivyokujuza hapo awali kuhusu pambano la nguvu dhidi ya ufalme wa giza kwa Musa, basi sasa nawiwa kukupanulia swala hili kiupana zaidi. Hapa tutatazama hadi tukio la namna hii la Paulo mtume dhidi ya yule mchawi, pamoja na Daudi na Goliathi. Karibu:
Musa na Fimbo ya Haruni kwa Farao
Mungu alimpatia Musa ishara ya fimbo yenye kugeuka nyoka. Fimbo huwakilisha mamlaka, utawala, uchungaji, pigo na hata heshima kwa mtu wa aina fulani. Mfano, kuna makabila ambayo kijana akifikia umri fulani hukabidhiwa fimbo, au huruhusiwa kutembea na fimbo. Rungu na fimbo, huwa na muktadha unaofanana sana kwa baadhi ya jamii. Kumbuka pia fimbo ni silaha ya ulinzi, makabila yenye utamaduni wa ufugaji, au kuishi porini hili wanalifahamu sana. Pia fimbo, ni ishara ya kuwa nipo tayari kwa safari. Jamii za kale zililijua sana hili; ndiposa katika Kutoka 12 wana wa Israeli walipaswa kula nyama ya Pasaka wakiwa na fimbo mikononi mwao. Ili nini? Ilikuwa ni sehemu ya ishara kwao ya kuwa, wamekaa mkao wa kisafari. Viatu miguuni, mshipi kiunoni, viliwakilisha pia.
Inapogeuka na kuwa nyoka, ni swala la ishara yenye miujiza ndani yake. (Ishara ni kiwakilishi, maana yake ni kwamba, ukiona alama au jambo hili, fahamu kuna hiki nyuma yake. Kuna alama mtu akiionyesha maana yake ni kwaheri au anakuaga. Nyingine ni anakuita, au anakwambia subiri. Alikadhalika, kuna vitu kama ishara vikitokea, hukujulisha kuwa Mungu yupo hapa. Ama ni MUNGU mkuu ndiye aliyelifa ya hili, na kadhalika.)
Ukikumbuka vyema somo lililopita, utafahamu ya kuwa; nilikuimiza ya kwamba, somo hili la Pambano la Nguvu, linanuia sana kukusaidia kuwa na vita vyenye ushindi dhidi ya ulimwengu wa roho. Usipojifunza kupigana, hakika kuna mahali hutaenda. Paulo mtume aliwahi kukiri ya kwamba, kuna sehemu alitaka kwenda; Shetani akamzuia!
Paulo alikuwa muungwana sana, kiasi cha kukiri ya kuwa Shetani alimzidi maarifa na nguvu na akafanikiwa kumzuilia kuliendea kusudi la Bwana. Ashukuriwe Mungu, awamu nyingine alikuja kupata mpenyo na kuwaendea watu hao tena.
Sasa, somo hili hapa halilengi tu kushinda vita, bali moja kwa moja limejikita (specificied) katika vita dhidi ya wakal fulani katika eneo lako, au utumishi. Huyu ni wakala au muwakilishi, au mpiganaji ama balozi wa kambi pinzani yaani Shetani.
Ni muhimu kumtaka Bwana akufundishe vita, hutakaa upanue mipaka ya huduma yako, na kuondoa vizingiti ulivyosemewa yakuwa hutazidi hapa; kama hutaamua kupanua mipaka kwa maombi ya vita. Kama hupigani vita, utasalia pale pale. Kuna watu wanakuzunguka, kumbe wao ni mipaka ya kutokupanuka kwako.
Daudi alilijua hili; Zaburi 144:1 Na ahimidiwe BWANA, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana.
Zaburi 18:32 Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu. (Mshipi huwakilisha Kweli Kiunoni, na Kweli ni Neno la Mungu). Na Kiuno Huwakilisha Moyo. Katika 1 Wafalme 19, anaposema Elia akakaza kiuno, maana yake akajipa moyo au akajitia nguvu nafsini mwake.) Kwa hiyo, hiyo Zaburi humaanisha ya kuwa, Mungu humpatia neno moyoni mwake.
33 Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. (Wepesi wa vita).
Ni wapendwa wa chache sana, utakaowakuta wakifunga na kuomba, wakimtaka Mungu awafundishe vita. Sii wengi wanaodiriki kufanya jambo hili kama sehemu ya hitajio lao la maombi.
34 Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba.
Mchawi, mganga, mtu yeyote anayesimama katika upande wa kukupinga; huyo ndiye huyu wakala au mjumbe wa ufalme wa giza. Usifike mahali pa kujisemea mbona huyu ananipinga sana, anapingana na kila jambo jema kwangu, amefikia hatua ya kutokunisalimia au kuninunia bila sababu, na sijui nimememkosea nini?
Ulichomkosea ni wewe kuamua kuokoka, kukubali kuwa mwakilishi wa ufalme wa mbinguni, hilo ndilo kosa. Unajua, unapokuwa kazini, au kwenye eneo lako la biashara kama mtu aliyeokoka wewe ni kijinga cha moto! Wewe ni taa inayowaka, iliyoko juu ya kiango au sehemu iliyoinuka. Na nuru yako inaangaza.
Unaweza usijijue, ila ufalme wa giza unakujua zaidi. Ndiposa hata wakiwa na mazungumzo yasiyofaa, wakikuona tu, wanaanza kubadilisha mazugumzo. Kwa nini? Kuna mlokole ameingia. Kuna mtu wa ufalme mwingine kaja. Kwa hiyo, kivyovyote mawakala wa adui, ni lazima wauwakilishe ufalme wao hapo.
Katika eneo fulani, kulikuwa na mchungaji mwenye kanisa akichunga, na katika mji huo kulikwepo na mganga wa kienyeji ambaye alikuwa maarufu sana. Watu wengi walikuwa wakienda kwake, pikipiki nyingi sana. Na huduma ya huyu Mchungaji ilikuwa imedorora.
Siku moja akasikia kukasirika moyoni, akaingia kwenye maombi ya siku 10. Mara baada ya hapo, mganga akahama, na kuamia eneo jingine katika mkoa mwingine. Kuanzia hapo sasa, kanisa na huduma ya huyu mchungaji ikaanza kuchanua. Watu wakaongezeka, utoaji wa sadaka uliokuwa umedorora ukaanza kuchanua. Na akaanza kujenga jengo la ghorofa. Tazama nini kilichokuwa kimezuia haho yote?
Utagundua kuwa, kuna mwenye mamlaka aliyekwepo katika eneo lake. Ambaye alikuwa na uwezo wa kuzuia hadi watu kuokoka, na sio kuokoka tu, alikamata hata utoaji wao. Alipoondoka, ndipo kanisa likaanza kustawi.
Yamkini mfano huu sio wa moja kwa moja, ila ukiugeuza una somo ndani yake. Katika Biblia tunajifunza kuhusu mpinga Kristo. Maandiko husema ya kuwa, amekwisha kuja, ila yupo azuiaye, ambaye ni kanisa. Sasa akinyakuliwa, huyu atatenda kazi waziwazi.
Sasa, katika upande mwingine ni kwamba, Shetani naye ni azuiaye, anao uwezo wa kuzuia kustawi kwa kanisa au huduma yako. Usipomuondoa, kamwe hutaweza kuwafungua watu walioshikiliwa mateka. Sasa, utajiuliza kama ninapambana na Shetani huyu mchawi, mganga au wakala wa Shetani kwa ni wa nini?
Kwani, Shetani huwa "anapambanaga" na Mungu, Yesu au na sisi? Anapoleta ajali, magongwa, mishale kama ya uzinzi kwa watumishi na kanisa; anamlenga nani?
Sasa kama ni sisi, wewe unapata uzito gani kupambana na mawakala wake ambao wengine ameamua kuwapadana makanisani hivi leo! Adui akifanikiwa kukufunga fimyra, kuna mahali utakwama tu.
Kuna namna tunayatumia na kuyaelewa vibaya maandiko yake ya kuombea mema adui zetu. Wapendwa wengi wamekataa kabisa kuitumia Zaburi ya 35, ni kana kwamba aliyeiandika hakuwa ameokoka vizuri. Hii yote ni hila za adui katika kutupumbaza kifikra. Yesu kumvumilia Yuda msaliti, au lile fundisho la kuacha magugu yamee na ngano! Vikitumika vibaya, vitatufanya kuendelea kuvumilia na kuabudu na wachawi, na mawakala wa kuzimu. Sifundishi kuwafukuza kwa kuwatamkia kanisani, maana kila jambo na hekima yake, ila kufanya maombi ya kupambana nao, kama Elia alivyofanya ni swala la lazima kabisa.
Tumuone Musa na Haruni: Kutoka 7:10 Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.
11 Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.
12 Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.
Ubishi uliishia hapo, hakuna namna wapinzani wake wangeweza kuendelea kujitutumua tena. Kama ni vita basi vinachukuwa sura mpya.
Fahamu: Najua huwezi kupigana na kila mtu katika eneo lako, au na yeyote anayekupinga. Ila ukiwa ni mtu wa Rohoni vizuri, ni lazima utajua huyu unapaswa kumshughulikia. Ule mfano wa yule mchungaji, kuna sehemu nimekwambia ya kuwa alijisikia vibaya. Unaposikia kukasirika, ni ishara ya kuwa hiyo ni hasira ya Roho Mtakatifu dhidi ya wakala huyo. Lakini pia, ni wajibu wako kuwa na maombi ya namna hii kimapambano kila siku. (Usipuzie). Hakuna mtumishi aliyewahi kufanikiwa bila kuvipiga vita.
Tusipopigana vita; hatuitendei haki mamlaka tuliyopewa. Ni sawa na askari mwenye rungu, na bunduki, alafu hatumii zana hizo. Badala yake anatengeneza urafiki na adui au majambazi.
Mamlaka tulizopewa, ni kwa ajili ya vita. Hatukupewa ili ijulikane tunazo. Na njia nzuri ya vita, ni kupambana na mawakala wa huu ufalme. Uwe na utamaduni wa kutangaza kupambana na mawakala wa Shetani katika kanisa au utumishi wako. Tangaza maombi ya kung'oa kila pando ambalo halikupandwa na Baba wa mbinguni (Mathayo 15:14). Pamoja na mizabibu mwitu. Bagua mbuzi katikati ya kondoo. (Usiingie mwili kuwabagua, wewe bagua tu katika maombi). Mungu katika kuyajibu, anayo hekima yanamna ya kutekeleza maombi hayo.
Kuna hatua na kuna mahali hutafika kama kwenye Melikebu unayoiendesha kuna wazamiaji haramu. Wakina Yona wanapaswa kushushwa. (Haya sio mafundisho ya imani nyingine, ila ni njia ya Kiroho kabisa katika kufika unapopaswa kufika.) Juya au nyavu za uvuvi huwa na tabia ya kuvua au kukusanya kila kitu, sasa ni wajibu wako kuondoa ambavyo havihitajiki.
Tumekuwa tukiabudu na wachawi makanisani kwa miaka au muda mwingi sana, imefikia hadi hatua watu wanaoa wachawi. Kisa ni binti tu wa kanisani. Kuna binti yetu mmoja aliwahi kuolewa na mchawi kabisa. Kisa kajifanya ameokoka, kumbe kahamia ili apate mke huko.
Binti anasema siku anaenda kwenye harusi, akapitiwa na kitu kama usingizi; akaliona joka kubwa sana kama chatu. Akafahamu Mungu anamsemesha kuhusu ndoa ijayo. Akampigia mchungaji wake, naye akamuonya kuwa hana amani na swala hilo ni ishara isiyo sahihi au salama.
Binti alikaza. Nadhani inatokana na imani ni mtu wa kanisani, na ni dhehebu moja nasi, na anahaminishiwa hivyo na mchungaji wake. Kumbe ni mchungaji aliyepoteza uwezo wa kung'amua haya maswala. Na hii hutokana na kutokuwa na utamaduni wa kufanya MAPAMBANO YA NGUVU katika huduma zetu.
Binti anasewa, ndipo alipohisi na kuona vitu kadhaa. Wala hapo mumewa hakuwa na hofu tena kumueleza. Sasa binti anawaza atorokeje, maana alikuja kugundua ni mtu hatari tena sana.
Siku moja, akiwa naye, akapita mama mjamzito. Huyo mumewe akamwambia kuwa, mimi ninashida na mtoto wa kumla nyama/damu alafu huyu mama kumbe ana mimba! Ngoja usiku ufike.
Kesho yake, huyu mke anasikia yule mama mimba imetoka! Ndipo anapokuja kugundua ya kuwa ni wazi huyu ni mtu hatari kwake. Akatoroka kisirisiri na kuondoka kabisa. Ndipo kanisa lake linakuja kuigundua siri hii!
Mwingine tena ni mchungaji aliyewahi kuoa mke mchawi. Natumai nafasi aliyoifikia baba huyu ni ya uangalizi katika dhehebu letu. Sasa, siku moja akaamua kuweka kwenye vitendo kile anachokisikia kwa kumtaka Mungu amdhibitishie. Ni kwamba, alisikia kwa muda Kuwa mke wake anatuhumiwa kuwa ni mchawi.
Akaazimia kuingia kwenye maombi ya siku tatu. Akiwa katika hayo maombi, akamuona mke wake usiku wa manane anatokea dirishani akiwa uchi. Ndipo alipomshika, na kumuuliza unaenda wapi? Mkewe akaanza kukiri na kumueleza kweli yote. Kumbe alimuoa akiwa mchawi; ni miongoni mwa wapendwa walioko makanisani walio wachawi. Jaribu kufikiri, kama mama mwangalizi wa kanisa hilo lenye jina la kuwa hai ni mchawi! Hilo kanisa linakuwa salama kweli?
Maana ni lazima ataaminika, na atakuwa na uwezo wa kuingia kwenye kila mfumo na kupanda cha kwake huko. Nasi twajua ya kuwa, wachacwi wengi walioko makanisani ni vinara katika utumishi! Karibia kila nafasi wapo, hata zile za usafi kanisani na kupamba madhabahu huwakosi! (Kwa bahati mbaya sana, kanisa leo; halitaki kusikia sana kuhusu maswala haya!) Na huu ndio mtaji mkubwa wa Shetani.
Kwa nini tunafika huku? Ni matokeo sii ya kupoa tu kiroho, bali ni kuzidiwa kimaarifa au kimbinu katika eneo la vita au mashambulio ya kiroho. Ukiona kunguru na njiwa wanakaa pamoja, ni tatizo la akili za njiwa. Wala sio kunguru. Ninao ujasiri wa kurudia tena na kusema ya kuwa; ukiona njiwa na kunguru wanakaa pamoja, basi akili za njiwa zimepumbazwa huku akili za kunguru zikiwa na werevu wa nyoka.
Ukiona swala na simba wanaishi pamoja, ni tatizo la ufahamu na akili za swala, na ni ushujaa wa kiwerevu kwa simba. Ukiona taa inawaka na giza bado lipo; uwe na hakika unapaswa kugombana na taa. Maana kama ingaliangaza vilivyo: giza lisingekwepo. Chui au mbwa akifanikiwa kuishi na kondoo pamoja; uwe na hakika kuna akili kapokonywa kondoo, na kuna werevu aliopewa chuo au mbwa huyo.
Yesu anasema huko njee wapo mbwa! Sasa, ukiona humu ndani ndimo walimo mbwa, kuna shida ipo mahali. Ninalofahamu, moto uliokaribia kuzima (wanaopikia kuni) ndipo paka au mbwa husogelea yale mafiga na kuja kuota. Kijijini kwetu, mkishapika na kuondoka mkaenda kulala, mtakuta mbwa au paka kaja kulala karibia na yale mafiga. Hata yule nungunungu mdogo, hasogelei makaa yenye moto mkali. (Yakionyesha kupoa kabisa, ndipo huyazima na mate yake na kuanza kuyala: maana hula makaa)
Lazima tukubali ya kuwa ni kupoa kiroho ndiko kunakoweza kutufikisha hapo. Ukiona mawakala wa kuzimu wanapewa hadi uongozi makanisani! Ni picha ya wazi ya akili kulogeka kiasi cha swala kuishi vizuri na chui. Kama kwenye kwaya kuna njiwa na kunguru, uwe na hakika kuna tatizo mahali. Maana kama tuna aina ya macho, yasiyoweza kutofautisha ndege hawa wawili; basi kuna kitu tumekipoteza.
Mapigo Kumi kwa Farao na Nchi Yote ya Misri.
Baada ya ishara ya fimbo ya nyoka, iliyokuja kumeza nyoka au nguvu au malaka zote za waganga wa Farao; ndipo yanakuja mapigo kumi.
Kwa hiyo, kama ni mapigo kumi, maana yake, kipimo cha dozi au adhabu kilichohitajika dhidi ya ufalme wa Farao ni hicho. Wanatheolojia wanasema ya kuwa, kila aina ya pigo, liliwakilisha miungu iliyokwepo Misri. Pigo la mvua ya mawe, ni dhidi ya mungu mvua. Maji kuwa damu ni mungu maji na kadhalika. Wanataja na majina ya hiyo miungu iliyokuwa ikiiabudiwa huko.
Sasa, ni kwa nini mapigo kwa hiyo miungu! miungu hiyo ndiyo iliyofanyika kama kizuizi kwa wana wa Israeli. Na ilibidi ipigwe ili wana wa Israeli waweze kutoka wakiwa salama. Bila hivyo hata wangelitoka, bado kamba za hii miungu zingewafuatilia tu.
Nasi twafahamu jinsi utawala wa miungu ya kigeni unavyodhofisha hali za kiroho za kanisa la Mungu wa kweli. Maana kupoa kwa kanisa, mara nyingi ni matokeo ya hii miungu au roho zinazotawala katika eneo fulani.
Kwani, hukuwahi kuona kanisa ambalo kila watumishi wanaoteleza au kuanguka kiroho ni dhambi fulani tu. Ama washirika wanaoanguka ni aina fulani ya dhambi. Uwe na hakika ndizo roho zinazotawala hilo eneo. Anga la hilo eneo lipo chini ya huyo mkuu mwenye hizo roho au tabia. Ezekieli 16, inazunguza bayana ya kuwa, asili ya yale makabila pale, ndiyo iliyofanyika baba na mama zao wana wa Israeli.
Tunafahamu kibaolojia baba na babu zao ni wakina Ibrahimu, Isaka na Yakobo, Sara, Rebeka na Lea au Raeli wakiwa ndio bibi na mama zao. Ila Mungu anayataja hayo makabila kama asili na wazazi wao! Maana yake hali ya kiroho ya hiyo miungu, imefanyika uridhi wa kihalali kitabia kwao; ndiposa wakajikuta hawafanani na asili ya wakina Ibrahimu; bali ni ile ya Wahiti na Waamori. Wakaabudu miungu kama wao.
Sasa, Mungu alinuia kuwadhibiti mapema, ili wasije wakaondoka na asili ya miungu ya Misri. Wana wa Lutu wale binti zake, waliondoka Sodoma sawa. Wakajikuta wanaiamishia Sodoma kule Soari kwa kulala na baba yao, walimlevia kisha kulala naye. Ndiposa, kila baada ya pigo; Mungu alipoona moyo wa Farao umelainika, alikuwa anafunua au anaachilia utawala au anaruhusu utendaji wa mungu mwingine. Naye akishampiga kwa pigo husika, moyo wa Farao unalainika tena, maana mwenye kuushikilia kashapigwa.
Ndiposa utaona ni kwa nini moyo wake ulikuwa unabadilika badilika. Biblia inatumia lugha ya Mungu kuufanya moyo wake kuwa mgumu tena. Kiuhalisia ni Mungu kuruhusu utendaji wa nira ya mungu mwingine kutenda kazi. Na ndiyo mahusiano ya mapigo na hali ya moyo wa Farao.
Tujionee maneno haya ya Mungu katika pigo la kumi yaani la mwisho. Mungu anasema ndipo atakapoipiga miungu ya Misri. Lakini tazama kwa makini kinachopigwa hapo! Ni mtoto wa kwanza wa kila mnyama na binadamu pia. Kwa nini? Katika ulimwengu wa roho, walichukuliwa kama ni sadaka au mali ya hiyo miungu. Na ndizo zilizokuwa nguvu zao za utendaji.
Tazama; Kutoka 12:12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA.
Swali kwako, je, katika eneo lako la biashara, ofisi ama huduma au unaloishi; kuna miungu gani inatawala hapo? Au kuna wakala gani wa kuzimu anayepingana na wewe ama na kile ulichobeba katika hilo eneo? Usipojifunza kumpiga, hutakaa utoke katika nchi ya Misri. Utaiona Kanani yako. Utasalia utumwani daima.
Na ishara ya kuwa upo utumwani ni mambo yako kutoka kwenda. Ni mambo yako kugoma kwenda. Kuwa mtu yule yule kila wakati. Kudumaa sio mpango wa Mungu. Lakini huwezi kumiliki au kuchanua ukiwa Misri. Lazima utoke, na huwezi kutoka kwa sababu hujakaa mkao wa vita. Na ni kwa sababu umeamua kuwa na maisha yenye kufanana na wale swala waliaoamua kuishi pamoja na simba, chui na kadhalika.
Paulo Dhidi ya Elimu Mchawi: Pigo la Upofu.
Wakati Paulo alipotambua ya kuwa yupo Liwali au kiongozi wa kiserikali anataka kuokoka; na akagundua yupo azuiaye, hakumuacha. Alishughulika naye moja kwa moja. Na mara baada ya pambano hilo la nguvu, ndipo wokovu ukapenya kwa liwali. Kumbe mtu mmoja, aliye mchawi, adui anaweza kumtumia kuzuia wengine kumjua Mungu!
Hapo, kijijini kwako, au eneo lako la kihuduma, ni wangapi wanaofanana na huyu mpizani, wanaozuia watu kumjua Mungu? Ni wangapi wanaozuilia wateja kuja kwako, na wanakuchafua kwa maneno ya kashifa nyingi tu? Ni lazima, ujifunze umuhimu wa kuwaadhibu, ni lazima kutumia pambano la nguvu, ili kupingana nao.
Tazama; Matendo ya Mitume 13:6 Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; 7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.
8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.
9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, Matendo ya Mitume 13:10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?
11 Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.
12 Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana. (Unapomuhubiria mtu, na kikundi cha watu kujaribu kumfuata ili kung'oa ulichopanda ndani yake, juwa hao ni wakina Elima; mshahara wao ni mmoja tu. Ni pigo la kinidhamu: nikimaanisha pambano la nguvu. Ni lazima uwadhibitishie kati yao na Mungu wako ni nani aliyemkubwa.)
Ukitazama huyo liwali, utakuta kuwa amekuja kuyaamini maandiko, mara baada ya pambano hili. Ukifeli eneo hili la pambano, utaishilia kupanda mbegu na adui kuja kung'oa usiku. Vita vya kiroho havina huruma, na unapaswa kuchagua moja; Elima asaliye na macho; alafu liwali arudi nyuma kiroho. Ama Elima mchawi apofuke, kijiji kizima kiokoke. Mume wa huyo mwanamke aliye okuokoka aendelee na ubabe alafu mkewe arudi nyuma kiroho, au ashughulikiwe na Bwana kisha mkewe asimame katika wokovu.
Mume mmoja akawa anamzulia mkewe kwenda katika maombi ya mkesha, mke wake akapeleka jina lake katika maombi. Siku moja akakutwa na ugonjwa mzito, ikabidi wamtake akaombewe kwenye mkesha. Akapelekwa na kuombewa hapo; toka siku hiyo akawa anampa mkewe ruhusa ya kwenda kwenye maombi ya mkesha. (Pambano la nguvu ni muhimu.) Sauli mpinzani wa injili alipookoka, ilikuwa ni pigo sana katika ufalme wa adui). Kusanya majina ya wakuu wa boma wanaozuia familia zao kuokoka, kisha achilia roho ya wokovu juu yao hao kwanza. Utashangaa wanakuwa wakwanza kuja kanisani. Na hata wasipookoka, hii roho ikiwa juu yao, watajikuta wanaupigia debe wokovu tu. Na wataimiza watu wao sana kwenda kanisani.
Ufalme wa mbinguni, ni swala la nguvu za kiroho. Ni jambo la pambano au mapambano ya kiroho, ni lazima kulijua hili. Tazama; Luka 16:16 Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.
Walegevu kamwe hawawezi kupata mpenyo wa kiroho. Ndio maana kuna hatari ya kuishilia kuwa kama kanisa la dini au kidini kama tusipopambazuka na kurudi katika maisha ya vita. Najua wapo wanaopambana, ila baadhi yetu tumebweteka sana. Uwokovu umejikuta ukiingiliwa na ustaarabu kama wa dini tulizotoka kabla ya kuokoka. Na tumeshaanza kuona hicho ndicho kiroho.
Maneno ya Yesu; Mathayo 11:12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.
13 Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana.
14 Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja. Kwa hiyo pia, alikuja akiwa na roho ile ile ya Elia ya mapambano ya kivita!
Pambano la Daudi Dhidi ya Goliathi: Jiwe na Kombeo na Kukatwa Kichwa kwa Goliathi.
Goliathi alijiinua dhidi ya taifa la Israeli, akalitukana na kuyatukana majeshi ya Bwana kwa muda wa simu 40. Na wewe sijui hapo kijijini au katika mtaa wako ni nani aliyeinuka na kulisema vibaya kanisa la Bwana. Goliathi wako katika biashara, au huduma yenu ni nani?
Uamsho mkubwa ulioletwa na Daudi katika Saweli ile ya kwanza 17 ulitokana na ushindi dhidi ya Goliathi. Walikuwa chini ya kipindi cha utumwa yaani kupoa kiroho au kutawaliwa kiroho kwa muda wa siku 40, Daudi kijana mdogo akasema inatosha sasa. Sijui kama wewe upo tayari kuwa Daudi wa dhehebu lako, kanisa au eneo lako unaloishi. Au umekubali na wewe kuendelea kunyanyaswa na huyo Goliathi wenu!
Kwa ujasiri akachukuwa jiwe zuri la mtoni/kivita, na kulitia katika kombeo. Akampiga Goliathi la kicwa na kumzimisha kabisa. Hapo ndipo alipokuja kupata mpenyo wa huduma yake. Kumbuka sura ya 16 inamuonyesha akiwa kwa Sauli na akimpigia kinubi, lakini ya 17 Sauli anadodosa huyo ni kijana wa nani, ni kana kwamba hamjui kabisa. Sasa, mara baada ya kumpiga Goliathi; hakuna namna Sauli aliweza kumsahau tena. Akamuinua na kumuweka juu ya jeshi au kikosi cha watu 1000.
Kumbe, kuna aina ya watu au falme ziking'ooka katika maisha yetu, ndipo tunaweza kuchanua na kutambulishwa katika ulimwengu! Sasa, usikubali kuendelea kumuacha Goliathi wenu kuwasumbua. (Hakuna jambo la kumshinda Mungu, muwe tu na moyo mkuu).
Ujasiri huu tunauhitaji; 1 Samweli 17:40 Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
42 Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri.
43 Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.
44 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni.
45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.
46 Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.
47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.
48 Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti.
49 Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi.
50 Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake.
51 Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.
Shindalo la Elia na Manabii wa Bahali (1 Wafalme 18)
Sijui ni watumishi gani wa imani ya uongo waliokuzunguka na wanakinzana na utumishi wako? Ninachofahamu sana ni kwamba, Elia aliondoka na vichwa vyao wle manabii wa Baali 400. Lazima ufalme wa miungu unaokuzunguka pamoja na hao wajumbe wake wahukumiwe, ndipo heshima ya Mungu wako iweze kuwepo. Nje ya hapo usitegemee mpenyo.
Heshima, sio kuwa na Mungu mwenye kuheshimiwa. Bali heshima huja pale, Mungu wako anapokushindia vita. Na Yeye anakuhitaji wewe uvae utayari wa vita. Hutegemea sana upiganaji wako. Ndiposa, fahamu na akili zako ni chombo muhimu sana katika haya mafanikio. Zikipumbazika kama zile za njiwa anayeishi na kunguru, uwe na hakika kuna siku kunguru atakupeleka kuja jalalani, na kwenye machinjio ya wanyama; mazingira ambayo njiwa hajaumbiwa kabisa. (Mtaji mkubwa wa adui kwa kanisa hivi leo; ni aina ya fikra tulizo nazo. Ndio maana Wachungaji waliokuwa wachawi kabla ya kuokoka, hata wakikaa katika madhehebu yetu, ni rahisi sana kupata mpenyo; maana wanautumia ulimwengu wa roho vizuri. Sisi tuliouzoelea wokovu, tunaona mambo ni marahisi na mepesi sana, hapana shaka inawezekana tumezurura sana na kunguru, kwa hiyo tumelishwa vya machinjioni. Ambavyo sii halali kwetu kuvila, kwa hiyo; tukajikuta tunawahurumia wanaotuudhi kwa kujiloga katika matumizi mabaya ya maandiko, tukijidanganya watabadilika. Tumesahau Isaya husema wabaya ni kama bahari iliyochafuka, na hakuna amani kutoka kwao; tena asema Bwana wa majeshi.)
Mchungaji mmoja akamwambia Mungu, kama huyu nabii/mtumishi anayetuzunguka hapa ni wa kwako akae, ila kama sii wa kwako aondoke. Haikupita muda, alifungasha kila kitu na kuondoka. Pambano kama hili ni muhimu.
Tazama kwa Elia; (Soma hiyo Wafalme wa kwanza 18, ukiweza pamoja na 2 Walme 1:1-14, Utamuona Elia alivyoshusha moto. Kumbuka hili pambano, ndilo lilompa kibali kwenda kwa mfalme. Moyo wa mfalme ulilainishwa hapa.)
Fahamu: Madhara moja wapo makubwa na hatari ya kukaa na wachawi au mawakala wa kuzimu makanisani ni hii. Huwa na tabia ya kutengeneza mtandao wa kichawi. Baada ya muda mchache tu, utashangaa hata watoto wa mchungaji na wazee wa kanisa ama washiria, nao ni sehemu ya huo mtandao. Wale washirika dhaifu, huunganishwa huko. Na kuja kuuvunja ni kazi kubwa sana. Lakini pia huwa na tabia ya kudhoofisha kazi ya Mungu.
Binti mmoja akasimulia nakusema ya kuwa, wakati wanafanya mkutano wa injili, wao walikuwa na kazi ya kuwarudisha nyuma kiroho wale waliokuwa wakiokoka. Yaani, nyie mnapambana watu waokoke, lakini mshirika mwenzenu ambaye ni kunguru au mbuzi kiroho; anang'angana kuwazuilia kusimama katika imani. Hawa hata mipango ya kanisa ya kiroho huwa wanapingana nayo sana kichawi.
Anasema pia, kazi yao kubwa ni kumwaga roho za usingizi makanisani. Kubana fahamu zao wasielewe neno, na kuleta uzito katika anga. Ugumu wa maisha, na mafarakano makanisani ama kumwaga roho za dhambi kama uzinzi na kuua moyo wa utumishi; ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. Kuna nyakati wanahusika hata na mauti za mwilini, kama vifo vya ghafula na ajali. Hata magonjwa sugu au yenye mateso.
Kwa hiyo, ni muhimu kujifunza kuwa na maombi ya vita dhidi ya mitandao ya kuzimu makanisani.
Ni njiwa tu waliologwa akili, ndio wanaodiriki kufika mahali pa kusema hatuwezi kukemea vivyo maana makanisani hakuna wachawi. Mawakala hawawezi kukaa huko. Huyu hapana shaka ni swala anayeweza kuishi vizuri na chui. Nasi twafahamu shida imeanzia wapi. Maana ukiweza kula anachokula au kunywa chui, ni lazima mtafanana tu.
Paulo na Sila Dhidi ya Kijakazi wa Mpunga Pepo: Misingi ya Mji Kutikiswa
Ni kweli kabisa kuna madhara kadha wa kadha huweza kujitokeza punde tu anapoamua kufanya pambano la nguvu. Na madhara moja wapo ni kama yale yaliyomkuta Paulo Mtume alipokuwa na Sila. Ndio maana ni muhimu kujifunza kufunga roho za malipizi, au za kisasi kutoka kwa adui Shetani. Maana sifa moja wapo ya mapambano ni kupigana, sasa katika kupigana adui huweza kukuotea na akakujerui.
Katika mji huu, kulikuwa na kijakazi wa mtu mmoja mshirikina. Ambapo alikuwa akimtumia ili kubashiria watu na kadhalika, alijipatia fedha kumpitia. Roho wa Bwana akawaka hasira ndani ya moyo wa Paulo Mtume na kumtoa huyo pepo. Mungu alinuia kuufungua huu mji, ndio maana akaanza pambano dhidi ya roho zinazotawala hilo eneo. (Ni sawa na pambano lile la Yesu na yule Mgelasi, mtu yule alikuwa ni wa Dekapoli. Sasa, Yesu alipomfungua, ni alikuwa anapambana na roho za ule mji. Alikamatiwa kwenye madhabahu za Wagelasi, zilizokuwa makaburini. Ndio maana mara baada ya tukio hilo, Yesu alifukuzwa na wakaazi wa huo mji. Maandiko husema kuwa, akaondoka mipakani mwao. Ulitegemea wangefurahia kichaa kupona, badala yake, wanamfumuza Yesu).
Ndicho kilichotokea kwa wakina Paulo na Sila; walijikuta wanafanyiwa gasia na watu wa mji ule. Na kuishilia gerezani; Matendo ya Mitume 16:16 Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.
17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.
18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.
19 Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;
20 wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;
22 Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.
23 Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.
Kwa wakina Paulo, kwenda kwao gerezani kulikuwa na faida pia. Kuna kitu kilikuwa kinatafutwa na Mu gu, kitu cha kiroho hapo.
Ukitaka kuamini faida yake, nenda katazame kitu kilichotokea mara baada ya Mungu kushuka. Ni misingi ya gereza kutimiswa. Sasa, tafuta maana ya misingi? Utafahamu ni mambo muhimu na vifungo muhimu au nguvu muhimu za utendaji wa ufalme wa giza, na kiserikali vya mji husika vilitimiswa. Gereza maana yake, ni eneo la adhabu dhidi ya wanaokiuka utendaji wa mamlaka husika ya mjinau eneo. Kwa hiyo, kuna namna mamlaka za mji ule zilikuwa zinatikiswa.
Kazi ilianzia kwa kinakazi, ikanidi imalizikie katika gereza. Tena katika misingi yake, ikiwakilisha misingi ya mamlaka husika. Ilikuwa sio misingi ya haki, ni misingi mibovu na pinzani dhidi ya injili. Ndio maana waliweza kuwakamata, na kuruhusu kupigwa fimbo kwa watu wasio na hatia na kuwaweka gerezani. Makadhi wanaotajwa hapo ni mahakimu, waamuzi. Kinachowafanya wasiwe wenye haki ni misingi yao.
Tazama; Matendo ya Mitume 16:26 Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.
Tazama Kinachotokea! Ni Uwokovu Kuingia Mjini. Ikupe Kufahamu ya Kuwa, Kuna Vitu Haviwezi Kutokea Katika Hilo Eno Lako la Kihuduma au Kibiashara; Hadi Umetikisa. Mpaka Patikiswe, Ona; 30 kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?
31 Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. 32 Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.
Kitabu Kikitoka Kitafute
Zaidi: Usiache Kuitembelea Blogu Yetu:
https://ukombozigospel.blogspot.com/?m=1
Karibu Ujiunge na Chaneli Yetu ya WhatsApp
https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni