Alhamisi, 1 Agosti 2019

NAMNA YA KUMJUA NABII WA KWELI NA WA UONGO.   Mwalimu Oscar Samba wa Ug Minisry.
Ujumbe huu ni sehemu ya kitabu changu cha Wito na huduma ya Nabii,
(a) WA UONGO:
1. Tazama Misingi yao ya Kihuduma, Hawana msingi wa neno, Hofu ya Mungu haipo pamoja nao, mambo muhimu ya kiroho kama Ubatizo, Toba ya dhambi, Ujazo wa Roho Mtakatifu, Msisitizo wa kudumu katika imani ya kweli, msisitizo katika maombi ya kufunga na kuomba katika Roho na Kweli, au matumizi ya jina la Yesu hayatakuwa yakitumika kama ilivyo amriwa, na kamwe hawezi kuitumia Damu ya Yesu.
Kumbuka hata akijifanya kujitahidi kubatiza, hataweza kutumia utatu mtakatifu au maji mengi, na kuwafunza watu wake katika Roho kuhusu huo ubatizo.
Mambo hayo yatazame sana katika huduma ambayo unaitilia shaka.
2. Chunguza Matunda yao, Yesu alituhusia na kutufahamisha kuwa tutawatambua kwa matunda yao, akibainisha kuwa mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, alikadhalika mti mbaya huzaa yaliyo mabaya.
Mathayo 7:15 Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?

17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
Kumbuka utumishi wao kuwa ni wa uongo ni mti au ni shina la mabaya, na matunda yake ni haya; hawawezi kukemea dhambi, hawafundishi kweli ya Mungu, mafundisho yao yamejawa na stori na hadithi zisizo na maana, yaani maneno ni mengi.
Hawana mwenendo mzuri katika jamii, na matunda mengine ya uovu utayaona hapo mbeleni, kama tamaa ya fedha na kadhalika.
3.Fahamu tabia zao, maana tuliambiwa na Kristo kuwa tutawatambau kwa mtunda yao, Mathayo 7:15-16.
(A) Tabia za Manabii wa Uongo:
(i). Hukinzana, au kupingana na kweli ya Mungu, Mfano Nabii mze kwenye 1 Wafalme 13, alipindua, ujumbe wa kweli kwa yule nabii wa Mungu kuwa asipite njia ile, wala kula au kunywa chochoye, akijidai nae ni mtumishi wa Mungu;
1 Wafalme 13: 17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.
Kumbuka hawa watumishi wa Ibilisi wamebeba au wanaongozwa na roho ile ya nyoka, iliyo mwambia Hawa ati! Ambayo ilipindua kweli, kwa kumwambia kuwa hakika hutakufa, huyu Mzee anaye alimwambia hivyo ivyo, akipindua ile kweli, lakini alikuja kufa, na Hawa na Mumewe, walikuja kuzama hatiani.
Hata kama anatumia Biblia, ukimuona anakinzana na kweli, kaa naye mbali.
(ii) Hutumia, Hila, Uongo, na Ujanja-ujanja mwingi au Hulagai, Ati ya nyoka, ilibeba hila, na kwenda kinyume na ukweli wa Mungu kuhusu kanuni ya mti ule wa ujuzi wa mema na mabaya;
2 Wakorintho 11:3 Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.
Mathayo 24:11 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.
24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.
Kwa hiyo uongo wao unalenga kuwapoteza watu, kama walivyompoteza mfalme Sedekia, kipindi kile cha Yeremia, walivyomdanganya mfame Ahabu kipindi kile cha nabii Mikaya, kisha kwenda kufa.
Kumbuka au fahamui uongo wao ni wa hila, yaani sio wa wazi-wazi, nyoka alitumia akili na werevu mwingi, maana hawezi kukutabiri kitu hewa, huyo atakuwa ni nabii wa uongo anayetumia akili zake, ila wa uongo anayetumiwa na Ibilisi, na mwenye roho ya uaguzi au pepo la utambuzi kutoka kuzimu, hotoa mambo ambayo huweza kutukia, au ni kama vile yatatukia, akijaribu kutumia hata maandiko, kwa hiyo kupima, kuna hitaji utulivu, na uwe mtu wa neno kweli, kweli, nyakati hizi mpendwa sio za kusoma na kufuatilia mahubiri jumapili kwa jumapili tu, ni hatari mno, bali fanya hivyo kila uchwao.
( Matendo 11:13 Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.
11:14 Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.)
2 Petro 2 :
2.1 Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.
(iii) Hufanya kazi kwa Masilahi Binafsi, yaweza kuwa ni fedha, kumuona ni pesa, kuhudumiwa naye ni pesa, ukiona hayo, juwa hiyo roho iliyo ndani yake, haitoki kwa Mungu, soma 2 Petro 1:2 yote;
2 Petro 2:3 Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.
Utaliona pia kwenye Tito na Yuda 1:11.
Pesa ni sehemu kubwa sana ya mahubiri yao, injili yao imegeuka kuwa roho ya “chuma ulete”.
Ezekieli 22:25 Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake.
Mika 3:11 Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea Bwana, na kusema, Je! Hayupo Bwana katikati yetu? Hapana neno baya lo lote litakalotufikia.
Lakini pia katika masilahi binafsi lipo swala la kutafuta ajenda binafsi au kibali au matakwa binafsi, hata cheo au heshima au ili kujipatia kitu fulani hapo.
Utaliona hili jambo kwa manabii wa uongo waliokuwa wakitumika chini ya himaya za wafalme, kwao walikuwa tayari kupotosha kweli, ili tu, uhai wao uwe salama, au wapate kula vinono, vya Ikulu, au mezani kwa mfalme.
Pamoja na hayo, huweza kuwa ni ili kufanikisha kitu fulani au kutumiwa na watu fulani, kwa kupewa ujira fulani, kama Baalam.
Mfano Sanbalati na Tobia, walikuwa ni maadui wa kazi ya Mungu wakati ule wa ujenzi wa ukuta kipindi cha kurudi kutoka uhamishoni chini ya Nehemia,  walimuajiri nabii mke aitwae Noadia na manabii wengine, ili kumtisha Nehemia, lakini janja yao ilibainika, kwa hiyo, walitoa ujumbe batili, wakiwa wameajiriwa, wala haukutoka juu;
Nehemia 6:12 Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.
13 Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.
(iii) Wana Ulimi wa Kujipendekeza, kwa hiyo hupenda kutamka amani amani, hata kama hakuna amani, hupenda kuwatamkia watu pokea baraka, hata kama hajatimiza kanuni, au hajalisikia na kuliamini Neno, muda wote ndimi zo zinanena maneno laini, ili wajipatie kibali kwa watu, wakijua unabii wao utawapatia mali au kufanya watu kutoa, au kuwakaribisha makwao, injili zao ni pokea tu, pokea, hawakemi dhambi, wala kutoa maonyo kwa wakosaji, utawasikia wamuonapo kiongozi, au mtu fulani kwenye jamii awezae kuwainua, au kuwapa kitu kidogo, wao ni kusifia tu na kubashiria mafanikio, hata ukiwa mkosaji, watakutamkia msamaha;
Yeremia 14: 13 Ndipo nikasema, Aa, Bwana, MUNGU! Tazama, manabii huwaambia, Hamtauona upanga, wala hamtakuwa na njaa; bali nitawapa amani iliyo thabiti mahali hapa.
14 Ndipo Bwana akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili,
na hadaa ya mioyo yao.
Tabia hii alikuwa nayo, Hanania, Yeremia 28:15 Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo.
(iv) Huwa na Injili au Mahubiri ya kushambulia Watumishi wa Kweli, Hufanya kazi ya kuwashambulia kwa maneno, na hata kwa fitina kwa watumishi wenza au viongozi wa kiserikali, fahamu hawa ni watumishi wa Ibilisi, kwa hiyo humsaidia baba yao kuifanya kazi ambayo yeye alipaswa kuifanya.
“Yaani mpinga Kristo au waeneza injili ya Kweli.”
Utawakuta wakiwasema vibaya, na kuwachafulia watumishi wa Mungu kazi zao au huduma zao, ufahamu hawakuanza leo, bali toka kipindi cha Biblia, walimfanyia pia hivyo Nabii Yeremia, wakijipanga kumpiga kwa ndimi, yaani maneno, kumsema vibaya na kumtumia mashutumu na laumu za uongo, tabia hii ukiiona, fahamu huyo mtumishi, anatumika, na fanya hima kumkimbia, utamkuta yeye kazi yake ni kusema tu vibaya wengine, utazani ndio kazi aliyoitiwa, haoni mema yao, bali hutafuta kasoro zao tu, mchana kutwa;
Yeremia 18:18 Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.
(v) Hubashiri kwa kukisia, kubahatisha, au kubuni, Ukiwakuta manabii wa uongo ambao hutumia sana akili zao, nikiwa na mantiki msaada wa mapepo ya uaguzi na utambuzi ni mdogo kwao, mara nyingi katika werevu wao,  hufanya kazi zao kwakumuangalia mtu, na kujaribu kumsoma saikolojia yake, alafu ndipo huanza kubuni matatizo yake au mambo yake.
Huweza kutazama mavazi yake, muonekano wake wa kiafya, na huweza kupata hisia au kubashiri hali inayomsumbua, nami ninakutaka kuwa ukikutana na mtumishi anayekwambia ninaona kama vile, una… yaani haneni kwa uhakika, fahamu huyo, ni kibaraka cha kuzimu, nawe ng’oa nanga mapema, kabla hajakuvua au kukunasa kwa ndoa ya hila za maneno yake huku akikutupia uvuli na upofu fikrani mwako kama ilivyo kwa hao wafuasi wake, ambao huwa tayari kumtetea hata katika upuzi na kumsifia huku wakisahau kuwa Utukufu na Hesima ni kwa Yesu pekee, (Ukimuona Nabiii anyependa sana kusifiwa hyo naye ni wa uongo).
Maana nabii wa kweli anakwambia, ninaona moja, mbili tatu, na huwa hivyo, huyu wa kuna kama vile, kama vile, kuna tatizo fulani, ni mjanja wa mjini.
 Maana Hutoa ya mioyoni mwao, au akilini mwao, (Ezekieli 13: 2 Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la Bwana;
3 Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!
4 Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa.)
(vi) Hakemei dhambi, Tunaliona jambo hili kwa manabii wa uongo kipindi cha Yeremia, na mfalme wa Yuda Sedekia, hawana ujasiri wa kukaripia, au kutabiri ili kuonya au kuzuilia uovu;
Maombolezo 2: 14 Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa.
Walio wa nyakati za leo, katika makanisa yao hawana ujasiri wa kukemea dhambi, hawatenge wala kukaripia adharani.
Na hata wakifanya hivyo kujaribu kuonya, huwa sio kwa kumaanisha, bali ni ili kuwafanya waliomaanisha, kutokuona kuwa wamepotea kiroho au hawapo mahali sahihi, yaani huwa ni mchezo wa maigizo ili kuweza kuwapata walio wema na wale wa ovu wenzao, bali sio katika roho na kweli.
(vii)…….
NB: Manabii wa Uongo ni waigizaji, wamevaa uhusika ambao sio wao, na ukikaa nao kwa ukaribu au ukibahatika kuwapeleleza, utabaini kilichopo moyoni mwao kuwa sio utumishi wa kweli, ukiyagundua hayo fanya hima na ukimbie hapo haraka.
Mfano, utajua kuwa kipaumbele chao kikubwa ni fedha, wala sio injili, ni kujitafutia utukufu na umaarufu wala sio kufanyika msaada wa kweli, maana hawaguswi na mahitaji ya watu, bali huguswa na fedha au mali za watu;
Mathayo 7:15 Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
(b) WA UKWELI:
(ii) Tabia za Kiroho za Nabii wa Kweli:
(i) Husema Kweli, Utaliona hili kwa habari za Yeremia, ambazo zilikuja kutukia kama zilivyonenwa, Mikaya nabii pia kile alichokinena machoni pa Ahabu mfalme kilikuja kutukia.
(ii) Hafanyi kwa kumfuraisha mtu au kutaka kujikomba ama kujipendekeza kwa mtu, wakati manbii wale wa Ahabu bandia wakijikomba kwake, Mikaya, alinena wazi wazi, na hata yule akida alivyomtaka kubadili msimamo alimkataliwa dhairi;
2 Nyakati 18: 12 Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema.
13 Mikaya akasema, Kama aishivyo Bwana, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena.
Ukijisomea habari za nabii Yeremia, utaona kuwa kuna wakati au nyakati kadhaa alikamatwa, ila akiwa chini ya ulinzi wao, alipohojiwa au kumkusanyikia, bado hakubadili msimamo, bali alinena aliyoyanena, lakini wa uongo, hubadili ubashiri ili kuwa salama.
(iii) Jumbe zao zina Uvuvio wa Roho Mtakatifu, nataka jambo hili liwe ndicho kipimo chako kikuu.
Uwepo wa Roho Mtakatifu, upo vinywani mwao, na maneno yao, yanabeba amani yake, na tumaini lake, na upako wake, au hakikisho lake.
Maana wanao ongozwa na Yeye ndio wana wake; Warumi 8:14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.
 Na mtu wa kiroho, hawezi kumsahau mwenzake, ni hatari kondoo akashindwa kutofautish kondoo mwenzake, na kujikuta akichangamana na mbuzi bila kujua, hata kama amejipaka rangi, na kuwa kama wao, kwani hata macho, na sauti yatakujulisha tu.
(iv) Humtetea Kristo, Kunapotokea hali yoyote inayotishia ustawi wa kanisa, hawawezi kunyamaza, na huwa hupande wa kweli kwa kunena waziwazi bila woga, tunaliona hili kwa Nabii Elia, alimtetea Mungu dhidi ya manabii wa Baali;
1 Wafalme 18:36 Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.

(v) Hatwai Utukufu wa Mungu, Nabii wa Kweli na anayetumika katika Roho na Kweli, au kwa kumaanisha, hatwai au ashiriki utukufu wa Mungu hata kidogo.
Akifanya jambo au mujiza ukitendeka katika mikono yake, hawezi kukubali yeye kupokea sifa, au kuchukuwa utukufu wa Mungu, maana anajua yeye ni mjoli au ni mtumishi tu wa Bwana, na hatafuti shauri lake bali ni la Bwana.
Ila ukimuona nabii anachuku utukufu, na kutafuta kusifiwa au kuonena kuwa yeye ana upako mkubwa, huyo ni wa hila, au ameshaachwa ama ataachwa na Mungu punde.
Tunajifunza sifa hii kwa nabii wa Kweli Elia, Mtishibi, baba huyu alitamka kuwa anafanya yale mbele ya manabii wa Bahali, ili watu wamjuwe Mungu wake, sio ili yeye apate kibali, au atambulike kama ilivyo watumishi wajanja- wajanja wa leo;
1 Wafalme 18:37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.
(vi) Ni Mlinzi wa Kiroho katika Kanisa, na Jamii yake, jukumu la ulinzi kiroho, lipo katika kuwa na macho ya kuona, kusimama kwenye nafasi, kama ilivyokuwa kwa nabii Habakuki, alipotangaza kukaa kwenye zamu, ndipo alipoletewa njozi yenye maono au hatima fulani ijayo, kisha kuihabarisha jamii husika, ili yamkini watubu, ili waweze kuwa salama dhidi ya pigo lijalo kama walivyofanya wakina Isaya, Yeremia, Ezekieli, Mikaya na wengine.
Na pili ni ili kusimama kama muombezi, Musa aliilinda jamii yake, mara kadha kupitia maombi, na nabii wa kweli, huwa na hili jukumu hata leo, kabla ya baya, hutoa ubashiri, ili watu wake yamkini watubu, au kuwataka waombaji kuomba, na yeye pia kuomba, ili kuzuilia baya lijalo, ama jamii hiyo kuwa na taadhari fulani.
Nabii asiyefanya hili jukumu, unabii wake una mashaka tena makubwa, na kama anafanya hivyo kwa makusudi, afahamu kuwa damu hiyo itakuwa juu yake, na kama hajui au hana uwezo wa kuona, huyo sio nabii, ama ameshakengeuka kwa hiyo Mungu amemuacha, jambo linaloyafanya macho yake ya kiroho kutokuona hatari ijayo.
(Ezekieli 3: 17 Mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.
18 Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
19 Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.)
(vii) Amebeba Majibu ya Kweli ya Watu wake, au Yako, hapa sineni habari za unabii utakao timia, hapana! Maana nabii wa uongo naye huweza kubahatisha au kunena jambo ambalo kweli likatukia, kupitia pepo la utambuzi, au uaguzi, ila hapa ninanena habari za mtu kupokea majibu yake ya kweli.
Nabii Yeremia, aliwapa watu wa Israei majibu yao yaliyolenga kusalimisha uhai wao, kuwa wakienda kwa Wakalidayo, huko watapona au wataziokoa nafsi, zao;
Yeremia 38:2 Bwana asema hivi, Akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atokaye kwenda kwa Wakaldayo ataishi, naye atapewa maisha yake yawe kama nyara, naye ataishi.
3 Bwana asema hivi, Bila shaka mji huu utatiwa katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, naye atautwaa.
Lakini pia alimpatia mfalme Sedekia majibu yake ya dhati, kuwa akitaka kuwa salama na ili Yerusalemu isiteketezwe, hana budi kuhakikisha kuwa, anakimbilia Babeli;
Yeremia 38: 17 Ndipo Yeremia akamwambia Sedekia, Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama ukitoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi nafsi yako utaishi, wala mji huu hautateketezwa; nawe utaishi na nyumba yako; 18 bali ukikataa kutoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi, mji huu utatiwa katika mikono ya Wakaldayo nao watauteketeza, hata na wewe hutajiepusha na mikono yao.
Unapokuwa chini yake, na kama ni wa kweli, utakuwa ukipokea majibu ya maisha yako, sio tabiri tu! Hapana, Ibilisi huweza kukutabiria matatizo yako, ila hataweza kukupa majibu au Suluhu la hayo matizo.
Huweza kukwambia, huna kazi, una maisha magumu, ila hawezi kukupati kazi, au kukupa amani kwenye ndoa, au kukupatanisha na watesi wako, na hata ikija kazi, haiwezi kuwa ya kudumu, bali hufanya ili kukuteka kiakili, bali wa kweli, hukupa majibu ya Mungu, ambayo huwa ni ya kudumu, na ya dhati.

Kama hujaokoka na unataka kuokoka ama ulirudi nyuma kiroho na unataka kutengeneza na BWANA kwa upya leo, tafadhali fuatisha nami maneno haya kwa Imani, Sema: BWANA YESU, NINAKUPENDA, NINAKIRI NA KUAMINI MOYONI MWANGU KUWA WEWE NI MUNGU, ULIKUFA NA KUFUFUKA KWA AJILI YANGU, INGIA NDANI YANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU LEO, AMENI.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo.

Na Huduma ya UKOMBOZI GOSPEL, Arusha Tanzania, Kwa Maombi, Ushauri, Maswali au Sadaka wasiliana nasi, Barua pepe: ukombozigospel@gmail.com  Simu: +255 759 859 287 pia waweza itumia kwa M-PESA. Zaidi www.ukombozigospel.blogspot.com  
Pia #Like #Penda Page/Ukurasa wetu au kundi la Fb, ili kupata habari hizi kwa haraka, zaidi. @ugukombozi Gospel
 PAGE: https://www.facebook.com/ugukombozigospel/
Kikundi: https://www.facebook.com/groups/2268418230050621/
Pia kwenye mtando Mpya wakitanzania wa
2 DAY SKY: https://www.2daysky.com/ukombozigospel
 Pia TAZAMA VIDEO ZETU HAPA  https://www.youtube.com/channel/UCv1tghnugOSpbmb5h6ebJtA  (Ukombozi Gospel)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni