Bwana Yesu aifiwe Mpendwa, leo tunageukia kitabu changu cha Wito na Huduma ya Uinjilisti, na tunaangazia kipengele kimoja;
MAMBO MUHIMU KATIKA UINJILISTI:
Na Mwalimu Oscar Samba, wa Ug Ministry.
Kumbuka mada hii inahusiana na utendaji, maana yake namna ya kufanya unapokuwa shambani, au namna ya kujindaa kwa ajili ya kuingia katika eneo la mavuno, wala hapa sineni habari za mfumo, au tabia za Mwinjilisti kama huko awali.
Mambo haya yatake sana kuyajua ili uwekeze nguvu kubwa hapo katika maandalizi, maombi na hata wakati unahubiri:
1. Watu Kumuamini Yesu, 2. Kumkiri, na 3. Kumpokea kama Bwana.
Warumi 10.9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.
1. Kuamini, jambo la Kwanza kabisa ni kuhakikisha huyu mtu anamuamini Yesu, kwa hiyo maneno yako, au mahubiri yako, yabebe matumaini kwake, kuwa Yesu anaweza kumsaidia, kwa kuutaja ukuu wa Yesu, ambao ni uweza uliopo ndani yake, kuwa anampenda, ni mfariji, ni mponyaji, atamuokoa na moto wa Jehanum na kadhalika.
Vitu vya kufahamu katika watu Kumuanini Yesu:
Warumi 10.11 Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.
10.13 kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
10.14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?
10.15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!
10.17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.
Hatua ya Kwanza, (a) Ni Muhubiri kuzinena habari za Yesu, tunaipata kwenye mstari wa 17b, “kusikia huja kwa neno la Kristo.”
Akiwa na mantiki kwamba kitu kinacholeta imani ya wokovu ni maneno ya Kristo, kwa hiyo ni muhimu muhubiri kuhakikisha anatimiza wajibu wa kuhubiri au kumshuhudia Kristo.
Pili, (b) Ni Mtu Kuisikia Injili, katika 17a, “Basi imani, chanzo chake ni kusikia.” Mara wakati muhubiri akimsema Yesu, kinachofuata kwa huyu mtu ni imani kuanza kujengeka ndani yake kwani ameshayasikia maneno ambayo huzaa imani, maana imani chanzo chake ni kusikia, lakini ni kulisikia neno la Kristo.
Kwa hiyo, wakati unaomba, Muombe Mungu akuwezeshe uweze kunena maneno ya uzima, wala sio ya dini yako, au unayoyataka wewe, maana hayo hayataweza kuumbia imani ndani ya mtu.
Alafu, hakikisha unaombea kusikia kwao, Ibilisi ana tabia ya kupofusha fikra zao, na hapo hawataweza kusikia, ukiona watu unawahubiria alafu wana kebei, fahamu adui ameshakamata kusikia kwao.
Kuna namna anawasikilizisha sauti nyingine, ili kuwazuilia wasisikie ile ya Kristo. Maana hali hii ilikwemo kwa Mafarisayo na wakuu wa kidini, Yesu akasema kuwa wana masikio lakini hawasiki, kwa nini? Adui amewapofusha, ili nini?
Wasije wakasikia akawaponya au wakaongoka, ama ikawazukia ile nuru, ambayo ni wokovu.
Kemea hizi roho, na kila aina ya upofu wa kidini, maana kitu adui anafanya ni kutumia mafundisho ya dini zao, kama nta itakayokaa kwenye masikio yao ya ndani ili wasisikie vyema ile injili, ambayo huumbika na kuzaa imani ndani ya mioyo yao.
Ili kumsaidia huyu mtu, unahitaji kuondoa hilo kiza la kifikra ndani yake, maana wakati unahubiri, fikra zake zitakuwa zikisimama kama ukuta, kwa kumjengea hoja za dini yake.
Ukisema Yesu ni Mungu, zitamwambia hapana, ni Nabii Isa, ukisema ukiomba kwa jina lake utapona, zitamletea kwa jina la Bikira Maria, maana zimefunzwa hivyo.
Maombi muhimu ni wewe kunyunyiza Damu ya Yesu kwenye hizo fikra, ili kuziyayusha, au kuzisambaratisha.
Pili, angusha hayo mawazo yaliyosimama kama ngome, na kuzitisha hizo fikra zipate kumtii Kristo, fanya maombi ya vita;
2 Wakorintho 10:4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)
5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo.
Tunapewa upana mkubwa kutokana na hili andiko kuwa kila kitu kijiinuacho, kinyume na uinjilisti twaweza kukitiisha, na tunaweza kuteka nyara, au mateka, kila fikra, na kuyataka mawazo yake kumgeukia Kristo.
Kwa hiyo, mnatakiwa kuingia katika maombi maalumu, wewe na timu yako, kuhakikisha kila aina ya upinzani, unaotaka kuwafanya watu hao wasiisikie injili, kwa namna yoto ile, mnaupiga.
Na mteke au muzifanye fikra zao kuwa mateka, kumbuka mateka, huenda atakako aliyemteka, lakini huwezi kumfanya mateka kabla ya kumpiga adui aliyemkamata, kisha, unaweza mfanya mateka, tangaza kuteka nyara hizo fikra, na kuamuru hizo ngome zianguke,
kisha mawazo yao uyaamuru kwa mamlaka ya jina la Yesu yapate kumtii Kristo, yaani katika mioyo yao, waseme ndio.
Ushuhuda: Niliwahi kuomba maombi kama haya, na niliuona utukufu wa Bwana.
Kulikuwa na binti fulani, aliyekuwa wa dini fulani, tulimuombea mapepo ili yatoke, ila ilituchukuwa muda sana, nasi tulifahamu ni kwa sababu ya uhalali wayo kwake, na akiokoka, hayatapata huo uhalali tena.
Lakini tulipomgusia wokovu alikana, na aliyekuwa akiishi naye, alituambia kuwa amejaribu bila mafanikio, na kila akiambiwa anataja dini yake.
Niliomba kukaa naye faragha, nilimwambia kwa kina, huku kimoyo-moyo nikiomba hayo maombi ya kutiisha fikra zake zimtii Kristo, nilianza na kuangusha hizo ngome, za mapando ya elimu iliyo kinyume na ile ya Kristo, nikijua hiyo ngome maana yake ni ukuta, unaozuilia elimu ya Kristo kupata kibali moyoni mwake, yaani injili au habari njema za Wokovu.
Baada ya hapo, nikatiisha mawazo yake, yapate kumtii Kristo, na kuyataka yamuongoze katika kusema ndio Bwana, nikiwa katika hali hiyo, aliniambia nimpe muda kidogo ni tafakari. Nami nilimpa dakika chache nikiwa naye hapo hapo. Huku nikiendelea kuomba.
Punde, si punde, aliniambia yupo tayari, nami bila hiyana nilimuongoza sala ya toba.
Umejione kitu hapo! Natumai jibu ni ndio, kwa hiyo muda wa kuita watu mbele, waombaji, wawe pia wanaomba haya maombi, huku wakiwa walisha yaomba kabla pia ya kuanza mkutano, na kama ni ushuhudiaji, yafanye ukiwa hujatoka, na wakati unamshuhudia mtu, ukiona upinzani wa fikra, omba kimoyo-moyo, na kama mpo timu, wakati mmoja au baathi wananena naye, wengine, wanayaomba.
Kumbuka kwa mujibu wa Warumia 10:9-0, tunaarifiwa kuwa imani hukaa moyoni, maana kwa moyo mtu huamini, “ukiamini moyoni mwako”… na kwenye moyo huka mawazo pia, Ukisoma habari za Yesu katika injili, utafahamu upinzani huu wa Fikra au mawazo moyoni, ulimkabili sana, naye aliweza kutambua jambo hilo;
Mathayo 9:2 Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako.
9.3 Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru.
9.4 Naye Yesu, hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu?
Waandishi na Mafarisayo ilikuwa ni vigumu sana kuipokea injili, kwa sababu ya hizi kuta, za mawazo, zilifanyika kizuizi sana, maana hapo tunaona Uinjiisti ukimfikia mtu, na kuambiwa na Yesu kuwa amesamehewa dhambi zake, ila hawa hakuweza kumwamini Yesu, kwa sababu ya upizani uliokwepo mioyoni mwao.
Tupate hakikisho la hii hoja la mawazo moyo kwa kinywa cha Bwana Yesu mwenyewe; Mathayo 15:19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya,…. Pia Marko 7:21.
Kama upinzani huu unatoka kwenye viongozi wao wa kidini, au wa mji, ama wachawi, na waganga, fanya maombi ya kutawanya hicho kiburi kilichokaa kwa mfumo wa mawazo mioyoni mwao;
Luka 1:51 Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao.
Tatu, Ondoa huo utaji katika mioyo yao, utaji ni kitambaa cha giza, kiroho kicho beba roho ya wakuu wa giza, watake au waamrishe kiroho kumgeukia Kristo;
2 Wakorintho 3:14 ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo.
16 Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa.
Lakini pia, upo moyo wa jiwe, huu moyo huyafunga kabisa masikio yao ya ndani, na hawezi kuisikia injili kwa jinsi ya rohoni.
Ukimkuta mtu hataki hata kukupa muda wa kukusikiliza, anakukatisha na kukuzuilia kumnenea habari njema, fahamu fika, huyu mtu, moyo wake ni wa jiwe.
Kwa hiyo, katika maombi yako, yayusha hiyo mioyo ya jiwe, na kuifanya kuwa ya nyama, kama ule wa Zakayo, uwe ni mwepesi wa kuipokea injili, tuna ambiwa kuwa alishuka upesi, alafu akamkaribisha kwa furaha, na aliupoke wokovu kwa furaha hiyo hiyo, na kabla ya hapo, tunaiona kiu ya kuokoka au kutamani, hadi kuamua kupanda juu ya mti.
Kuna watu unafika kwenye miji yao, wanaikubali injili kwa wepesi sana, ukiyaona hivyo fahamu mioyo yao, ni ya nyama.
Kabla ya kuhamia katika jambo la pili, nawiwa kukufahamisha kitu muhimu hapa.
Kwamba mtu wa ndani ambaye huundwa na nafsi, roho, na hatimae moyo, huwa ana msikio, ambayo ndiyo tunayoyanena hapa.
Nimekufahamisha hapo juu kuwa moyo ukiwa mgumu, na masikio huwa mazito, au magumu pia, waliokuwa wakihubiriwa injili na Stefano walikuwa na moyo huu, na tunafahamishwa kuwa ni wenye shingo ngumu, na kibiblia kuwa na hali hii maana yake ni kuwa mkaidi au mshupavu hali inayoushupaza moyo;
Matendo 7:51 Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.
Tunaliona jambo la ugumu wa moyo, likielekezwa pia kwenye masikio, lakini matokeo yake, hapo tunafahamiswa ni wao kumpinga Roho Mtakatifu, kwa nini?
Mioyo na masikio yao ni mashupavu, hawana tohara ya ndani. Hali hiyo, iliwapelekea kumuwa Stefano;
Mtendo ya Mitume 7:57 Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja.
Tunajione hapo kuwa waliziba masikio yao, hilo ni jambo la kiroho linatajwa kuwa kile alichokihubiri, hakikuweza kufanyika imani kwao, na sababu kubwa ni kwamba hawa watu waliziba masikio yao, ikiwa na maana masikio yale ya ndani, (injii isipopokelewa moyoni, hataka je mtu akisikia na haya masikio ya mwili damu na nyama, imani haiwezi kuzaliwa), alafu baada ya kuyaziba, tunawaona wakimrukia na kuanza kumpiga, ukiendelea utaona mauti yake.
Nilitaka ufahamu kuwa, unapohubiri mahali nakupata upinzani, juwa jambo hili lipo, la watu kuziba masikio yao, au kuwa na ushupavu moyoni, hali inayowafanya kutokusikia, kwa hiyo, Ibilisi huweza kupata mwepesi wakuwatumia ili kuleta upinzani, ukisoma kitabu changu cha SHINDA, TEKA NA UMILIKI, utajipatia hapo njia za kuikabili vyema hii roho husani inapogeka na kufikia hatua ya kuzuilia injili.
2. Kukiri kwa Kinywa, Imani ikisha imarika ndani ya mtu kwa njia ya mahubiri, kinachofuata ni huyu kutakiwa kukiri kwa kinywa chake kile alichokiamini ili kuelekea katika wokovu.
Ndio maana hatuwaongozi watu sala ya toba mwanzoni, bali huwa hivyo mwishoni, ikiwa na mntiki ni baada ya wao kuamini.
Hakikisha unamfikisha huyu mtu kwenye hatua ya kukiri, waite mbele, au waambie wale ambao wapo tayari kuokoa, au waiomuamini Yesu, waamuwe kukiri kwa njia ya maneno utakayo wafuatisha.
Ni muhimu kuombea ukiri wao, maana wapo watu ambao huishia kuamini, ila hawawezi kufikia hatua ya kukiri, wengine hutoa hudhuru kuwa siku nyingine watafanya hivyo, lakini hizo huwa ni hila za ibilisi. Kwa hiyo ni vyema kuzipinga kwa njia ya maombi.
Kuna binti mmoja, alihubiriwa injili kwenye mkutano mmoja na kufikia hatua ya kuamini vyema, ila alipohitajika kukiri, ili aweze kumpokea Yesu, aliomba udhuru ya kwamba naomba akamuage mchumba wake, kwanza alafu atakuja kuongozwa sala ya toba, na aliweka bayana kuwa hata kama atakataa, yeye ataokoka.
Alipokuwa akitoka kwenye mkutano, ghafla ilitokea gari na kumgonga akiwa kwenye eneo lile lile anavuka barabara, tazama hapo! Amekufa, hajaokoka, ila alishaamini, lakini hatua nyingine hakuifikia.
Hakikisha unamuomba Mungu akupe upako wa mkubwa wakati wa kumalizia, ili watu waweze kufunikwa na uwepo huo wa Roho Mtakatifu ili kukata nira za kumkiri Yesu, wapo watu ambao nira hufanyika ni wazazi wao, au walezi wao, au dini zao, hutamka kabisa kwenda kuomba kibali kutoka kwao ili waweze kuja kumkiri Yesu wakisharuhusiwa ndo waje kuokoka, piga hizo roho.
Ipo nguvu katika kukiri, ndio maana kanuni hii inakuwa na nguvu na umuhimu mkubwa hivyo, kwamba kwa kinywa mtu hukiri hata kupata wokovu, Warumi 10:10, kwani imani inampatia tu mtu haki, ila ukiri, unakamilisha wokovu wake.
Kumbuka maneno ni nira, na nira ipo ile ya Kristo, ambayo ni laini, kwa mujibu wa Mithali, tunafahamishwa kuwa mtu hujifunga kwa maneno ya kinywa chake mwenyewe;
Mithali 6: 2 Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako.
Kuamini pekee hakukufanyi kuingia katika hili Agano, bali kuamini, ni ishara ya kukubali kuingia katika Agano Jipya, na kukiri, ni kutilia sahihi mkataba wa Agano hili.
Kumbuka yule mwizi pale msalabani alikuwa na hofu ya Mungu, maana yake alimuamini Mungu, ila bado hakuwa na wokovu, ukitaka kulihakiki hilo; alimkemea mwenzake na kumwambia kuwa wewe humuogopi hata Mungu?
Hali inayodhiirisha kuwa yeye alimuhofu Mungu, yaani alikuwa na imani juu yake, maana ile ni hofu ya uchaji, ambayo huja kwa imani.
Lakini hakuweza kupokea wokovu, mpaka alipokiri kwa kinywa, kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, na kumuomba kuwa amkumbuke, hapo alipokea Wokovu.
Ufunuo huu ukupe, kuwasaidia watu wanaokubali kuwa hakuna kumuona Mungu nje ya wokovu, ila wamekuwa wazito kukiri.
3. Kumpokea kama Bwana na Mwokozi, Hatua hii ni ya tatu, ila pia ni ya pili. Nikiwa na maana kwamba, mtu anapoamini ni shariti amini kuwa Yesu ni Mungu, na alikufa na kufufuka, alafu akiri kwa kinywa chake hayo aliyo ya amini moyoni mwake, na tatau, moja kwa moja, anahamishwa kwenye ufalme wa nguvu za giza na kuingizwa katika ule wa pendo la mwana wake.
Ambao, Yesu, husimama au hutawala kama Bwana, na pili Mwokozi wa maisha ya muhusika.
Na ninenapo ya pili ni kwamba, kabla ya kukiri, ni lazima moyoni mwake, ile imani, izae uhakika, utakao muweza kumuona Yesu kwa jicho la Kiungu.
Ikiwa na mantiki ya kuondoa au kuukataa utawala wa Ibilisi na kuukubali huu moyoni mwake, alafu anapokiri, ndipo jambo hilo huwa halisi kwake, ila inaweza kuwa hata ya pili kiroho moyoni mwa mtu, ila bado halijawa halisi, ili liwe halisi kiroho ni lazima akiri, alafu ahamiswe, jambo hili halihitaji mtu kufanya, bali ni matokeo ya imani, na ukiri wa kweli, unaokuja au utokanao na moyo wake kuridhiwa kuwa chinini ya imaya ya Kristo Yesu.
Kama mtu haja amini, hajakiri kwa kuaminishwa, hatua hii haitokeo, na kiroho atakuwa hajaoka.
Hapa ndipo penye andiko la kwamba na kondoo wengine Yesu anao ila wameingilia dirishani ikiwa na mantiki yakuingilia penginepo ambapo sio mlango, na hii ni hatari maana hawa ni wasindikizaji, hii pia ni sababu ya wainjilisti kuhudumu makanisani.
Fahamu, Bwana maana yake ni kiongozi, na kama kuna mwalimu, maana yake kuna mwanfunzi, kama kuna askari kuna mwalimu, kama kuna dakitari, yupo pia mgonjwa.
Kwa hiyo, Yesu akiwa Bwana, huyu mtu huwa ni mtumwa, na mtumwa sio mkuu kuliko Bwana wake, maana hiyo, unapo okoka ipo chini ya amri, na kanuni za Kristo, akikwambia leo kanisani, nenda, unapaswa kushuhudia, kafanya hivyo.
Ni muhimu kulijua hili, ili ifahamike kwamba, tupo chini ya Kristo kama Bwana, kwa hiyo kuna mambo ambayo atatuzuilia kufanya, na ambayo atataka tuyafanye, kama alivyomuajiri kwa muajiriwa wake.
Kama mwokozi maana yake, ametuokoa, kutoka kwenye dhambi, vifungo, kwa mantiki kwamba, anahitaji kupewa heshima yake, na muhusika kuto kurudi tena huko alikokwisha kuokolewa.
Unapomuonyesha mtu kuwa yupo kwenye mateso, maana yake unamtaka aliitie jina la Bwana, ili aokolewe, mfano mtu anayezama maji, hupiga kelele za kuomba msaada, mtu ambaye nyumba yake inateketea kwa moto, anawaitaji askari wa zima moto waje kumsaidia.
Wakija, huja kama waokozi, na mtu huyu unapomuita mbele mbele ili kuokoka, au kuongozwa sala ya ukiri, maana yake, unamtaka amuite na kumpokea Yesu kama mwokozi.
Na katika mafundisho yale ya walimu, ni muhimu kumfunza kuwa ameokolewa kutoka kwenye mateso, asirejee tena huko, maana mtu aliyekuwa akizama na maji akiokolewa harejelei tena ile adha, ndio maana alipiga kelele za kuomba msaada.
NB: Na wiwa kukufahamisha kuwa kipo kiwango kikubwa cha Uinjilisti chenye kuleta wepesi ambacho ni cha mtu au watu kufikia hali ya kuliitia jina la Bwana kwa moyo wote;
Warumi 10:11 Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.13 kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
Hali hii huwa ni kabla ya kuhubiri injili, au kumaliza, mtu mwenyewe anakuwa na hamu na shahuku ya kuongozwa sala ya toba, hata huweza kuomba au kutamani kukukatisha, ili muda usiendele kusonga haja okoka.
Tuonalioona hili kwa yule mlinzi wa gezeka kwa wakina Paulo na Sila; Matendo ya Mitume 16:30 kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?
Hali hii huweza kutokea panapokuwa na upako mkubwa wa Roho Mtakatifu uliopo ndani ya Muhubiri, lakini pia, mtu kushukiwa na nguvu za Mungu, na mtu kujawa na imani kubwa, ambayo huweza kuja kwa kulisikia neno, au kiziona ishara na maajabu ya Mungu ama kukutana na uweza wa matendo makuu ya Mungu.
Utaliona kwa Yesu, mara kadha kuna watu waliamini baada ya matendo fulani kutokea, na wengine kutaka kumfuata kila alipokuwa akienda.
Ukija hata kwenye tukio la kufufuliwa kwa Lazaro, utajione jambo hili, kuwa wengi waliamini;
Yohana 11:45 Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini.
Kwa hiyo ni muhimu pia wewe Muhubiri, licha ya kutumia lile andiko la Zaburi la mtakeni Mungu na nguvu zake, pia hakikisha matendo makuu yanatokea katika ishara na miujuza ili wengi waamini na kuokoka, katika hali ya urahisi na nyepesi, hilo nalo liweke katika orodha ya maombi yako.
Lakini pia, waweza muomba Mungu akupatie karama ya Matendo ya Miujiza, na ile ya Kuponywa wa gonjwa, maana alisema zitakeni sana karama za rohoni.
Fahamu: Uinjilisti unahitaji kuwezeshwa, kwa hiyo usiache kumuomba Bwana akuinulie watu watakao kuwa wakikuwezesha, kiuchumi, na kivifaa, na pia kimaombi.
Wapo watakao husika katika kukupeleka, au kukusafirisha, na hata kukutunza, ili uweze kuwafikia watu, katika kuanza na kutimiza adhima ya kuwahubiria, ili kuanza kuwapandia imani;
Warumi 10: 14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?
15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!
Kama hujaokoka na unataka kuokoka ama ulirudi nyuma kiroho na unataka kutengeneza na BWANA kwa upya leo, tafadhali fuatisha nami maneno haya kwa Imani, Sema: BWANA YESU, NINAKUPENDA, NINAKIRI NA KUAMINI MOYONI MWANGU KUWA WEWE NI MUNGU, ULIKUFA NA KUFUFUKA KWA AJILI YANGU, INGIA NDANI YANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU LEO, AMENI.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo.
Na Huduma ya UKOMBOZI GOSPEL, Arusha Tanzania, Kwa Maombi, Ushauri, Maswali au Sadaka wasiliana nasi, Barua pepe: ukombozigospel@gmail.com Simu: +255 759 859 287 pia waweza itumia kwa M-PESA. Zaidi www.ukombozigospel.blogspot.com
Pia #Like #Penda Page/Ukurasa wetu au kundi la Fb, ili kupata habari hizi kwa haraka, zaidi. @ugukombozi Gospel
PAGE: https://www.facebook.com/ugukombozigospel/
Kikundi: https://www.facebook.com/groups/2268418230050621/
Pia kwenye mtando Mpya wakitanzania wa
2 DAY SKY: https://www.2daysky.com/ukombozigospel
Pia TAZAMA VIDEO ZETU HAPA https://www.youtube.com/channel/UCv1tghnugOSpbmb5h6ebJtA (Ukombozi Gospel)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni