Jumanne, 12 Aprili 2022

JIFUNZE KUMUONA MUNGU NYUMA YA PITO AU JARIBU LAKO

 Ujumbe huu ni Utangulizi wa kitabu chetu cha MUONE MUNGU NYUMA YA PITO AU JARIBU LAKO

Na Mwalimu Oscar Samba (#Share ujumbe huu kwa Wengine ili Tuvuke pamoja nao)

Kimwili tunaweza kuwaona adui zako kuwa ndio waliokusukumiza kwenye hilo shimo, ndugu zako, wapendwa na hata mchungaji wako. Kumbe Mungu yupo nyuma ya tatizo hilo ili akufanye kuwa waziri mkuu kwenye nchi ya Misri.

Unaweza ukawa na kila sababu za kuwalaumu viongozi waliokuwa wakimzunguka mfalme Nebukadreza ama Dario kwa kutengeneza sheria batili na kisha kumfanya mfalme kukutupa kwenye tundu la simba ama lile tanuru la moto! Kumbe nyuma yake Yesu yupo ili ajitukuze kwa mfalme, dunia yote na kisha kukuokoa ukiwa mshindi na mwenye kuinuliwa kicheo.

Jifunze kumuona Yesu kwenye kila nyuma ya pito au tatizo, ama nyakati ngumu unazokuwa unazipitia. Hii itakupa kunufaika vilivyo na nyakati hizo. Kuna tatizo limenikuta kipindi hiki; limetumika sana kunisukumia kwenye kusudi lake.

Ndio maana nina ujasiri wa kukufundisha kuhakikisha unamuona Mungu kwenye kila pito unalolipitia. Epuka kuwaona wanadamau, maana utajikuta unakwama kwa kukwazika na kuumia kila uchao. 

Kitabu hiki kina nia ya kukusaidia kunufaika kikamilifu na nyakati ngumu zinazokuja mbele yako. Ni wachache wanaonufaika nazo vilivyo, wengi wao wanakwama, na hata wakiliendea kusudi huwa kama vile halikupangwa kupenyezwa hapo.

Yusufu aliyajua yale, alifahamu kabisa mpoyoni mwake kwamba nyakati zile kuna kusudi zimebeba, ndio maana hakuwaweka moyoni ndugu zake; japo kiuahaliasia aliumia tena mno. Jibu hili ni ishara ya kuzielewa vilivyo nyakati hizi; 

Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Mwanzo 50:20

Watu wengi tunaweka kisasi na kujakuwalipa mabaya waliotukosea ikiwa ni matokeo ya kutokulifahamu jambo hili. Kumbuka hili daima; nyakati ngumu zipo ili Mungu ajifunuwe kwetu kiutofauti.

Ukitaka kuwa mtumishi wa kawaida basi huhitaji nyakati ngumu, ila ukihitaji kuwa mtu wa tofauti uwe na hakika ni lazima ujiandae kupitia nyakati kama hizi. Na zote hizo lazima kuonewa, kuzalilishwa, na kuadhibiwa pasipo haki kujitokeze. Ukitaka kutendewa haki kwenye kila jambo, uwe na hakika hufai kuandaliwa kwa ajili ya nyakati kama hizi. Kuna muda unaonewa kabisa, hata anayekuongoza anajua kakuonea, hapo napo unatakiwa kuwa na moyo wa msamaha. Unapitia huku ukijiambia nimekusamehe; ili nini? Ili unufaike vyema na matokeo ya kupita kwako.

Stefano na Yesu ni kielelezo muhimu sana katika hili. Walipokuwa katika mateso makubwa jambo muhimu kutoka katika maamuzi ya midomo yao ni kuwatangazia msamaha waliokuwa waliwaudhi! Ndio, hapo ndipo unapompa Mungu nafasi ya kukupigania, pamoja na kukuonyesha alichokusudia kwako. Hawezi kukifunua bayana kama utaingia kwenye shimo na adui zako. Maana katikati ya shimo Yesu yupo kama mtu wa nne.

Huko kuna malaika wanaowafunga vinywa makanywa yao ili wasije kukudhuru. Sasa ukiingia na adui zako huko uwe na hakika vidonda vya tumbo, magonjwa ya moyo havitakuacha. Vitakaundama daima. 

Kitabu hiki pia kina lengo la kukutia moyo kama Yes alivyofanya kwa wanafunzi wake. Mambo mengine yanakuja yakiwa ya muda mfupi tu. Ni kweli yanapokuja huwa na maumivu makubwa, ila maumivu hayo ni ya kitambo kama ilivyo kwa mambo hayo. Ila ipo furaha idumuyo milele: ama matunda yake ya kaa kuliko hayo mamivu;

Yohana 16:20 Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 

21 Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. 

22 Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye.

Inatakiwa ifike mahali pa kuiyona furaha ya matokeo ya huzuni ya muda, unapokuwa kwenye huzuni yenyewe; “lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye.”

Ukifika hapo Shetani hata kubabaisha, wala hutafanya maamuzi ya ajabu, maana huzuni na uchungu imewapelekea wengi kuhama madhehebu,kuhama makanisa, kugawanyika, au kutengana, na roho ya uasi nayo huwa na tabia ya kuvizia mazingira kama haya na kisha kupanda mbegu na hata kuwa na matunda katika majira kama haya. Wengine wanarudi nyuma kiroho kabisa. Kumbuka hakuna jaribu la kudumu, ila maamuzi yako yanaweza kuzaa hali ya kudumu!

Unajifungua, lakini hauoni huzuni ya uchungu na maumivu ya kujifungua, bali unaiona furaha ya kuwa na mtoto wakati wa maumivu makali ya kjifungua. Mwilini una maumivu, lakini moyoni kuna matokeo ya kjifungua. 

“Ndio maana hakuna mama anayetoroka labor/leba”.  Maana anafahamu matokeo yake yalivyo na vigelegele, na wewe usitoroke au kunungu’nikia pito, tazama matokeo yake yalivyo na shangwe, nderemo, furaha na kuinulia. Hongera na wenye zawadi hawaji ukiwa “leba,” wanakuja baada ya kujifungua! 

Wakati wa maumivu, una watu wa chache, wewe na mkunga, ila wakati umeshajifungua, uwe na hakika unao wengi. Kila mtu atataka kumbeba mtoto! Yesu aliachwa peke yake, ila alipofufuka tu! Wakaanza kuambizana, kafufuka, kaonekana, hayupo kaburini! Hata Petro aliyemkana alikuwa wa kwanza kutaka kushuhudia hilo! Mbio hadi kaburini! Maana huu ndio wakati wenye matunda kwetu. Akiwa kwenye shimo, na walipomuuza, walikuja na “stori” kuwa amekufa, wakalia na kuomboleza ikaishia hapo. Ila walipopata taarifa kuwa ni waziri mkuu! Wao na jama zao walimwandamia na kumfuata! Ingekuwaje kama Yusufu angekufa kwa vidonda vya tumbo na magonjwa ya moyo! 

Haka jina lake lingekuwa kama wengie! Kuna umuhimu wa kujifunza kuachilia, na kusamehe na kumtazama Mungu katika nyakati kama hizi, kama kweli tunataka kufika mbali na Mungu. Kama unatembea peke yako sawa, ila kama unatembea na Mungu au una mpango wa kuongozwa na Yeye hili ni jambo muhimu sana kulifahamu.

Kipindi hiki nimejikuta nikiuelewa sana ule wimbo unaosema kuwa sio kazi rahisi kutembea na Yesu, katika safari au akikuongoza katika safari. Kutemeba na akili zako ni rahisi, ila kama Yesu ndie kiongozi wako, hakika ni jambo gumu. Lakini lin  matunda mema kupita utamu wa asali kama utajifunza kushikamana na kanuni zake. Miaka kadhaa iliyopita nikamwambia lakini nimezalilishwa sana, nimedhiahakiwa au kushushwa heshima. Ndipo aliponikumbusha kilichompata msalabani, ambapo naye alifanyiwa vivyo, ila alisamehe na kuchukuliana vyema na adui zake. Huku akikaza katika kulitazama kusudi lililokwepo mbele yake. Nawe jifunze kuliishi ili kufikia malengo yako. Ukikwama hapa ni umekwama eneo kubwa sana la mafanikio ya maisha yako. 

     Karibu kwenye Kitabu hiki;

Kitabu kikitoka Kitafute..

Kama hujaokoka nikutie moyo kufanya hivyo tafadhali. Maana maisha ya dhambi hayampendezi Mungu. Wanaokufa kwenye dhambi mshahara wao ni moto, ila wanaokufa katika neema ya wokovu ni kuishi na Mungu milele. Tafadhali usiseme leo sijajiandaa, ama kesho, au kesho kuta, siku nyingine sio jibu sahihi. Hujui siku wala saa ya kuondoka kwako hapa ulimwenguni. Wapo wanaokufa kwa kugongwa na gari, kuugua ghafula na hata kufia usingizini. Alilala vizuri ila ndo hakuamka tena, alipoaga usiku mwema, kumbe alimaanisha usiku mwingine! Nani ajuaye wako! Huna hakikisho la kuishi milele na hujui siku wala saa, huwa inakuja ghafula.

Sasa fuatisha kwa imani Sala hii ya Toba pamoja nami: Sema, MUNGU BABA, NINAKUJA MBELE ZAKO, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NISAMEHE, NIOSHE, NITAKASE KWA ILE DAMU YAKO, FUTA JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, LIANDIKE SASA KWENYE KITABU CHA UZIMA WA MILELE; Amen.


Hongera kwa kuokoka, na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo. 

Kwa maombezi, Maswali, Ushauri na hata Sadaka yako kwa Mpeswa, Usisite kuwasilaina nasi. 

Mawasiliono; Simu au WhatApp: +255759859287 Baruapepe: ukombozigospel@gmail.com au tembelea pia YouTube Channel yetu ya Ukombozi Gospel au Ug Tv , www.ukombozigospel.blogspot.com 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni