Alhamisi, 14 Aprili 2022

FAIDA ZA KUSHINDA JARIBU AU PITO ( Majaribu ni Mtaji)

 Na Mwalimu Oscar Samba (Tafadhali #Share na kwa wengine ilia nao Wanufaikae)

Sehemu nyingine ya Kitabu chetu cha MUONE MUNGU NYUMA YA PITO AU JARIBU LAKO. Ni katika mada yetu ya kwanza ya ; 1. Jinsi Mungu Anavyoweza Kuwa Nyuma ya Jambo Gumu Linalokusonga. Na pwenti ya kwanza pia ya mada hiyo: 

 1. Mfano wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Napenda sana sentensi yao hii muhimu katika pito, na kwa wale wasomaji wa kitabu cha CHAKUFANYA UNAPOKUWA NJIA PANDA; wanaweza kunielewa kwa upana. Vijana hawa walimnenea mfalme kuwa hata kama Mungu hatawaokoka bado hawawezi kumuacha.

Kwamba kuwaokoa ni jambo jema, na ndilo wanalolisubiria, la hata asipofanya hivyo bado hawawezi kumuacha. Wasomaji wa kitabu cha Waebrania hususani ile sura ya 11 wanaweza kuelewa kuwa kuna aina mbili ya imani tajwa pale. Ya kwanza ni ile iliyoleta wokovu na ya pili ni ile iliyowawezesha kufa katika Bwana yaani bila wokovu kwa jinsi ya mwilini. Hawa nao ni mashujaa japo hawakuokoka katika mateso bali waliyafia mateso;

35….Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; 36 wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; 

37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; 

38 (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.

Wakati mstari wa 33-35 A ukitaja jinsi mashujaa walivyoshinda miliki za wafalme, walifunga vinywa vya samba, walivyozima nguvu za moto kipindi kile cha mfame Nebukadreza, na jinsi walivyokuwa hodari katika vita na huku wanawake wakipokea wafu wao; mstari wa 35 unaendelea na kutupasha jinsi wengine walivyo uawa kwa kukatwa na misemeno, upanga, namna walivyovaa mavazi duni na dhaifu, maisha ya uhitaji yalivyowakabili, wakiteswa na kutendwa mabaya! Lakini hawa nao ni mashujaa wa imani (japo imani yao haikuwakoa matesoni). 

Ushujaa hauji tu pale Mungu anapokutoa kwenye tanuru la moto. Wakati mwingine hata ukiteketea na kuwa majivu kabia Mungu napo hutukuzwa. 

Wasomaji wa vitabu mbalimbali vya historia ya kanisa watakubaliana nami kuwa wapo wafia dini ambao waliishilia kuuawa kikatil, ila nyuma yao walizaa watu wengi na wakati mwingine hata askari au watu waliohusika kiukaribu kuwaangamiza walikuja kuvutwa na ushujaa wao. 

Sijui kama uliwahi kujiuliza jambo hili! Nabii Elia Mtishbi alikuwa na uadi mkubwa sana na nyumba ya kifalme, kipindi cha mfalme Ahabu, maadui zake wakubwa walikuwa ni hii nyumba. Lakini miongoni mwa aliyekuja kumfuatia yaani Elisha, alikuwa karibu sana na ufalme ambao ulifuatia baadae kidogo. Alipata heshima kubwa mno. Lakini hawa wote ni watumishi wa Mungu. Na kila mmoja alitimiza kusudi la Mungu katika wakati wake. Huyu akiwa adui, na huyu akiwa na heshima katika ufalme. Sasa wewe kama ni Elia usilazimishe kuwa Elisha, na ni hatari na ujinga Elisha kalazimisha au akatamani kuwa Elia.


Sasa tuendelee: Sentesi yenyewe ya hawa mashuja ni hii; 3:14 Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? 

15 Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?

16 Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili.

17 Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. 18 Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.

Mstari wa 17 wanakiri ukuu na uweza wa Mungu kuwaokoa, ila 18 wanafika mbali zaidi na kusema kama sivyo, yaani hata kama hawataokoka na huo moto, wao hawapotayari kupiga goti kwa mfalme.

Ni nani aliye jasiri wa kusema leo, Mungu wangu najua atanipa mume au mke, na hata kama hatanipa mume, au mke, mimi sikotayari kuolewa kienyeji, sikubali kuolewa na kafiri, mlevi, mpagani au mtu ambaye hajaokoka!

Unajua wale wanaosema kuwa nimechoka, nimeomba nikafika mwisho, mimi hata akija mlevi, kafiri au mpagani mimi nitaolewa tu. Niko tayari hata kuwa mke wa pili! Ni matokeo ya kusalia kwenye mstari wa 17, hajafika hadi wa 18!

Mungu akinipa mtoto sawa, ila hata asiponipa Yeye ni Mungu kwangu. Sitaikana imani kwa sababu Mungu hajajibu. Ukimsikia mtu anasema; “Mungu asiponijibu hadi wakati fulani mimi na Yeye basi.”” Uwe na hakika kaishia mstari wa 17, hajafika wa 18. “Mwaka huu ukiisha Mungu hajafanya hiki na kile…msinilaumu wapendwa!” Msaidieni kufika mstari wa 18.

Kwamba Mungu akiniokoa sawa, ila ikibidi kukatwa na msemeno, kufa kwa makali ya upanga, napo nitasema Yesu ni Bwana.

Katika maisha yangu ukiniuliza miongoni mwa maandiko magumu kwenye Biblia, japo yakihubiriwa saa uwepo wa Mungu ni mkubwa tunakuwa wepesi wa kuitikia ‘ameni’, ni hili hapa; ugumu wake sio katika natharia bali ni katika vitendo. Ukutane na uhalisia kwenye “field.” 

Warumi 8:35

Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?

Turudi:

Sasa turejelee mukutadha halisi wa kitabu chetu. Hawa mashujaa watatu waliweza kufanikiwa kunufaika kikamilifu na uwepo wa Mungu nyuma ya lile pito au jaribu walilokuwa wakilipitia. 

1 au Mosi; Uwepo wa Mungu Ulijidhiirisha kwa Jinsi ya Mwilini. Kwa ujumla Yesu alijifunua katikati yao kama Mtu wa Nne. Mstri wa 24 mfalme anawauliza mawaziri wake kuwa mbona walitupa watu 3 kwenye moto na yeye anawaona wameongezeka na kuwa 4, uzuri alipokea na ufunuo na kujikuta katika mstari wa 25 anataja na sifa zake ambazo zinatupa kufahamu kuwa alikuwa ni Yesu mwenyewe. (25 Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.)

Yesu alikwepo pamoja nao tuoka mwanzo, kabla hawajaingia kwenye shimo, ila walipotupwa kule akajidhiirisha ama akajifunua. Wengi tunamtaka Yesu ajidhiirishe ndipo tuingie kwenye shimo. Sasa hiyo sio imani tena. Imani inapimwa katika kuwa na hakika ya mambo ambayo hayaonekani mwilini kana kwamba yamekwisha kuonekana bayana au dhairi ama wazi kabisa.

Pili, Wanatambulika Rasimi kama Watumishi wa Mungu. Hapo awali mfalme aliwachukulia kama watu wenye kiburi, na jeuri,ndiposa akawauliza ni kwa makusudi au kwa bahati mbaya hawakuisujudia sanamu yake!  Ila mara baada ya kuuona mkono wa Bwana juu yao, alikiri adharani kuwa hawa ni watumishi wa Mungu kwa kuwaita. Heshima siku zote huja baada ya ushujaa, ukikwepa kupigana na Goliathi wako uwe na hakika unakwepa kuinuliwa. Goliathi aji ili kukuaibisha, anakuja ili kukupa cheo cha kuwa amiri wa mfalme, kutoka kwenye kupiga kinubi mbele yake na kuwa mkuu wa kikosi cha askari elufu moja. Sasa endelea kumnung’unikia Goliathi wako uone ni kwa jinsi gani unajikwamisha kuinuliwa!

Ona mstari wa 26, Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto.

Tatu, Huo mstari wa nyuma yake na inayofuatia inatupa kujua kuwa Mungu Aliwapa Ushindi Kwenye Lile Jaribu. Moto haukuwa na nguvu juu yao, wala dhara lolote halikujitokeza kwenye maisha yao. Mstari wa 27 unatupa kupata hili hakikisho kinagaubaga; Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo.

Nne, Mfalme Alimuabudu na Kumuadhimisha Mungu. Mstari wa 28 unatuhakikishia hili; Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.

Watu wengi wanataka Mungu wao abudiwe na kupata heshima kazini lakini hawana ujasiri wa kusema wameokoka. Hawana udhubutu wa kusimamia misimamo yao kiimani. Wanataka ndugu zao waokoke, jamaa zao zimjue na kumgeukia Mungu wao ila wao wamepoteza ujasiri kabisa wa kumtaja na kumsimamia huyu Mungu. Wakijaribu kufanya hivyo na wakitishiwa kidogo tu moja kwa moja wanajikuta wanakuwa wapole na kunywea. Alafu wanataka heshima ya Mungu wao katikati ya ndugu wanaoabudu miungu mingine.

Wakiwa nao wanajikuta watoa michango ya kununua mbuzi ambaye anatumika kwenye matambiko, michango ya shehere zao nao hutoa, huambiwa lakini wewe hata kama hunywi pombe utakuywa tu soda na hata maji. Njoo tu ili uonyeshe kuwa tupo pamoja! 

Wenzako waliisimamia imani, waligoma hata kula chakula kizuri kwa mfalme, ili nini? Wasijitie unajisi kwa vyakula vyao, walikuwa radhi kula chakula kisicho na viwango mbele zao ili tu kutunza utakatifu, wewe vinyango vya nyama viwili na chakula cha siku moja vina kukaba shingoni/(kuvimezea mate) hata huwezi kuvigomea! Pole, sahau kuleta mabadiliko. Na kumbuka kuwa usipobadilisha utabadilishwa wewe, usipopindua utapinduliwa wewe.

Tano, Mungu wao, yaani Wetu Alichukuwa Nafsi ya mungu Yule wa mfalme. Mfale hapo awlai alijigamba naye, akizania kuwa hayupo kama yeye. Alifika mbali nakusema ni Mungu wetu hawezi kuwoakoa na mkono wake mfalme ambapo alikuwa akimaanisha mkono huwa wa mungu wake uliojuu yake. Ila baada ya kukutana na udhiirisho huu moja kwa moja nafasi ya mungu wa sanamu ya dhahabu alipewa huyu Mungu wa Israeli. 

Jionee katika msatri wa 29, Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.

Wengi wanatamani kijiji chao au mtaa wao, familia na hata ukoo wao upinduliwe na kufikia hatua ya Mungu wao kupata heshima kubwa namna hii ila hawapo tayari kulipa gharama ya ujasiri kama hii. Wakitishiwa na balozi au mjumbe tu wa nyumba kumi na hapo sio hata mwenye kiti wa kijiji wala polisi kesho yake humkuti akihubiri tena kwa sauti. Vyombo vinapunguzwa sauti na ukimya unatawala. 

Akitishiwa tu na mlevi sokoni kesho harudi tena hapo. Alafu anatamani alete heshima ya Mungu wake kwa miungu ya kigeni kusalimu amri kwenye eneo lao. Sahau kabisa, na uwe na hakika mungu wa dhahabu wa ukoo wako, a mtaa wako ataendelea kuwika kwenye eneo lako hadi hapo utakabobadilika. Ukiwa muoga kukaa mahabusu na kusota jela kwa ajili ya Kristo uwe na hakika utapoteza kitu kikubwa sana. 

Waleta mapinduzi, (hata wale wa dunia hii) ni watu waliokubali kupitia mambo magumu na mazito. Waoga waliishilia kujikomba na kujibaraguza mbele za wafame na watawala waliokuwa wakiwatawala. Ila majasiri ndio walioleta mabadiliko. Na hapo walipitia sio kwamba walishilia katika ujasiri tu bali ujarisi wao ulidhiirika katika au jinsi walivyoyakabili magumu yaliyokuwa yamewekwa kama vikwazo mbele yao. 

Sita, Mashujaa Wanainuliwa. Sura hii inamalizikia na mstari wa 30 unaotupa kujua au kufahamu kuwa mshujaa hawa walipata heshima, kibali na upendeo kwa mfame. Hatima ya kuvumilia ilikuwa ni kuinuliwa kwao; Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli.

Unajua ni kwa nini hupandi viwango, ni kwa sababu gani heshima yako ipo pale pale yaani haiongezeki, wakati uliowatangulia kwenye utumishi na wokovu wanazidi kuchanua wewe umedumaa tu pahala pamoja! Ni kwa sababu ya uwoga na mashaka, na kitu kinachoitwa leo hekima na ustarabu wenye nidhamu ya woga, kaunafiki na kujibaraguza ndani yake.

Kujikomba na kutaka kutokuonekana wabaya kumewafanya watumsihi kutii kila kitu hata taratibu ambazo sio sahihi na zenye mrengo wa kudumaza wokovu. Ni kama vile tumemwagiwa maji ya baridi na hatutaki kusogelea joto la Roho Mtakatifuli kutuondolea unyonge huo. Wakina Petro na wengineo walipotishwa-tishwa dhidi ya kuhubiri na kupigwa pigwa, moja kwa moja waliliendea joto la Roho Mtakatifu, walimtaka awape/awarejeshe ujarisi, na walipojaa tena Roho ndipo wakazidi kuisema ile kweli katika ujasiri wote. Sasa wewe endelea kujikunyata kwenye jokofu “friji” badala ya kukoka moto ili uwe salama. Ukiukumbatia woga ni umejifungia kwenye jokofu la barafu  hakika watakugandisha kweli. Ndio maana siku hizi kazini na kwenye biashara yako humsemi tena Yesu. Ukiwa na ndugu zako ujasiri huna, kisa walikukaripia na kukutishia: wewe achana na hiyo hali jifunze hapa;

Matendo ya Mitume 4.

18 Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. 

19 Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; 

20 maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. 

21 Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka; 

22 maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini. 

23 Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. 

24 Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; 

25 nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? 

26 Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. 

27 Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, 

28 ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. 

29 Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, 

30 ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. 

31 Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

Ujasiri hauji kwa nguvu wala akili zako, bali hutoka juu, hutoka kwa Roho Mtakatifu. Mueleze bayana kuwa siku hizi umepowa kutokana na vitisho na mateso au adha. Aje akupe joto lake nawe utoke katika ubarafu uliokuwa nao. 

Sasa turudi tu kwenye uhalisia. Tumeziona faida zote hizo zilizowakuta hawa mashujaa watatu. Labla tujiulize kama kuna mtu alijua kuwa Mungu yupo nyuma yao kwa viwango hivyo ili kuwatukuza na Yeye kujiinua? Jibu ni la. Hata kama imani ipo, si rahisi kujua kila kitu, maana ukishajua kila kitu haiwi tena imani,  (itakuwa tu ni ujasiri wa kihodori) ni kweli kuna kuwa na taraja sawa ila sio katika madhiirisho ya namna hiyo. Macho ya ndani yanapaswa kujawa na matumaini zaidi ya akili ambazo hutamani kuona tukio likiwa dhairi.

Lakini ni kweli Mungu alikwepo hapo ili awatendee hayo yote aliyoyatenda. Hii ikupe kujua hata katika pito lako yup hapo ili akujibu na kukutukuza zaidi na zaidi. Maana kama sivyo asingekuacha upitie hapo.


Kama hujaokoka nikutie moyo kufanya hivyo tafadhali. Maana maisha ya dhambi hayampendezi Mungu. Wanaokufa kwenye dhambi mshahara wao ni moto, ila wanaokufa katika neema ya wokovu ni kuishi na Mungu milele. Tafadhali usiseme leo sijajiandaa, ama kesho, au kesho kuta, siku nyingine sio jibu sahihi. Hujui siku wala saa ya kuondoka kwako hapa ulimwenguni. Wapo wanaokufa kwa kugongwa na gari, kuugua ghafula na hata kufia usingizini. Alilala vizuri ila ndo hakuamka tena, alipoaga usiku mwema, kumbe alimaanisha usiku mwingine! Nani ajuaye wako! Huna hakikisho la kuishi milele na hujui siku wala saa, huwa inakuja ghafula.


Sasa fuatisha kwa imani Sala hii ya Toba pamoja nami: Sema, MUNGU BABA, NINAKUJA MBELE ZAKO, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NISAMEHE, NIOSHE, NITAKASE KWA ILE DAMU YAKO, FUTA JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, LIANDIKE SASA KWENYE KITABU CHA UZIMA WA MILELE; Amen.


Hongera kwa kuokoka, na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo. 

Kwa maombezi, Maswali, Ushauri na hata Sadaka yako kwa Mpeswa, Usisite kuwasilaina nasi. 

Mawasiliono; Simu au WhatApp: +255759859287 Baruapepe: ukombozigospel@gmail.com au tembelea pia YouTube Channel yetu ya Ukombozi Gospel au Ug Tv , www.ukombozigospel.blogspot.com Asante.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni