Jumapili, 17 Aprili 2022

FAIDA ZA USHINDI WA MATESO NA KIFO CHA YESU KATIKA SURA YA PITO LAKO

 Na Mwalimu Oscar Samba (Tafadhali #Share na kwa wengine ili nao Wanufaike)

Sehemu nyingine (3) ya Kitabu chetu cha MUONE MUNGU NYUMA YA PITO AU JARIBU LAKO. Ni katika mada yetu ya kwanza ya ; 1. Jinsi Mungu Anavyoweza Kuwa Nyuma ya Jambo Gumu Linalokusonga. Na katika pwenti ya mwisho ya mada hii: 

. Mfano wa Mateso ya Yesu na Msalabani: Nawiwa kukuhitimishia mada hii kwa mfano wa Yesu katika mauti ya msalaba. Leo sisi tunaweza kulielewa jambo hili maana faida zake kwetu zi dhairi ila kwa wanafunzi wake na jamii ile halikuwa jambo jepesi. Ndio mana ukisoma kisa kile katika Luka 24 cha wananchi wale waliokuwa wakielekea Emau utaelewa kiupana sana. Kuna mitazamo walikuwa nayo kuhusu ujio wa Yesu. Walimtazama kama mfalme na mkombozi wa dunia ile au kwa Wayahudi kwa jinsi ya kisiasa na kibinadamu.

Maana taifa hili lilikuwa chini ya utawala wa dola ya Kirumi. Kipindi cha nyuma walipokuwa chini ya tawala kama hizo kuna namna kuliibuka watu maalumu waliowakomboa; mfano walipokuwa chini ya Wafilisti Mungu alimuinua Samsoni na kuwakomboa: Waamuzi 13 na kuendelea. Walipokuwa chini wa Wamidiani waliibuka Gideoni na kuwatoa utumwani kwa mkono wa Bwana; soma Waamuzi sita utajionea pale.

Ndiposa katika Matendo ya Mitume 1 wanafunzi wake waliuliza swali kama hili. Sasa leo hii huyu mkombozi anatangaza kuwa atakufa, na hatimae kweli akafa; unaweza kuona ni huzuni na maumivu makubwa kwa kiasi gani kwamba aliyetazamwa kama mfalme wa kuwatoa utumwani ameshindwa na kusalimu amri mbele za watawala! Ni hakika ilionekana kama matumaini hayo tena. Na hata wale pia waliokuwa wamemuona kama mkombozi na kiongozi kwa jinsi ya rohoni akiwa ndie mwana wa Adamu bado haikuwaingia akilini maana mtu mkuu kama huyu kwao isingali kuwa raisi kuona anashindwa nguvu na maadui ambao hawakuwa na uweza kama wake.

Ndio maana Yesu alilazimika kuhakikisha anawaanda kisaikolojia na kiimani kabla ya tukio lile. Sasa mimi nataka maandiko haya yafanyike yako leo. Maana kuna mambo yanaweza kukukuta wewe ukaishilia kuona kama wanafunzi wake Yesu kuwa ni ishara ya kushindwa na kuaibika hali itakayofifisha ama kuzorotesha matumaini yako kabisa. Kama ilivyo kwa wanafunzi wa Yesu nasi leo kuna mambo hivyo, hivyo huweza kuwa na mtazamo nayo kumbe mbele yake yamebeba ushindi na furaha iliyo kuu kama nilivyokudokezea kwa kina kwenye utangulizi wetu. Kama hujusoma tafadhali hakikisha unasoma maana maandiko haya nimeyachambua katika upana wake kimfano zaidi;

Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye. Yohana 16:20-22.

Yanakuja kama mabaya kumbe ni mema! Unatakiwa kuona wema katikati ya ubaya! Hapa inatatikana kuwa na tumaini na kujifunza kumjua Mungu katika viwango vikubwa.

      Dhahabu ingeweza, ingegomakuingia kwenye moto. Maana maumivu yake ni makubwa na makali. Ila matokeo yake yana thamani nzuri na yenye tija zaidi. Uvumilvu na ustaimilivu wake ndio inayoifanya kuwa na thamani kuliko pale mwanzo. Bei yake huwa tofauti, ila ni baada ya kuvumilia. Mungu lazima atuandae kwa ajili ya thamani kubwa zaidi. Ukishilia kuona maumivu ya moto kama mateso na kutoroka kwenye tanuru hakika ni unajizuilia kuwa na ubora mkubwa zaidi. Uwe makini na Mungu akujalie hekima ya kunielwa!

Kwake Yesu:

1 au Mosi, Ilimpa Kutimiza Mapenzi ya Babaye. Maneno haya ya kutimiza mapenzi ya Babaye yamerudiwa sana hususani kwenye kitabu hiki cha Yohana. Mateso na kifo chake ndivyo vilivyobeba hatima kubwa ya makusudio ya ujio wake humu ulimwenguni. Na neno kubwa lilokuwa na changamoto katika maisha ya Yesu kuhusu kutimizwa ni hili. Ndio maana alipokuwa pale bustanini usiku ule wa kuamkia mateso ya msalaba na kifo chake kitu kikubwa mwili wake uliokuwa unapingana nacho ni hiki. Ila alimalizia vyema kwa kumwambia Mungu kuwa sio kama atakavyo Yeye Yesu bali mapenzi yake kama Mungu yatimizwe. Na hakika yalitimizwa. 

Na wewe tafuta sana mapenzi ya Mungu katika mambo magumu yanapokukabili. Usiwe mwepesi wa kulaumu adui zako au waliokusukumia huko kwenye shimo. Ndiposa utulivu na hali ya kumshukuru Mungu ni muhimu mno kama ninavyokufunza kwenye mada ya pili ili hali iyo ikupe kumsikia Mungu baada ya wewe kuwa na utulivu ambao hata akiongea utaweza kumsikia na kisha kumuelewa vyema na hatimaye kukubaliana naye.

Pili; Alifanikiwa Kushinda. Yapo mengi aliyoyashinda, adui wengi hapa walishindwa. Huku mmoja wapo akiwa ni Kifo na Mauti. Kitabu chetu cha ZIJUIE NA UZISHINDE ROHO ZA KABURI NA MAUTI kitakusaidia kuelewa zaidi hapa. Maandiko yanaposema na adui wa mwisho ni mauti hapo ni katika sura yeye hitimisho la hukumu ya pili. Ila ushindi wake ulianzia pale msalabani. Maana Yeye hakuona uharibifu kama Matendo ya Mitume inavyomnukuu Daudi katika Zaburi. Waebrania 2:14-15 inatueleza vyema kabisa jinsi mauti ya Yesu ilivyokuwa na nguvu kwa utendaji wa dhambi inayotokana na nguvu za mauti kwa Ibilisi. Ndiposa huweza kumshinda kwa Damu ya mwanakondoo na huo ushuhuda wake. Somo la Yesu kama Adamu wa Pili litakusaidia sana, natumai kwenye kitabu chetu tajwa hapo juu na kile cha SABABU ZA DAMU YA YESU KUWA NA NGUVU ILINAYO, na kile cha YESU KAMA NEEMA NA KWELI pamoja na kile cha MJUE YESU KROSTO vitakusaidia. Kwa jumla alirejesha ule Uadamu ambao ni sura ya Mungu uliondolewa na dhambi kupitia mauti yaani ule UHAI WA KIUNGU NDANI YETU. 

Ukijifunza kiupana somo la Damu ya Yesu utaelewa ni kwa nini katika Mambo ya Walawi 11:17 damu inatajwa kama Uhai, sasa uhai wa Damu ya Yesu ulirejesha uhai uliondolewa na mauti kwa kosa la Adamu. Maana waliambiwa hakika watakufa, na kifo kimoja wapo hapo ni kile kilichoondoa ushirika wetu au mahusiano yetu na Mungu. Ndio maana Damu ya Yesu huleta upatanisho kati yetu na Mungu. Ikirejesha ule uhai yaani mahusiano. Ndio maana baada ya hukumu ya pili ndipo mauti atamemezwa kabisa kwa maana kuwa hataweza kututawala wala kuitawala dunia tena ikimaanisha dhambi na kadhalika. (Niruhusu nitoke hapa na niendele na pwenti nyingine..) maana kuna upako nausikia naweza kuganda hapa muda na ni somo pana kidogo..

Tatu; Alitukuka na Kuinuliwa Juu Sana. Waebrania pale mwanzoni inaelezea jinsi jambo hili lilivyo. Ukija kwenye Wafilipi 2 anafafanua jinsi kunyenyekea kwake ikiwa na maana kuwa tayari kuachana na utukufu wa kimbingu na kuja kwetu kulivyomfanya kupata jina lipitalo majina yote ikiwa ni matokeo ya ujio huo pamoja na ushindi uliotokana na mateso na mauti ya msalaba. Tazama hapa; Matendo ya Mitume 2:36 Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

Alifanywa hivyo baada ya kufa na kufufuka. Tazama hapa tena: twende tena kwenye Waefeso 1:

20 aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; 21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; 22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo 23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.

Sasa unaweza kuelewa kuwa nini kingetokea au ni hasara kubwa kiasi gani ingetokea kama angekwepa mateso na mauti ya msalaba! Najua ilionekana ni kama ishara ya kushindwa na kuzalilika alipokua akilisema kabla ya kuipitia masikioni kwa waliowengi. Ndio maana Petro alimchukuwa kando na kumkemea. Kwa Wayahudi kutundikwa mtini ilikuwa ni adhabu yenye laana ndani yake. Ndio maana mzoga haukupaswa kulala au kushinda ama kuingia jioni ukiwa mtini (kusudi laana yake isiwe juu ya nchi). Alilaaniwa atundikwaye mtini. Wahalifu kama wezi ndio walikuwa wakipaswa kupitia hayo.

Sasa mtu wa heshima kama askofu, mwalimu mashuhuri wa sheri ama Rabi, mfalme wa Wayahudi ama Masihi anawezaje kutuambia kuwa anatakiwa kutundikwa mtini! Anatuambiaje atapitia ama imempasa kupitia mateso mengi huko Yerusalem! Haikuwaingia akilini, ila Yesu hakukubali kukwamishwa na mitazamo yao maana alijua faida yake ni kubwa mno. 

Ninakujuza haya maana kuna mambo unaweza kupitia leo yakaonekana ni kama uzalilishaji kwako ila uwe na hakika kuwa Mungu yupo nyuma ya hayo mambo ili akufanye kuwa mkuu sana. Ni kweli yanahuzunisha na kuzalilisha ila fahamu yamebeba kitu na hatima muhimu sana kwenye maisha yako ya sasa na ya baadae. Muda huu kweli ni aibu na uzalilishaji, ni kweli kabisa. Ila vumilia maana siku yatatu ilibeba ushindi na vigelegele kwa Yesu.

Alipokuwa kaburini walisema wamemshinda, wakasemezana kuwa yule mjanja alisema atafufuka. Kwa hiyo wanafunzi wake wanaweza kuja kumuiba na kusema kafufuka; wakapeana mbinu ya kulilinda kaburi ilikumzuilia. Uwe na hakika siku ya tatu ikifika tetemeko litakuja juu ya uso wa nchi na kukutoa kaburini. Ndoto yako leo inaweza kuonekana imezikwa ila uwe na hakika siku yako ya tatu inakuja nayo itatoka tu!

Wakijfanya kukaza kuizuia ndipo watapigwa na usingizi kama wafu! Nawe utatoka na kupita mjini kwa ushindi mkuu mno. Leo ni pa gumu maana kila mahali wanakuzomea ila siku ya tatu ikifika ushindi wako utajulikana tatu.

Kwa Wanafunzi, Kanisa la Kwanza na Kwetu Sisis Leo:

1 au Mosi; Alifungua Mlango wa Ujio na Uwepo wa Roho Mtakatifu Kwetu ama kwa Kanisa; Yohana 16.

5 Lakini sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi?  6 Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. 7 Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.

(Mali pengine anasema nitamuomba Baba naye atawapa, Yoh 14:16.) Ukisoma kitabu chetu cha NAFASI YA ROHO MTAKATIFU utayaelewa sana maneno haya.

Sote tunafahamu faida na utendaji wa Roho Mtakatifu kwa kanisa la kwanza na kwetu hivi leo! Huyu bila Yesu kuondoka asingekuja. Utendaji wake ni wa muhimu sana hususani kwa hatua au msimu mwingine ambapoo kanisa lilipaswa kuingia. Hata ukiendea na hayo maandiko hapo sura ya 16 utaona baadhi ya faida tajwa hapo.

Pili, Walifanyika Kuwa Mashahidi au Mashuhuda Wake. Ushindi wake upo katika ushuhuda wake. Na hawa ndio walioubeba na kuudhibitisha kwetu. Lakini pia huo ushuhda ndio nguvu ya injili tulinayo. Maana ushuhuda ndio neno. Hawawezi kuwa mashahidi nje ya ushuhuda. Ilibidi washuhudie ama wapitie hapo walipopitia ili kusudi waone na kusikia ndipo waweze kuwa mshahidi ama mashuhuda washuhudiaji. Ndiposa kuwanyamzisha ilikuwa ngumu sana, maana ukweli na uhalisia ulikwepo mioyoni na vinywani mwao.

Hakuna namna ungemzuia Filipo kwenda Samaria na kushuhudia, hakuna namna ungejaribu kumnyamazisha Stefano hata kama ni kwa kupigwa na mawe maana ushuhuda wake ulikuwa ukipiga kelele ndani yake. Hawakuweza na wasiningeweza kuwanyamazisha mitume maana waliona na kusikia;

Matendo ya Mitume 4:

18 Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. 19 Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; 20 maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. ni

Tatu, Injili Yetu Si Bure. Bali ni uweza wa Mungu uletao wokovu, kwa mchaga na mjaluo, mzaramo kwa mlugulu, mndengereko pia;  mmakonde kwa mmasai, mjaluo kwa mkikuyu, mbuganda kwa muuganda,mhuti kwa mtusi, mzungu kwa mwafrika. Kama Kristo asingalikufa basi kuhubiri kwetu kungekuwa bure, bali leo tuna ujasiri wa kumwendea mwarabu kwa mchina na mkorea tukiwa na nguvu hii ya wokovu.

Injili sio hadithi za kizee zilizotungwa na wanadamu bali ni uweza wa Mungu uletao wokovu na ondoleo la dhambi. Nje ya kifo cha Yesu hakuna hakikisho na uweza huu. Wengine wana vitabu na maandiko yao ya dini ila hayawezi kuwaokoa na dhambi wala kuwaepusha na jehanum ya moto na ule moto wa milele maana hakuna nguvu hii ya wokovu ndani ya maneno hayo ya vitabu vyao. 

Paulo mtume natuhakikishia hili; 1 Wakorintho 15:

14 tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. 15 Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. 17 Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. ni

Hakuna ondole la dhambi kama Yesu asingalifufuka. Kwa hiyo kama ungekwepo kipindi cha Yesu na kujaribu kumzuilia kufa msalabani kwa kuona kuwa ni kujiaibisha na kuiabisha taraja lenu juu yake ungekuwa unajaribu kufanya tukio lenye hatari kubwa sana sio kwako tu bali na kwa ulimwengu wote. Ungempatia Shetani mtaji kubwa sana. Maana hata yeye alikuja kuingia kwenye majuto maana hakujua alifanyalo. O

Kuna muda anajifanya mjuaji na kutupangia matukio magumu akizania anatukwamisha ila anapokuja kushangaa tulivyovuka na kuinulia anaishilia kujilaumu sana. Kama huwa anakuwaga na sehemu ya kujificha uwe na hakika huwa anaenda analia na kisha akija adharani anajifuta-futa machoziil tusijue kuwa kasikitika. 

Na kwa vile hatuna maandiko kumuhusu ili kupta taarifa zake baadaya kufufuka kwa Yesu hakika tungeona majonzi yake. Hapana shaka aliitisha kikao cha kujadili maumivu huko kuzimu. Uwe na hakika ndivyo inavyokuwa na kwetu tunapochomoka salama kwenye tanuru la moto na shimo la simba wakali. Ungeweza kufunuliwa kuzimu na ukamuona hakika ungemuona jinsi anavyokunja sura na kuinama chini.


Hata hilo unalolipitia leo, ndivyo lilivyobeba ushundi mkubwa na wenye shangwe  kubwa na zenye heri kwa wengine. Yesu angekwama, mimi na wewe pia tungekwama. Paulo mtume na mitume wengine wangekwama kwa yaliyowahi kuwakuta hakika mimi na wewe kuna mahali tugepungukiwa.

Na wewe ukikwama uwe na hakika wengi watakwama. Yona alitaka kukwama Mungu akahakikisha hakwami, ni kwa nini? Ninawi ingekwama. Na wewe kuna Ninawi yako. Umeandaliwa kwa kusudi tafadhali hakikisha unalifikia kwa ajili yako, ufalme wa Mungu na kwa ajili ya wengine pia.

Siwezi kumaliza kuelezea faida za ushindi wa Yesu ikiwemo kutukabithi sisi mamlaka maana baada ya hapo ndipo alipofufuka na kutuambia kuwa amekabithiwa vyote na kuviacha mikoni mwetu pia. La muhimu ni kufahamu faida za wewe kuvuka kama Yesu alivyovuka. Ila hili haliwezekani kama hatutajifunza kumuona Mungu nyuma ya pito ili uweze kulivumilia kwa  nia ya kunufaika na faida iliyopo.

Kitabu kikitoka kitafute tafadhali..o

Kama hujaokoka nikutie moyo kufanya hivyo tafadhali. Maana maisha ya dhambi hayampendezi Mungu. Wanaokufa kwenye dhambi mshahara wao ni moto, ila wanaokufa katika neema ya wokovu ni kuishi na Mungu milele. Tafadhali usiseme leo sijajiandaa, ama kesho, au kesho kuta, siku nyingine sio jibu sahihi. Hujui siku wala saa ya kuondoka kwako hapa ulimwenguni. Wapo wanaokufa kwa kugongwa na gari, kuugua ghafula na hata kufia usingizini. Alilala vizuri ila ndo hakuamka tena, alipoaga usiku mwema, kumbe alimaanisha usiku mwingine! Nani ajuaye wako! Huna hakikisho la kuishi milele na hujui siku wala saa, huwa inakuja ghafula.


Sasa fuatisha kwa imani Sala hii ya Toba pamoja nami: Sema, MUNGU BABA, NINAKUJA MBELE ZAKO, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NISAMEHE, NIOSHE, NITAKASE KWA ILE DAMU YAKO, FUTA JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, LIANDIKE SASA KWENYE KITABU CHA UZIMA WA MILELE; Amen.


Hongera kwa kuokoka, na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo. 

Kwa maombezi, Maswali, Ushauri na hata Sadaka yako kwa Mpeswa, Usisite kuwasilaina nasi. 

Mawasiliano; Simu au WhatApp: +255759859287 Baruapepe: ukombozigospel@gmail.com au tembelea pia YouTube Channel yetu ya Ukombozi Gospel au Ug Tv , www.ukombozigospel.blogspot.com Asante.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni