Alhamisi, 16 Septemba 2021

KARAMA YA KUONYA

Bwana Yesu asifiwe ndugu yangu katika Bwana. Hapana shaka u mzima tena buheri wa afya? Kama sivyo basi Bwana Yesu akupe amani na furaha tele, huku ukimtwika Yeye yale yaliyokulemea na iruhusu furaha yake itawale maisha yako.

Leo Bwana amenipaka mafuta kukuletea ujumbe huu muhimu sana. Sio mara kwa mara utasikia ukifundishwa japo ni kitu ambacho hutakiwa kukifanya kila sehemu. Mashuleni kuna maonyo, kazini, njiani, kwenye vyombo vyetu vya usafiri utasikia nako wakionyana, kwenye makusanyiko mbalimbali hili nalo lipo. Nyumbani na hata makanisani twapaswa kuonyana.

Nawiwa kukueleza kwa upana wake namna ambavyo tunapaswa kuonyana, na jinsi ambavyo karama hii hutakiwa kuwa na vitu muhimu ambatanishi aidha iwe tabia au roho fulani au karama saidizi kwayo. Haijalishi ni karama zinazojitegemea ila hapa zinapaswa kuambatana na hii, alikadhalika tabia ama tunda la Roho.

MSINGI WA KARAMA KIUJUMLA

1 Wakorintho kinaeleza kiupana kuhusu aina 9 za karama, na mbele yake kuna huduma tano zinatajwa. Lengo la karama na huduma ni kujenga mwili wa Kristo kama Waefeso inavyotanabaisha;

4:11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 

12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.


Tunaiona nia ya huduma/kipawa/karama ikiwa ni ili kuujenga mwili wa Kristo, na katika ile 1 Wakorintho 12 ananena jambo kiundani sana la kuujenga huu mwili kwa kila mtu akimaanisha sawa sawa na karama au kipawa chake ni mjenzi kwenye mwili huu yaani kanisa. 


Hapo anatumia pia neno kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu. Kumbe kazi moja wapo ya karama au kipawa ni kutukamilisha. Huku akitupa dhima nyingine ya kuhakikisha kazi ya huduma inatendeka. Ndiposa wachambuzi na waalimu wa mambo haya husema karama au kipawa ni silaha au dhana ya kutendea kazi, “tool” kama ilivyo kalamu, na dafutari na ufutio na rula kwenye ofisi au kwa mwanafunzi, alikadhalika, jembe, rato na fwekeo kwa mkulima bila kusahau panga na shoka.


Kazi moja wapo ya karama ni kuhakikisha huduma inatendeka. Nina somo huwa ninafunza na hata ukinikuta nafundisha kuhusu uongozi siachi kunena habari za jambo hili. Huwa ninawataka wachungaji, ama watumishi wanaongoza huduma makanisani kujifunza kutambua thamani au “potential” ya vitu ambavyo Mungu ameweka ndani ya watu wanaomzunguka ili aweze kunufaika navyo.


Musa kweli aliitwa, na alipewa maono ya ujenzi wa hema, na vitu vilivyokuwemo ndani yake, lakini kiukweli hakuwa amepewa kila kitu ndani yake kinachoweza kukamilisha hayo yote.


Ndi maan alimuhitaji fundi stadi ajaue kuuchonhga mti wa mshita n akumtengeneza sanduku la Agano, na ajuaye vyema kucnganya au kuifanya dhaabu ipambe mbao hizo. Alihitaji watu waliopewa karama na vipawa malaumu na Mungu li kufanikisha kilichomo ndani yake:


Kutoka 31:1-5 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda;

 nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,

 ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.


Ukisoma jambo hili katika sura zinazoendelea utajipatia upana wake zaidi. Kumbe ili Musa afanikiwe alihitaji watu, tena watu ambao Mungu amewekeza vitu vya thamani ndani yao.


Tatizo kubwa leo  ni kwamba watumishi walipewa thamana kama Musa wengi wanajiona wao ni Alufa na Omega, hawajui kuwa hata Mbinguni kuna Mgawanyo wa majukumu!

Ndio maana tuna nafsi ya Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, yupo aliyekuja na kutufia, yupo anayekaa ndani yetu sasa na kadhalika.


Ubinafsi umewafanya wengi kushindwa kutimiza maono yao, na leo wanajiuliza wamekosea wapi! Nakupa “Home Work” ya kupitia sura zinazofuatia na ujionee majukumu yalivyofanyika ambapo hata vitambaa na mavazi yalihitaji watu maalumu.


Sasa ujiulize ni kwa nini kanisani au kwenye huduma yako unataka ufanye kila kitu wewe? Hata kuombea sadaka ni wewe, kuzihesabu ni wewe, na wakati mwingine hata wanaohesabu huwaamini, vyombo ufunge wewe, kuimba uanzishe wewe, kinanda apige mwanao, gitaa apige ndugu yako, alafu unataka kufanikiwa. Pepo tu kukemea unaita familia yako! Ukiulizwa; unaogopa kupinduliwa ndo jibu lako!


Unaonaje Musa kama angehitaji kufanya kila kitu! Jifunze kwa ujenzi wa Hekalu la Sulemani, utapata kufahamu jinsi vipawa na vipaji vilivyotumika kusaidiana naye kwenye jambo lile! Sasa aliyekwambia na mwili wa Kristo yaani huduma aihitaji wajenzi mbalimbali ni nani! 

Ndio maana lugha ya hata huduma itendeke, kuwakamilisha Watakatifu na Kuujenga Mwili wa Kristo ikatumika sanjari na kila mmoja kuwa Kiungo katika huu mwili.


Usipojifunza kutambua nafasi ya wajenzi wenzako pamoja nawe utakwama tu! Sio kwamba utachelewa kufika bali hata kufika hutafika.


Wanaojenga barabara kwa njia au viwango vya lami huweza kunielewa, wajenzi wa nyumba kama za tofali na magorofa mbalilimbali huweza kunielwa. Hata zile za fito, utagundua kuwa huwezi kujenga mwenyewe, utahitaji wa kukushikia fito. Sasa kama wewe hata timu ya kusifu na kuabudu huwaamini utafika wapi sasa! Na Mungu akiona kuna vipawa umevikandamiza uwe na hakika kuna watu wazuri zaidi hatawapitisha mikononi mwako, maana aliyemwaminifu kwa kidogo hupewa zaidi, wewe mkandamizaji hata hao unaowapuuza kuna siku hutawaona tena na kwa ujinga utahesabu ni jaribu, kuwa adui anakupiga vita kumbe umejiloga kwa upumbavu wako mwenyewe!


Tatizo lingine ni jibu la swali hili; kwamba ni nani mwenye kibali kwako! Pili ni yupi anayepata nafasi katika utendaji wako. Ni lazima kujifunza kutenganisha hisia na upendo wako binafsi na jambo la majukumu. Yesu alimpenda sana Yohana aliyekuwa akiegema kifuani pake, ila ilipofika swala la kuweka sadaka aliona Yuda ndie mpakwa mafuta katika hilo. Ilipeofika jambeo la nani kiongozi mkuu wa kundi alimpatia Pita au Petro jukumu hilo.


Wangekuwa wahubiri wa leo Yohana huyu angepewa kila kitu.

Nataka kusema nini hapa! Kuna watumshi wanaochagua watu kutokana na wao kuwa na vibali zaidi mioyoni mwao. Huyo asaliye kuwa tu rafiki ila sio katika majukumu. Maana hatafanya kazi kwa sababu unampenda, kumpenda hakutampa ufanisi, bali kipawa na karama viwe kipaumbele.

Musa angeweza kumchag mtu yeyote katika ujenzi wa hema na vitu vyake, ila alifahamu ni nani ambaye Bwana amempaka mafuta katika hilo. Na Bwana akikuonyesha mtu ambaye hampatani, humpendi basi fanya matengenezo ya kimahusiano katika njia mbalimbali ikiwemo kutafuta ukaribu naye, pamoja na kuliombea jambo hilo ili ukuta huo udondoke na sio kwa ajili yako tu bali ni kwa ajili ya kuujenga ufalme wa Mungu.

Kamwe na abadani asilani fahamu kuwa Mungu hatahamisha kipawa cha uimbaji au utumshi kwa mtu fulani na kumpatia mtu uliyemchagua kwa mtakwa yako binafsi.


Turejelee swala la ni nani anakibali kwako. Kwa wengine ni wale wenye fedha, ni wale wanaowaletea maneno ya umbea, na masengenyo, kwao wale wanaoleta taarifa tena mbaya za uchonganishi kuhusu kundi hao ndo marafiki wao. Wapelelezi ndio maswaiba wao!

Ukifikia hapa uwe na hakika adui amekuvisha roho ya mambo ambayo Mungu anayachukia sana, utajisomea ile Mithali 6. Kuna Mithali pia ambayo huonya kuhusu maneno ya mchongezi, ni kama moto ambao huwa na mathara makubwa sana, mbegu ya chuki moyoni mwako itapandwa nakumea polepole baada ya muda tutashangaa tu una hasira na chuki kali kuhusu mzee wako wa kanisa hadi jamii inashanga ni kwa nini umemchukia hivyo mchungaji wako msaidizi na unamsambuli vikali, uwe na hakika kuwa hayo  ni matunda tu na usishangae uwepo wake bali chunguza upandwaji wake. Ni Mithali 26. 


Wengine mwenye kibali ni yule anayetoa sana sadaka, au mwenye kipato kikubwa. Hivi majuzi niliudhuria semina fulani mahali na nilimsikia muhudumu akisema kuwa kwenye simu yake hakuna jina la mtu ambaye huwa anamuomba fedha, majina yaliyopo ni ya watu wenye kumtumia fedha na alitaja na viwango. Na kushauri kuwa tusiwe na majina au na uhusiano na watu ambao hawatakupa kitu, aina ya watu huamua aina fulani ya maisha.

Ila si Yesu, Yesu alikula na maskini na matajiri pia. Maisha yake mengi aliambatana na maskini. Aliweza kushuka ama kujishusha na kuambatana na watu kama wakina Petro, walikuwa wavuvi na wasio na elimu. Mafarisayo waliokuwa wasomi na Masadukayo wenye sifa ya kuwa watawala hakuwa rafiki yao.


Roho ya kupenda fedha ikikutawala itakupa tabia za kuwapapatikia hawa watu. Ninamshukurtu Mungu hapa ni miongoni mwa maeneo ambayo nimepona. Toka nikiwa shuleni tena ya msingi na sekondari watu wa kawaida ndio rafiki zangu hadi siku moja mkuu wangu wa shule sekondari aliniita na kuniambia mbona ninaambatana sana na wanafunzi wa madarsa ya chini. Ila ukweli ni kwamba tabia za wanafunzi wa darasa langu hazikunivutia, baathi ni wavuta bangi na kadhalika. Hata leo marafiki zangu ni walio soma na wasio soma. Kuna watu wengine ubagua, ila haikuwa tabia ya Yesu.


Akija mwenye gari, mwenye kazi nzuri huyo baada ya muda atapewa uzee wa kanisa. Daudi alipokuwa anahitaji watu wa kumsaidia kuteka nchi Mungu alimletea wenye madeni, maskini na wenye majeraha mioyoni mwao, hao ndio waliokuwa askari wake wa kwanza. Kitabu chetu kile cha HEKIMA YA UONGOZI kimechambua hili bayana. Ila jiulize ni nani mwenye kibali kwako.

Kabila na undugu na ufamilia umeliteka kanisa leo, hawaangalii uwezo bali kuna sababu yuma yake.


Mambo hayo huwazuilia wengi kuwa na huduma yenye mafanikio maana pia huwanyima wenye karama ama vipawa kutumika vyema.

Wivu ni sababu kubwa sana. Hofu ya kuogopa kupinduliwa au kuwa na kibali zaidi yako. Musa angekuwa nayo hii hema la kwanza lisingefanikiwa. 

Tukiendelea na ile Waefeso 4 tunajifunza tena kuwa vipawa ama karama hutuwezesha kuwa na umoja wa imani, na kutuimarisha kiroho kiasi cha kuukuliwa wokovu kwa viwango vikubwa hali inayotufanya kuepukana na matatizo ya uchanga kiroho.


13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; 

14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. 


Kwa hiyo kanisa ambalo halikui kiroho, jibu moja wapo au mahali pa kuanzia ni katika matumizi ya vipawa na karama mbalimbali. Mchungaji ambaye anajiona yeye ni mungu mtu yaani ni yote katika yote (huku akiwa yu kipofu maana hata Mungu anamgawanyo wa majukumu katika nafsi ya utatu lakini pia malaika humsaidia, na watumsihi kama wewe na mimi tunajukumu hilo kwani Mungu hafanyi kila kitu, vingine ametuachia sisi) huduma yake haiwezi kuchanua ama washirika wake hawezi kukua. Umati wa watu sio hoja, maana pia ukiendelea hivyo napo kuna siku wataanza kupungua. Na wakipungu usiseme kuwa umepoa kiroho ama upako umepungua, bali fahamu sana kwamba ni matokeo ya wewe kuwa mbinafsi. Fundi mwashi, ama seremala pekee hawezi kuikamilisha nyumba. Tena siku hizi ameongezeka na fundi wa kuchomelea, maana milango na madirisha sasa wengi huchomelea, seremala huja kukuwekea vioo, na “fanicha” za ndani, bila kusahau kuwa paa aliezeka yeye.

Mwashi alichima na kujenga msingi na kupandisha kuta na kupiga palasta. Sasa ni zamu ya fundi rangi.


Vyoo vya ndani na miundombinu yote ya maji humuhitaji fundi bomba. Lakini pia siwezi kumsahau na fundi umeme. Ukimgomea utakaa gizani. Siku hizi kuna na fundi madishi ya runinga. Usipomtambua dishi likiyumba utasalia kuona chenga tu kwenye runinga yako.


Unathani na kufikiri kuwa kwa Mungu mambo haya hayapo! Yapo! Ndio maana tuna huduma kuu tano, na karama nyingi tena nyingi mno. Ili nini ili mwili hujengwe.


Kwani hata hosipitalini hakuna dakitari mmoja. Kuna wa vidonda, mwingine ni tumbo tu, tena la chakula maana la uzazi lina mtaalamu wake. Mwingine ni mtaalamu wa meno, huyu sikio, yule ni Ini yamkini na Figo, huyu ni mifupa na kadhalika.


Hakukosea kuwa na mgawanyo huo. Makanisani ukikataa karama za kinabii na huduma ya nabii na neno la maarifa uwe na hakika meamua kutembea gizani. Hapo nakujumlishia na ile ya kupambanua Roho.


Ukibeza na kuwa mvivu katika karama ya uponyaji, matendo ya miujiza na imani uwe na hakika hapo umemaua kumruhusu adui kuwa na nguvu katika miili yenu. Roho ni ya Mungu ila mwili Shetani atamiliki tu!


Mkigoma kunena kwa lugha sawa, ila fahamu kuna mambo hayataenda, maana ile … “ 1 Wakorintho14.4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake;..” ni sawa na kuwa na simu na “komputa” iliyoondolewa neno siri. Kuna mambo adui hawezi elewa unapoamua kuwasiliana na Baba kwa lugha hii. Najua kunena ni kwa kila mtu ila kuna kule kulikojaliwa zaidi. Nako kuna matunda makubwa zaidi makanisani. Waefeso 4 inatuongezea jambo tena:

15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. 

16 Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo. 


Shika sana neno “kwa msaada wa kila kiungo,” ambapo ulionapo hilo waweza weka neno kwa msaada au utendaji wa kila mwenye karama au huduma. Ambapo hulifanya kanisa kushikana, au kuwa na umoja na kuongeza upendo kanisani. Kwa hiyo ukiona umoja na upendo umepungua uwe na hakika kuwa kuna udhaifu kwenye utendaji huu. Mana hayupo mwenye kukarimu, yupo mwenye kufadhili, yupo mwenye kutembelea walio shindwa kuja kanisani, yupo mwenye kutia moyo waliovunjika, yupo pia mwenye kuonya na kukaripia ili kulifanya kanisa lishikane. Maana yake lisilegee bali liwe imara katika nguvu na uweza. Gari ambalo “matahiri” yumba huwa na shida sana linapotembea. Madereva wa pikipiki na baiskeli huweza kunielewa, kuendesha baiskeli yenye “play” yaani iliyolegea gurudumnu ni hatari na karahaa pia.


Ndivyo ilivyo huduma ambayo karama nyingine zimefinyiliwa. Na wnegine hajazifinyilia ila adui amewapiga upofu washirika wasijitambue au watumsihi pamoja na mtumishi. Na wengine adu amewaweka jela kam Yusufu amabye na akili na hekim azake zote alikwua jela hadi Mungu alipomoa na kuisaidia nyumba ya Misri na dunia yote kwa ujumla.


Ni muhimu kwa mtumishi kujifunza kuliombea kanisa au kuiombea huduma yake ili anaowaongoza na wanaomsaidia karama zao adui aziachie na kuwaombea wahusika wasiwe ama wasimezwe na shughuli nyingi…namuomba Mungu anipe kibali cha kukuandikia kitabu kihusucho karama, naona ipo haja maana ni muhimu kujua maadui wa karama hizi akiwemo mtu mwenyewe, na watu wengine pia, Yufu aliuzwa na kuondolewa nyumbani, Daudi wazazi wake hawakutambu kilichomo ndani yake na kuishilia kumsukumia tu porini, Sauli alimpiga vita hali iliyomuyumbisha haya yeye mwenyewe, Farao alipotambua kilichomo ndani ya Yusufu alinufaika na kufanikiwa sana. Alipata heshima duniani ambayo yakaa hadi leo kutokana tu na akili na hekima iliyokumwe ndani ya Yusufu. Ila angepuzia angekwama mahali.


Mistari hii miwili na unaweza kuongeza na ule unafuatia, itakupa kupata onyo muhimu kuwa usienende kama wengine ifikapo swala la matambuzi na kutoa nafasi kwa vipawa hivi. 

17 Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; 

18 ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao.

Sasa mara baada ya hapo niruhusu nikupatie dondoo muhimu kuhusu KARAMA YA MAONYO.

Ni karama yenye changamoto ya aina yake. Tofauti na nyingine, kama ya utendaji wa miujiza na ile ya uponyaji, mara nyingi hupendwa na kushangiliwa na kila mtu. Za ukarimu, na kutia watu moyo, zenye fadhili ndani yake huwa na changamoto tofauti na hizi. Mara nyingi ni kutoka kwa anaekuonea wivu. (Japo muhusika huwa hatarini na kutekwa na kiburi au kutwaa utukufu wa Mungu. Changamoto ambayo ni hatari sana, sifa na kujikuta unajenga mahusiano na watu ya kiutukufu ni hatari moja swapo nyemelezi.)

Ila hii ni moja kwa moja kutoka kwa watu unaowaonya, au unaowasaidia.

Na adui ni rahisi sana kuwatumia na kuwafanya kuwa adui zako. Wakati mwingine hata watu kama wachungaji huweza kukukasirikia kwa hofu ya kuogopa kupoteza washirika.

Wengine wakionywa hukimbia kanisa, wengine hukusema vibaya na kuna ambao hulegeza ushirika na wewe na wapo ambao hukuchukia kabisa kwa maana nasio kwamba tu wanalegeza ushirika na kuwa mbali na wewe bali huwa ni adui yao moja kwa moja.

Chanzo kimoja wapo cha ujumbe huu ni leo asubuhi nikiwa kwenye maombi ya asuhubi hapa chuoni, nilijikuta ninakumbuka kisa fulani. Kuna binti ambaye ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana naye, na ilikuwa ni nyumbani kwao, mama yake ni mtu aliyeokoka vizuri tu. Na binti huyu alikuwa anasoma chuo kikuu.

Ghafula roho yangu iliugua sana, na kujikuta nashindwa kustaimili, ndani yangu yalitoka maonyo, na nilimuita pembeni na kuongea naye. Sasa kibao kilikuja kunigekia kwa mzazi wake kufikia hatua ya kuhisi labla nilimpenda mwanae ndio maana nilifika nilipofika.

Aliamaua hadi kuchunguza maisha yangu ya kindoa ili kujua kama nimeoa au la maana yamkini nataka kuchumbia kwake. Sikumlaumu, na wewe usiwalaumu wanaofika mbali hivyo, japo nia yake inawezakana sio mbaya ila uelewa wake ukawa ni mbaya.

Kusingiziwa tuhuma, na hata kushutumiwa moja kwa moja na kwa ukali ni shemu ya mirejesho ya huduma kama hizi.

Kuna mabinti fulani waliokuwa wakisoma kitacho cha sita, matokeo yao ya mtihani mmojawapo wa kujipima kabla ya ule wa mwisho yalikuwa mabovu sana. Nami nikiwa kama baba yao kiroho, ndani yangu kuliwaka hasira kali, ambayo sikuweza kuizulia, nami niliiachilia katika ukali kama ilivyostahiki, na kuonya sana kuwa mbele hawatapita au kufanikiwa kama hawatabadilika.

Watoto wale walinichukia hadi leo, imepita miaka kadhaa lakini chuki ile ingalipo. Sasa sijui hawakutaka kuonywa au kukemewa, ama walifikiri kuwa baba ni maneno matamu tu. hawakufamu kuwa baba ni zaidi ya kuitwa ”Dady,” nafasi hii ina ambatana na majukumu muhimu ikiwemo ya kuonywa, na wakati mwingine kwa ukali na kwa makaripio, fimbo na rungu ni kwa ajili pia ya maonyo. Kwa bahati mbaya sana matokeo yao hajakuwa kuwa mazuri! Unajua ni kwa nini?

Nia moja wapo ya maonyo ni kukugeuza, Mithali husema kuwa geukeni kwa maonyo yangu! Unapo  yakubali maana yake unanui au unakubali kugeuka, napo ndipo msaada wa Kiungu huwa pamoja nawe, fadhili na rehema huambatana na yule aliyeyakubali maonyo. Kitu Roho alichonishuhudia kuwahusu ni kigumu hata zaidi ya kutokufaulu kwao vizuri katika matoke hayo. Ni kwamba kuna ukuta walijiwekea ambao utawasumbua hata kwenye ajira. Sasa leo sizungumzi kuhusu anayeonywa, ambapo nimemuandikia vitabu kadhaa ikiwemo cha MOYO WA UFAHAMU, NAFASI YA AKILI KATIKA KUKUNUFAISHA KISHANI, na kadhalika. Wasomaji wa kitabu cha Mithali huweza kunielewa kiupana sana, na kama nikipata kibali cha kukuandikia kitabu cha KARAMA basi hapana shaka kipengele hicho nitakiandika katika sura ya kikarama sasa.

Ni kweli ile ye 1 Wakorinth 12 inatupatia karama 9, ila biblia imeendelea kutuchambulia zaidi. Tujionee kwenye Warumi 12. 6 Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; 

7 ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; 

.8 mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.

Hapo ndipo panapotupatia karama ya kuonya. Kuonya huwa na maana ya kukataza, au kumueleza mtu kuwa hayupo kwenye njia sahihi na badala yake humtaka kuachana na njia hiyo na kuendea iliyo sahihi. Maonyo humtaka mtu asitende, ama kutubia alichokitenda. Kumfanya mtu kujiona mwenye hatia ni kusudio la maonyo, kumfanya mtu kuona uchungu pia ni kusudio la maonyo, sio ili angamie bali ni ili ajirudi, ndio maana kwa mwenye ufahamu sahihi wakati anamtenga mtu kanisani hatakiwi kumfanya au kumchukulia kama mtu aliyechukiwa bali ni sawa na kumtoa mtu funza, humtoi kwa kuwa unamchukia bali ni kwa kuwa unampenda. Na kuvumilia mabaya ni kumchukia mtu bali kumpenda ni kumuonya. Upendo ndio unatufungulia pazi lifutalo:

KANUNI AU TABIA AMBATANSIHI KATIKA KARAMA HII YA KUONYA.

Kipengele hiki kitaisaidia huduma yako kutokuwa na mikwaruzo isiyokuwa na mantiki, itamzuilia pia adui Shetani kupata uhalali wa kuidhuru au kuishambulia, au kupenya hapo. Maana kuna wakati badala ya kuonya kwa lengo la kusaidia huwa tunaonya huku tukizaa maumivu na majeraha, kitu ambacho sio lengo. Kama ni maumivu na majeraha basi yawe ni kama kidonda cha “oparesheni” ambacho nia yake ilikuwa njema kabisa, na muhusika atatulia na kukitunza. Ndio maana kuna na huduma au karama ya kurehemu, kutia moyo na kadhalika.

1. Onya kwa Upendo. Upendo uwe ndio msingi wa kuonya kwkao, mweney kuonya kw aupendo atafuatilia hadi mwisho wa muhusika, hata kama muhusika atamjibu vibaya ataweza kuchulina naye maana upendo huchukuliana, hata kjama jeraha la kupasuliw akwe limechukuw amuda kupona upendo utatafuta dawa. 

Ukiona mtumishi amemuonya mtu na hataki watu waende kumtia moyo, uwe na hakika huyu amejawa na roho ya chuki, na maonyo ya aina hii ni mabaya sana. Ukiona unamuonya mtu na hutaki kukutana naye, au ukikutana naye ile hasira bado inawaka ndani, uwe na hakika kuna roho nyingine ilikuvaa na hukuonya katika hekima wala msukumo wa Kimugu.

Tumuone Paulo mtume baada ya kuwaonya hawa watu, utagundua kuwa alikuja kurudi tena kwao akiwa na dhima ya kufuatilia maendeleo yao. Panya buku akiwa anamngata mtu huwa anapuliza kwa lengo la kukupa ganzi ili aendelee kukungata, ila sisi huwa tunapuliza kwa lengo la kukuponya, ndio maana baada ya upasuaji huwa kuna dawa unapewa za kuponya kidonda, kwa maana upasuaji ulikuwa na lengo zuri tu! Na uponyaji ni muhimu maana na uonyaji huo ulibeba nia ya dhati.

2 Wakorintho 7:8 Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu. 

9 Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. 

10 Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. 

11 Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.

Kumbe nia ya kuonywa ni ili utubu, huzuni inayokuja ndani yako ni ili utubu! Ndiposa kwa unayeonywa ni muhimu sana kuwa makini, maana huzuni ijapo ukiingiza kiburi itageuka na kuwa huzuni ya mauti, ambayo sio ile ya Mungu.

Yuda Iskariote alipogundua kosa ilizaliwa huzuni ya mauti na hatimae kujinyonga, ila Petro alitubu ni kwa sabahu ilikuwa ni huzuni ya Kiungu.

Wote wawili walionywa na Yesu, ila Petro alipokumbuka maonyo alitubu. Mwenzake aliishilia kujitundika.

Unapoonywa kanisani na kukimewa kwa kosa fulani huwa unafanya nini? Huwa unatubu na kubadilika, au huwa unajinyonga kwa kuhama kanisa au kuzira huduma, au kumsema vibaya anayekuonya?

Sijui kama huwa unafahamu maana ya andiko kuwa kwa mwenye kiburi kuna fimbo..ni andiko la Mithali. Unapoonywa na kuzira kuimba kwaya, uwe na hakika umetumia fimbo ya kiburi, umeamua kumuadhibu anayekuonya kwa staili hiyo. Unapoonywa na kuogoma kwenda kanisani, uwe na hakika umetumia fimbo ya kiburi kumaudhi aliyekuonya, naye akiwa dhaifu siku nyingine hatakuonya tena. Unapoonywa na kugoma kutoa sadaka au kufanya jambo ulilokuwa unalifanya uwe na hakika unatumia fimbo ya kiburi.

Kwa hiyo ukimpenda mtu utafuatilia na mwenendo wake badaa ya kuonywa. Ukio na kidonda hakiponi, utamuombea na kumtia moyo. Kuna aina fulani ya mahusiano ya karibu utayajenga ili kuponya jereha ndani yake.

Unaweza kuonya kwa njia sahihi kabisa, ila muhusika akajeruhiwa kutokana na upumbavu wake, au jinsi alivyopokea vibaya maonyo hayo. Au maneno ya wapambe, ambao huja na kumueleza kinyume cha nia ya muonyaji, huyu naye anahitaji msaada wako. Kuna wengine kweli hutumia njia isiyosahihi ambayo huzaa majeraha, napo unahitaji kujishusha na kuomba radhi, ikiwa ni kusanyiko sawa, maana kujeruhiwa kwa mtu mmoja huweza kusababisha mthara kwa kunsanyiko kubwa.

Na muhusika mtafute muombe radhi. Huwa najifunza kwa Yesu jambo hili. Petro alipomkata mtu sikio Yesu aliomba msamaha! Sasa kama Yesu aliomba radhi kwa kosa la Petro, wewe si zaidi kwa makosa yako, au kwa makosa yaliyofanywa na kiongozi wa kwaya, au mzee wako wa kanisa. Msamaha ni dawa kwa aliyejeruhiwa na kwa kwaya nzima, au idara fulani.

Lakini pia Upendo Hauvumilii Mabaya. Kumpenda mtu ni kumuonya, upendo ukitawala maisha yako, hutaacha kuonya. Yesu alimpenda Petro na Yuda Iskariote ndiposa aliweza kuwaonya. 1 Wakorintho 13 tunaifahamu kuwa inabeba thima muhimu ya pendo, ambapo pia hatuachi kuutazama kama karama huku pia likiwa  ni tunda la Roho. Kwa hiyo ni zana ya utendaji na ni tabia katika/kwa Mkristo na huduma au na Ukristo. Mstari ule wa 6 unatumia neno muhimu sana; “ haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli.” Ukijiona unamezea mabaya ya mzee wako wa kanisa, uwe na hakika sio kwamba unampenda bali ni kwa sababu anakupaga mikate, ukiona unavumilia au unachekelea na kufunika makosa ya mtu fulani, sio kwa kuwa ana kibali moyoni pako bali ni kwa kuwa upendo ule wa kweli umetoweka na una upendo wa maslahi binafsi. Maana kama ungempenda kipaumbele chako kingekuwa ni yeye kwenda mbinguni. Ukiona umefikia mahali ambapo bora aende jehanum ila wewe unufaike na fedha zake, uwe na hakika umeshavamiwa na roho ya kikatili tayari.

Ukiona unahubiri kwenye kanisa ambalo mchungaji wake hataki ukemee dhambi, uwe na hakika upendo wa Kiungu ndani yake ulishakufa, bali amesalia na upendo tumbo. Yesu alihubiri injili ngumu na badae akagundua wameenda na kumuacha, aliwagekia wakina Petro na kuwauliza na ninyi mwataka kwenda!

Sasa sina maana kuwa ukose hekima na kuanza kuropoka huku ukitawanya na kusema kuwa bora kubakia na watu wawili wanaoenda mbinguni kuliko watu wengi wasio sahihi!

Maana adui pia amewamezesha watu roho za namna hii. Hekima ni muhimu sana. Ezekili 34 inanena vizuri sana kuhusu kuwafunga majeraha na kurejesha walio fukuzwa, haya ni majukumu yako. Kunakupiga kwa kuuwa na kuna kuchapa kwa kufunza. Kuna namna unamkabili mshirika na kwa usalama wake inabidi suluhu liwe ni yeye kuhama hapo. 

Nilipokuwa mdogo kuna siku nilikuwa na mfundisha mbwa wangu maoezi, sasa sikutumia akili, labla shauri ya utoto, nilikuwa namrusha juu kama mpira, nikithania ndo mazoezi ya mbwa hayo. Mbwa aliendelea kunivumilia, ila siku moja, alichomoka na kwa mbio alizochomoka nazo nilijua kabisa huyu hawezi kurudi.

Na kwa kweli hakurudi hata na hivi leo. Kuna washirika wanajeruhiwa vikali kutokana na kukosekana kwa hekima, na mbio wanazochomoka nazo ni sawa na mtu aliyetolewa jela kwa msamaha wa rais, huwa harudi tena kumsalimia bwana jela, bora hata aliyemaliza kifungo ila aliyetoka kimuujiza huwa ana kahofu fulani.

Kumbuka pia upendo huchukuliana, huvumilia, hakumbuki wala kuhesabu mabaya, Mistari ya juu yake imebeba hii dhima, kwa hiyo utamuonya kwa kumchukulia, sio kama mtu aliyemchoka na kumkinai sio kana kwamba kosa lake haliwezi kubadilishwa. Maana hata Yesu asingechukuliana nasi basi tusingeweza kufanyika wake. Kama pendo lake lilivyotuvuta na sisi upendo utuongoze vivyo.

2. Onya kwa Upole: Ni kweli neno upole kwenye biblia halina maana ya kuvumilia mabaya na kuwa mkimya katika mambo yasiyofaa, maana hata Yesu anaitwa mpole na mnyenyekevu wa moyo lakini bado alipindupindua meza, na kuwambia kuwa mmefanana na makaburi ambayo ndani yake yana mifupa ya wafu na nje yake chokaa, akisema kuwa kamwambieni yule mbweha leo natoa pepo ... na kadhalika na kadhalika.

Lakini bado dhima ya upole huwa inajulikana. Kuna aina ya ukali ambao sio upole, na kuna aina ya ukali usio sehemu ya upole. Hasira zisizo na maana ama zilizo na chanzo cha chuki, na majeraha, na zile hasira ambazo hazitendi haki ya Mungu ni kinyume cha upole. Ndani ya upole kuna dhima au nia au hali au taadhari ya kuhakikisha muhuska hajeruhiwi. Bali anaponywa. Sio jambo la nia tu bali na njia ya kufikisha jumbe.

Upoleo  haumpi mtu kukurupuka, kuhamaki, kwani hauna ghabu ambayo inamfanya mtu kulipuka, na akidli ikikaa sawa huja kuomba radlhi au ndipo hugundua kuwa alifanya makosa.

Upole hauna hasira ambayo hutajwa kama mwenda-wazimu. Kuna aina ya hasira ambayo humfanya muhusika kuwa kama kichaa. Huyu kakosa upole. Kitabu chetu cha IJUE NA UISHINDE HASIRA kimefafanua hili bayana na kiunaga ubaga.

Unaweza kumuonya mtu naye akawa anacheka, na kufurahi ila kwa njia ya ndani onyo limepita na kumuingia sawasawa. Japo sina maana ya kwamba ukali usitumike, ila sio ule wa hamaki, jaziba, na kulipuka. 

Huo huaribu, na kuna muda tu katika utulivu huweza kuachilia matengenezo.

2 Timotheo 2.24 Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; 

25 akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli. 

26 wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.

Upole ni njia ya kuwapata watu wengi sana, maana yake bila taharuki, bila jaziba, bila kuropoka na kuongea maneno yasiyofaa, bali katika hoja, katika kuonyesha tatizo na ufumbuzi wake, ndipo tunavyopaswa kukabiliana na watu. Maneno kama mtalaaniwa, wajinga nyie, na kila vitisho sio sahihi kwa mahali fulani au wakati fulani, vitisho vipo sawa, japo navyo katika hekima yake, ila katika upole kuna namna unatawasilisha maonyo vizuri zaidi maana upole huficha ile jaziba ambayo utashi na ufahamu wa kawaida wa kibinadamu hutoweka unapokuwa au unapowakwa na hasira! Majuto kama ilikuwa ni hasira tu nisamehe hayawezi kutokea.

Ukiendekeza hali ya jaziba utajikuta unaugua magonjwa ya moyo! Licha ya kujeruhi wengine utajikuta na wewe unajeruhiwa! Hukuwahi kuona wachungaji ambao siku wanaonya au kukaripia na ujumbe mzima unavurugika!

Msipokaa vizuri mtajikuta mnahubiriwa majeraha tu yaliyoko moyoni mwake, na anaonya au kumuonya mtu mmoja lakini kundi zima au wote walioudhuria ibada siku hiyo wanajeruhiwa!

Unaonya, alafu baada ya hapo unatabasamu, na kuendelea na kazi ya Mungu vyema. Ila ukionona umenya kanisani, hadi nyumbani ile hasira imekuka, au hasira ya makaripio ya kikao cha jana alasiri na wazee wako wa kanisa zimeamakia kwenye ibada jumapili, uwe na hakika upole umekaa pembani, na kwa hatari hiyo magonjwa ya moyo yanakusubiria mlangoni. Kuna watu wakiumizwa au kuchukizwa wanageuka mbogo! Anakasirika hadi vikombe na vijiko vinatamani vijifiche. Kama kuna paka karibu au mbwa atakimbia kama ni kuku atoa sauti ile anayoito amuonapo kicheche au mbweha maana hatari imekaribia!kama ni njiwa basi utawaona wakiruka na kukimbia! Ukifikia hapo kuna shida katika upole. Kitabu chetu cha TUNDA LA ROHO na kile cha TUNU ZA UNYENYEKEVU vitakusaidia sana.

Wagalatia 6 : 1-18 

6:1 Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. 

2 Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.

Upole na upendo vinatupa kuchukuliana mizigo. Hutaishilia tu kumuombea kikawaida, bali utakuwa ukifunga na kuomba kwa ajli yake. Utachuka muda zaidi na kuandaa mafundisho na kumpatia, sanjari na kuhakikisha unamsaidia zaidi na zaidi kuhakikisha anaichukia hali aliyonayo na kuhitaji msaada wa Mungu.

Kuna watu ambao hawajitambui, wanaona tabia na mienendo yao ni sehemu ya maisha, mnaowaonya mnachukuliwa  kama vile mnawachukia. Sasa upole utakupa kuwa na muda naye, na kumuelewesha jinsi jamii inavyomtazama na kuchukia hali yake au ainayotazama na kuwatazama watu wenye madhaifu kama hayo, huku ukimsomea na kumuonyesha kwenye maandiko athari za hali hiyo, na jinsi waliofanya vitu au kuwa na mwenendo kama huo jinsi walivyokuja kuishilia mahali pa baya. Na zaidi utamtia moyo Mungu anaweza kumsaidia, na kumvusha hapo. Ya kwamba aliyembadilisha Paulo na Petro na kuwafanya kuwa vyombo viteule yu aweza na kwake pia.

Ya kwamba aliyemgeuza Rahabu aliyekuwa kuhaba na kumuingiza kwenye ukoo wa Yesu anaweza kuyabadilisha na maisha yake pia.

Fahamu sana kuwa upole ni tunda la Roho, kwa hiyo muombe Mungu akujazi baraka na neema hii au tabia hii ya Kiungu.

Japo anayeonywa naye hutakiwa kulipokea hilo neno katika upole; Yakobo 1:21 Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.

Ukiona unamuonya mtu anarusharusha mikoni, mishipa inamtoka, uso unakuwa mwekundu, huku akikunjia ndita uwe na hakika kuwa kuna shida kwenye moyo wake. Uwe mpole na uwe mtu mwenye kuonyeka. Hauonywi kwa sababu umechukiwa bali ni kwa sababu umependwa, ni sawa na kutoa kupe kwenye ngozi ya ng’ombe sio kwa sababu haumpendi na unafurahia mamivu anayoyapata bali ni kwa sababu unampenda.

Uliwahi kuchomwa na mwiba! Vipi uliuacha hapo hapo mguni au uliutoa! Natumai uliutoa! Sasa wakati unautoa hukuumia!

Mbona unasema na unaendele kushikilia maneno kama vile ameniumiza sana, amenijeruhi sana! Natumia ulipochomwa na huo mwiba ulipaka hapo dawa baada ya kuuchomoa!

Sasa mbona na wewe haupaki ya rohoni! Au  uanyunyizi Damu ya Yesu kwenye moyo uliojeruhiwa na mahubiri yale! Kama alikosea muachie kosa lake yeye mwenyewe, wewe songa mbele, na kama ni tabia yake wewe ombe upewe ngao kwenye moyo wako ili likija jingine lisikupate bali ligonge hapo kwenye ngao.

Mistari ya juu yako hapo kwa Yakobo kabla ya kukutaka kupokea hilo nenn kwa upole, inakutaka kuwa mwepesi wa kusikia maonyo kuliko kujibu na kujibishana ama kuwaambia wenzako lakini alinionea, mbona hakuniita kwanza pembeni, mbona aliongea sana  au alifanya hivi na vile, na wengine unapowaonya ni wepesi sana wa kujitetea, na wapo ambao ni wepesi wa kukasirika, badala ya kufurahia maonyo;

Yakobo 1:19 Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; 

20 kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.

3. Uwe na Hekima Inayoendana na Rika, Cheo au Heshima ya Anayeonywa. Ni lazima kujua kuwa kuna utofauti wakuonya mtoto, kijana, mtu mzima, mzazi wako, mzee w amanisa, Shemasi au Kiongozi wa Idara na hata Mtumishi wa nafasi moja na wewe.

1 Timotheo 5 :  

1 Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; 

2 wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote.

Kuna mambo mnaweza kuonyana nyumbani na mke wako, usiyalete mbele za watu na mengine ni ya chumbani sio mbele ya watoto na wageni. Wazee wako wa kanisa malizaneni ofisini alikadhalika na watumshi wenzako. Kosa likifikia la madhabahuni ni kwamba ufumbuzi umeshindikana ofisini kabisa. Na hata kama ni kosa  lililotendeka madhabahuni kama halina athari kubwa mnaweza tu kuja kuonyana kwenyo vikao na hata kwa njia ya simu.

Fahamu sana kuwa unapoonya madhabahuni kuna hatari ya kujeruhi wengi, hususani kama kosa halina ukubwa huo ama njia kama itakuwa mbaya yenye jaziba au uzalilishaji ndani yake.

Zingatia umri na cheo cha mtu au nafasi yake, kuna wengine unapaswa kuonya kama vile unashauri sio kila mmoja utamkaripia. Mchungaji mwenzako hata kama ni maskini au umri wake ni mdogo, heshimu nafasi yake. Epuka kutumia njia ya kuonya kama sehemu ya kumzalilisha mtu ili kumuondolea kibali na heshima au hathi fulani. Kuna hatari ya hali hii kuja kukurudlia wewe, husani kama muhusika ataamua kumgeukia Mungu.

4. Tumia Njia ya Ukali. Kuna muda ukali unahitajika, makaripio na makeo makali pia, la muhimu ni lugha isiwe ya kibabe, ya kuzodoa, kubeza, matusi, mazalilisho, kiburi, yenye majivuno na kila aina ya maneno ambayo sio sahihi kibiblia na kimaadili. Kuna ukali usio na maneno yenye kuudhi bali wenye kuonyesha hisia za kukerwa na kutokurithishwa na jambo. Utakwa na njia nzuri kama tu muhusika anayeonywa hatajawa na uchungu na ile hasira ya kibinadamu badala yake iwe ni hasira takatifu ili itende haki ya Mungu. Japo katika ukali kumbuka kiasi, tunda la kiasi ni muhimu sana hapa. Sijaliweka huku ila katika kuonya, muhusika lazima ajawe pia na kiasi, sio kila siku, kila wakati wewe ni makaripio na maonyo tu. Kuna na muda wakupongeza; Haleluya haleluaya, natumai tunaelewana vyema.

Yesu alipopindua pindua meza ilikuwa ni ukali, pale huwezi zipindua ukiwa umeketi au na maneno laini, lazima maneno mazito na vitendo vikutoke. Sasa sina maana na wewe ukavunje vyunje vyombo vya sauti la! Nataka tu kukuonyesha dhima ya ukali hapo. 

Paulo huyo huyo aliyemtaka mwanaye kuwa na mbinu ya kuonya kutoka na rika na mahali pengine kutuambia kuhusu upendo na kiasi, ndie huyo huyo anayetaka matumizi ya ukali yawepo. Akitumia maneno kukaripia na kukemea;

2 Timotheo 4:2 lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.

Ila usisahau na kuvumilia kupo, lakini pia mafundisho kama tutakavyojionea hapo mbeleni.

Andiko nikupalo licha ya kuunga mkono hoja hii inayokutaka kutumia ukali, nikiwa na maana kwamba pia ni njia sahihi tu, lakini pia inatupa kufahamu kuwa ukali huu unapaswa kuwa ni mbadala ya upendo, na upole, na upendo tajwa hapa ni ule wenye nia ya kumsaidia mtu kwa kumfanya kwanza kuwa rafiki, kuna muda unajenga urafiki na mdhaifu ili umsaidie, japo Paulo kwenye ile Wagalatia anatutaka kuwa makini ili tusimezwe naye. Ninaongea hili kwa nia ya kuepuka hoja kwamba katika ukali hakuna upendo la, upendo ndio msingi wa maonyo yoyote yale, nje ya hapo ni kufanya vita na mtu!

Kwa hiyo, kuna njia mbili hapa, ya ukali na upole wenye pendo wa urafiki au ukaribu ndani yake. Paulo anauliza swali hili akitupa kufahamu jambo muhimu hapo. Ingawaje kuna kosa jingine ndani yako moja kwa moja inakuja njia ya ukali, na hii ina mazingira yake. Mruhusu Roho akuamulie, ila usiwe na fikra za kila wakati ni ukali, au kila wakati ni upole ule wa utulivu, kuna muda unahitaji ukali japo ndani yake kutawaliwe na upole ule wa Yesu na Upendo wake;

1 Wakorintho 4:21 Mnataka vipi? Nije kwenu na fimbo, au nije katika upendo na roho ya upole? 

5. Fundisha, Kuonya kwa kufundisha ni muhimu sana. Pia uwe na muda wa kuwafundisha namna ambavyo wanaweza kukabiliana na tabia au roho wasizozipenda. Kuna wenye kiburi lakini hawakipendi, na wanateseka namna ya kutoka kwenye hilo gereza. Kitabu chetu cha IJUE NA UISHINDE HASIRA ni matokeo ya msaada nilioombwa na binti fulani akinitaka kumsaidia kuepukana na hasira. Ambayo licha ya kutaka kuadhiri masomo yake pia ilikwa ikihasiri uhusiano wake na mzazi wake au jamii kwa ujumla.

Kitabu chetu cha TUNDA LA ROHO, TUNU YA UNYENYEKEVU na hata kile cha YESU KAMA NEEMA NA KWELI, vimejaa mbinu muhimu ya kupukana na vitu kama hivi, sanjari na kile cha MOYO SAFI. Ni muhimu kuwafunza na kuwatia moyo.

Mapito ya ndoa na vikwazo kadhaa vilinipelekea kuandika kitabu cha ISHI SALAMA KWENYE NDOA CHANGA, kitabu kinachowafundisha wanandoa namna ya kukabiliana na madhaifu ya mwenzako, ikiwemo kuyaombea, nakadhalika. Ni muhimu kujua kuwa kazi moja wapo ya msalaba ni kuchonga tabia zetu, na hakuna jambo la kumshinda Yesu. 

6. Iombee Nafsi yako Kwanza, Ponya Moyo wako. Kuna wakati mambo mengine yanatokea na hutujeruu sana. Ila fahamu kuwa sifa ya moyo uliojeruhiwa ni kujeruhi wengine. Sasa ili uweze kuwa na maonyo yenye ufanisi, yasiyojeruhi na kumpa adui nafasi ya kukutawanyia kundi au kukuachilia hukumu ndani, huna budi kuhakikisha kuwa unajiombea uponyaji.

Tuna kitabu cha UPONYAJI WA MTU WA NDANI, kitakusaidia sana. Ila la muhimu ni kutubia kosa husika, ukiwaombea rehema na kujiombea pia yamkini kuna mahali uliachilia mlango hilo likatokea.

Kisha omba uponyaji, mtake Mungu akuponye, akuondolee uchungu na huzuni zote. Kubwa zaidi aondoshe hasira ya majeraha ndani yako. Hali hii itakusaidia sana na kukupa kuonya katika hekima yote.

Kumbuka kuwa hasira hukaa kifuani pa mpambavu. Na tabia moja wapo ya upumbavu ni kuizuilia hakima kufanya kazi, ndio maana mwenye kuwaka hasira huweza kufanya matukio ya ajabu kama mwenda-wazimu au kichaa maana ufahamu wake hauna matunda.

Ukisikia amani ndani uwe na hakika umepona. Jiombee kumpenda, na kuweza kuchukulina na kosa husika, sasa baada ya hapo likabili katika maonyo.

7. Muombe Mungu Akupe Kibali cha Kuonya na Hekima. Ukikosa kibali siku hiyo usilazimishe, kuongozwa na Roho ni muhimu sana. Lakini pia akupe na hekima ya kufiksha ujumbe huo sanjari na upako. Hukuwahi kuhubiri mahali ujumbe wa maonyo nao ukapokelewa vizuri sana kias ambacho ulikuwa na mashaka kwamba uenda ukatawanya na kufukuza!

Uwe na hakika Roho Mtakatifu alikwepo kazini kama hapa: Matendo ya Mitume 2:37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? 

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Sina maana wale walioonywa na kuamua kumrukia Stefano baada ya hasira kuwaka ndani yako kwamba Stefano alikosea la! Hii ikutie moyo maana kuna muda unaonya na kuishilia kupokea kipigo, aidha cha ngumi au cha maneno ama cha wao kuhama kanisa au kuzira huduma, kama Mungu alikuwa pamoja nawe uwe nahakika utamuona akiwa katika mkono wa kuume na kujaa Roho katika nyati hizo ngumu kama Stefano. La Muhimu ni kujifunza kuwoambea rehema kama Stefano maana ni hatari unaowaonya wakigeuka kuwa adui zako, na kama ni watu wako wa karibu hilo litakuumzia zaidi. Kwani ulikuwa na mahusiano nao mazuri na ghafula yamekatika. Moyo huwa unaumia na kusononeka sana.

Unathani ingalikuaje kama nabii Nathani angemuendea mfalme Daudi kichwa kichwa au kwa kukurupa! Hakika ujumbe usingepokelewa na angekutana na mathara. Japo sina maana kuwa Yohana Mbatizaji alikosea kwa jinsi alivyokabiliana na kosa la Herode ila nia yangu hapa ni kumuhusisha Roho Mtakatifu katika hekima yote. Muda mwingine hekima yake huweza kuwa ya moja kwa moja au yenye njia ya mafumbo kama ya nabii Nathani.

8. Fuata Taratibu Mbalimbali. Kuna mathehebu mengine yana taratibu kadhaa za namna ya kuonya kiongozi mwenye nafasi fulani, kama askofu, mwangalizi, mkuu wa idara, mchungaji nakadhalika. Zifuate hizo. Zipo serikali na taasi au kampuni zenye mfumo fulani, fuata huo.

Biblia nayo ina mfumo na utaratbu wake; Mathayo 18:15 Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo. 

16 La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. 

17 Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.

Onyaneni ninyi kwa ninyi, ikishindikana fikisha kwa kiongozi wa idara au mtu waheshima kati yenu kanisani ambapo huweza kuanzia hapo pia, ikishindikana nenda kwa shemasi, likiwa gumu wapo wazee wa kanisa, kisha mchungaji na kadhalika.

Kwenye familia nako kuna ngazi zake, shuleni na kwenye kazi pia. Kama sio jambo la haraka kipolisi basi onana kwanza watu wa ngazi husika, na yale ya kifamilia kuna walezi wa ndoa, au wakuu wa boma, kuna watumishi wa Mungu na ikishindikana hapo ndipo njia kama za ustawi wa jamii na polisi. Likiwa la kifamilia nako polisi kuna dawati la jinsia usikimbilie kufungua kesi moja kwa moja. Japo maswala kama ya ubakaji na uaji au jinai yenye uzito waweza anzia polisi huku kanisa au jamii ukiipa shirikiano wake.

9. Tambua Thambni na Nafasi ya Krama Nyingine Ambatansihi, Pendo, na Upole na Kiasi nimekwisha kukuandikia, pamoja na Kukarimu na Rehema. Lakini pia Neno la Maarifa, Unabii na Utambuzi wa Roho (roho) ni karama muhimu sana.

Unaweza kusimama kwa mara ya kwanza kwenye huduma, na hakuna mtu yeyote aliyekueleza jambo hilo na Roho Mtakatifu akafunua karama hizo ndani yako. Ukajikuta unaonya, na kukemea, na kutengeneza.

Anaweza kuja mtu na kukueleza mambo yake ya ndoa, akimshutumu mwenza mwenzake kuwa ni chanzo na sababu ila ghafula Roho Mtakatifu kupitia karama hizo akakupa kutambua kwamba huyo ndie chanzo. Ukajikuta unamuonya na kumkemea, na kumuasa kubadilika. Macho ya kiroho ni muhimu sana, yatakupa kulionya kusanyiko vizuri mno. Maana ni hatari kutarajia kuambiwa au kusikia kila kitu. Mengine ni mambo ya sirini, mengine hata mhusika hajajua kama litatokea.

Yesu alijua moyo wa Yuda kuwa ulipanga kumsaliti, hakuna aliyemwambia wala kujua, ndio maana hata wanafunzi wake walishangaana nakuulizana ni nani huyo! Hata wao wenyewe walijishuku ndiposa maneno kama ni “mimi Rabi” yalikwepo.

Yesu alijua kuhusu tukio la wanafunzi kumucha nakuchukizwa naye, alitambua litakalo mpata Petro na kumuonya mapema, na Petro alipokuja kukumbuka ndipo maonyo yalipata nafasi. Wewe onya tu siku akikosea ndipo ufahamu utamjilia na kutubu baada ya jokogo kuwika.

Kumbuka sana kuwa Roho Mtakatifu akionya pamoja nawe ni raha sana! Ukibisha mulize Petro, baada ya jogo kuwika hapo alijikuta akitubu, nawe ukitaka kuwa na mafanikio kama haya jifunze kumuomba Mungu ajifunue na kukuongoza  unapojindaa kuonya, kutenga, au unapopewa ujumbe wowote wa onyo! Tufanye nini basi tupate kupona? Waliuliza  wale walionywa moyoni na maneno ya Petro siku ile ya Pentekoste! Kwa nini Roho alikwepo kazini! Maonyo makavu hayana toba wala gueko la kweli!

Unaweza kujiandaa kumtenga mmoja, na maadamu uliombea ibada hiyo, uwe na hakika kuna kilio kitasikika huko cha wengine wakitubia dhambi kama hiyo! Ila ukiweka mipasho na misuto hapo utakomaza mioyo ya dhambi.

Roho Mtakatifu ananiongezea na karama ya Hekima. Hekima ni muhimu sana, Neno la Hekima litakupa kujua cha kunena na kuongea kwa wakati huo.

Na Mwalimu Oscar Samba

10.

Tafadhali kama hujaokoka, mkabithi Yesu leo maisha yako ili afanyike kiongozi wako. Fuatisha sala hii ya Toba kwa imani; 

Sema, BWANA YESU, NINAKUJA MBELE ZAKO, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NINAKUKABITHI MAISHA YANGU LEO, NISAMEHE NA UNIOSHE KWA DAMU YAKO, FUTA JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU NA ULIANDIKE KWENYE KILE CHA UZIMA SASA, NINAKUAMINI KUWA WEWE NI MUNGU, Ameni.

Tafadhali tafuta kanisa la waliokoka ukasali hapo.Mawasiliano: Simu, (+255) 0759859287, barua pepe ukombozigospel@gmail.com 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni