WAPOLE WATAIRITHI NCHI.( Upole, Unyenyekevu kama Silaha ya Kivita.)
Ijumbe huu utaupata katika kitabu chetu cha #TEKATAWALANAUMILIKI
. Fahamu: Wapole Watairithi Nchi; Upole ama Unyenyekevu ni miongoni mwa silaha muhimu sana ya kivita, (fahamu sana kuwa upole unaotajwa kwenye maandiko sio wenye maana ya ule unaokuwa rathi kupokonywa haki yako, au kukosa ujasiri wa kujitetea, ama uzubaifu, la ! Ni upole kama tunda la Roho au kama tabia ya Rohoni, maana hata Yesu aliwahi kupinduapindua meza, kuvuruga gulio pale hekaluni akiitetea kweli ya Mungu, lakini bado alikuwa mpole, aliwahi pia kuwaambia nendeni kamwambie yule mbweha, akimlenga Herode aliyekuwa mtawala, pia aliwahi kumkaripia Petro vikali akimwambia rudi nyuma yangu Shetani, na kadhalika ila bado alikuwa mpole, twajifunza pia kwa Musa, alikuwa mpole lakini ifikapo swala la uhusiano na Mungu wake kuna namna upole ule haukuwa kikwazo maana ulikuwa ni tunda la Roho na sio hulika ya kawaida ya kibinadamu, au ule upole ambao ni matokeo ya "slow mindi" ama ufahamu uliopumbazika.
Mathayo 5:5 |
Tukija katika huu upole, nataka ufahamu kuwa kwanza ni sehemu ya unyenyekevu, ambapo utajionea hilo katika kitabu chetu cha TUNDA LA ROHO, na kile cha TUNU ZA UNYENYEKEVU, pili na muhimu ni kwamba upole huu unatajwa kama silaha ya kumuwezesha muhusika kumiliki, au kurithi, ama kutawala au kuteka; Mathayo 5:5 Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.
Yesu alipokuwa katika mateso ya msalaba alitumia sana silaha hii, ambayo Ayubu hutuambia kuwa ukimywa au kunyamaza pia ni hekima, hali ya Petro kujipigania kwa kumkata mtu sikio ilikuwa ni sehemu ya kushindwa kuitumia hii silaha, na ukweli ni kwamba miili yetu haikubaliani kwa haraka na hii silaha, ndiposa unahitaji sana kuwa muombaji maana hata Yesu aliwaambia wakeshe ili wasije wakaingia majaribuni akijua fika ni vigumu kwa miili yetu kukubali kunyenyekea hata mateso tena ya msalaba: pili kujazwa Roho Mtakatifu ili aweze kuutiisha huo mwili, "yule malaika aliyeshuka na kumtia Yesu nguvu pale Gethsemane uwe na hakika kuwa ilikuwa ni nguvu ya Roho Mtakatifu," kujishusha kwa Stefanao fahamu sana kuwa ilikuwa ni matokeo ya yeye kujaa hizi nguvu, ndipo ukisoma utakutana na sentensi isemayo kuwa, " Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu," ni Matendo ya Mitume 7:55.
Yesu asingalijishusha angejikuta akirusha ngumi, akijibizana nao kwa hasira, "fahamu kuwa maandiko yasemapo kuwa hakufumbua kinywa chake haina maana kuwa hakuongea, au hakusema neno la ! Bali maana yake ni kwamba hakujibu kwa ubaya, hakugombana, hakushutumu, hakutoa lugha kali, maana kama kuongea kuna mahali alijibu shutuma japo kwa mafumbo na hekima, sasa ile ni kuongea, ila tunajuzwa kuhusu dhima ya upole hapo katika kutokujipigania kwa jinsi ya mwilini !"
Kwa kifupi, silaha hii inakuvusha mahali ambapo ni lazima upite, ila adui amekutegea akijua huluka ama silika, ama "personality" ya mwanadamu ama tabia zake kisaikolojia zitamkwamisha, sasa Roho akikaa hapo, anajua ile hulika na asili, kama ilivyokuwa kwa Yesu na kwa Yeremia pia, jifunze kwa Petro aliyeshindwa kuutawala mwili wake kwa jinsi ya Roho kwa kushindwa kuomba kama Yesu na alichokuja kukifanya, wapo wapendwa ambao wanasukumwa kuingia kwenye maombi kama Yesu pale bustanini ikiwa ni muda mchache kabla ya jaribu, na wakiingia wanashangaa na kustaajabu jinsi walivyovuka kwenye hilo jaribu ! Na wanajiuliza mahali huo upole ulipotokea !
Embu ona hapa, napo utaelewa kweli upole ama unyenyekevu huu ndio uliompa kurithi, maana kukirimiwa ni kurithi; Isaya 53:7 Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.
Sasa tazama alichokuja kukirimiwa, au kurithishwa ! " Ni Jina LIPITALO MAJINA YOTE." Wafilipi 2:8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; 10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
Tunaambiwa kuwa, alinyenyekea, nawe jifunze kunyenyekea, wala unyenyekevu sio utumwa, bali ni utumishi, maana kitu kinachotokea ni wewe kupata daraja la kuvukia, kwani adui alinuia kukukwamisha ila kwa kunyenyekea unajikuta ukivuka.
Kuna wakati kazini kunatokea vita, kwenye ndoa kunatokea malumbano, wakuu wako kiroho au kihuduma wanakuinukia, wewe usife moyo, wewe usikate tamaa, wala usijipiganie, bali uwe mpole, maana yamkini adui anajua mwezi ujao utapanddishwa cheo, wiki ijayao mtapokea mujiza wa kiwanja wewe na mwenzi wako, kwa hiyo anaanza kuibua vita mapema ili akukwamishe, (mkikombana au kuachana, mujiza unapeperushwa, au milango yake kufungwa,) anafahamu fika kabisa Mungu amenuia kukirimia kitu, kihuduma ama kiutumishi kwa hiyo anawatumia wakuu zako ili kukuzuilia, ama kukukwamisha, sasa ukiinua pembe au mabega, ama ukijibizana nao kimwili kiholela bila hekima hapo unajikuta umepoteza mujiza wako na ule urithi ama kuteka, na kutawala na kumiliki kwako kunapotea.
Ndiposa ikanenwa kuwa wapole watairithi nchi, haifai kurushiana maneno, haifai kulipiza kisasi, haifai kujiwekea kinyongo au kisasi, wewe wapaswa tu, kuwa nao upole ule wa Roho Mtakatifu, ambao hata ukichukuwa hatua za kisheria ni katika Roho, hata ukijitetea ni katika hekima na busara kama ilivyokuwa kwa Yesu, maana nje ya upole ni hasira na hamaki, sasa hapo palipo na hasira kuna matendo ya mpumbavu, maana hasira hukaa kifuani mwake kama kile kitabu chetu cha IJUWE NA UISHINDE HASIRA KISEMAVYO !
Adui amekuwa akitikisa miti ya matunda ya wapendwa wengi na kuyapukutishia mbali na hata kuikata kabisa kwa sababu ya kukosa hili tunda la upole ! Ukosefu wa unyenyekevu umewafanya kupoteza mema yao mengi sana, Ayubu asingekuwa na upole dhidi ya adui zake asingehesabiwa haki !
Najua unaweza jitetea kuwa umeonewa, umedhulumiwa, umenyanyaswa, ni kweli, maana hata Yesu ilikuwa vivyo, kwani hata Isaya ile 53, inadhibitisha hilo jambo, lakini, upole ndio uliomvusha ! Sasa jaribu kufikiri kuwa Mungu ameshapanga mwezi ujao unainuliwa kazini kwa kuongezewa cheo na mshahara pia, lakini wiki hii kunatokea mgogoro na wenzako kazini na wewe kupigana, au kuacha kazi kwa hasira, embu niambie hasara i wapi hapo ?
Yeremia ni kielelezo katika hili, maana aliweza kuvuka na kuepukana na hila zilizonuia kumuangamiza kiutumishi mara baada ya kuitumia hii silaha iliyo muhimu katika vita vya kumiliki, au kutawala ama kuteka !
Yeremia 11:19 Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.
Wakitaka kukukatilia mbali ili jina lako lisikumbukwe tena katika hiyo ofisi kwa wewe kufukuzwa kazi watakuibulia kisa, na ukipigana au kususa tu, tayari wanapata shitaka, kwa mkuu wako ! Ukibisha kajifunze kwa wakina Meshaki, na Danieli, utagundua kuwa walipoanza kung'ara kulitengenezwa njama ili kuwaondoa kwenye nafasi, ila upole wao uliwadumisha, maana hawakufanya vita na adui zao kwa jinsi ya mwilini, walimtumaini Bwana na kukaza katika kuomba, na mwisho wake ulikuwa mwema kwao, na mchungu kwa adui zao !
Fahamu sana kuwa Yesu aliyanena haya; Mathayo 10:16 Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.
Alijua kuwa upole utakuwezesha kuepukana na wanadamu wenye tabia kama za mbwamwitu, ambao humtishia kondo aliyeoko zizini, na kuhakikisha anaruka uzio na kukimbia ovyo vichakani maana walio zizini hawezi kuwatwaa, licha ya kwamba mchungaji yupo, lakini pia kuna ukuta ambao hawezi kuuingia.
Nasi ndivyo kazi zetu, na utumishi wetu unavyolindwa, ila adui akifanikiwa kuhakikisha kuwa tunaacha wokovu, tunatenda dhambi kwa kujipigania wenyewe, basi hapo ndipo hufanikiwa kutudhuru ! Siku zote kifaranga kinacholiwa na mwewe ni kile kisichokaa karibu na mamaye, maana mamaye akiona adui, huviita na kuvikumbatia kwa mbawa zake.
Sasa busara, na upole, vitakuhifadhi, jifunze kwa nyoka, akishajua hii vita haiwezi haachi kutafuta penye kichaka, au mawe, au shimo na kujificha, sio kwamba ameshindwa kupambana ila ni busara yake ! Kuna nyoka wengine usipowaona,au wakijua hujawaona, wanatulia kimya na unaweza kumkaribia kabisa lakini akijua huna haja naye, hutamsikia akijigusa, hiyo nayo ni busara !
Ni kweli aliitumia vibaya kumzalia adui matunda pale busatanini kwa kumlagai Hawa, sawa ! Maana amepewa werevu,na nenda kajisomee uone hekima aliyoitumia, ila mimi nataka sasa wewe uitumia vizuri katika kuishi na adui zako ambao hunuia kukuzuilia kuteka, kutawala au kumiliki kwako, iwe kiroho au kimwili. " Lakini rohoni siku zote, endelea na mapambanao, mcheke usoni, ila rohoni mpige tena kwa hasira kuu na ghadhabu, wala huu sio unafiki ila ndio Ukristo ulivyo maana yeye hana shida ila Shetani aliyeko ndani yake ndie adui yako, na katika sala hupigana na kinachofanya kazi ndani yake, uwe na hekima katika ukaribu wako naye mwilini pia, maana adui ni adui, kwani Mafarisayo na maadui wa Yesu mara kadhaa walitaka kumdhuru mwilini ila Yesu litumia akili kuishi nao na kuwakwepa pia, kuna mahali pengine alijificha na kutoka nje, am kuwachomoka." Hiyo nayo ni busara, mjinga angejifanya kushusha moto kama Elia alafu anashangaa mbona haushuki ! Bila kujua kuwa kila silaha ina mahali pake, sehemu nyingine ni upole na busara tu vya tosha !
Na kama hujaokoka na unataka kufanya hivyo sasa tafadhli kwa imani kubwa nakuu kabisa fuatisha pamoja nami maneno haya, au sala hii ya toba ili uweze kuokoka, Sema;
BWANA YESU, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NATUBU MBELE ZAKO LEO, NISAMEHE NA NINAKUOMBA UFUTE JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, TAFADHALI LIANDDIKE KWENYE KITABU CHA UZIMA, NINAKUKIRII NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU, HAKIKA WEWE NI MUNGU NA ULIFUFUKA KATIKA WAFU, Amen.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, kwa maombi, sadaka kwa njia ya M-Pesa, kupiga simu au Wasats App, ni +25559859287. Tupo Arusha Tanzania.
Kwa undani wa Mafundisho au Habari zetu tembelea; www.ukombozigospel.blogspot.com .
#MwalimuOscarSamba #UgMinistry #UkomboziGospel #MwalimuOscarVitabu #Neno #Biblia #Zaburi #Pic #Picha #Tanzania #Afrika
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni