Alhamisi, 2 Mei 2019

SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASIKINI Na Mwalimu CHRISTOPHER MWAKASEGE


Utangulizi: (Namna ya mkristo kuishi katika hali ngumu ya uchumi bila kumkosea Mungu).
      Kati ya mambo yaliyotabiriwa kutokea katika siku hizi za mwisho ni dhiki katika mataifa, pamoja na hali ngumu ya uchumi. Soma mwenyewe katika Luka 21:25-26 na Ufunuo wa Yohana 6:5-6.

Pia, tunasoma kutoka katika biblia ya kuwa biashara na uweza wa kuuza na kununua utafuata mfumo fulani uliojaa dhuluma, ambao utatawaliwa na kundi fulani ulimwenguni. Watu hawatauza wala kununua bila ya kupatana na watu wa kundi hilo, na hasa kiongozi wao. Na asomaye na afahamu. Soma kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura yote ya 13.
Si hivyo tu, bali biblia inaeleza wazi kabisa kuwa katika siku hizi za mwisho kutakuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya utajiri na uasherati na pia kati ya biashara na uasherati. Soma kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura za 17 na 18. Lakini pia unaweza kuwa na utajiri na ukafanya biashara bila kujihusisha na uasherati na mambo mengine yaliyo kinyume na maadili ya Mungu.


Tutawezaje kupona katika hali ya namna hii tusimkosee Mungu wetu aliyetuita katika utakatifu ndani ya Mwana wake mpendwa Yesu Kristo? Kwa nini wakristo wengi wanaishi katika hali ngumu kiuchumi kama vile kuna mtu aliyewawekea vikwazo vya uchumi wasifanikiwe?
Watu wengi wanapenda kuishi maisha matakatifu na wengi pia wanapenda kuokoka na kudumu ndani ya kristo, lakini swali linalowasumbua ni wafanyeje katika hali ngumu hii ya uchumi wapate chakula, malazi na mavazi kihalali bila kumkosea Mungu?
Ni watu wachache wanaofahamu uwezo wa mawazo katika kuongoza maneno na matendo yao ya kila siku. Ni budi ufahamu ya kuwa maneno yako na matendo yako ni matokeo ya jinsi unavyowaza. Kwa maneno mengine naweza kusema ya kuwa maisha ya mtu yanategemea mtazamo wa mawazo yake.

Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba jinsi ulivyo ni matokeo ya jinsi unavyowaza; kwa kuwa unayowaza ndiyo unayoyasema na kuyafanya.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyewapangia kuwa maskini. Na hata wakristo wengine kudiriki hata kuuona umaskini kama sehemu ya utakatifu na unyenyekevu.
Lakini Biblia haisemi hivyo, wala haifundishi mawazo hayo. Ni lengo langu kukueleza katika ujumbe huu ya kwamba SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI.

Nataka ufahamu pia ya kuwa nitakapokuwa natumia neno wakristo katika ujumbe huu, ujue namaanisha wakristo wale wanaomkiri Yesu Kristo ya kuwa Bwana na Mwokozi wao; ambao pia humwabudu Mungu katika Roho na Kweli.
Ni maombi yangu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo kuwa atakuwezesha kusoma na kuelewa somo hili, ili wote tulio wakristo tusimame katika haki zetu zote zilizopatikana pale msalabani. Nia hasa ni kukupa mafundisho ya msingi ya kukusaidia uweze kuishi hata katika hali ngumu ya uchumi bila kumkosea Mungu. Kila wiki nitakuwa nakuwekea sura mojawapo ya mafundisho haya.
Mafundisho ninayotarajia kukufundisha yatakuwa na mfululizo wa masomo kama yafuatayo:

· Kwa nini si mapenzi ya Mungu tuwe maskini?
· Mafundisho manne yasiyo sahihi unayopaswa kuyatambua
· Nani anaupenda wokovu wa kimaskini?
· Utajiri wake Kristo usiopimika
· Uchumi wa ufalme wa mbinguni
· Tofauti ya zaka na dhabihu
· Ukitoa tegemea kupokea
· Sadaka na wokovu
· Natoa lakini sipokei – nifanyeje?
· Ufanyeje katika hali ngumu ya uchumi?
Haya ni mafundisho ambayo nitayaweka kwa namna ambayo yatakupa changamoto ya kuyasoma zaidi wewe binafsi na kuyaweka katika matendo. Kwa hiyo usitegemee kupata majibu ya maswali yote uliyonayo juu ya mambo niliyoorodhesha hapa juu, bali tegemea mwongozo wa changamoto itakayokusaidia katika kujifunza zaidi juu ya utajiri na mkristo.

KWA NINI SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI?
Napenda kuanza kukuambia ya kuwa si mapenzi ya Mungu uwe maskini. Kwa sababu tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu huu, Mungu hakupanga kuwa watu wake aliowaumba wawe maskini; bila kujali rangi, kabila, wala taifa.
Nafahamu ya kuwa katika Mathayo 5:3, Yesu Kristo alisema; “Heri walio maskini wa roho; maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Watu wengi wanapousoma mstari huu, wanadhani Yesu Kristo alisema “Heri walio maskini wa mahitaji ya MWILI; maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Lakini Kristo hakusema hivyo.

Mtu maskini maana yake ni mtu mhitaji. Yesu Kristo aliposema “Heri walio maskini wa roho …….” Alikuwa ana maana ya kusema ‘Heri walio wahitaji wa mambo ya rohoni; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Ndiyo maana aliongeza kusema, “Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao watashibishwa" (Mathayo 5:6).
Mtu aliye maskini wa mambo ya mwili ni yule aliye mhitaji wa mambo ya mwili. Na mambo ya mwilini ninayoyasema ni mavazi, chakula na mahali pa kulala. Yesu Kristo hakusema heri wale walio na mahitaji ya chakula, mavazi, afya na malazi.

Ninaposema mahitaji ya mwili usije ukachanganya na matendo ya mwili yaliyoandikwa katika Wagalatia 5:19-21 ambayo ni uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda na ulevi. Mimi siyazungumzii hayo ninaposema juu ya mahitaji ya mwili. Mahitaji ya mwili ninayoyasema ni mavazi, chakula, nyumba na matibabu.
Kwa hiyo si sawa kabisa kwa mtu kuhalalisha umaskini wa mwili, yaani ukosefu wa chakula, mavazi, matibabu na nyumba, kwa kutumia maneno ya Bwana Yesu Kristo yaliyo katika Mathayo 5:3:
Nataka kurudia tena; si mapenzi ya Mungu mtu awe maskini.
Unaweza ukaniuliza na kusema, “Bwana Mwakasege kama si mapenzi ya Mungu mtu awe maskini, mbona basi kuna matajiri na maskini, je! Mungu hakuwaumba wote?

Ni kweli kwani hata imeandikwa katika Mithali 22:2, kuwa “Tajiri na maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote” . Lakini fahamu ya kuwa ingawa matajiri na maskini waliopo wote waliumbwa na Mungu; tangu mwanzo wa uumbaji Mungu hakuyaweka matabaka haya mawili.
Hapo mwanzo Mungu alipomuumba mtu, hakuweka ndani yake utajiri na umaskini pamoja. Wala hakuumba watu wengine wawe matajiri na wengine wawe maskini.
Tunafahamu ya kuwa mtu aliumbwa kwa mfano wa Mungu na kwa sura ya Mungu. Na naamini ya kuwa utakubaliana nami nikisema Mungu wetu si maskini kwa hiyo hatukuumbwa kwa mfano wa kimaskini wala sura ya kimaskini.

Kwa nini nasema na kusisitiza ya kuwa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini?
Ninazo sababu nne ambazo ningependa kukushirikisha:
1. Mungu ndiye atupaye nguvu za kupata utajiri
“ Bali utamkumbuka Bwana , Mungu wako, maana ndiye akupaye NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo” (Kumb. 8:18).

Si mapenzi ya Mungu tuwe maskini kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye atupaye nguvu ili tupate utajiri! Kama basi Mungu anatupa nguvu za kupata utajiri, ina maana ni wazi kwamba Mungu hapendi tuwe maskini wa mambo ya mwilini.
Lakini fahamu ya kuwa si matajiri wote waliopo duniani wameupata utajiri kutokana na nguvu walizopewa na Mungu. Wengi wamepata utajiri kwa njia ya dhuluma. Na ndiyo maana sehemu nyingi katika Biblia matajiri wa jinsi hiyo wamekemewa. Soma Amosi 5:11, 12. Kwa sababu hii Mungu hayuko upande wa matajiri hawa. Hii pia haimaanishi kuwa Mungu yuko upande wa KILA maskini aliopo duniani. La hasha! Mungu yuko upande wa yule ayafanyaye mapenzi yake awe tajiri au maskini (Mathayo 7:21)

Watu wengi wametajirika kwa njia ya rushwa na kutokusimamia haki pamoja na uchoyo. Na hii si sawa hata mbele za Mungu. Ni dhambi zilizo wazi kabisa. Na wote wafanyayo hayo wanahitaji kutubu!
Ngoja nikueleze jambo muhimu: Mungu anapokupa nguvu za kupata utajiri, anakupa akiwa na lengo na kusudi muhimu.
Ni lengo gani hilo?

Imeandikwa, “………. Ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako,
kama hivi leo”
Na Yesu Kristo alisema, “ ……. Kikombe hiki ni AGANO JIPYA KATIKA DAMU YANGU, inayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:20).
Mungu akikupa nguvu za kupata utajiri ni kwa ajili ya kulifanya imara agano lake katika damu ya Yesu Kristo. Na hii ina maana utajiri utakaokuwa nao kutoka kwa Mungu ni kwa kueneza injili! Ni kwa ajili ya kueneza habari njema ya ukombozi kutokana na dhambi, mauti, magonjwa na umaskini. Habari njema hii inatakiwa kuenezwa kwa maneno na kwa matendo.

Kwa kuwa tu kuna matajiri wasio wa haki basi haimaanishi kuwa matajiri wa haki hawapo. Ni budi tuweze kutofautisha utajiri ulio wa haki na utajiri usio wa haki.
2. Mungu ndiye atufundishaye kupata faida
Mungu wetu tunayemwabudu na kumtumikia katika Kristo Yesu si Mungu wa hasara bali Mungu wa faida. Imeandikwa hivi;
“ Bwana, Mkombozi wako, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi;Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye katika njia ikupasayo kuifuata” (Isaya 48:17).

Ndiyo maana kila mtu ndani yake ameumbiwa kupenda kufundishwa ili apate faida katika mambo anayoyafanya. Mungu akikufundisha kupata faida; njia utakayotumia kupata faida itakuwa njia ya haki. Na faida hiyo haitakuwa kwa ajili yako mwenyewe, bali utawashirikisha na wengine pia faida hiyo .
Watu wengine kwa kutokuwa wavumilivu, na kutokujali mafundisho ya Mungu; wameamua kujipatia faida kwa kuwadhulumu, kuwakandamiza na kuwanyonya wengine. Na inasikitisha jinsi wanavyomshirikisha Mungu katika faida najisi namna hiyo waposema ya kuwa ni Mungu aliyewasaidia ‘kudhulumu na kunyonya’. Ni wazi ya kuwa Mungu hakuwasaidia kupata faida kwa njia ya udhalimu.

Si mapenzi ya Mungu tuwe maskini, ndiyo maana anatufundisha ili tupate faida ya halali. Kwa ajili hiyo imeandikwa; “Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji” (Waefeso 4:28).
Je! Si jambo la kushukuru hili, la kuwa na Mungu ambaye hapendi tupate hasara?

Kama Mungu asingekuwa anapenda tufanikiwe katika mahitaji yetu ya mwili, basi ingeandikwa wazi katika Biblia. Lakini badala yake naona maneno kama yafuatavyo; “Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo YOTE na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”
(3Yohana 1:2).
Kwa maneno mengine anatuombea ya kuwa kwa kadri roho inavyofanikiwa basi tufanikiwe vivyo hivyo katika mahitaji ya mwili – yaani tuwe na chakula, mavazi, n.k.

3. Vitu vyote vyema ni mali ya Bwana, na vyote vya Bwana ni vyetu ndani ya Kristo
Katika Zaburi 24:1 imeandikwa; “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana; Dunia na wote wakaao ndani yake”
Na pia ukisoma katika Hagai 2:8 unaona imeandikwa hivi “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi”
Ngoja nikuulize swali; Je! unadhani vitu vyote hivi Bwana amemwekea nani? Unadhani alimwekea shetani na watu wanyonyaji wachache?
La hasha!

Mungu aliviweka vitu hvi vyote na mali hii yote kwa ajili ya watu wake wote, ili itumike katika usawa. Kwa nini? Kwa kuwa Mungu hapendi watu wake wawe maskini. Ndiyo maana mtu alipoumbwa aliwekwa awe wakili wa mali yote ya Mungu hapa duniani.

Utajiri uliomo duniani umetawaliwa na watu wachache na nchi chache siku hizi kwa sababu ya dhambi za uchoyo, ubinafsi, uonevu,unyonyaji, unyang’anyi na dhuluma zilizoingia ndani ya mwanadamu.
Na hii imefanya watu wengine kufikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyegawa matabaka haya mawili, ambavyo si kweli. Na si vizuri kumsingizia Mungu katika jambo ambalo mwanadamu mwenyewe amejiletea uharibufu.

4. Yesu Kristo alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri
“ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” (2 Wakorintho 8:9).
Je! unafahamu kwa nini Yesu Kristo aliamua kuwa maskini? Ni “…….. ili kwamba ninyi mpate kuwa MATAJIRI kwa umaskini wake”.
Najua kuna wengine watashangaa kuusoma mstari huu; lakini ndivyo ilivyo.
Nimewahi kusikia mkristo mmoja akisema:

“ Mimi ni maskini kwa kuwa Yesu Kristo alikuwa maskini”.
Na mwingine alisema; “ Napenda kuwa maskini kwa kuwa Yesu Kristo alikuwa maskini”.

Nadhani kuwa kuna wakristo wengi ambao wana mawazo kama haya. Ni kweli kwamba Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini. Lakini hakuwa maskini ili sisi tuwe maskini; bali alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri! Kama alikuwa maskini ili sisi tuwe maskini kama wengine wanavyodhani, basi kazi hiyo haina faida kwetu. Lakini Yesu Kristo asifiwe kwa kuwa alikuwa maskini ili sisi tuwe MATAJIRI.
Na ndiyo maana alisema katika Luka 4:18a ya kuwa; “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri MASKINI habari njema.”

Je! kuna habari njema kwa maskini zaidi ya kumwondoa katika umaskini wake?
Injili ni habari njema. Na injili ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye (Warumi 1:16). Kuokoka si kuenda tu mbinguni; bali kuokoka maana yake ni uokolewe usiende motoni bali uende mbinguni ukifa, PAMOJA na kuokolewa kutoka kwenye matatizo ukiwa hapa duniani ambayo ni pamoja na umaskini.

Petro aliposema “Bwana niokoe” alipokuwa anazama katika maji unafikiri alikuwa anataka wakati huo aokoke aende mbinguni? La hasha! Yeye Petro alitaka aokoke ASIZAME KATIKA MAJI. Na Yesu akasikia kilio chake akamwokoa. Hivi leo kuna watu wengi mijini na vijijini wanalia Yesu awaokoe kutokana na njaa, kukosa mavazi, magonjwa, maonezi, nakadhalika. Kanisa kama mwili wa Kristo linatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu hao, kwa kuwa kazi hii ni sehemu ya utume wake.

Wakristo wengine utawasikia wakisema; hapa duniani hawahitaji kitu bali thawabu yao wataipata mbinguni. Lakini matamshi ya namna hii yanaeleza ukweli nusu na usiokamilika. Kuwa mkristo kuna thawabu duniani na kuna thawabu mbinguni.
Kama hakuna thawabu yoyote tunayoipata tukiwa hapa duniani kwa kumfuata Yesu Kristo; basi ukristo wetu hauna maana na hauna msaada wowote kwa mwanadamu. Ukristo usiotatua matatizo ya mwanadamu ya kila siku, ni ukristo usio na uhai.

Mtume Petro naye aliwahi kusumbuliwa
sana na jambo hili, hata ikabidi amuulize Bwana Yesu.
“Ndipo Petro akajibu, akamwambia, tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata, TUTAPATA NINI BASI?” (Mathayo 19:27)
“Yesu akasema, Amini, nawaambiaeni, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa MARA MIA SASA WAKATI HUU, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Marko 10:29,30).

Majibu haya ya Bwana Yesu, yanazidi kutudhihirishia ya kwamba si mapenzi ya Mungu tuwe maskini. Yesu Kristo ameeleza wazi kabisa ya kuwa atakayemwamini na kufuata maagizo hayo atapata MARA MIA SASA WAKATI HUU akiwa bado duniani. Na kati ya vitu atakavyopewa ni pamoja na nyumba na mashamba!

Ni kweli Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini baada ya kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo anazungumzia juu ya “….. utajiri wake Kristo usiopimika”. (Waefeso 3:8). Na katika Wafilipi 4:19 tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”.

Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na magonjwa yetu , na kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16,17; 1Petro 2:24). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi kwa ajili yetu,
“ Ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linahubiri habari za ondoleo la dhambi kwa yeyote atakayemwamini Kristo.

Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alikuwa maskini, ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini wake sisi tupate kuwa matajiri (2 Wakorintho 8:9). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili mtu aondokane na umaskini.

Somo litaendelea...

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni