Jumatano, 27 Februari 2019

MAANA YA MBEGU ILIYODONDOKA KANDO YA NJIA:

Mahali: TAG Ushiri, Rombo:     Tarehe 27/2/2019, Na Mwalimu Oscar Samba

Mathayo 13:3 Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.
4 Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;
( Luka, zikakanyagwa:Luka 8:5 Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila.)
19 Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.
Kwa hiyo, kutokulielewa neno, huifanya mbegu hiyo kukosa makao mazuri moyoni mwa muhusika, maana hapo huambiwa yule asikiaye, lakini asielewe yu sawa ama ndie aliyepandwa kando au pembezoni mwa njia, ambapo adui huja na kulitwaa hilo neno, ama kukanyagwa na kuharibiwa.
Maana ya Mbegu: Mbegu ni Neno la Mungu, mpanzi ni Muhubiri, ama Roho Mtakatifu moja kwa moja, au kumpitia mjumbe wake aliye Mtumishi wake;
Luka 8:11 Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu.
Shamba ni Moyo: Luka 8:12 Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka.
Kama huondolewa moyoni, maana yake lilipandwa hapo, kwa hiyo, kama mbegu ni neno, na moyo ni shamba, kwa mantiki hiyo mahubiri, au mafundisho hupandwa moyoni mwa muhusika.
Zile aina za mahali mbegu zilidondokea, yaani njiani, penye udongo mchache, penye miiba, na udongo mzuri, maana yake ni aina ya mioyo ya watu wanaolisikia neno la Mungu.
Mpanzi au mkulima apandapo, ili mbegu iwe imedondokea sehemu ipi, ni matokeo ya moyo ulio nao, kwa hiyo ukitaka kuwa na mafanikio, ni lazima kuhakikisha unajitengenezea moyo mzuri, ili neno lijapo, lidondoke mahali sahihi.
Kusudi la Mungu Kukutaka Mbegu yake Isipandwe kando ya Njia.
Kumbuka sana kuwa Mungu kama mkulima hataki au hapendi kupanda njiani, ila mazingira ya moyo wako ndio huifanya mbegu kuelekea hapo !
1. Ili Kuua na Kuuhuisha; Yohana 12:24 Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.
25 Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa mikulala
26 Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
Kitu neno hufanya ni kuua aina fulani ya maisha yasiyo ya Kiungu, na kuhuisha yaliyo sahihi, Warumi hutuambia vyema kuwa kufa kwa Yesu ni kuua mwili wa dhambi na kufufuka ndimo mlimo na mantiki ya kufufua utu mpya.
Mungu akitaka kuua visivyo vya kwake kwako, na kuhitaji kuhuisha vya kwake, huliachilia neno lake, au mbegu yake, sasa ikianguka mahali sahihi, ndipo hufanikiwa sana, unaposikia alikuwa mwizi na kuacha, maana yake, alipokea neno lililouwa wizi na kuhuisha uadilifu,ambao ni tunda la Kristo.
2. Kukufanya Uzae, na Huwezi zaa kama mazingira sio rafiki kwa uzalishaji, mfano wa mazingira rafiki;
Mathayo 13:23 Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathinhuu.
Kwa hiyo, ukihitaji kuwa na utumishi wenye mafanikio kwako, kuhakikisha kuwa unajiwekea mazingiira mazuri ya kupokea neno la Mungu linalonuia kukubadilisha kitumishi ni muhimu sana, ukihitaji kufanikiwa kimaisha, ni shariti moyo wako uwe na mazingira rafiki katika uzalishaji wa matunda na  hauwezi zaa, kama mbegu haijamea, ikidondoka njiani, haitamea, ya udongo haba au juu ya mwamba, itanyauka yakija mpito, na ile iliyosongwa haiwezi kuivisha kama Luka isemavyo.
Ujumbe huu ni jibu tosha na muhimu sana kwa yule anayehitaji kufanikiwa, au kustawi kihuduma, kimaisha, na kuwa mti mkubwa kama ufalme wa mbinguni ufafanuliwavyo, wengi hutamani sana kufanikiwa kihuduma, ila kuna mahali wamekwama, ambapo ni hapa, mfano utakaouona hapo mbeleni wa mti ulioanza na mbegu ndogo na kisha kupanuka na kuzaa,na ndege kukaa juu yake, ni muhimu kujua kuwa, asili yake ni mbegu, ila sio iliyodondoka njini, wala kusongwa, wala juu ya mwamba, bali ni ile ya udongo au moyo mzuri, kwa hiyo, nawe ukihitaji kufanikiwa katika jambo fulani ni lazima kujua au kuijua hii Kanuni !
Nakupa tena maandiko kuhusu dhima ya mbegu, katika kuuwa na kuhuisha kitu fulani, maandiko haya yakupe kuhakikisha unanufaika vilivyo na neno la Mungu, kama kuna vitu ndani yako huvitaki, na untaka vichipuke vya kiungu, maandiko haya hunena habari za nyakati za mwisho kuhusu kubadilishwa kwetu, ila hapa nataka ujionee thana ya mbegu, na ili iwe na matunda lazima ife, kufa ni kubadilika, kutoka katika mbegu, na kutoa mche, neno la Mungu lililopo kwenye biblia halina matunda hadi liingie moyoni mwako, na kuanza kuzalisha mabadiliko! Mbegu ambayo haijafa,ni mbegu, sasa hatutaki mbegu, tunataka matunda, na ili tuyapate ni lazima tupande, kisha imee, sasa wengi kiroho hutaka mbegu, ila kubadilishwa au kuiruhusu, ama kuipa nafasi ili iwabadilishe, kisha wawe na matunda hawataki, atakuwa ni mkulima wa ajabu sana ambaye ataishilia kununua mbegu, ila hataki mazao ! Na ndivyo wakristo wengi walivyo leo, husoma sana neno, huenda sana kanisani, ila hawairuhusu injili iwabadilishe! Usizini, usiibe, wahi kanisani, uwe mtoaji, toa zaka kamili, ila bado wako pale pale, hawaruhusu neno hilo, kuingiza mabadiliko mapya ndani yao, tujionee maandiko !
(1 Wakorintho 15:35 Lakini labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani?
36 Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa;
:37 nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo;
:38 lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake. )
Kumbuka/ Fahamu: Mungu ni Mpanzi, na Shetani naye ni Mpaanzi, kwa hiyo moyo wako usipopandwa mbegu njema, utapandwa mbaya, na nia ya mbegu njema, ni Ufalme wa Milele;
(1 Petro 1:23 Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. )
Mungu alipoiumba dunia, alipanda pando jema, adui akaja, baada ya kulala kwa Adamu, akapanda pando baya, hii ikupe kuenenda kwa umakini humu ulimwenguni;
Mathayo 13:24 Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;
:25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.
:26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.
27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?
Ukindelea mbele ya hayo maandiko utapata kujua kuwa magugu yanatakiwa kuachwa hadi siku ya mavuno, kwa hiyo inawezekana nawe katika kwaya, au utumishi ama kanisani u gugu, ila bado umeachwa haimaaniishi parapanda ikilia nawe utakuwa mawinguni, la!
Bali utaingia jehanum ya moto, hekima ya kuachwa kwa magugu haikupi kuingi mbinguni, maana siku ya mavuno, itachambuliwa ngano na kufungwa matitamatita, kisha kuwekwa ghalani, na magugu nayo yatafungwa, ila yatatupwa motoni, na huko ndimo mlimo kilio na kusaga meno, sasa hii ikupe kutengeneza na Bwana, yaani uruhusu mbegu njema, ambapo mimi kama mpanzi kwa uweza wa Mpanzi Mkuu, ninanuia kupanda moyoni mwako leo, au majira haya, ili sasa pando jema liwe ndani yako, na kuuwa kila pando baya, yaani ufisadi, ulafi, uasherati, wizi, matukano, kiburi, dharau na kadhalika.
3. Kumbuka Hauwezi Kufika Hapa kama Mbegu yako haikupandwa Sehemu sahihi; Mathayo 13:31 Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake;
32 nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.
Ni dhairi kuwa ukihitaji kuinuliwa, au kupanuka kimaisha na kiroho, na kihuduma, ni lazima kuhakikisha kuwa moyo wako una mazingira sahihi katika kulipokea, na kulitunza neno la Mungu, mkulima makini huliandaa shamba vyema na kulitilia mbolea, nawe kama Mkristo makini, hakikisha moyo wako ni uliopondeka.
Isaya 66, hutuambia kuwa mtu ambaye akilisikia neno la Bwana hutetemeka, huyo ndiye Mungu humuangalia, kwa maana kwamba huyu mtu moyo wake, u na mazingira mazuri, akionywa huonyeka, akihaswa huzingatia, iwe hivyo kwako !
Madhara ya Kupandwa Kando ya Njia, au Nia ya Adui Anapoweka Mazingira moyoni mwa mtu ili Neno lipandwe kando ya Njia:
Kuna vijitabia ambavyo Shetani huvitumbukiza ndani ya moyo wa mtu, na wengi hawajui ni kwa nini ! Nia yake ni kumuwekea muhusika mazingira ya mbegu au neno alisikialo lisidondoke sehemu sahihi !
Mathalani kiburi, huyu mtu asikii maonyo, asikii mahusia, maana njia yake imenyooka machoni pake mwenyewe, ikiwa na maana kwamba kile akiwazacho, akionacho, akipangacho hukiona ni sahihi hata kama atashauriwa, kwenye kiburi kuna upumbvu, pia ujinga, ukija katika Obadia 1:3-4, utagundua kuwa kiburi pia hudanganya, yaani hupotosha, kwa hiyo kitamuaminisha kuwa njia hii ni sahihi, wazo hili ni sahihi, kama ilivyokuwa kwa mfalme Sauli, maana kiburi kilimpa kujiamini hata kama Mungu atakuwa amemuacha, maana kii na mbinu na tabia ya kudanganya, mtu hujiona yu salama kumbe sivyo !
Mazingira mbayo ni hatarishi sana kwa Neno kuweza kuchipusha linalotakiwa kuhipusha !
1. Ili Aweze Kuinyakuwa, au kuiharibu, ama Kuizuilia Isichipuke: Luka 8:12 Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka.
Unapohubiri na mtu kusema ananisema, au moyoni mwake kuwa na mawazo mengine, kimawazo kuwa mbali ama kiakili,ama anapofanikiwa kubana akili ama fikra zake, au ufahamu wake ili asielewe, uwe na uhakika kuwa baada ya mahubiri, au neno hilo, adui huja na kulinyakuwa, ama hukanyagwa !
2. Ananuia Kukuzuilia Kunufaika na Kile Kilichokusudiwa na Mpanzi; Yohana 12:40 Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya..
Wakati wakina Bartomayo kipofu wakipokea miujiza yao, Mafarisayo, haikuwa hivyo kwao, hakuna mahali wananufaika na injili yaa Yesu isipokuwa Nikodemu aliyejua kuweka kiburi cha kidini na elimu pembeni na kukubali kunyenyekea, sio kwamba hawakuwa na mahitaji la! Walikuwa nayo, ila tatizo ni mioyo yao kugoma kuipokea hiyo mbegu !
Sasa maandiko hayo hutuambia kuwa ni ili wasije wakapokea nuru ama mwanga kisha kuweza kuponywa na Kristo Yesu, kwa hiyo, unapohubiri na watu kutema chakula, maana yake, adui amefanikiwa kuwazuilia kubadilishwa na hilo neno, dalili kubwa ya mtu ambaye mbegu haijadondoka njiani ni mabadiliko yake, ukiwa na mshirika asiyebadilika, kuwa makini na shamba upandalo mbegu, kama hana kiburi, sio mwenye madharau, na mkataa maonyo, basi ombea ufahamu wake, maana kuna namna umefungwa,katika mpanzi huambiwa kuwa mtu anapolisikia hilo neno na kushindwa kulielewa hapo ndipo huja adui na kulinyakuwa, kwa hiyo adui akifanikiwa kuzuilia au kubana uekewa wako ama wake uwe na uhakika amezuilia jambo kubwa sana.
Katika kitabu chetu cha IJUWE HUDUMA YA UINJILISTI, nimewataka wainjilisti kuhakikisha kuwa wanaombea hii mioyo, yaani wanaandaa hili shamba vyema, ila katika upandaji, waweze kupanda mahali sahihi, hakuna mpanzi atakaye kupanda njiani, ama mahali pasipo mzalia matunda !
Sasa wachungaji, na wale wanaombea ibada, ni lazima sana kujifunza kuelewa usikiaji wao, fahamu zao, kama akikamata fikra, ama mioyo yao na kuitia uzito hufanikiwa kuwazuilia kupata wokovu, basi wewe ombea hizo fikra ziangushe hizo ngome za mawazo mbaya, na kila fikra zijiinuazo kinyume na elimu ya Kristo, kisha zitiishe, hii ni siri kubwa sana,hakikisha unaombea usikiaji wao, maana hapo ndipo adui huwekeza sana, ndiposa wakati wa ibada hujitahidi sana kupambana na usikiaji wao, asipoamisha mawazo, basi atafinya hata mtoto ili aliye, kwa nia ya kuondoa usikivu !
3.
Mazingira Rafiki na Hatarishi kwa Mbegu:
1. Roho na Tabia ya Kupuzia Maonyo, au Mahubiri, ama Mafundisho, ama Makaripio: Mithali 1:28 Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione.
29 Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.
30 Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote.
31 Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.
32 Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.
33 Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.
Kuna Hatari ya Kupotea, na hata Kufa: Mithali 5:23 Atakufa huyo kwa kukosa maonyo, Naye atapotea kwa wingi wa ujinga wake.
Suluhu lake: Tilia Moyoni, Luka 2:49 Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?
50 Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia.
:51 Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.
Mamaye na Yesu, hakuwa kama wengine, alitilia moyoni, hapo ukiniuliza sababu ya wengine kutokutilia moyoni, nitakwambia i katika huo mstari wa 50, kwamba hawakuelewa, sasa utaniele ni kwa nini adui huhakikisha kuwa watu wakisoma biblia hawaelewi, wakisikiliza mahubiri hawaelewi, huishilia kusema kile kitabu ni kizuri, somo alihubiri visuri, ila mulize alichoambulia hapo, hana! Anachokumbuka ! Labla kichekesho ama kitu kilichomfanya ama kuwafanya kucheka! Hii ni hatari sana.
Sasa ikupe kuhakikisha unapoonywa, unapokatazwa, unatilia moyoni unayoambiwa, unaposikiliza neno na kugundua dosari yako hapo, kinachotakiwa kufuata ni mabadiliko, ukisikia injili ya onyo kwa wasiotoa zaka,moja kwa moja anza kutubu, kisha msihi Mungu akuumbie tabia na mwenndo mpya, sasa huyu ndiye anayeitwa kuwa humfurahisha Mungu, ama ndiye mtu ambaye Mungu humtazama, tumuejionea kwenye Mithali hapo juu kuwa wapo wamuitao, ama wamtafutao kwa bidii ila hawamuoni, maana wamekataa maarifa, na sababu ni kudharau monyo, sasa leo tuna waombaji wazuri sana, wanataka kumuona Mungu kwenye jambo fulani, ila hawajui kuwa ameshagoma kuwasikiliza maana alinyoosha mkono hawakuutazama, wanamtafuta kwa bidii ila kauficha uso wake kwa maana walikwepa maonyo !
( Kutilia Moyoni ni Kuhifathi: Mwanzo 37:11 Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.)
Ona Mukutadha wa Kutokutilia Moyoni hapa: Isaya 42:18 Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona.
19 Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? Au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani? Naam, kipofu kama mtumishi wa Bwana?
20 Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii.
Pili Kubali kuonywa; Kusudi la Maonyo ni Kukugeuza: Mithali 1:23 Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.
24 Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu;
:25 Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu.
Nia na kusudio kubwa la maonyo ni kukugeuza, kama huo mstari wa 23 uanzavyo, ni sawa na mtu anayetaka kuelekea uwanja wa ndege wa KIA, ila kapanda gari la kuelekea Dar es salam, na kashafika Tanga, anaulizwa na mtu unaenda wapi, KIA, anaambiwa kuwa umepeotea, geuka,anagoma, sasa ni sawa na mtu anayeonywa, kuwa ukitaka kufanikiwa kielimu, achana na ngono, ukitaka kufaulu, acha kiburi, ila bado ni jeuri, baada ya muda, hujikuta amepotea, ila akisiliza, hugeuka, na hapo huelekea njia iliyo salama !
Kuna mahali maonyo hukuelekeza na kukuwezesha kufika, maana ni njia;
Mithali 6:23 Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima.
Maonyo kuna kitu yamebeba, ukiyakubali, huweza kunufaika na kilichobebwa nayo, mfano hekima; Mithali 29:15 Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.
Na kama hujaokoka na unataka kufanya hivyo sasa tafadhli kwa imani kubwa nakuu kabisa fuatisha pamoja nami maneno haya, au sala hii ya toba ili uweze kuokoka, Sema;

BWANA YESU, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NATUBU MBELE ZAKO LEO, NISAMEHE NA NINAKUOMBA UFUTE JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, TAFADHALI LIANDDIKE KWENYE KITABU CHA UZIMA, NINAKUKIRII NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU, HAKIKA WEWE NI MUNGU NA ULIFUFUKA KATIKA WAFU, Amen.

Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, kwa maombi, sadaka kwa njia ya M-Pesa, kupiga simu au Wasats App, ni +25559859287. Tupo Arusha Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni