Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya cha MOTO WA UAMSHO KATIKA BIBLIA. Ni kitabu kinachochambua kila Tukio la KiUamsho Ndani ya Biblia nzima.
Na Mwl Oscar Samba
Kitabu cha Kutoka. Sura ya 12 ...
Somo la...... UKOMBOZI KWA NJIA YA DAMU: Kristo Yesu Ndiye Pasaka.
1 Wakorintho 5:7 Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;
8 basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.
Tunajulishwa ya kuwa Kristo ndiye Pasaka wetu, na ili kumuenzi au kuyaishi maisha yake basi tunapaswa kuwa na mwenendo au moyo safi ama weupe wa moyo. Tuifanye karamu hii katika hali au kusudio lililokusudiwa pale msalabani ambalo ni la ukombozi wa kutoka dhambini. Tumaanishe katika wokovu, kwa lugha nyingine Ukristo sio dini tu, bali kunabeba maana pana ya kuyaishi yale aliyoyaishi Yesu Kristo.
Kuyaacha mambo ya kale, maisha ya Misri yako, maisha yenye michanganyiko na chachu za dhambi, uzinzi, masengenyo, biashara za magendo na kadhalika. Ukristo ni Kuokoka, hakuna utofauti kati ya wokovu na Ukristo. Anayejiita Mkristo na hajaokoka huyo ni mpagani mwenye dini. Lazima uiondoe chachu inayokufanya kuwa donge lisilofaa, uwe na maisha safi, maisha bila chachu.
Miongoni mwa imizo kubwa la Mungu katika siku hii ya Pasaka kule Misri ilikuwa ni kula mikate isiyotiwa chachu kwa muda uliopangwa. Lengo lilikuwa ni mkazo wa kiroho katika picha ya maisha ya wokovu, ambapo ni maisha bila mawaa. Sijui unakisoma kitabu hiki ukiwa wapi, na ni lipi dhehebu lako; na inawezekana linasherekea na Pasaka, na yamkini huamini kuhusu wokovu! Pole ni nyingi kwako, maana karamu hiyo unaifanya kwa hasara. Paulo anatutaka kuifanya kwa faida. Bila chachu ndani yake; 1 Wakorintho 5:8 basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.