Jumatano, 3 Januari 2024

Ni Sehemu ya Kitabu Chetu Tarajiwa cha MAANA YA UZIMA, NA UZIMA WA MILELE. Pwenti ya 2, katika mada ya pili ya Uzima wa Milele

 Mwl OSCAR SAMBA ( #NasahazaMwlOscar )

#FaidayaJaribu: #Usiogope

Na Mwl. Oscar Samba

Kwenye Kipengele cha Faida za Uzima wa Milele

2. Tunakula Matunda ya Mti wa Uzima. Huu ni mti wa ajabu sana. Kumbuka mti huu ndio uliowafanya Adamu na mkewe kuondolewa kwenye bustani ya Edeni. Mimi na wewe leo hatupo hapo bustanini kwa sababu ya hii dhambi. 

Mungu alihofia wasije wakala na kisha wakaishi milele. 

Ufunuo wa Yohana 2:7 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu. (Nikutie moyo pia kuhakikisha unashinda vita, majaribu, maana mbingu ni mji wa washindi! Sio sehemu ya walioshindwa! Hili lijue na ulifikiri daima maana ni taswira halisi unayopaswa kuwa nayo kwenye fahamu zako.) 

Tujione Siri hii muhimu kule Edeni:

Mwanzo 3:22 Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; 23 kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.

24 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.

Kilichowafanya kuondolewa sio uzuri wa bustani! Sio kwamba wameshafanya dhambi kwa hiyo hawastaili tena kuendelea kula mema ya hiyo bustani, la! Bali ni kwa sababu ya uwepo wa huu mti. Ndiyo sababu kubwa Mungu anayoitoa anapowaondosha hapo. 

Na ukitaka kuamini tazama huyu malaika analinda nini? Utagundua halindi bustani bali analinda njia. ".... akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.

Sasa ufahamu ndio mti ambao tukienda mbinguni tutaula. Shetani alifikiri amefanikiwa kutunyima mti huu au matunda yake, kumbe Mungu amekusudia kuturejeshea kilichopotea. Sasa utauewa ule msemo wangu ya kuwa Mbingu Mpya na Nchi Mpya ni Edeni ya pili. Na ninaposema YESU ni Adamu wa pili kama Biblia inenavyo ni kwamba nina maanisha na ni ukweli huo. Lakini pia utauelewa ule msemo wa kwamba Adamu alileta mauti kwenye mti wa uzima, lakini Yesu alileta uzima kwenye mti wa mauti.

Yesu ameturejeshea mti wa uzima tena! Ningekuwa mimi ni wewe ninge "pause" ama ningetulia kidogo: na kaunza kumuazimisha Bwana kwa zawadi hii kubwa....

Lakini pia hii ikupe kupenda kufa! Maana kama Adamu na mkewe wasingekufa kwa kula hili tunda, ina maana kwamba mimi na wewe tusingekufa, na kama tusingekufa ni dhairi kuwa tusingefanikiwa kuingia katika maisha ya Mji Ule wa Yerusalem Mpya tunaoutarajia ambako ndani yake zipo faida nyingi. Maana huko hakuna kilio tena, hakuna machozi tena, wala misiba. Hakika tungekosa mengi.

Kwa hiyo, tukifika mbinguni tutachuma haya matunda na kuyala, na huko hatutakufa tena. (Tunaambiwa pia mbinguni hakuna laana. Na laana moja wapo hapa ni ile iliyoachiliwa kwa Adamu na mkewe pale Edeni.) Hili lifahamu sana....Ufunuo wa Yohana 22:3 Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia. (Juu yake anataja huu mti, na mandhari ya hiyo Mbingu Mpya na Nchi Mpya.


Mti huu Unazaa Matunda 12! Ufunuo wa Yohana 22:2 katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.

Mti huu upo pande kuu mbili za huo mto, ubavu wa huku na wa upande mwingine. Na unazaa kila mwezi matunda mapya. Tofauti na miti yetu huku ambayo huzaa yamkini mara mbili na hata moja kwa mwaka. Kwetu msimu wa maembe na matunda mengine ni mara moja tu kwa mwaka. Mti unaojitahidi, jitahidi walau mara kadhaa ni mlimao na mti wa ndimu. Mingine ni hadimu sana. Ila huu ni kila mwezi.

Lakini pia kama nilivyotangulia kusema hapo, ni kwamba huzaa matunda 12, tumezoe mpera hauzai machenza wala fenesi kuzaa limao, huku mbinguni mambo ni tofauti kabisa. Mti huu huzaa matunda 12, jaribu hata kuorodhesha tu matunda unayoyapenda kama sita hivi, alafu ujaribu kufikiri ndo unaenda kuyakuta kwenye mti mmoja yote tena na bado 6 kama hayo!

Unaweza kuelewa sasa ni kwa jinsi gani kosa la Adamu na mkewe lilivyotuondolea mambo muhimu na yenye kupendeza! Lakini haina haja ya kulaumu wala kulalamika, maadamu Yesu kama. Adamu wa pili ameturejeshea hadhi ile, basi tukaze mwendo ili kusiwe na hata mmoja wetu atakayeikosa hii raha. Ndivyo mwandishi wa kitabu cha Waebrania anavyotuambia; Waebrania 4:1 Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.

Usikubali kuikosa! Yawe ni maombi yako. Usipitwe na raha hii. Usikubali ukapitwa nayo. Maana ipo ahadi ya kuingia humu, dunia na mambo yake visije kukukwamisha. Hilo andiko ukisoma mazingira yake utagundua kuwa alikuwa akinena na Waebrania katika tishio la kurudi nyuma kiroho kutokana na ugumu wa safari hii ya wokovu. 

Ambapo anawapa na mfano wa jinsi ndugu zao katika Agano la Kale walivyokwama kwa kufanya makosa kadhaa. Anataka na hawa wasije kukwamia hapa maana ipo ahadi ya kuingia rahani mwake. Ipo Sabato kuu, yaani pumziko la Milele na Milele. (Kwenye kipengele cha Taswira ya Uzima wa Milele utaliona hili kiupana.)

Faida nyingine ya mti huu wa uzima ni kwamba majani yake ni dawa. Ni dawa kwamba majani ya mti huu ni dawa ya kuyaponya mataifa; Ufunuo wa Yohana 22:2 ... na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.

Inawezekana katika ulimwengu huu umekuwa ni mtu wa mapito magumu, kila kona ni mateso na misiba. Umejeruhiwa na kuumizwa; usijali lipo tumaini. Licha ya kufutwa machozi mbinguni lakini pia ipo na dawa ya kutuponya mataifa. Mimi na wewe tujiandae tu kuchuma majani yake, lakini kwa sasa tukaze katika kumtumikia. Tuhakikishe tunashinda vikwazo ili kuja kupokea hii dawa. Ukikata tamaa na kuacha wokovu hutanufaika na dawa hii, badala yake utaishilia katika moyo wa milele na milele. Hakuna faida katika kukata tamaa ila ipo faida katika kusonga mbele. Ukitaka kuamini, tazama andiko lijalo. Anaposema heri uwe na hakika ya kwamba maana yake ni wamebarikiwa. 

Ufunuo wa Yohana 22:14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. 15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.

Nikutie moyo tena na tena ya kwamba unapaswa kuelekea mti huu wa uzima. Kuzifua nguo maana yake ni kuulinda na kuupalilia wokovu. Vazi ni wokovu, utakatifu na kadhalika. Kwa hiyo, wamebarikiwa wale ambao muda wote wanajiandaa kwa kutunza huo utakatifu katika shabaha ya kuielekea mbingu. Wakijua fika ya kuwa huko upo mti wa uzima. Sijui wewe; ila mimi nimejiandaa kunufaika na heri hii. Huku ukipaswa kujua kuwa huko nje ya wokovu wapo mbwa, wachawi na mashetani, hawatakuacha salama kama ukiamua kurudi nyuma.

Lakini pia kwa wale wahubiri, ama waandishi wa vitabu na hata makala kama mimi huku, na waimbaji; tunapaswa kuwa makini dhidi ya hatari yoyote ile ya kuongeza neno katika mafundisho yetu ama kupunguza. Ugonjwa huu upo sana pia kwa wanatheolojia wenzangu. Kuna namna wanapenda sana kuongeza fafanuzi ambazo hata ukitazama unapata shaka, wanaziita "schoolary gesses" yaani makisio ya kitaaluma. Na wengine badala hata watumie maneno kama vile inasadikika, inakisiwa inasemekana; wao huenda moja kwa moja kulisemea kana kwamba ndivyo lilivyo.

Wapo ambao wameamua kujiwekea misingi ya imani katika mafundisho ambaho sio ya Kibiblia kabisa. Wakisingizia ni mafunuo, na wakati kila ufunuo lazima upimwe kwa sura na mizani ya Biblia! Wengine wameamua kupunguza baadhi ya maandiko na kutokuyapa kipaumbe, ama kwa hila wameyapindua.

Mambo haya yote yana hadhari kubwa katika huu mti wa uzima. Maandiko hutuambia kuwa watapunguziwa, utajikuta unapewa kipimo kidogo kwa kupunguza au kuongeza lisilotakiwa kwenye Biblia au mafundisho yako. Kuna makosa ambayo yanaweza yasikuzuilie kuingia mbinguni ila yakakuondolea sehemu ya huo utukufu na katika mti huu.

Ufunuo wa Yohana 22:19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

Wale walioamua kuibadili Biblia na kupachika huko maneno yao, au kujiongezea vitabu vyao, na wengine hata kupunguza; adhabu yao yakaa zaidi. Na wale ambao wanaijua kweli, wanaijua Biblia sahihi, lakini wakaamua kufundisha au kutumia isiyo sahihi: uwe na hakika hawa ni waliopotea kama hao walioziunda hizo na adhabu zao za kaa pia. Nami nimeshakueleza ya kwamba Biblia sahihi ni ile yenye vitabu 66, na kitabu cha Danieli kina sura 12 na sio 14, na kitabu cha Esta nacho hakijachakachuliwa kama ilivyo kwa Bibilia zilizotiwa mikono ya kibinadamu na falme nyingine.


http://www.ukombozigospel.blogspot.com

Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h 

Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD

Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk 

Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv

Kwa Maombi +255759859287 

Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL 


Nikutakie Siku Njema


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni