Jumatatu, 8 Januari 2024

NDOTO ZA UZINIFU au MAPEPO MAHABA, ama Kuota Unazini Ndotoni Maana yake ni Nini?

Na Christopher Mwakasege_


 Leo nataka tujifunze juu ya “Mwongozo wa kutafakari na kuombea ndoto zenye UZINIFU AU UASHERATI ndani yake”.

Maneno haya ‘uzinifu na uasherati’ yanahusu ufanyikaji wa tendo la ndoa usio halali kibiblia. Uzinifu linatumika zaidi wakati tendo la ndoa limefanywa na mtu ambaye hajaoa au hajaolewa. ‘Uasherati’ linatumika zaidi wakati tendo la ndoa limefanywa nje ya ndoa na mtu ambaye ameoa au ameolewa.


Mtu anayepata ndoto zenye mambo hayo, huwa zina madhara makubwa sana ya kiroho, na ya kimwili – kwa aliyeota ndoto hizo!

Kumbuka kwamba: Neno la Mungu la biblia, kwa kushirikiana na Roho Mtakatifu, linatuongoza kujua namna ya kutafsiri na kuziombea ndoto za aina yo yote – ambazo ni pamoja na hizi zenye mambo ya uzinifu au uasherati ndani yake.


Ni muhimu kwako kupata nafasi ya kusoma, na kutafakari mistari ya biblia, ambayo nimeambatanisha na somo la leo. Hebu tujifunze somo la leo kwa mtiririko ufuatao:


(1) Ukiota unazini kwenye ndoto maana yake nini? Ina maana ya kwamba: 


(a) Umeunganishwa kiagano na roho ya (au pepo la) uzinifu au uasherati – kufuatana na aina ya mtu uliyekuwa unazini naye. Soma 1 Wakorintho 6:16,17.


(b)  Unapoteza uwezo wa kufaidi matunda ya ufalme wa mbinguni. Soma 1 Wakorintho 6:9


(c) Ni ishara ya kwamba mwili wako umepandikizwa mbegu ya kukuzuia usiweze kuomba, au usiwe mwombaji. Soma 1 Wakorintho 6:18 – 20.


(d) Umepandikizwa roho na mbegu ya kumwasi Mungu tunayemwabudu katika Yesu Kristo. Soma 2 Mambo ya Nyakati 21:11 na Ezekiel 16:26


(e) Ni njia ya kupanda ‘mbegu’ ya uzinzi, au ya uasherati, ambayo isipoondolewa kwa damu ya Yesu, itachipuka katika maisha ya baadaye ya mtu aliyeota hiyo ndoto. Soma Mathayo 15:18, 19 na Mathayo 5:27, 28.


(2) Ukiota unazini kwenye ndoto na ndugu yako wa karibu – kama baba au mama mzazi, au dada yako, au kaka yako, au mkwe, au mjomba au mke wa mjomba….ina maana ya kwamba, maana yake;


(a) Unaandamwa na roho ya kukataliwa na kutengwa na wale wa imani moja na wewe kiroho! Soma 1 Wakorintho 5:1 – 5.


(b) Utasumbuliwa na magonjwa au hatari zingine kwenye mwili wako kwa lengo la kukuua. Soma 1 Wakorintho 5:1 – 5.


(c) Unaandamwa na roho ya mauti. Soma Mambo ya Walawi 20:11 – 14.


(d) Unaandamwa na roho ya kurithi iliyobeba uovu. Soma Mambo ya Walawi 20:17, 19, 20.


(e) Utasumbuliwa na tatizo la kutokuzaa watoto. Soma Mambo ya Walawi 20: 20, 21.


(f) Unafungulia roho ya ukahaba. Soma Mambo ya Walawi 19:29


(g) Umepandikizwa au unapandikizwa roho au pepo la kukataliwa na waliookoka (Ikiwa uliyeota ndoto hiyo umeokoka); au wakristo wanaokufahamu. Soma 1 Wakorintho 5:9 – 13;

(3) Ukiota ndoto unazini au unafanya uasherati na mtu wa “imani” nyingine maana yake nini? Ndoto ya namna hii ina maana ya kuwa kuna roho au pepo lililoingia nafsini mwako ili:


(a) Kuua na kuharibu imani yako ili uiache na ufuate imani nyingine ya huyo uliyezini naye kwenye ndoto. Soma Kutoka 34:15, 16 na Kumbukumbu ya Torati 7:1 – 4 na Hesabu 25:1,2 na 1 Wafalme 11:1 – 5, 7 – 9.


(b) Kukufanya urudi nyuma kiroho, na usiweze kumfuata vizuri Mungu unayemwabudu katika Kristo Yesu. Soma 1 Wafalme 11:1, 2, 6.


(c) Inafungua mlango wa maadui kuinuka juu yako na dhidi yako, na kupata nafasi ya kukusumbua na kukufanya ukose utulivu. Soma 1 Wafalme 11:1, 2, 14, 23.


(d) Inafungulia pepo la mauti likiwa na lengo la kukua, kwa nia ya kujitafutia sifa kwa ‘mungu’ wake. Soma Hesabu 25:1 – 13.


(e) Inafungulia roho ya wivu (Kutoka 34:14 – 16 na Hesabu 25:1, 2, 10,


 13) inayozaa ugomvi wenye kisasi mara kwa mara (Yakobo 3:16)


(14) Ukiota ndoto unazini na mnyama – ina maana gani? Kwa mfano – kuna mama mmoja aliniandikia kuwa aliota yuko uchi kwenye banda la ng’ombe, na ng’ombe dume akazini naye! Alipoamka toka usingizini alisikitika sana!

Ukiota ndoto za kuzini na mnyama maana yake ni hii:


(a) Umevamiwa na unaandamwa na roho ya mauti, Soma Kutoka 22:19 na Mambo ya Walawi 20:15,16.


(b) Umechafuliwa kiroho ili uwepo wa Mungu ukae mbali na wewe. Soma Mambo ya Walawi 18:23


(c) Unapandikizwa laana. Soma Kumbukumbu ya Torati 27:21.


(5) Madhara ya ziada yanayoweza kumpata MWANAUME akiota ndoto anazini au anafanya uasherati ni pamoja na:


(a) Kupata tatizo la kutoweza kutumia akili vizuri (Mithali 6:32, 33),à katika kufikiri kimaisha!


(b) Maendeleo yake kiroho na kimaisha na kifikra yanakwama kwa kuwa nafsi yake ‘inanaswa’ (Mithali 6:26). Nafsi yake iliponasia ndipo panapoweka kipimo cha maendeleo yake (3 Yohana 1:2).


(c) Nguvu za kiume za uzazi zinapungua au zinapotea kabisa (Mithali 5:3 – 10)

(6) Madhara ya ziada yanayoweza kumpata MWANAMKE, ikiwa ataota anazini, au anafanya uasherati kwenye ndoto, ni pamoja na pepo kupata nafasi ya kuingia, na kukaa kwenye kizazi chake (Mambo ya Walawi 20: 20, 21); na kumletea madhara kama ifuatavyo:


(a) Kuvuruga mzunguko wake wa damu ya mwezi;

(b) Kuweza kuharibu mimba –ikiwa – huyo mwanamke aliyeota ndoto alikuwa mja mzito alipokuwa akiota ndoto hiyo;


(c) Kuvuruga uwezekano wa kupata mimba – ikiwa ameolewa;


(d) Kuharibu viwango vya utendaji kazi wake kama mwanamke akiwa nyumbani kwake;


(e) Kupandikizwa magonjwa kwenye kizazi chake, au/na kwenye damu yake


(7) Ukiota unazini au unafanya uasherati kwenye ndoto wakati umekwisha chumbiwa au umekwisha chumbia; au wakati zimebaki siku chache za kufanyika kwa harusi yako – ujue maana ya ndoto hiyo ni hii:

KWAMBA: Kuna pepo lililopata nafasi kwako, ili kuvuruga mipango yako ya harusi isifanyike; au hata kama utaolewa, au utaoa – hilo pepo litatengeneza mazingira ya wewe kuachika, au kuachana na huyo mwenzi wako! Soma Kutoka 22:16


(8) Ukiota ndoto unazini, au unafanya uasherati na kichaa au mchawi – ujue maana ya ndoto hii ni;

KWAMBA: Shetani anapandikiza hila zake kwenye maisha yako, ili kukusababishia ukataliwe na watu wako! Soma Mambo ya Walawi 20:6


(9) Ikiwa ‘eneo’ ulilofanyia uzinifu au uasherati kwenye ndoto uliyoota linaeleweka …yaani kama nyumbani, ofisini, jikoni, makaburini, darasani – nakadhalika – ndoto hiyo inakupa ujumbe gani wa ziada?

Ndoto kama hii – yenye kukuonyesha uzinifu, au uasherati ulipofanyika, inataka ujue ya kuwa – kiroho eneo hilo ‘limenajisika’, na ‘kuchafuka’, na lisiposafishwa kwa damu ya Yesu mapema, litatoa nafasi kwa mapepo kujitengenezea ‘kituo’ chao! Soma Mambo ya Walawi 18:20 – 30 na Ufunuo wa Yohana 19:2

(10) Hatua zifuatazo zitakusaidia katika kupanga mambo ya kuomba juu ya ndoto za namna hii:


(a) Fanya maombi ya Toba kwa ajili ya mlango uliofunguka na ukaota ndoto za namna hii


(b) Vunja kwa damu ya Yesu aina yo yote ya muunganiko wa kiagano, kati ya nafsi yako (uliyeota ndoto) na roho ya kipepo iliyojiunganisha na nafsi yako, kwa kupitia kwenye ndoto hiyo


(c) Kemea kwa jina la Yesu kila aina ya roho ya kipepo iliyokuja kwako kwa kupitia hiyo ndoto;


(d) Haribu kwa damu ya Yesu aina yoyote ya mbegu ya uzinifu, au ya uasherati au ya ukahaba iliyopandikizwa ndani yako kwa njia ya ndoto hiyo


(e) Omba uponyaji wa eneo lo lote lililopata madhara kwenye roho yako, au kwenye nafsi yako, au kwenye mwili wako, au kwenye mahusiano yako na watu wengine, au kwenye mipango yako, nakadhalika


(f) Omba neema ya Mungu ikusaidie kurejesha kwa upya mahusiano yako na Mungu katika Yesu Kristo


(g) Omba utakaso wa damu ya Yesu ufanyike kwenye eneo ambalo kufuatana na ndoto hiyo – uzinifu ulifanyika hapo.

LA KUKUMBUKA: Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya kuku panulia wigo wa ufahamu, juu ya eneo lingine linalohusu ndoto za namna hii ambalo sijaligusia hapa. Mungu azidi akubariki.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni