Felix Mbwanji:
SAMEHE NA KUSAHAU (BY MWL, C.MWAKASEGE)
TABIA YA MUNGU YA KUSAMEHE NDANI YAKO
Ulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, ulipokea tabia ya aina gani?
" Bali wote waliompokea (Kristo) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu." (Yohana 1:12,13)
Ulipozaliwa mara ya pili kwa Neno la Kristo ulifanyika kuwa mtoto wa Mungu.
Watoto wa Mungu wana tabia ya namna gani?
Kwa kuwa wamehamishwa toka ufalme mwingine na uzazi mwingine, na kuingizwa katika ufalme wa Mungu na uzazi wake (Wakolosai 1:13); watoto hawa wanatakiwa wawe na tabia nyingine.
Kabla ya kuzaliwa mara ya pili, kabla ya kumkiri Kristo ya kuwa ni Bwana: ulikuwa na tabia ya dunia hii iliyoongozwa na mfalme wa dunia hii ambaye ni shetani.
Ulipozaliwa mara ya pili na kuukiri wokovu katika Kristo, ulipokea tabia mpya inayoongozwa na Mungu mwenyewe aliye ndani yako.
" Kwa kuwa uwezo wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa (Utakatifu), kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno; za thamani,ili kwamba kwa hizo mpate kuwa Washirika wa TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa." (2 Petro 1:3,4)