Na Mwalimu Oscar Samba
Ujumbe huu ni shehemu ya Kitabu chetu cha CHAKUFANYA UNAPOKUWA NJIA PANDA, katika mada ya Kwanza inayohusu aina ya Imani inayohitajika Ukiwa Njia Panda. Kumbuka ni kitabu chenye kuelezea mazingira ya mtu aliyegubikwa na maamuzi zaidi ya moja ikiwa ni matokeo ya mahali anapopitia. Yaani Njia panda ya kiroho au Kifikra na hapa ni katika pwenti ya pili
2. Tazama Nguvu Zako. Kwanza fahamu mtu anapokata tamaa, hususani katika kiwango cha kuwa radhi kuachana na mapenzi ya Mungu hata kama anayajua dhairi, au kufikia kiwango cha kutamani kufa; ni nguvu zimemuishia! Kwa kifupi amelemewa na aina ya dhiki aliyonayo;
Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi. 2 Wakorintho 1:8
Nguvu zao zilizidiwa, kilichofuata ni wao kukta tamaa ya kuishi! Sasa utaelewa ni kwa nini Elia alijiombea kufa katika ile 1Wafalme 19! Wengi wanashangaa na kukosa majibu maana huku nyuma tu katoka kufanya tukio kubwa na la kushangaza! Ni kwamba vita viliibuka upya, na nguvu hakuwa nayo!
Imani haikai hewani, kuna mahali inakaa. Eneo moja wapo ni kwenye nafsi, na inategemea sana nguvu zilzizopo kwenye nafsi yako. Ndio maana Yesu alipoishiwa nguvu alianza janja ya kutaka kukwepa mapenzi ya Baba yake! Sio kwamba alikuwa hajui umuhimu wake, la! Alijua sana tu. Ila nguvu zilipunguka.
Usiwe mwepesi wa kuhukumu unapomuona mtumishi kaamua kukimbia huduma, kaamua kukabithi kanisa kwa Mwangalizi na kurudi nyumbani au kijijini na kuendelea na kilimo au uvuvi! Wakati mwingine unapaswa kuwa mtu wa kumsaidia badala ya kuhukumu kirahisi kuwa hana wito au hakuitwa! Ndio maana ukikaa kwenye darasa kama hili hutabeza mtu anapokwambia kuwa amechoka au anajisikia kukata tamaa.
Wiki kadhaa zizilizopita niliwahi kumuelezea mtumishi mmoja chuoni ambaye niko naye darasa moja rafiki yangu Lwitiko kuwa mimi ni mtu niliyekata tamaa, nilimpa mkasa wa swala langu la ndoa ambalo ni mwaka wa nane sasa siko na mke, na baya zaidi sikuishi naye zaidi ya miezi sita kwenye ndoa na wala sina hakika kama miezi mitatu ilitimia nikiwa naye ndani, na baya pia aliniacha kwa kuchukuwa vitu vya ndani na kutoroka.
Nilimueleza kuwa imefikia hatua katika matukio mawili ya wanafunzi kufariki hapa chuoni kumuliza Mungu ni kwa nini anachukua watu wanaotamani kuishi na kuniacha mimi niliyechoka kuishi! Nilimuonyesha mlango wa kanisa ambapo tulikwepo tunafanyia mzungumzo hayo, (Chaple) na kumwambia kuwa ningekuwa na hakika muda huu nikipita pale na fariki ningepita, ninatamani kufa hata muda huu maadamu tu nikifa naenda kwake Mungu.
Najua mwenzangu hakubeza maneno haya, maana hata ukisoma kifungu hiki cha 2 Wakorintho 1 hapo nipolitwa huu mstari, utajionea kuwa Paulo anabainisha kuwa kuvuka kwao kulitokana na maombi ya hawa watu!
Kama hujapita hapa ni rahisi sana kukemea roho za mauti, na kusema mchungaji kweli unafikia hatua hiyo! Mimi sio mwema kuliko Elia, wala sio wa kiroho kulipko Paulo mtume aliyeyaandika haya! Wala sijafikia viwango vya Yesu aliyekuwa akikwepa jukumu la kupita msalabani maana unaweza niona nami nilikuwa nikikwepa jukumu la kumtumikia Mungu. Kuna dhiki nyingine zinabeba hali ya mauti ndani yake, kama Paulo anavyoelezea kwenye mistari inayofuatia baada ya huo wa 8, anaelezea kitu hapo kiitwacho hukumu ya mauti! Tuendele;
Kumbuka pwenti hii inakutaka kutazama nguvu zako. Unapojina umefkia hatua ya kukata tamaa kwa viwango hivi, uwe na hakika kuwa jaribu limekulemea. Ndio maana Yesu aliomba msaada wa maombi kwa kuwakusanya wale wanafunzi watatu na kuwa nao karibu. Ukisoma mukutadha wa kifungu hiki kwa Wakorintho utagundua kuna watu walisimama kuwaombea wakina Paulo walipokuwa kwenye dhiki huko Asia.
Usijaribu kupuzia, usife na tai shingoni. Niliwahi kumueleza mzee mmoja wa kanisa kuhusu hali niliyokuwa nayo, japo alianza kwa kunihubiria kuwa nimewaza kama mke wa Ayubu ila ninachojua waliniombea. Niliwataka kuingia kwenye maombi ya siku tatu na kuwa na maombi mengine endelevu. Paulo alijua umuhimu wa kuombewa ili kuongeza nguvu zake za kiroho. Au za kwenye nafsi. Fahamu sana kuwa nguvu zikidhurika, na imani nayo itayumba tu! Imani ikiyumba, hutaona thamani ya watu kukuombea. Kwa hiyo kabla ya imani kudhurika fanya hima kuhitaji msaada. Ukimuona aliyechoka na hataki tena kuinuka uwe na hakika kuwa nguvu ziliisha na imani nayo ikadhurika.
Nikiwa katika hali kama hiyo, kulikuja kutokea jaribu jingine kubwa lililonipelekea kusimama masomo kama muda wa kama mwaka mmoja hivi! Jaribu kufikiri, nini kingalitokea kama nisingehitaji msaada mapema! Ndio mwanzo wa kusikia yule muhibiri aliyekuwa na maono makubwa karudi kwenye kazi yake ya zamani.
Andiko hili limekua msaada kwangu sana ninapokuwa mahali pa gumu;
Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache. Mithali 24:10
Kwa hiyo, ninapokuwa taabuni au kwenye dhiki kama hii ambayo niko nayo sasa inayokaribia mwaka wa 10 huwa ninajizuia sana kuzimia, kuzimia ni kufikia hatua ya kuvunjika moyo kwa viwango ambavyo imani ya kusonga mbele na sababu za kusonga mbele vina kuwa havipo kabisa.
Maana ukifikia hapo, likija wimbi jingine unazolewa, kwani hata aliyepata ajali majini, akiogelea na kufikia kiwango cha kuchoka, au aliyejishikiza na kipande cha mbao au kushikilia mahali, kabla ya kupata msaada wa wokozi akiwa ameishiwa nguvu kabisa, likija wimbi jingine ni rahisi kuzolewa maana nguvu za kushika hazipo, na wengine hujiachilia wafe maana wamechoka kujishikilizia hali inayoondoa sababu ya wao kutamani au kuhitaji kuendeela kuishi. (Wimbi lililokuja lingenizoa kama nisingepata msaada mapema.)
Ukitaka kujua umuhimu wa nguvu, soma Isaya 40, hasemi kuhusu kuwoangezea imani, bali anaongea habari ya nguvu! Sijui kama unajua au unaelewa kiundani kuhusu nguvu ninayoisema hapa! Kuna wakati unahitaji kuongezewa imani, ila kuna wakati unahitaji kuongezewa nguvu!
Yesu alipochoka hakuongezewa imani, bali nguvu! Imani ilikwepo, ila ngvu ilipngua! Ndio maana andiko la Mithali likakutaka au kukujuza kuwa ukizimia wakati wa taabu ngvu zako ni chache!
Imani ni sawa na “dripu” ya maji au maji ya dawa, au ya damu. Sio kila mtu anaweza kuongezewa hivyo, kuna mgonjwa mwingine ukimuongezea vinarudi. Haviendi, kwa nini? Ni kwa sababu mwili hauna nguvu tena ya kupokea msaada huo.
Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia. Isaya 40:29-31
Katika andiko lifuatalo nataka uone uwiano uliopo kati ya utendaji wa Mungu (unaweza weka imani), na nguvu ndani yako. Ili ikupe kuchukulia kwa mzigo punde unapoona nguvu zimepunguka, na uelewe ni kwa nini wazimiao wanahitaji nguvu mpya ili waendelee na waweze kuruka juu kama tai, na ni kwa nini Yesu alihitaji kuongezewa nguvu. Kumbuka sana kuwa mwana-riadha akiishiwa nguvu uwe na hakika hatamaliza mwendo wake vilivyo. Nia anayo ila nguvu hana, na wewe waweza kusalia na imani ila nguvu huna, na walioishiwa kabisa, na nia inaweza kudhurika pia, hususani kwenye fikra zake kunapojengeka mgogoro mpya, maana wengi wanaoshindwa kumuelewa Mungu ni matokeo ya kuishiwa nguvu, na aina mpya ya mgogoro mpya kuibuka. Elia alipoinuka na kula, aliweza kusonga mbele maana mgogoro mpya haukuwa umeinuka. Tulione;
Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu. Waefeso 3:20.
Hasemi kwa kadri ya imani, ila nguvu; japo imani nayo ina nafasi yake. Mungu hatujibu kutokana na nguvu iliyopo mbinguni au kwake, ila ni kwa mujibu wa nguvu iliyopo ndani yetu. Leo huduma nyingi zimezorota si kwamba nguvu za Mungu zimepungua la, bali nguvu ndani yetu.
Wataalamu wa umeme watakubaliana nami kirahis sana tu! Kuwa umeme naotumika ndani sio kwa mujibu wa uwezo washirika la umeme au nyaya za umeme unafuliwa au kuzalishwa nchini, bali ni kwa mujibu wa chombo chako cha ukutumia huo umeme pamoja na mfumo wako wa umeme wa ndani na kutoka kwenye nguzo ya umeme sanjari na kwenye kituo husika mfumo huo ulipoanzia yaani nje ya nyumba yako.
Umeme unaozalishwa ni mkubwa, ila unatumia kulingana na uwezo wa chombo husika. Ndio maana mwingine anautumia kwenye kusagia mahindi, au kukamulia alizeti na viwadani, ila wewe unautumia kwenye kuchajia simu na kutazama runinga nyumbani, ukipandisha kiwango sana ni umepasia nguo au kusagia “juisi” ama kujichemshia maji ya kunywa.
Usijaribu kugombana na shirika husika kuwa lina upendeleo mbona wenzako hutumia zaidi ila jitazame wewe na mahitaji yako, ama na uwezo wa vyombo vyako. Sasa adui akifanikiwa kudhuru nguvu zako ni amefanikiwa jambo kubwa sana.
Akikuachia nguvu robo kilo, uwe na hakika na uweza wa Mungu hautazidi robo kilo. Umeme wa kwenye “transifoma” ya umeme ukiulazimisha kupita kwenye chaja yako ya simu, ni kusababisha shoti tena kubwa tu! Kwa hiyo epuka kuzozona na Mungu bali ongeza uwezo wako.
Nayasema haya kwa maana kuna watu hapo awali walikuwa na uwezo mkubwa sana tu, ila toka adui afanikiwe kuwapitisha mahali fulani aliponyonya kama siyo kufyonza nguvu na uweza wao wa kiroho, hadi sasa wameshapubgua viwango, na hawajajua mahali walipotelezea.
Andiko hili linaweza kuwa na mukutadha mwingine ila somo kubwa tunalolipata hapa ni kwamba Mungu anaweza kukutia nguvu. Kwa hiyo msihi akutie nguvu kama katika mada ya pili nilivyokufunza pia; Wafilipi 4:13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
Eneo moja wapo linaloweza kukuongezea nguvu ni maneno ya faraja. Usipuzie wanapokuja watu na kukutia moyo, yapokee na yakubali, maana yanauia kukutia nguvu; 1 Wathesalonike 5:14 Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote.
Maana hapa kilichochoka ni nafsi, kama vile maneno yawezavyo kuvunja moyo, uwe na hakika na maneno mazuri nayo pia huweza kuhuisha na kuinua nafsi iliyokuwa katika hali ya kuinama. Sitashau walioinuka na kunitia moyo kwa maneno yao, wengine walishilia kuniambia tu tunakuombea, najua kwa maombi yao nimeinuka tena na kulitazama kusudi la Bwana, na wale walionifariji nawakumbuka pia. Ukijisikia kumfariji mtu kama huyu usisite kufanya hivyo, na hata kama kuna mahali alikosea, huo sio wakati wake, ni hatari kumkuta mtu aliyevunjika na kutupwa kando ya barabara yupo mtaroni baada ya kupata ajali ya gari, badala ya kumsaidia ukaanza kumlaumu kwa kutumia barabara vibaya.
Mwenye hekima humchukua, humfunga jeraha: humpatia huduma zote muhimu za kwanza na kisha kumuwaisha hosipitalini. Laumu katika nyakati kama hizi, huvunja moyo, asije kusema kama Daudi kwenye ile Zaburi ya 69 kuwa laumu imenivunja moyo, nikatazama wa kunifariji wala sikumuona! Kuvunjwa moyo kwa laumu ni kubaya zaidi, alipita hamali pa gumu, na badala ya kutiwa moyo akaishilia kulaumiwa tu, kana kwamba yote aliyowahi kuyafanya ni mabaya machoni pao. Hali iliyomvunja moyo.
Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu. Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao. Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki. Zaburi 69:10-12
Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu. 20
Bali maneno mazuri huganga jeraha, na kumvusha mahali; Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; Ni tamu nafsini, na afya mifupani. Mithali 16:24.
Kuna mahali Daudi anasema kuwa amejeruhiwa shauri ya upumbavu wake; hii itupe kutambua kuwa muhusika huwa anajua moyoni mwake kuwa lililomkuta ni matokeo ya kukosea mahali fulani, alitumia barabara vibaya, kwa hiyo naona sio wakati muafaka wa maneno kama situlikwambia,… ona ona sasa,.. asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu… na kadhalika.
Una kazi ya kumuasa binti yako kuachana na mahusiano kabla ya wakati, ila akipata mimba, sio wakati muhafaka wa kumpiga kwa maneno, ndio maana wengi hutoa mimba maana wanakwepa matokeo ya kosa walilolifanya.
Sijui kama naeleweka masikioni pako! Zaburi ile ya 38 ina mukutadha huo wa kujeruhiwa shauri ya upumbavu wake. Inamaanisha kuwa alikosea ndio maana akakumbana na madhara yaliyomkuta. Lakini hakuishilia kujilaumu kupita kosa, bali alihitaji msaada wa Bwana. Anachonifuraisha ni jinsia alivyoamua kukabiliana na adui zake.
Anasema kuwa ameamua kuwa kiziwi, na bubu mbele yao. Anamaanisha kuwa hasikii au atilii moyoni yale yanayoendelea kunenwa na adui zake kumhusu, wala hajibizani nao. Mbinu hizi ni muhimu sana maana ukiyatilia moyoni maneno yao itakudhuru sana, kwani kwa mujibu wa Zaburi na Yeremia, pia kitabu chetu kile cha NGUVU YA MANENO KWENYE ULIMWENGU WA ROHO na kile cha NAMNA YA KUISHI WAKATI WA MAJARIBU AU MAPITO, maneno ni kama mshale au mkuki, ama panga, ukiyapa nafasi tu yatakudhuru vikali. Na kunyamza kimya pia ni hekima kama Ayubu anavyotufumza, alipowaambia adui zake kuwa ni bora wangenyamaza maana ingehesabiwa hekima kwao. Ayubu 13:5.
Kila kosa linafunzo lake, lakini kwenye kila kosa lazima umuone adui pia, na ujifunze kuyaona mapenzi ya Mungu hapo pia. Epuka kujilaumu kulikopitiliza, laumu ndani yako iwe ile tu itakayokusukuma kwenye toba ili kuleta matengenezo. Sio ile itakayukupelekea kuvunjika moyo kama Yuda Ikariote, bali ile yene kicho cha Bwana kama Petro na kufanya matengenezo.
Usitishwe na kukosea, tishwa na kutokukubali kuwa umekosea, maana kama ni makosa hata Petro alifanya, ila aliporejea Bwana alimuinua tena, na kuendelea na jukumu la kutunza kundi la Bwana. Hokumu iliyopitiliza itaadhiri sana nguvu zako za kusonga mabele, Kama Paulo mtume anavyotutadharisha hapa;
2 Wakorintho 2:5 Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu, bali kwa sehemu (nisije nikalemea mno), amewahuzunisha ninyi nyote. 6 Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi; 7 hata kinyume cha hayo, ni afadhali mmsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi.
8 Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu.
Wao hupaswa kukuonyesha upendo. Ila ukipunguka, na mashutumu kuwa mengi, na kukung’onga kwa wingi, ndipo ile Zabur ya 38 inapaswa kuingia kazini, uwe bubu yaani usijibizane nao, na uwe kiziwi katika mashutumu yao, yaani usiyatilie maanani. Na ukiweza wazuie wanaokuletea maneno ya umbea au shutumu zao, au wanaotumika kama wajumbe wakutoa maneno huko na kukuletea, maana uwe na hakika kuna hatari ya wao pia kuchukuwa kwao na kuwapelekea wao.
2 Wakprintho 7:8 Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu.
9 Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote.
10 Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.
11 Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.
Natumai hapo tumeelewana vyema! Kuwa unapaswa kuwa makini na aina ya huzuni inayojengeka ndani yako! Isiwe na hali ya kujikinai yaani kujihukumu kunakoleta kutokujiona kuwa huna thamani, bali iwe ni katika kujinyenyekesha na kuhitaji msaada wa Mungu. Kama Petro. Yuda alizalisha aina ya hukumu iliyompelekea kujinyonga.
Kumbuka tena kuwa iliyonje ya Kristo hudhoofisha nguvu zako za kusonga mbele, fahamu hili daima. Baada ya kosa, wanadamu wanaweza kusimama na mabango ya lawama, lila uwe na hakika kuwa Mungu husimama na damu yake, akiita na kukwambia inagwa dhambi zako zimekuwa nyekundu sana, atazisafisha na kuzifanya kuwa yeupe pee! Isaya 1:18.
Nawiwa kukurudisha tena kwenye ile Zaburi ya 18. Unajua ni kwa nini ni muhimu kwako kuwa kimya!
Ni kwa sababu kujibu, kuna kufanya kupigana vita. Sasa kama upo kwenye vita A, unaweza kjikuta unazalisha vita vya pili vita B na uwezo wako unaweza kutokukuruhusu kuvipigana vyote kwa pamoja. Kama utavipigana baadae uwe na hakika na neema yake itakuja, ndio maana kuna wakati wa kunyamza na kujibu. Wakujibu utafika tu. Ila vingine vinayayuka bila wewe kujibu neno hata moja. Mungu huweza kukutetea mwenyewe au kuvisambaratishia hewani.
Pili ni kwamba kipindi kama hiki unaweza kujibu na kukosea, hali itakayokufanya kuongeza makosa au kumfanya adui kupata sababu ya kukushitaki maradufu.
Kuna hali ilinitokea nikiwa katika mapito kadha wa kadha kama haya, ina wezekana nawe pia imekutokea, na kujiuliza kama mimi. Ni kwa nini walionijeruhi wamekuwa na chuki juu yangu badala ya mimi kuwachukia? Yaani wameniumiza wao, mimi nikiwaona nina tabasamu na kufurahi, ila wao wana hasira na chuki ya dhairi kabisa. Nikiwa katika kujiliuza hili ndipo hili andiko liliponijilia moyoni mwangu; Walimchukia waliyemjeruhi.
Kwamba, watu wamekujeruhi, badala ya kukuonea huruma na kukufunga jeraha, wanakuchukia tena!
Sasa sikia nikupe sababu moja wapo kubwa.Ni kwamba roho iliyowasukuma kufanya hivyo, imegundua kuwa imemuongezea chura mwendo. Kuna muda unampiga chura teke ukithania kuwa unamuua au kumdhuru au kumkwamisha unakuja kugundua kuwa kumbe mbele yake kulikuwa na dimbwi au jabali naye alikuwa akiwaza namna ya kuvuka hapo ili aingie mtoni, nawe ukampiga teke na kujikuta unamvusha!
Walitazamia kuwa wangekukwamisha hapo, kumbe wamekuongezea yota begani mwako, wamekupa alama ya cheo badala ya alama ya uchafu. Kwa hiyo adui ndani yao anawaka hasira, ndiposa sio busara kuwa karibu na watu kama hawa kwa muda kadhaa maana ile roho iliyo ndani yao inaweza kukubambikizia kesi nyingine. Andiko la kutokuwa na amani kwa wabaya asema Bwana ni muhimu sana kulifahamu.
3.
4.
Kitabu kikitoka Kitafute..
Kama hujaokoka na nikuimize kufanya hivyo..inawezekana imeishiwa nguvu kiasi cha kutamani kufa na una uhakika ukifaa utaelekea jehanum ya moto, umefikia hata kutamni kunywa sumu..nikutie moyo kuwa Yesu akiingia ndani yako atakupa Amani tele na kukupa uwezo wa kuyashinda hayo..hakuna jambo la kumshinda Yeye..sasa fuatisha kwa Sala hii ya Toba pamoja nami kwa Imani..
Sema; MUNGU BABA, NINAKUJA MBELE YAKO, NIMEGUNDUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NINAOMBA UNISAMEHE SASA, NA FUTA JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, LIANDIKE SASA KWENYE KITABU CHA UZIMA WA MILELE Amen.
Hongera kwa kuokoa na tafuta kanisa la Watu waliokomaa ukasali hapo..Asante..
Mawasiliano yetu: Simu..0759859287. Baruapepe: ukombozigospel@gmail.com Pia kutembelea www.ukombozigospel.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni