Jumamosi, 27 Februari 2021

Kitabu chetu cha: MAMBO MUHIMU YA KUFANYA AU KUZINGATIA KUNAPOKUWA NA ADHABU YA KIUNGU INYOIJUMUISHA ENEO ULILOPO AU JAMII.

Na Mwalimu Oscar Samba 

Neno Kiungu huwakilisha kutoka kwa Mungu au Shetani, ujumbe huu ni sehemu ya hiki kitabu chenye mada na pwenti kadhaa, ila hapa nimezicha,bua mbili tu; #Corona #Covd19 #Tsunam #Majanga  #Kimbunga #magonjwayamlipuko  #tanzania

1. Lifanye Eneo Unloishi kuwa Ghosheni yako. 2. Ijue na Uitumie Damu ya Yesu ya Pasaka; 3. Mulize Mungu kama Daudi; 4. Litengenezee Kusudi la Mungu Kisafina kama Musa, ama Nuhu; 5. Jifunze Jambo kwa Mke wa Lutu;

6. Sadaka kama Ulinzi; 7. Sadaka kama Sehemu ya Rehema, Mfano ile ya Daudi kipindi cha adhabu ya Tauni, 8. Taka Kujua pigo Hilo au Adhabu hiyo Inataka nini ili Ujisalimishe kwa Bwana, Mfano Rahabu, na Epuka kosa la Farao.

 9. Yajue na Uyaombe Maombi ya Musa ya Kulitengeneza Boma, 10. Mtafute na Umuondoe Akani, 11. Jitenge na Kusanyiko, au Kiunganishi cha Kusanyiko ama Waadhibiwa, ondoa jina lako kwenye watu wanaotakiwa kupewa hiyo Adhabu kwa Damu ya Yesu.

 

12. Tafuta Maelekezo Maalumu ya Mungu juu yako, kama Isaka dhidi ya Janga la Njaa na Wazazi wa Yesu. 13. Unapoisikia Hofu Usiipuzie, Taaka Kujua ni Aina gani ya Hofu ala Uikabili..

 

14. Tafuta Kukumbuka kama Mungu Aliwahi Kukujuza hapo Awali na Hukumsikia Vyema au Hukumbuki. (Amosi 3:7 Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.) Sijui sana ni kwa nini kanisa la leo lina uzito kwenye hili,  nijualo ni kwamba uwezo wa kusoma alama za nyakati, au majira umekuwa ni adimu sana kwa kizazi cha leo! Nafahamu kuwa hali ya kupuzia ndoto, kutokutambua jinsi Mungu anavyoongea, na mafundisho manyonge kuhusu uhusiano wetu na Roho Mtakatifu ni miongoni mwa sababu ambatanishi.

 

Kama kuna mahali Shetani amefanikiwa leo ni kuondoa, ama kuzimisha kama sio kufifisha karama ya unabii, na huduma ya nabii, pamoja na neno la maarifa!

 

Na anatumia njia kuu kama mbili hivi, moja ni kuhakikisha kanisa linapoteza imani na manabii au wanaotumiwa na karama hizi, kwa kujiwekekea manabii wa uongo, ili kuwakatisha watu tamaa na kuwafanya wa waone hata wale wa Mungu nao ni kama hao wengine!

Pili analitumia kanisa lenyewe, kwa kufikia hatua ya kupinga, na kukataa, na kuzimisha huduma na karama hizi, na sababu zao ni nyingi ila hazina hoja timilifu kibiblia, maana kama kuna wimbi la mafundisho na huduma potofu, suluhu bado sio kuzima na kukataa ile ya kweli, bali wafunze watu namna ya kutambua kweli na uongo. Mchele ukiwa na chuya, dawa sio kukataza nyumbani wasipike tena mchele bali ni kuwafunza kuzitoa, na kama ni mcahanga basi watake kuwa makini kuchambua maana mawe mengine ni yale meupe, kwa hiyo yanafanana kwa karibu na mchele, lakini pia kama ni vigumu, wafunze kupembua au kuuchambua wakati wanauosha na maji, njia ambayo ni salama zaidi.

 

Maharage yakiwa na mchanga au mawe, hayamwagwi, bali huchambuliwa! Na wewe ukiona dosari katika hudumka na karama hizi, hakikisha unazikabili!

 

Maandiki yako wazi kabisa katika biblia kuwa tunatakiwa kujifunza na kuhakikisha kuwa tunasoma alama za nyakati, au tunajua mabadiliko kwa kuzitambua dalili zake, mkulima asipojua kusoma uso wa nchi, hakika atakuwa akipitwa na maamuzi dhabiti katika majira husika, wakati wengine wanandaa mashamba yeye atashindwa kufanya hivyo, ama atajikuta akiwacheka wengine, maana kwa wengine ili walime ni hadi waone mvua imenyesha bila kujua kwa kufanya hivyo ni gharama zaidi maana aridhi husumbua kwani kulima kwenye tope ni kugumu zaidi! Pia ipo hatari ya kushindwa kufanya vyema maana kuna uwezekano wa kunyeshewa! Kuna kuchelewa pia kupanda, maana wakati wa kuotesha wewe ndo kwanza unakwatua udongo.

 Hosea hufananisha jambo la kuukwatua udongo sawa na kuomba, maana husema tumtafute Mungu, akitangulia na kututaka kuukwatua udongo wa mashamba yetu! Kiroho kuna vipindi kama hivi! Kuna kipindi cha kumtafuta Mungu kabla ya adahabu haijaja! Ukichelewa gharama yake ni kubwa sana! Unaweza kujikuta umeshapoteza ndugu wengi, ama hasara kubwa imeshatokea!

 Mama yangu wakati ugonjwa huu unaingia au umeanza kushamiri, ndipo aliponitaarifu kuhusu ndoto aliyowahi kuiota! Japo hakuwa ameielewa kipindi hicho! Ila nataka ufahamu kuwa Mungu alikuwa ameshaongea naye!

 Elimu na ufahamu wa kuzijua nyakati ni muhimu sana, na ni kiroho kabisa, jihakikishie kwa watu hawa, ambapo hata leo makanisani wapo, na kama hawajafungwa

midomo na wachungaji ama watumishi waliokosa ufahamu sawia, basi kwa maeneo mengi hawajajitambua bado! Maana kama dunia au jamii uliyonayo na hata wewe hauona maelekezo ya kutosha kuhusu kinachoendela leo, ama umejikuta umeingia ama mmeingia kwenye janga kwa kushutikizwa, yaani bila kutambua rohoni! Uwe na hakika kuna watu waliopewa jukumu hili na hakupiga panda, hakutoa taarifa! kama ni wewe katubu, maana uliwekwa juu ya kuta kama Ezekieli alivyoagizwa, na hukutoa taarifa, ile kwamba hukuona, maana yake ulikuwa umelala! Tafuta kujua kilichokupofusha! Ile uliona hukusema, fanya toba kubwa! Maana ni nani ajuae kuwa kwa kupitia wewe watu waliokufa, hasara iliyotokea isingetokea!

 

1 Mambo ya Nyakati 12: 32 Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.

Biblia ya Kiswahili rahisi imetumia haya maneno: Watu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya,

walikuwa wakuu 200, pamoja na jamaa zao

wote chini ya uongozi wao.

Akili za kujua nyakati, ufahamu wa kujua majira, ikibeba neno ili kuwajulisha wana wa Israeli nini cha kufanya! Wasomaji wa sura au mukutadha huu wanafahamu kuwa hao ni mashujaa wa mfalme Daudi! Ni kikosi kilichomuwezesha kushuinda vita! Vinatajwa kwa makabila yao, na wana hawa wa Isakari walipewa kipawa cha kuweza kusoma majira! Swali langu ni katika hoja ile ile, kwamba wewe umepewa nafasi hii! Na katika kansa lako hawa watu wapo, na kama wapo wanajitambua, na wanatambulika, wanatumiwa!

Daudi alikuwa na watu ambao wanajua nini cha kufanya kabla ya vita, na wakati wa vita!

 

Na kwa bahati mbaya sana hata Mungu anapozungumza na mtumishi au mtu binafsi kuhusu hatari iliyopo mbele, wengi hupuzia! Sijui huwa unafikiria au huwa “unajiulizaga” kuwa nini kingalitokea kama mfalme wa Misri Farao angeamua kupuzia ndoto alizoziota au tafsiri aliyopewa na Yusufu!

 

Sasa jaribu kufikiri kuwa Farao kapuzia, na njaa imeingia Misri, na kuna watu wanakufa kwa njaa, na sio katika Misri tu, bali dunia nzima inateseka na janga la njaa na hawana msaada!

 

Uwe na uhakika, hata familia ya mzee Yakobo ingeteseka japo ni taifa teule! Na ndicho kinachoendelea kwa dunia inapofika kipindi cha mapigo kama hiki! (Na kanisa nalo linatandikwa!)

 

Watoto wanakufa, wazazi au watu wazima nao wanakufa, wakiwemo wafungwa magerezani, matajiri na fedha zao wanapoteza maisha kwa njaa pia, lakini tatizo ni uzembe wa Farao kupuzia ndoto (Ujumbe)! Ama kama Yusufu naye asingekaa kwenye nafasi yake!

Nataka tu kukufikirisha kuwa, huenda tumefika hapa tulipofika leo kwa sababu ya mtu mmoja au wawili, yaani Farao na Yusufu wetu kutokukaa kwenye nafasi zao au yao vyema!

 

Kukitokea vita kwenye jamii, kukitokea njaa ama ukame, magonjwa na majanga ya kimazingira au kijografia ama kibaolojia kama haya ya kiafya, usiwe mwepesi wa kumtazama Mungu kwa jicho la kumuhoji maswali magumu, bali tafuta kujua kama wapo wakina Yusufu waliozembea, huku na wewe ukijipeleleza! Na inawezekana haukuwa na ujumbe wa taifa lote, ila ulikuwa na ujumbe wako binafsi, jiulize uliufanyia kazi!

Tuendelee kujionea jambo hili kibiblia.

 

 

Mfalme Herode alitambua fika kuwa hakuna jambo tena hasa ama hususani linaloweza kuwahusu wana wa Israeli lisiloweza kuwa lilishanenwa, ndiposa alipopata taarifa za kuzaliwa kwa Yesu, kabla ya kuleta majanga au janga alilokuja kulileta la kuangamiza watoto wote wa kiume, alitafuta kujua jinsi ilivyokuwa imetabiriwa! Sasa huyu ni mtu asiyeokoka, ila alijua siri hii! Cha ajabu kansia la leo, lemedumaa mahali!

 

Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii,

“Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.” Ni Mathayo 2:2-6.

 

 

Ni mchungaji ama ni mtumishi gani leo mwenye kuweza kuwakusanya watu wake wa maombi na kuwaambia nawapa siku kadhaa nataka mniletee jibu la Mungu kwanini janga hili leo! Ama mwenye uwezo wa kuingia gharama na kutafuta kilichonenwa! Ninachojua sana sana mara nyingi kwenye majanga kama haya ni kumkemea Shetani, na kuomba rehema ambayo mtu hajui ni kwa nini anaiomba, kwa hiyo huwa katika kubahatisha, yamkini Bwana tumekutenda dhambi, yamkini kuna hiki na kile! Ni vyema, kuomba hivyo, ila ni kwa nini usifike mahali pa kutaka kujua kiunagaubaga nini kilichosababisha kwa kutaka kufahamu kama hapo awali Mungu aliwahi kuongea au kulidhibitisha hili la leo!

 

Mafarisayo nao hawakuwa nyuma, walikuwa wakiyapekua maandiko, wakitafuta sana kujua habari za Kristo, na Yesu alilijua hili, ila upofu uliwagubika kiasi cha kuona ila wakijifanya hawaoni, kiasi cha kunyimwa kufunuliwa waziwazi ili wasije wakaongoka!

Yohana 5:39 Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.

Kuna vitu walitaka kuvihakiki kutoka kwa Yesu! Na hakuna mahali pengine walifahamu wanaweza kuvipata nje ya maandiko! Ila kanisa la leo mambo yanapokuwa magumu haliwi jepesi kwa kutaka kujua hapo awali kama ilishanenwa au kutaarifiwa! (Jifunze kuchunguza-chunguza.)

 

Na kama hujui pa kuanzia, jambo hili lisikusumbue, wewe ingia kwenye maombi, ukimsihi Roho akufunulie lilowahi kusemwa, ama akuinulie mtu atakayekupasha, au akukumbushe kama uliwahi kuambiwa na hukumbuki! Naye ni mwaminifu, uwe na hakika kama Manoa na mkewe yaani wazazi wa Samsoni walivyoomba yule malaika arudi tena ili kuhakikiki ujumbe ule, naweitakuwa vivyo kwako!

 

Ni muhmu sana kujua pa kuanzia! Na sehemu sahihi ya kuanzia ni pale ambapo Mungu alishajifunua ama kulifunua jambo hilo!

 

Mafarisayo pia walitaka ishar ya mambo yajayo, au yaliyokuwa yakiendelea, hii ina maana pana sana! Yesu ni kweli alikuwa ni ishara! Ila kuna ishara nyingine ambatanishi kumuhusu! Sasa ile Yesu aligoma kuwaambia, wewe sio kazi yako kushikilia hapo, maana hawa waliuliza kinafiki, na Yesu hakuwa na haja ya kuwajibu kama mtu amjibuvyo mwanafunzi mwenye nia au dhamiri njema, wewe uliza, na mwambie najua utakuwa uliongea mimi sikuelewa, maana leo nipo kwenye janga, nataka kujua kwa nini sikuliepuka, au jamii yangu, ama ile jamii unayoiombea! Maana nilipaswa kujua mapema!

Na kama unaziona ishara au dalili za jambo lijalo, sasa kupitia ujuzi unaojuzwa hapa, hakikisha hutakubali kufanya kosa, bali utatumia maarifa haya vyema!

 

Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni. Akajibu, akawaambia, [Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu.

Na asubuhi, mwasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?] Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake. Mathayo 16:1-4

 

Kuna mambo mawili tunayoweza kuyapata hapa, mosi ni kwamba ishara ya Yona ni adhabu, kwamba hawa Mafarisayo walitumwa kama Yona, ila wakagoma kukaa kwenye nafasi zao, na jambo la pili ni siku tatu, mateso ya Yona, ambapo huwakilisha Yesu kufa na kufufuka baada ya siku tatu, kuwa katika hali ya kaburi siku tatu kuu sawa na kule kuwa katika tumbo la samaki kwa Yona. Hapa alilinyambua kidogo;

 

Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Ni Luka Luka 11:29-30.

Kitu muhimu ninachotaka ujifunze hapo ni hiki! Watu hawa walitambua kuwa lazima jambo hili linaloendelea lina ishara ndani yake! Sasa walipekua na kupekua katika maandiko, yamkini waliona walichoona, maana kama waliweza kumjuza Herode kuhusu kuzaliwa kwa Yesu ni fika na maengine waliyaona na kuyajua! Sasa ya Rohoni zaidi, ama tafsiri zake, walitaka Yesu amalizie ama awasaidie! Maana hawa ni waandishi wa Torati, na Waalimu, na viongozi wa ibada, ni wanatheolojia wa maswala ya dini yao! Ila kuna vitu bila Roho huwezi ona!

Ninachotaka wewe ujiulize, je umeshalipa ghrama za kutaka kujua kama kuna wakati ulipaswa kujua, ila hukujua na sasa upotayari kufanya fidia ya kosa husika!

 

Natumai jambo hili, ama utakapoenda mbele za Mungu atakujuza kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wake! Walitaka kujua mambo yajayo, na wewe taka kujua yajayo pia, ila kama umeshachelewa na upo kwenye tatizo, usife moyo, mtake akukumbushe, tujionee hapa, maana ni muhimu kujua kuwa kila jambo linaloihusu dunia, iwe ni mabadiliko mabaya au mema linakuwa na ishara zake!

…. (mstr.3-4) Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye..... (Unaweza soma sura karibia yote ya Matahtayo 24.)

Jibu lao limekuwa nimsaada mkubwa sana kwao na kwetu! Walipata mskukumo wa kutaka kujua dalili, za mambo yajayo, na ujio wake Yesu mara nyingine!

 

Na sijui ni kwa nini kanisa leo halina kiu ya kutaka kujua dalili za mambo yajayo, na hata Mungu anapolifunulia hupuizia! Wengine hukemea, kana kwamba kila kitu kibaya ni pepo! Unaonaje kama wanafunzi wa Yesu wangekemea hizo dalili za mambo yajayo! Waanze kusema kwa jina la Yesu wa Nazarethi tetemeko la aridhi la kipindi hicho, na roho za vita, na njaa na hiki na kile vishindwe!

 

Sina maana ya kukemea ni vibaya la! Ni muhimu, ila ufahamu wetu ni lazima ukue, kwa kiwango kikubwa zaidi! Kukosa maandalizi ya kifikra ni miongoni mwa sababu ya kuwafanya watu waombe maombi ya kiholela!

 

Sasa usiache kuomba kwa hofu kuwa unaomba kiholela la!

Maana hata hapo pia Mungu yupo ili akujibu, na maadamu tuna Roho Mtakatifu ambae hujua kutuombea vyema maana sisi hatujui, usiwe na shaka wewe msihi na omba katika Roho atakusaidia tu!

Ila hii siyo sababu ya kuufunga ufahamu wako na kukuzuilia kukua katika kumfahamu Mungu kiupana zaidi katika jambo hilo!

Unaonaje watu wa dhiki kuu, au watu wa kipindi cha kukaribia kunyakuliwa kwa kanisa wakaishi ama tukaishi bila kuzijua dalili husika!

Dalili zipo ili kukusaidia kujua cha kufanya kabla, ili kuepuka kukosea, na kutenda vyema!

Ukimuona mpendwa mwenye mashaka, na wasiwasi, hajui cha kufanya katika kipindi cha janga kama hili, uwe na hakika kuna shida mahali! Na ni kwambie wazi tu kwamba, ukiona kanisa limefikia mahali pa kukosa majibu ya jambo kama hili, ni fika kuwa, kuna mahali halikukaa kwenye nafas yake! Kanisa ni jicho la Mungu!

 

Katika kanisa la Matendo ya Mitume, au kanisa la kwanza, kulitolewa unabii kuwa kutakuwa na njaa katika Dunia! Jibu na suluhu halikuwa kukemea pepo au roho ya njaa, bali lilikuwa ni kuweka akiba, au kuandaa changizo kwa ajili ya watu kama hao!

Ni kuhakikishie kuwa kama baadhi ya wapendwa wangekuwa wao ndio Yusufu yule wa Farao, hakika wangeingia kwenye  maombi ya kufunga na kuomba wakikemea na kuzuia pepo na roho ya njaa! Ila maelekezo sahihi yalikuwa ni kujiwekea akiba!

 

Kanisa leo linataka limuongoze Mungu! Sio liongozwe na Mungu! Ni sawa na wale wanaopuzia mashariti na maelekzo ya wataalamu wa afya katika nyakati za majanga kama haya! Wanasema tunamuamini Mungu, kwa hiyo kuchukuwa taadhari kama za namna ya kujikinga kwao ni vigumu sana! Uwe na hakika kuwa wangekuwa ndio wakina Yusufu wa leo wangemwambia Farao, ni kweli imetabiriwa kutakuwa na njaa ila tumuamini Mungu, ninasema kama mtumishi wa Mungu hakutakuwa na njaa, na wakikukuta unajiwekea akiba wataanza kukushanga na kukwambia wewe huna imani!

Matendo ya Mitume 11:27-30

Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio.

Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi.

Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

 

Ujumbe huu ukupe kujichunguza kama kuna mahali ulipewa maelekezo fulani nawe ukajifanya wakiroho kuliko Roho, aidha ukiishilia kukemea ndoto! Maana sio kila ujumbe mbaya unahitaji kukemewa, mwingine unahitaji mbinu za kukabiliana nao, kama kujiwekea akiba, na kadhalika! Sasa ikupe kufahamu, na kisha kusahihisha makosa!

 

Andiko ama maandiko yajayo yanatupa upana sana, kuwa manabii walitaka kujua kuhusu wokovu ujao, na pia kuhusu mateso yaliyowahi kutabiriwa, sasa na wewe taka kujua mambo yatakayoikumba jamii, na unapojulishwa usipuzie, bali tafuta kufahamu ni nini cha kufanya, achana na ushamba wa kukemea kila kitu! Tafuta muda na Mungu ili utoke na maelekezo muhimu ya kufanya, Yusu alitupa ama aliisaidia dunia sio kwa kukemea ndoto, bali kwa kuwa na maelekezo muhimu! Petro alipopewa ujumbe na Yesu kuwa utanikana mara tatu, alikemea! Na wewe ukijifanya wakiroho kuliko Yesu sawa, ila uwe na hakika yatakupata kama ya Petro! Mwenzako alipogundua kosa alitubu, sijui wewe!

Kitu amabcho Petro abngwezeza kufanya ni kuomba maombi kama aliyoombewa na Yesu, au kuomba msaada zaidi wa amombi kama hayo! Mana Yesu alimwmabia kwua nimekuombea ili imani yako iimarike, na ukiimarika waimarishe na wenzako!

 

Unaonaje kama Yesu asingemuombea Petro! Na wewe unaonaje kama usipoomba! Tena kwa maarifa, sio kuomba ilimradi umeomba! Ishara ya jogoo, ilionyesha jambo! Na wewe taka kujua ni sihara ipi ilioamriwa katika majira! Maana kutokujua hakuondoi uwepo wa tukio usilolipenda! Bali kuchukuwa hatua kunaweza kuliondoa, ama kukupa namna ya kulikabili!

Tujonee hapa:

Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.

Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.

Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia. 1 Petro 1:10-12.

 

Mwalimu mmoja wapo aliyemzuri wa jambo hili ni Danieli, katika sura ile ya tisa ya kitabu cha Danieli tunajionea jinsi Roho alivyomfunulia, ni baada ya kuwa na kiu, au shahuku ya kutaka kujua muda ambao ulishatabiriwa! Na alipojua moja kwa moja alichukuwa hatua ya maombi, sasa huyu aliomba kwa maarifa, na majibu yakakapatikana, sijui wewe umejipangaje au unaombaje! Maana natumai kuwa wana wa Israeli walikuwa wakiomba siku zote, ama mara kwa mara, ila walipotambua, au walipofunguka ufahamu, uliokuja baada ya kujua yaliokwisha kunenwa moja kwa moja majibu yalipatikana, natumai pwenti ijayao itakupa maarifa zaidi.

 

 

15. Ombea Akili zako, au Msihi Roho Mtakatifu Azifunulie, ufunuo wa Kiungu ni kitu muhimu sana hapa! (Danieli 9:22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danielii, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.) Kuna aina ya akili, au ufahamu unaohitajika linapofika jambo kama hili!

 

Sijui kama unajua, ama wenzangu wanafahamu kiundani kuwa mapigo kama haya yanayoamuliwa juu ya dunia mara nyingi huwa na tabia ya kufunga fahamu za watu ili wasijui namna ya kujinasua! Ni kama vile funguo huwa zinafichwa au kufungiwa mahali! Ndio maana utawakuta wengi wananung’unika, wengine wanaomba ila sio katika maarifa!

 

 

Tukirejea katika mabo ya Nyakati tuliposoma, tunajione kitu muhimu sana pale! Akili/ufahamu kama semu ya kumuwezesha mtu kutambua nyakati, au majira, yaani kuweza kujua ni nini cha kufanya! Kumbe uwezo wa kujua cha kufanya umefichwa au umewekwa katika akili!

1 Mambo ya Nyakti 12:32 Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.

Biblia ya Kiswahili rahisi imetumia haya maneno: Watu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya,walikuwa wakuu 200, pamoja na jamaa zao wote chini ya uongozi wao,

Kanisa likifungwa ufahamu, hakika haliwezi kujua nini cha kufanya! Kunajanga kubwa lilikuwa likiikabili Israeli, (japo wanahistoria na ukisoma historia ya Israeli utaliona hilo, na yamkini bado haijaishia hapo,) ila Israeli ama Yerusalemu haikuweza kuliona hilo jambo!

Badala yake waliendelea na kupuzia mambo, ama kumkosea Mungu! Yesu aliyeona aliumia, aliugua, na hata kulia machozi!

Alitamani wachukue hatua zitakzowawezesha kuepukana na hatari hiyo! Tunafahamu miaka kadhaa baada ya kufa kwaYesu, mji ule uliharibiwa vibaya na dola ya Kirumi, watu wao waliteseka njaa hata mamilioni kuja kuuawa na Adolf Hitler, hadi leo Israeli imekuwa katika taabu ngumu, na kama hiyo haitoshi maandiko yanaelezea misukosuko kadhaa katika kipindi kijacho!

 

 

Yesu aliliona hilo! Ila akili ama fahamu zao zilifungwa, sasa ni nani ajuae kuwa na kwako, au jamii yako kuna tatizo kama hili! Ndiposa maandiko yakasema kuwa unaambiwa mambo mengi lakini hutilii moyoni! Ni kwa nini! Akili, na fahamu zimepofushwa! Sasa hata ifikapo wakati wa kutafuta suluhu, mambo kama haya husalia akilini mwa watu! Kama adui alimfunga mtu asitambue dalili au ishara, ili asiweze kuzuia lijalo, ama kujua namna ya kufanya, uwe na hakika hata kipindi cha taabu atafanya hivyo hivyo ili kumzuilia asiweze kujinasua hapo!

 

Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,

 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.

Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako. Luka 19:41-44.

 

 

Nataka ushike sana haya maneno, “Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako!”

Anatuambia kuwa yamefichwa machoni pako! Kuna mambo yampasayo amani! Yaani akiyatenda amani itakuja!

Asipoyatenda amani itatoweka.

Wana historia huelezea jinsi hata Hekalu linalotajwa hapo mbeleni katika mukutadha wa sura hii jinsi llivyokuja kuvunjwa, mji huu ulibomolewa kweli, adui zao waliuzingira kweli, na kipindi hiki kilikuwa kigumu sana kwa taifa hili! Ila kilishatabiriwa mapema, ilijulika, (ila hakutambua ishara, kwa hiyo hawakujua cha kufanya ili kuepukana na madhila hayo;) maana adui alipofusha fikra zao!

 

 

Sasa kama zimepofushwa, na unataka kutoa msaada, unafanyaje! Ni kuhakikisha zinapata kuona! Maana fikra huwakilisha akili na ufahamu, maana kuwaza au kufikiri kwako hutegemea sana akili na ufahamu wako!

 

Sasa unaweza kuelewa ni kwa nini Danili alipoingia kwenye maombi, Mungu alihakikisha anampatia akili, ili aweze kuwa na ufahamu! Na uwe na hakika, haikuwa kwa ajili ya Danieli kama Danieli tu! Bali juu ya wakina Nehemia, Ezra na wengineo ambao walitumika kama viongozi waliokuja kuwatoa wana wa Israeli ama Yuda uhamishoni, ama kuhusika katika kuujenga mji na Hekalu!

Nini cha kufanya, kuna tegemea sana akili zako!

 

 

Ndio maana katika janga linaloendelea sasa maombi yangu ya awali ama pale mwanzo licha ya kupambana na aina ya hofu iliyokuja juu yangu, nilijielekeza kwa wanasayansi ili Mungu awafunulie waweze kugundua chanjo na hatiamae dawa ya ugonjwa husika! Na hutawasikia wapendwa wengi wakiomba maombi ya aina hii!

 Maana kwao kuweka akiba ni kosa! Ni kuishiwa imani, ila kukemea pepo la njaa ndio kiroho!

 

Maandiko yajayo licha ya upana wake, lakini yanatupa somo kubwa sana, kuwa kuna aina ya akili ambazo mtu akizikosa hawezi kujua kutenda jema, au lililosahihi, atajikuta akitenda ovu, ama akikosa uwezo ama upeo au uwelewa wa kufanya tendo jema!

Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema.

Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja. Je! Wote wafanyao maovu hawajui? Walao watu wangu kama walavyo mkate, Hawamwiti Bwana. Ni Zaburi 14:1-4.

 

 

Ndio maana ninakuimiza kuombea akili zako, maana Mungu anapotaka kuleta msaada huwa hatumii mtu ni mtu, bali hutafuta mwenye akili, mwenye kujua ni nini cha kufanya!

Katika kipindi kama hiki epuka sana kuomba na kutenda kwa kufuata mkumbo!

Unahitaji maelekezo maalumu ya Mungu kama nilivyokujuza kwenye ile pwenti ya 12 tukajifunza kwa Isaka na kwa wazazi wa Yesu, lakini pia jifunze sana kuombea fahamu zako, ili uweze kufunuliwa cha kufanya.

 

Nilitaka kumalizia kwa aya hiyo hapo ili niingie pwenti nyingine, ila na wiwa kukudhibitishia jambo hapa! Nilikwambia kuwa Yesu kwa Wayahudi alikuwa ni ishara, kwa hiyo kitendo cha kumkataa kiliwafanya washindwe kusoma alama za nyakati, kutenda kwao vyema kulikuwa ku katika kumkubali Yesu!

 

 

Sasa sababu kubwa ni hii ya kufungwa fikra ama fahamu! Sio toka kipindi kile tu, bali hata sasa, ndio maana hata baada ya kukutwa na mambo magumu, na mazito, na hata wengine kujikuta wapo uhamishoni hadi leo, bado hawajaamua kumrudia Mungu!

 

Amekosekana Danieli wa leo, ambae kwa kuvisoma vitabu anapaswa kufahamu ile Luka 19 ilivyofafanua mambo yote yaliyowakuta, na yanayoendelea kuwakuta leo, maana kitendo cha kuishi katika aridhi yao kama watu wanaoikalia kwa mabavu wakati ni uridhi wao ni ishara kuwa kuna kitu hakija kaa sawa!

 

 

Warumi inaelezea bana jambo hili, ukipata muda jichambulie kwa makini ile Warumi 11, jionee hapa, ili uwe na hakika pia kwako, ama kwa jamii yako ama kitu husika kama ni adahabu ya Mungu hutangulia kwanza kutia giza, kuwapiga upofu ili wasijinasuwe kwa nia ya kuwapiga sawasawa, alikadhalika kama kuna mkono wa Shetani hapo!

Huku ni sawa na kufichwa kwa kufunguo, au mlango kufichwa! Kwa nia ya kumzuilia mtu kutoka! Sasa hata kama ni Mungu haimaanishi ukimsihi hatakusaidia, wewe jifunze kwa Danieli, ni adahabu ya Mungu, na Mungu alimpatia akili na ufahamu!

 

Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo. Na Daudi asema, Meza yao na iwe tanzi na mtego, Na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao; Macho yao yatiwe giza ili wasione, Ukawainamishe mgongo wao siku zote. Ni Warumi 11:8-10.

 

 

Sasa utaelewa ni kwa nini maandiko husema kwamba, atakuja kuwamwagia neena yake! Na kazi moja wapo ya hiyo neema ni ili kuwawezesha kumtafuta Mungu! Yaani kumgeukia! Na unapomgeukia utaji, au upofu huondolewa! Hapa akili hufunguka, ndipo mtu huweza kutambua cha kufanya!

Dhibitisha hapa, maana kunja aina ya utaji hauondoki kwa kuwa umeokoka, bali huondoka kwa kuwa umeutafuta uso wa Bwana, na kuutafuta uso wa Bwana hapa sio kuomba kiholela, au kwa kufuata mkumbo, bali ni katika ufahamu, ni vyema kulielewa hili! Maana ni muhimu kujua utofauti wa maombi ya Danieli nay a watu wengine! Hata Habakuki kipindi hicho alikuwa akiomba! Ila tunajionea utofauti anapoamua kukaa kwenye zamu yake! Hapo ndipo majibu ya Mungu yanamjilia!

Kuomba sio tija, sio tishio ila unaombaje, ambako hutokana na fahamu zako!

Jionee hapa kuhusu utaji, au upofu huu;

 

..nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika; ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo;  ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao.  Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. 2 Wakorintho 3:13-16.

 

Anatuambia kuwa, “ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao,”hata leo, unapowahubiria injili, unapowambia neno hilo hilo ambalo hulisoma, utaji huu unawazuilia, ni ili nini! Ili wasije kuona wakaongoka, wakatubu, wakaponywa! Maana kuna kanuni muhimu za kutoka kwenye mapigo kama haya. Ukielewa hapa, utaelewa sasa ni kwa nini kuna watu wanapigwa, ama wapo kwenye taabu kama hii, ila wameamua kutafuta msaada kwa miungu mingine! Na wapo ambao hawataki hata kumsikia Mungu wa kweli, ni kama vile hajui ama hawaoni kabisa kuwa msaada upo kwake! Uwe na hakika ni kwamba wamefungwa fahamu zao, ili wasije kumgeukia! Ili akawaponya!

Ndio maana neema ya maombi, na sio maombi ya kawaida, bali ni maombi yenye mrengo wa kumgeukiaMungu, ili kuwaondolea utaji!

 

 

Na baada ya hapo ndipo wanawezeshwa au akili na fikra na fahamu zao zinakuwa na uwezo wa kumkubali Yesu! Tazama kinachofuata!

Ni wao kuomba toba, kuomba rehema!

Hii sio toba ya kawaida!

Ndio maana kiu yangu ni kutaka kuona watu wanafunguliwa fikra au fahamu zao kwanza, ili wawe na toba kama hii!

 

 

 Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.
 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.
 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;
jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao.
Zekaria 12:10-14.

 

 

Kumbe kama changamoto moja wapo kwa watu au jamii yako ni kumgeukia Mungu, na kuna wapendwa ndani yake, ni wewe kuwaombea au kuwamwagia roho ya namna hii ya maombi, na neema, ili neema iwape upendeleo, au kibali kwa Mungu, ama kuwafanya wakubalike ama kuwapa uhalali wakujibiwa au kusikilizwa kwa maombi yao, pia neema hiyo ili iwape maarifa, na nguvu za maombi, ikisaidiana na hiyo roho ya maombi! Kisha hapo watajikuta wakielekea kwenye maombolezo kwa maana kwamba kosa lao au hatia yao wameshaijua!

 

 

Unajua wakati huu ninapoandika kitabu hiki ni kwamba ugonjwa huu ni kama vile ulikuwa umeshaondoka, au kupungua kwa kiwango kikubwa ila umerudi tena kwenye taifa letu, ambako ilionekana kana kwamba umetoweka!

 

Na wengi wanajaribu kutafuta sababu za kurudi kwake!

Unajua nikikupiga, unatakiwa kutaka kujua ni kwa nini nimekupiga ndipo uombe msamaha!

Kuna wanafunzi fulani wa mtumishi fulani, ilikuwa mwalimu akiwachapa shuleni baada ya kuchapwa humuuliza ni kwa nini amewachapa!

Sasa huyu mwalimu alikuwa anakasirika zaidi, na aliamua kumuliza mzazi wao, naye alimjibu ndivyo nilivyowafundisha, ili wajue kosa, wajue mahali pa kujirikebisha!

 

 

Kama nimekuchapa kwa kosa la kutokunisalimia, na wewe ukaomba msamaha ili nikumpunguzie adhabu, na yamkini fimbo ilikuwa ziwe kumi, nikaishilia kwenye fimbo mbili, alafu hujui ni kwa nini nimekuchapa ila ukaishilia kufurahia kwa kusamehewa, huoni hiyo ni hatari sana!

 

 

Maana kesho unaweza kujikuta unanipita bila kunisalimia, na kwa kuwa nilikupa adhabu ya fimbo kumi, nikakusamehe nane, uwe na hakika safari hii zinaweza kuzidi, na mlango wa msamaha ukawa mgumu sana!

Ni muhimu kujua kwa nini adhabu! Alafu uombe sio adhabu iondoke tu, bali na neema ambayo itawazuilia watu kumkosa Mungu tena, na ikiwezekana uwataadharishe kuwa tumesamehewa, kwa sababu hii na hii, msimuasi Mungu tena.

 

Hongera kwa kusoma ujumbe huu, nakutia moyo kuzidi kumtazama Mungu, na pia uwenda hujaokoka, yaani Yesu sio Bwana na mwokozi wa maisha yako! Nakutia moyo tena kuokoka sasa! Yamkini ni uchumi, fedha, hazipatikani, unazingirwa na nuksi na mikosi, kila unalofanya haliendi, unakabwa na mapepo, ! Wewe njoo kwa Yesu na hayo yote yatapita kabisa ! Sasa natumi u tayari!

 

Sema; MUNGU BABA, NINAKUPENDA, ASANTE KWA KUNIPENDA KWANZA, LEO NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NA NIPO TAYARI KUOKOKA, TAFADHALI INGIA NDANI YANGU, SAMEHE DHAMBI ZANGU, NA FUTA JINA LANGU KATIKA KITABU CHA HUKU, NA ULIANDIKE SASA KATIKA KITABU CHA UZIMA WA MILELE, Ameni.

 

Kwa kufanya hiyo umekwisha kuokoka sasa, na tafadhali tafuta kanisa la watu waliokoka lililopo karibu nawe ukasali, hapo, waambie kuwa umeokoa hivi karibuni, ili wakulee vyema kiroho.

 

Mawasiliano yetu, kwa M-Pesa au Simu: +255 759 859 287, barua pepe: ukombozigospel@gmail.com

pia temnbelea: www.ukombozigospel.blogspot.com . AU www.mwalimuoscarvitabu.blogspot.com

 

#Habari-Njem ni kwamba, tumefanikiwa kutoa kitabu cha UKULIE WOKOVU, na cha USIFIE JANGWANI, vimetoka kwa njia ya PDF, tayari kwa ajili ya kusomwa kwenye simu na kompta, bei ni shilingi 5,000 za kitanzania; ukivihitaji au kukihitaji wasiliana nasi kwa simu +255759859287, barua pepe: ukombozigospel@gmail.com pia zidi kutembelea: www.ukombozigospel.blogspot.com  #MwalimuOscarVitabu #MwalimuOscarSamba

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni