“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili
zako mwenyewe” Mithali 3: 5.
Akili zako zinza mipaka, ufahamu wako kuna mahali unafikia
ukingoni, utashi wako na upeo wako “ni-limited” nikiwa na maana kuwa kuna
mahali unaishia, ila ukuu wa Mungu huvuka na ushinda ufahamu wote, ni yote
katika yote.
“Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana,
Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.”
Isaya 40:28.
Embu nenda name sanjari katika andiko hili; “Msijisumbue kwa
jambo lo lote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru,
haja zenu na zijulikane na Mungu. Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu/akili
zote, itawalinda/hifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Wafilipi
4.6-7.
Ina maana kwamba, unapokuwa taabuni, au katika adha, kitu
kimoja wapo Mungu anachokifanya ni kuachilia Amani yake, ambayo huzidi akili
zako, na ufahamu wako, ikiwa na mantiki kwamba ukiiruhusu ndani yako, akili
yako au ufahamu wako utapata utulivu, na njia moja wapo ya kuiruhusu ni moja tu
ambayo ni kuweka Imani na tumaini lako kwa Mungu, ni kweli tumeumbwa ili
kutumia akili ila sio kuitegemea, wa kutegemewa au kutumainiwa ni Mungu pekee !
Kwa nini ? kwa sababu akili na uelewa wetu huwa na mipaka !
madakitari hutegemea akili zao, ufahamu na maarifa yao, wakishindwa watakwambai
hapa hatuwezi, wanasheria au mawakili watakueleza kuwa hapa haiwezekani,
mazingira ya uchumi au kiuchumi, ama mapito kwenye ndoa, au ugumu fulani
unaweza kufikia mahali na kukueleza au kukwambia kuwa hili haliwezekani tena !
ni kweli na ni jibu zuri kabisa maana akili zetu zina mipaka!
Ila sivyo kwa Mungu, maana akili na ufahamu wake havichunguziki,
alizifanya mbingu bila nguzo na kuzitundika hapo angani kama pazia, ameiwekea
bahari mipaka na wala haijawai kuasi, ameliegesha jua na mwezi angani bila gundi,
wala hakuna siku jua linaweza kuchelewa kuchomoza, wala kuzama !
Aliigawa bahari ya Shamu wana wa Israeli wakavuka,
alilishimamisha jua kipindi cha Joshua na mwezi wana wa Israeli wakashinda vita
kipindi kile !
Haijalishi mapito hayo ni kama maji mengi, wewe kumbuka tu
hayata kugaharakisha kama Isaya 43 inavyoeleza, na kumbuka sana na fahamu kuwa
hajasema hauta pitia hapo, la ! Bali amesema hayatakugarikisha, ikiwa na maana
kuwa watapigana na wewe , ila kukushinda ndo hawawezi kukushinda !
Haijalishi mawimbi ni makubwa kiasi gani, maji ni mengi kwa
kiasi gani, ila wewe mtazame Mungu, ukubwa au wingi wa maji hayo ni kwa ajili
ya Mungu kujitwalia utukufu, kwa wewe kuvuka na adui zako kuzama, unaniuliza
Mwali Oscar inakuaje ?
Jibu ni hili, maji kipindi cha Nuhu ndiyo yaliyowezesha
safina ya Nuhu kuelea, bila maji isingeelea, lakini maji hayo hayo ndiyo
yaliyowaua na kuwangamiza waliokuwa waovu siku zile !
Hujajua kuwa bila bahari ya Shamu wana wa Israeli bado
wangeendelea kuteseka au kufuatwa-futwa na jeshi la Farao ? ukweli ni kwamba ni
ndio !
Sasa nisikilize, maji yale yale yaliyogawanyika na Mungu kujitwalia utukufu kwa kuwavusha wana
wa Israeli, ndiyo hayo hayo yaliyojifunga na kuwameza wana wa Farao !
Sasa wewe waogopa nini ?
Jifunze tu kumtazama Bwana ! kwa hukuwahi kujifunza kwa
Danieli na wenzie ?
Moto uliandaliwa kwa ajili yao, ndio uliotumika kuwamaliza
adui zao ! sasa unadhania bila hivyo wale adui si wangezidi kuwatesa na
kuwasumbua, pili hawa vijana bila hili pito unadhani wangeinuliwa kama
kilichotokea ?
“ Na
maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja,
wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala
nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala
harufu ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadreza akanena, akasema, Na
ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake,
akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa
miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao
wenyewe. Basi
mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila
lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na
Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa;
kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii. Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki,
na Abednego, katika wilaya ya Babeli.” Danieli 3:27-30
Nani ajuiaye kuwa jaribu hilo ni kwa ajili ya kukutukuza, au
ni kwa ajili ya kukuinua ! ni kwa ajili ya kuwaaibisha adui zako na kumuinua
Mungu wako ?
Najua moyoni mako unasema lakini Mwalimu hali ni ngumu, ndoa
ni nzito, mwenzangu simuelewi, uchumi umekuwa mifupa mikavu ! “usiwe na shaka
wewe itabirie tu !”
Uwemda moyoni mwako umefika mahali pa kushindwa kumuelewa
Mungu ! wewe sio wa kwanza, hata Habakuki alisumbuliwa na hili, au alifika
hapo, Daudi naye aliwahi kupitia hapo, kiasi cha kushangaa kuwa mbona waovu wanastawi
na wenye haki kuteseka, hadi kufikia hatua ya kujifariji kuwa ni kama vile
wanapaliwa mkaa ili wangaamie vyema !
Yesu pale msalabani alifikia mahali pagumu sana kiasi cha
kusema Baba mbona umeniacha ! Hakika hayakuwa mazingira mepesi !
Lakini hakufikiria kuiacha Imani, hakufikiria kuukwepa
msalabani, kama wewe unavyofikiria leo yamkini kujiua, kujinyonga, kumuacha
Yesu !
Uwe kama Ayubu, ni kweli alipitia mahali pa gumu, ila
hakuiacha Imani !
Najua umeomba, na kulitolea sadaka jambo hilo muda na muda
sasa, ila usife moyo, majibu yako yapo, yanakuja, usione kama vile Mungu
hakusikii, la, Hasha ! yu akisikia, tena sana, ila muda huu upo darasani,
unapimwa, kama Ayubu, na punde utapokea majibu mema kama sura ya mwisho ya
kitabu cha Ayubu ilivyo !
Binti mmoja alisema kuwa, mwaka huu ukipita kwa kweli kama
bado sijaolewa, .. akija yeyote hata kama ni mlevi, mwisilamu, ..mimi twende tu
! hapana ndugu yangu, usifikie hapo !
Wachaga wa Rombo hupenda kusema kuwa, “usiache Yesu,” kweli
kabisa, usikubali kumuacha Yesu kwa sababu kama hizo, wana heri wale wavumiliao
majaribu, maana watapokea taji.
Wiki hii nilimpa binti yangu mmoja kazi ya kusoma kitabu cha
Yakobo chote, na kumtaka kuwa akifikia kile kipengele cha kumtaka kuwa na
uvumilivu kama mkulima akirudie mara baada ya kumaliza kitabu chote !
Mpendwa, hao walioshinda kwa uvumilivu, huitwa ni wenye heri
au Baraka, maana walivumilia kama mkulima aingojavyo mvua ya mwisho ya mazao,
nawe mngoje Bwana, mtumaini yeye, muhesabu yeye aliyekuaidia kuwa ni mwaminifu
na siku moja yaja.
Ni kweli ulichokiomba kikikawia au kuchelewa moyo huugua,
huumia, husononeka, lakini pia ni njia ya Mungu kukufundisha saburi na kukupatia uthabiti wa moyo kama Warumi 5
isemavyo, ikiwa ni mtaji utokao kwa Yakobo moja, lakini kikipatika kilichongojewa
moyo hufurahi, kama kwa Hana alivyompata Samweli, Sara hutuambia kuwa Bwana
amemfanyia kicheko na kila atakayesikia atacheka pamoja naye, sasa nawe
vumilia, na Bwana atakufanyia kicheko tu, haijalishi umri umeenda kwa kiasi
gani, wewe mtazame Bwana !
Sijui wewe, ila mimi niliwahi kupitia mahali pagumu sana pa
kukosa chakula, na andiko hili lilinitia moyo sana, maana nililisimamia, nawe
najua lipo ambalo Bwana amekupa, nilisimamie hilo daima, ona langu;
“Mithali 10:3 Bwana
hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia
mbali.”
Mpendwa, ninakuitimishia na andiko hili, ambalo ndilo
lilonipa mtaji wa waraka au makala hii, nilipolisikia darasani, moja kwa moja
liliumbia ujumbe huu ndani yangu, maana kama umeweka tumaini lako kwenye duka,
genge, au gari, siku likiungua moto, au kufilisika, ama kama ni kwenye elimu,
siku ikipoteza dhamani machoni pa watoao ajira, au kama ni kwa mtu siku akifa,
hakika uhusiano wako na Mungu utayumba tu !
Ni hatari kuuweka kwenye muda pia, kama wengine wafanyavyo,
kuwa imechukuwa muda sana Mungu hajanijibu, ndio maaana nilikata tamaa ! nani
alikwambia kuwa Mungu anafungwa na muda au na majira uyatakayo wewe ?
Andiko hili lina dhima nyeti sana, Zaburi 44: 6 Maana
sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa.
Usitumaini maombi, mtumaini anayejibu maombi ! usitumainie
sadaka, mtumainie aliyepokea sadaka !
Hatari kubwa ya leo ni hii, ukisikia mtu akisema kuwa
nimeomba sana, nimefunga sana, nimekesha sana, lakini Mungu hajanijibu, kwa
hiyo kaamua “kuacha Yesu,” maana yake aliweka tumaini kwenye maombi, sio
kwa mjibu maombi, hajuia kuwa hata Daudi aliomba tena alikuwa kwenye
dozi ya maombi ya siku 40 lakini Mungu hakumjibu, na bado mtoto alifariki.
Haimaanishi kuwa kuomba ni kubaya, ila shika hili sana,
“Mungu atabaki kuwa Mungu, hata kama hajajibu maombi yako,” kujibu au
kutokujibu hakumbadilishi Mungu, na maombi hayamlazimishi Mungu.
Sasa haina maana usiombe, la, Mathato 7:7-8, Yohana 15:7,
kuna imizo la kuomba hapo ili upewe, kuomba ni kanuni ya kupokea, na ukiomba
kwa bidii utapokea kwa uzuri na ushindi zaidi, kama hicho kitabu cha Yakobo 5 kisemavyo,
kwa hiyo kufunga, kukesha ni njia njema sana, ila usiitegemee hiyo, mtegemee.
Pia Mungu hafungwi na muda, wala hatishiwi na mtazamo wako
kimuda, sasa sio vibaya kuwa na muda moyoni mwako, maana imani ni kuwa na
hakika, ila usijaribu kuutegemea muda, mtegemee Mungu katika huo muda, hili ni
muhimu sana ili likuepushe kufikia walipofika wanaosema kuwa nimeomba sana, huu
ni mwaka wa tatu sasa, nimengoja sana na sasa ninazeeka, ngoja niangalie njia
nyingine, hawajui kuwa alijitwalia utukufu kwa Zakaria na mkewe, na Sara na
mumwe wakiwa katika umri mkubwa !
Hajui kuwa YESU japo alitambua wito wake kabla ya kuzaliwa lakini
alianza huduma akiwa na miaka 30, lakini Yeremia na Daudi walianza udogoni, na
kuna mfalme katika Israeli aliatwana na maika 8, na alitenda vyema, sasa
ukitaka kuiga sawa iga, lakini ujue kama sio majira ya Mungu utakwama tu, maana
ni sawa na kujaribu kuendesha gari lisilo na nishati, ni kweli kwenye mteremko
utatumia maji kama wengi wasemavyo, ila kilimani, tutajua tu umekwama !
Musa alianza huduma na miaka 80, sio kuanza tu, bali ndio
alipokea wito rasmi, na alijijua ana wito akiwa na miaka 40, ila ilimchukuwa
miaka mingine 40, sasa utaelewa ni kwa nini Mungu alimwambia Habakuki haya
maneno; “3 Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili
kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa
haina budi kuja, haitakawia.”
Haikuwa na maana kuwa Mungu hukawia la, tena ni la Hasha ! Maana
Yeye hakawii, wala hachelewi, ila hufanya kazi yake kwa wakati, shida ni kwamba
kwetu sisi huweza kuona kuwa amekawia, sasa hapo unaambiwa ingoje, lakini
kiukweli haitakawia, na itafanya kazi kwa wakati wake, iliamriwa, sio utakayo
iamuru wewe ?
Nenda kajiulize kuwa Yusufu ilibidi ipite miaka mingapi toka
aote ile au zite ndoto, ndipo zije kutimia ? kumbuka aliota akiwa na miaka 17,
nenda katazame aliovyoanza kutawala ! Au kuiwa malangoni pa Farao !
Nenda kwa Daudi, alikuwa kijana mdogo, wakati anapakwa
mafuta, nenda katazame alianza kutawala Hebroni au Yerusalemi na miaka mingapi,
kisha Israeli yote !
Wengi wanataka wakipokea ahadi ya Bwana leo, itimie leo au
kesho, hilo haliwezekani, kuku akitaga leo, ni lazima asubirie yao la mwisho,
ndipo yaje majira ya kutamia, kama ni kanga uwe na hakika kuwa atatamia mwezi
mzima, kuku ni siku 21, tembo hubeba mimba kwa miezi mingapi ? unaonaje kama angetaka
kubeba kwa siku 28 kama sungura ?
Hakika hata njiti asingezaa, na wengi katika mapito wamejikuta
wakikumbwa na huu ugonjwa au hii shida, Daudi angeweza kufanya mapinduzi ya
kijeshi, ili kuiharakisha ndoto yake, maana watu walimkubali, wengine walimfuata
mapangoni, wakimuhudumia, na hata wapo walioimba na kumsifia Zaidi, lakini
aliungoja wakati wa Bwana uliamriwa !
Ninayo mengi moyoni mwangu ila nikuachie hapo, ila nataka
ujue kuwa niliwahi kumwambia binti mmoja, au niliwahi kuhubiri mahali kuwa,
yamkini mumewe au mkeo, yupo chuo, sasa bado muda mdogo amalize, ukilazimisha
kuolewa au kuoa leo, utajikuta unachukuana na asiye sahihi, kwa hiyo ungoje wakati
wa Bwana.
Unajua kungoja kwa Daudi, kulimfanya kutiwa mafuta na wazee
wa mji mara ya pili ? na ya tatu ? nakufundisha nini ? kuna hatari kama angejipaka
mafuta mwenyewe, maana wenye mji wangekuwa hawajamkubali, leo hii tunahaha na kibali
cha huduma lakini kwa kweli tumejitia mafuta wenyewe !
Ukienda kwa Yeyu ni kwamba alipokuwa anabatizwa ndipo Roho
alipomshukia na kutamka kuwa huyu ndie mwana mpendwa na watu wamsikilize Yeye,
unajua maaana yake ?
Hapo Roho alikuwa akimtia mafuta !
Sasa angelazimisha kabla ya wakati ni kwamba, hili
lisingetokea, maana Yohana mbatizaji angekuwa hajaanza huduma bado, ni lazima
ujuwe dhamani ya kuvumilia wakati ufike, maana Yohana wako ni lazima atangulie
kwanza, sasa ukilazimisha kupita njia ambayo Yohana wako hajaisafisha uwe na
hakika utakwama tu, ukitaka kuanza huduma bila kubatizwa au tukio la Roho
kukupaka mafuta utakwa mtu, maana ili Roho aje ni lazima huduma ya Yohana iwepo
kwanza.
Atakayekusemea kwa Farao wakati wake bado, sasa wewe
vumilia, maaana yupo atakae kusemea, atakayae kutambulisha kwa Farao, kama Barnaba
kwa mitume dhidi ya Paulo, leo wengi huhaha kujitambulisha wenyewe na sababu ni
kwamba wameshindwa kuenenda na muda !
Wakulima hujua, hatari ya kuvuna matunda au mzao ambayo
hayajakomaa, au kuiva vyema, sasa na wewe uwe makini, jifunze kumngoja Bwana,
na huwezi kumngoja ambaye hujamtumaini, Zaidi ukipata kitabu chetu cha NGUVU YA
KUMNGOJA BWANA, au cha USIFIE JANGWANI, visome, kuna jambo kubwa hapa
utalipata, kipo pia cha FARAJA, USIOGOPE, JIPE MOYO na cha MTUMAINI BWAMA, pia
kingne ni cha MTU WA NNE, au cha KATITAKATI YA SHIMO MTAZAME BWANA, asante na
kwa heri.
Kama hujaokoka na unataka kuokoka, maana haii ni njia muhimu
ya wewe kuweza kumngoja na kumtumaini Bwana, lakini pia itakuwezesha kuhakikisha
ya kwamba unakuwa na uwepo wa kutosha wa Mungu, basi fuatisha sala hii;
Sema, MUNGU BABA, NINAKUPENDA, NIMETAMBUA YA KUWA MIMI NI
MWENYE DHAMBI, NINAKUAMINI NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA
YANGU, TAFADHALI FUTA JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, NA ULIANDIKE KWENYE
KITABU CHA UZIMA,AMENI.
Tafadhali sasa tafuta kanisa la watu waliokoka na ukasali
hapo, wambie umeokoka na watakupa maelekezo maalumu, ameni, na hongera sana kwa
hatua hiyo.
Kwa mawasiliano, au M-Pesa, 0759859287, Barua pepe:
ukombozigospel@gmaoil.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni