Jumamosi, 27 Aprili 2019

NAMNA YA KUOMBEA ENEO, JAMII AU MTU FULANI.

Chimbuko la ujumbe huu ni kiu ya Mwanafunzi wangu mmoja aliyeniuliza maswali kadhaa majira haya, nami kumjibu, nami pia kupokea imizo la ndani yangu, kukumegea ama kukudodoselea majibu hayo, ila kwanza tazama kiu yake;
"Bwana Yesu Asifiwe Pastor
Kheri ya Pasaka.

Naomba mwongozo
Kama mtu unaguswa kuomba kwa ajili ya kumuombea au kuombea
1. Mtu binafsi analiyetakwa na nguvu za giza na yeye peke yake hawezi kujikomboa hatua zipi unapitia  ( Yaani mwongozo wa maombi kwa mtu huyu inakuwaje)

2. Kama unataka kuomba kwa ajili ya familia ulikozaliwa kwa ajili ya kuwakomboa uzao wa tumbo la mama yako ili Mungu aingilie kati unaendaj
e mwongozo hapa...

Tatu, kama unataka kuomba kwa ajili ya ukoo (mfano ukoo wa mama yako au baba yako ) ili kusaidia kutoka katika nguvu za giza na ili Mungu awakomboe mwongozo unaendaje

Nne kama unataka kuomba kwa ajili ya kijiji chenu au mtaa wenu ili Mungu aingilie kati juu ya nguvu za giza zilizotawala na kukwamisha mambo mengi unaendaje..

Tano kama unaguswa kuombea familia ya rafiki yako ambao unajua wapo chini ya nguvu za giza nawe unataka kuomba ili Mungu aingilie kati ananasue mwongozo ukoje....

Naomba unisaidie mwongozo"
Majibu:
Jambo la umuhimu la kujua ni kwamba kesi hizo zote zina karibia kufanana au kushabihiana, maana zinakuhitaji kusimama kwa niaba ya wengine, ama eneo fulani ! Sasa kuhusu eneo, kuna kitu cha ziada nami nitakiweka na kukufahamisha hapo mbeleni.
Kanuni !
1. Ijuwe nafasi ya Kikuhani, na Kifalme kisha Uitumie, wakati wa Agano la Kale makuhani kama wakina Haruni walipewa jukumu la kuombea wengine, kuomba kwa niaba ya watu wenye matatizo na Mungu aliwafungua, na hata kuwasamehe.

Sasa katika Agano Jipya nafasi hii amepewa kila mtu aliyeokoka ! Kwa hiyo wewe nawe ni kuhani, kama andiko hili lijalo lisemlo ambapo pia linadhima ya nafasi ya kifalme nitakayoichambua hapo mbele kidogo;
Ufunuo wa Yohana 5:10 ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

Ukianzia mstari wa tisa kuna picha fulani utaipata zaidi, ila nalitaka upate hakikisho la hiyo nafasi, wasomaji wa Waebrania wanafahamu jambo hili la kikuhani kwa mapana yake !
Namna ya kuitumia au kukaa katika hiyo nafasi ni kujitakasa kwanza au kuomba toba kwa ajili yako, maana ndivyo ilivyoagizwa kwa wakina Haruni kuwa wajitakase kwanza kabla ya kufanya hizi shughuli za kikuhani.
Pili, tangaza kukalia hiyo nafasi, ukisema sasa ninasima kama kuhani juu ya kijiji changu, mtaa, familia fulani, jamii, ama mtu fulani !
Kuhusu ile ya kifalme ni kwamba mfalme ni mtawala, kisiasa na kroho neno la mfalme ni sheria, agizo lake ni kanuni wala halichunguzwi au kupingwa !

Na wewe ukisima kama mfalme au mtawala katika eneo au jamii unayoiombea ni fika kuwa utakuwa na uwezo wa kimamlaka, maana alipo rais wa nchi na vyombo vya dola vipo hapo, sasa wewe kama mfalme na kuhani, uwe na hakika serikali yote ya mbinguni i nawe, kwa hiyo utakalo tamka mbingu na malaika watatekeleza kwa haraka na wepesi mno la muhimu uwe na imani na ujiamini kuwa kweli nafasi hizo ni zako !
Kama Yesu alivyotukuzwa, na kuinuliwa kwa viwango vikubwa vya utawala uwe na hakika, nawe ndivyo ulivyo maana ile Ufunuo 5:9-10, haishii tu kutuambia kuwa ametufanya kuwa makuhani na wafalme, na tunamiliki au kutawala juu ya nchi, bali inaanza kwa kueleza kuwa alitununua, na kutufanya hivyo, sasa kama Yeye yu juu kuliko miliki na tawala zote ! Na maandiko husema kuwa tumeketi pamoja naye maana yake nasi tu watawala pamoja naye !

Waefeso 1:21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;
22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo.
Kwa hiyo, hapa unaweza kuomba toba kwa ajili ya eneo, ama mtu husika, ama jamii fulani, pia waweza kemea au kufukuza hayo mapepo, ama kutiisha huo utendaji wa adui ukiwa kama mfalme ama kuhani, ama nafasi zote kwa pamoja.
Katika ufalme jifunze tu kujiamini, ama kutangaza kusimama kama mfalme, kwa ajili ya eneo husika, nikiongeza kitu kuhusu ukuhani ni kwamba fahamu sana kuwa wewe ni wa uzao wa kikuhani ! Sasa mtu wa kabila la kichagga naye ni mchagga, alikadhalika mtu wa uzao wa kimasai naye ni mmasai, kwa hiyo ni zaidi sana nawe kuwa kuhani na mfalme maana Kristo ni Mfalme Mkuu na Kuhani Mkuu ikiwa na maana kuwa wasaidizi wapo, ndiposa awe Mfalme wa wafalme !

1 Petro 2:9 Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;
2. Fanya Toba, jifunze sana namna ya kuomba toba kwa niaba ya watu wengine ! Ama namna ya kuombea wengine ! Yesu anamwambia Petro kuwa lakini nimekuombea ! Nataka uione hiyo dhima ya kusimama kama Kuhani na kubeba wengine !
Sasa tukija katika toba za aina hii utaiona kwa Danieli, jambo la ajabu kwa Danieli ni kwamba aliuvaa ule mzigo au hili jukumu kwa uzito kana kwamba yeye ndiye mkosa, na anatumia nafsi ya kwanza wingi, akisema kuwa tumetenda dhambi, au tumekukosa !
Badala ya nafsi ya pili ama ya tatu ambapo angali sema wamekutenda au walikukosa,ama wamekosa ! Hapa naye anakuwa sehemu ya kosa hilo, maana kiuhalisia lilitendwa na wazazi au wakubwa zao.
Ukiifanya hii toba, usijihesabie haki, wala kujibagua, tubu kwa mzigo, zaidi utajionea katika Danieli 9, ila ona kwa kiduchu hapa !
Danieli 9:5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; :9 Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi;
17 Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana.
18 Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi.
:19 Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.
Ila pia ukija kwa Musa utalikuta katika upana wake, kwanza pale walipoabudu ndama, na pale walipokwama kutokana na habari mbaya za wapelelezi, Musa, aliingia katika toba ya kumaanisha, akiubeba mzigo huo kwa kujitoa ! Shida kubwa leo watu wanapowaombea wengine kuna kosekana hali ya kujitoa, kwa hiyo huomba maombi ya juu, juu tu! Hakuna hali ya kuugua kwa mzigo.

Musa alirudi mlimani siku arubaini, na kuzidi tena, akirejesha uhusiano,alianza na toba ! Leo hii watu kuombea yao ni wepasi, ila ya wengine ni vigumu, yake atajitoa ila ya mwingine ni kama mvua ya manyunyu ! Ndio maana matokeo huwa magumu ! Sasa wewe natumai umeamua na kumaanisha !
Huyu Musa alijenga hoja, na kuomba msamaha kwa kutaja maneno ya Mungu yenye kumbembeleza ili ashawishike na kusamehe, akimtaja kama asiye mwepesi wa hasira yaani mpole wa hasira na pia mwenye huruma, na rehema !
:18 Bwana ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne.
:19 Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. 20 Bwana akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa.

2. Fukuza ama Kemea au Eleza hitajio lako kwa Bwana, ama Amuru,ama Omba unachonuia Kukiomba, hapa ni kushuhulika na kiini cha tatizo, maana maombi ya toba yalikuwezesha kuondoa uhalali wa adui, na kumpa Mungu nafasi ya kufanya utakalo, au wewe kujitengenezea nafasi nzuri ya kiutendaji.
Kwa hiyo ingia kwenye maombi ya kuanza kutekeleza lile lilokufanya uamue kuomba, fanya haya kwa imani !

4. Kama ni Eneo, au Jamii, Alika Ufalme wa Mbinguni, sala ya Bwana iliyopo katika Mathayo 6:9.. , imebeba thana ya mapenzi ya Mungu ya timizwe kama huko juu mbinguni ikiwa na maana ya ufalme wake kuja kwanza !
Kwa hiyo, huu ufalme ukija, unakuja na mapenzi ya Mungu ! Ukiukaribisha katika eneo lako, au kijiji, au familia, nchi ama mtaa inakupa nafasi nzuri ya kuamuru ama kuamua kile unachotaka kitokee ama kukikomesha maana mazingira yanaruhuu utendaji wa serikali ya kifalme kufanya kazi !
Toba ya eno au jamii husika kama kuhani ama mfalme ni muhimu sana, maana Yesu kabla ya kuuachilia, aliimiza akisema tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia, nawe tubu ! Hiyo ni Mathayo 4:17.
Natumai kuna kitu umeondoka naho hapo !

Na kama hujaokoka na unataka kufanya hivyo sasa tafadhli kwa imani kubwa nakuu kabisa fuatisha pamoja nami maneno haya, au sala hii ya toba ili uweze kuokoka, Sema;

BWANA YESU, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NATUBU MBELE ZAKO LEO, NISAMEHE NA NINAKUOMBA UFUTE JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, TAFADHALI LIANDDIKE KWENYE KITABU CHA UZIMA, NINAKUKIRII NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU, HAKIKA WEWE NI MUNGU NA ULIFUFUKA KATIKA WAFU, Amen.

Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, kwa maombi, sadaka kwa njia ya M-Pesa, kupiga simu au Wasats App, ni +25559859287. Tupo Arusha Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni