Jumanne, 31 Desemba 2024

Mama Mchungaji: MUNGU AMEKUPA KIWANGO FULANI CHA BUSARA AU HEKIMA AMA AKILI.

B Mwl Oscar Samba

Ni sehemu ya Kitabu chetu cha NAFASI YA MAMA MCHUNGAJI; KATIKA HUDUMA YA MUMEWE. Kitabu kipo katika hatua ya mwisho. 

10. Mungu Amekupa Kiwango Fulani cha Busara au Hekima ama Akili. Nachelea kusema kuliko mwanaume: maana hili pia utaliona kwa wenza wakiume ambao wake zao ni wachungaji. Na wao (wachungaji wa kike) wanapaswa kujifunza sana kuwaheshimu, kwa kutanguliwa na utambuzi wa nafasi za waume zao katika hili eneo la utumishi wao. Unatakiwa uijue hiyo nafasi ya umakamo kuwa huwa inaambatana na hekima au busara au akili za namna hii; ili uzitumie kutatua migogoro.


 Mama mchungaji epuka sana kuwa mtu wa kukoleza chumvi inapofika swala la tatizo au mzozo fulani. Epuka  pia tabia ya kutaka kuwa upande wa mumeo ili tu kupata kibali kwake, angali unajua yeye ana makosa, au uamuzi wake sio sahihi.


Msuluishaji yeyote yule lazima awe na tabia na maarifa ya kuwa katika mizani ya haki na usawa. Usitafute kupata kibali, tafuta kutatua mgogoro. Mke wa Hamani inaonekana alijua ukweli, alifahamu mumewe hayupo sahihi, lakini hakumuonya. Hadi mambo yalipoelekea mrama au kwenda kombo, ndipo alipomueleza wazi wazi; ya kwamba huyu Modekai uliyeanza kuanguka mbele yake....., hili ni kosa.

Mke wa Hamani laiti kama angejua mapema ya kuwa, anguko la Hamani mumewe, ni anguko lake; basi angalichukuwa taadhari mapema. Hamani alipotundikwa, na mkewe na watoto nao waliuawa, wakapokonywa na nyumba yao. 

Una neema ya ajabu sana, itambue na uitumie vizuri (msisitizo upo katika kuitambua na kuitumia vizuri). Mama mchungaji wangu aliyenilea Arusha, siku moja alichungulia dafutari la mchungaji la matangazo, akaona tangazo la kuivunja kwaya. Alitumia hekima kuinusuru, alimuomba kuwa atazungumza nao. Na kweli alifanikisha jambo lile. Unaonaje kama angekoleza chumvi? 

Ndivyo walivyo wamama wachungaji wengi waliopungukiwa na akili hizi, wakiona moyo wa mchungaji haupo vizuri, kazi yao ni kuwasemea vibaya wengine. Hata kama ni kweli amekuumiza wewe, hakupendi, anakudharau! Lakini fahamu nafasi yako ni kubwa, wewe ni kama sehemu ya kiungo cha jicho la mumeo, funika udhaifu wa washirika wako ili kuwalinda na ghadhabu ya mkuu au mfalme! 


Ni wanaume wachache wenye uwezo wa kustaimili pale mke wake anapoumizwa na mshirika. Kiukweli ni wachache sana, ni wachache pia wenye kuwa makini na aina ya ushauri wanaoupata kutoka kwa wake zao. Ni wachache pia wenye hekima ya kutuliza maumivu ya wake hao! 


Fahamu sana ya kuwa hao pia ni watoto wako, kama ulivyo na watoto wa kimwili, na huwa unachukuliana nao. Basi fanya na vivyo hivyo kwa watoto wa kiroho. Wanakuita mama, sio mama jina tu; bali ni mama majukumu pia. Unao wajibu wa kutumia akili nyingi katika kukabidhiana na madhaifu au mapungufu yao. Usiwe mshitaki wao kwa mumeo, maana hata Yesu kwa Mungu Baba ni muombezi, sio mshitaki. (Fanyika wakili wao kwa mumeo. Japo haina maana utetee maovu, bali hekima ya suluhu lisilo na maumivu iwepo).

Unaonaje, kwa nafasi aliyonayo Yesu akawa anatushitakia? Kuna shitaka Mungu Baba atalikataa kweli? Je, nyuso zetu zingekuwa wapi? Ashukuriwe Mungu ya mwamba Yesu mwenye anasema ya kuwa ameketi mkono wa Kuume wa Mungu Baba, sio akitushitakia au akilalamikia madhaifu yetu, bali ni akituombea! Na wewe fahamu ya kuwa, kuna mkono umeketi pembeni mwa mumeo; na una nafasi muhimu yenye majukumu mawili, aidha kuwashitakia au kuwanenea mema.


Sio kwamba sisi hatumuumizi au kuujerui moyo wa Yesu, la! Hasha. Hufanya hivyo sana tu. Ila Yeye amejijengea fikra za ulezi, uwakili, ubalozi na kadhalika. Waombee mema wanao, wakikukosa waite waonye, usiwaseme ovyo kwa washirika wenzao. Huwa wanajisikia vibaya sana wanapogundua wamesemwa na mama yao, inaumiza na kuvunja moyo. Mama mchungaji unapaswa kuwa dakitari wa maumivu yao, na sio mkoleza jeraha.

Kuna muda unatakiwa sana kujihoji kama foleni ni kubwa ya kuelekea kwa mumeo mwenye kila hitajio au changamoto; kuliko ile ya kuelekea kwako! Kikawaida kutokana na nafasi yako, kuna aina ya matatizo kama ya ushauri yanapaswa kuja kwako sana. 


Wewe ni msaidizi, ukiona wanakukwepa wewe na kuelekea kwa viongozi wa chini yako kanisani kwenye kila jambo, lazima ujiulize na kujikagua. Tabia ya kusema ovyo washirika na ile ya kutokutunza siri ni sababu kubwa sana. Kukosekana kwa upendo, ni chanzo pia.

Kuna kisa kimoja muhimu sana hapa, wakati Yoabu anataka kuuangamiza mji fulani; mwanamke mmoja mwenye busara au akili; alisimama kwenye nafasi yake nakuunusuru huo mji. 


Ona; 2 Samweli 20:15 Na hao wakaja wakamhusuru katika Abeli wa Bethmaaka, wakafanya chuguu mbele ya mji, nayo ikasimama kuielekea ngome; na watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakavunja-vunja ukuta, wapate kuubomoa. 16 Ndipo akalia mwanamke mmoja mwenye akili toka mjini, Sikieni, sikieni; mwambieni na Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye. Kingereza: Then cried a wise/busara woman out of the city, ...

17 Basi akamkaribia; na yule mwanamke akasema, Ndiwe Yoabu? Akajibu, Ndimi. Ndipo akamwambia Sikia maneno ya mjakazi wako. Akajibu, Mimi nasikia. 18 Kisha akanena, akisema, Watu hunena zamani za kale, wakisema, Wasikose kuuliza huko Abeli; ndivyo walivyomaliza shauri. 

19 Mimi ni wa hao wenye amani, walio waaminifu katika Israeli; wewe unatafuta kuuharibu mji, na mama wa Israeli; mbona wataka kuumeza urithi wa BWANA? (asiye na akili au busara hufurahia kanisa linapobomoka au kutawanyika…haugui kwa ajili ya urithi wa Bwana) 

20 Yoabu akajibu, akasema, Isiwe, isiwe kwangu, niumeze wala kuuharibu. 21 Neno hili silo hivyo; lakini mtu mmoja wa milima ya Efraimu, Sheba, mwana wa Bikri, jina lake, ameinua mkono wake juu ya mfalme, naam, Daudi, basi mtoeni yeye tu, nami nitaondoka katika mji huu. Basi yule mwanamke akamwambia Yoabu, Tazama, kichwa chake utatupiwa juu ya ukuta.

22 Ndipo yule mwanamke akawaendea watu wote katika akili zake. Nao wakamkata kichwa Sheba, mwana wa Bikri, wakamtupia Yoabu huko nje. Ndipo akapiga tarumbeta, nao wakatawanyika kutoka mjini kila mtu hemani kwake. Naye Yoabu akarudi mpaka Yerusalemu kwa mfalme. 

Huyu aliunusuru mji! Na wewe tumia aina ya akili uliyopewa kubadili maamuzi yanayoonekana ni tishio kwenye huduma au mtu. Hata kama katenda dhambi, saidia adhabu isiwe ya kumuangamiza muhusika. Huruma za Kristo Yesu dhidi ya muhusika lazima ziwe juu yako. 

(Vaa moyo wa Yesu.)


Najifunza kwa mke wa Nabali, ambaye anaitwa Abigaeli, alipotambua kosa la mumewe, hakuunga mkono hasira za Daudi, bali alitumia akili kukimbia mara na kwenda kunusuru ghadhabu ile. Inafika mahali hadi Daudi anaisifia ile hekima. Kuna wanawake wamejawa na uchochezi asubuhi na jioni, wanachochea hata mada ambazo hawajazielewa vizuri! 


1 Samweli 25:13 Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao. 

14 Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. 

15 Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni; 

16 watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. 

17 Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye. 

18 Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.

23 Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. 

24 Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. 

25 Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. 

28 Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika BWANA atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya BWANA; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote. 

32 Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; 

35 Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako. 


Utakutana tena na tukio kama hili, lenye hekima kama hii kipindi cha maisha magumu ya kivita kwa Daudi, akili ya mwanamke iliwanusuru watoa habari wa Daudi; 2 Samweli 17:17 Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini.


18 Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake.

19 Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lo lote. 

Wengine wangepiga mbiu, kama yule aliyempelekea Sauli mfalme habari za Daudi kufadhiliwa na kulishwa mikate ya kikuhani! Kilichotokea ni makuhani na wasaidizi wao kuuawa na mfalme kwa kumlisha Masihi wake Daudi! Ila huyu alitunza siri. 


Kanisa likiwa na migogoro, bado unahitaji kutenda kwa akili sana, unahitaji kutumia akili nyingi mno. Kuwa mama mchungaji hakumaanishi kusimama upande wa mumeo kunapotokea nyufa kanisani, unatakiwa uwe mziba nyufa. Na sifa ya mziba nyufa ni kutokuwa na upande wa kuegemea. Sasa ukianza kuwasema vibaya mahasimu wa mumeo, rohoni ni unajitoa kwenye nafasi ya kuwa mtengenezaji wa mahali palipo bomoka.


Unafikiri inakuaje Mungu anafikia hatua ya kusema, nikatafuta mtu? Ili apajenge mahali palipobomoka! Alafu baya zaidi haoni mtu. Sio kwamba watumishi hawakwepo, ila kuna aina ya fikra za mziba nyufa hakuziona. Kila mmoja anapochagua upande wake kunapokuwa na sintofahamu baina ya pande kadhaa kanisani au kwenye huduma, ni wanajinyima au kujizuilia kuwa watengenezaji.

Sasa, tazama ushauri wa mama mchungaji wa aina hii! Utaukuta unanuia kuwasema vibaya adui wa mumewe au mahasimu. Hawezi hata siku moja kumueleza mumewe kuwa hili na lile halipo sawa. 


Mwanafunzi wangu mmoja aliwahi kunihadithia jinsi alivyomzuia mama Mchungaji yaani mke wake kuwa sehemu ya vikao vya baraza la wachungaji. Kisa alipingana na wazo lake, alitetea wazo fulani kinzani. Mumewe kamwambia unapaswa kuwa upande wangu, na kuanzia wakati ule akamkataza kabisa.


Nikamwambia ya kuwa amekosea, hatuandai wake zetu kutupigia kura ya ndio. Tunawandaa wawe na fikra mbadala katika maamuzi yetu. Ili siku ukiishiwa uwe na uwezo wa kwenda kukopa wazo kwake, nikamkemea na kumtaka amuombe radhi, na atengeneze mazingira ya kumfanya awe na ujasiri hata wa kumkosoa.


Ni hatari, ukatengeneza watu ambao ni ndiyo mzee. Wenye fikra za ndio ndiyo. Ni heri sasa kuwa mwenyewe maana mawazo yao ni mawazo yako. Hatujiandai kushinda kimawazo inapofika eneo la maamuzi ya baraza, tunajiandaa kupokea wazo moja mbadala linalozalishwa na mawazo ya wengi. Kama sivyo hakuna haja ya baraza. Ukijiona wewe ni mwanzo na mwisho basi vunja baraza, sadaka ajiri watu wa kuhesabu.


Lakini fahamu hata Mungu mwenyewe anahitaji ushauri. Ndio maana anasema njooni tusemezane, anasema pia leteni hoja, na sio hoja tu dhaifu bali ni hoja zenye nguvu! 


Mke, ana nafasi ya kukupa wazo mbadala, kama ilivyokuwa kwa mke wa Pilato, akatoa wazo kwa mumewe. Kazi kwako, kulipokea au kulikataa. Hakuna mshauri anayeajiriwa ili atoe ushauri wa ndiyo, ndiyo tu. Ana nafasi ya kutoa mawazo yake, tena kama ipasavyo.


Kuna kitu nataka kufahamu kama umekinasa kutoka kwa Abigaeli na Nabali. Mke huyu alienda kwa Daudi, ili kunusuru uhai wa mume wake. Lakini kwa mujibu wa maelezo ya Daudi, kama asingenusuriwa, moja kwa moja familia nzima ingeangamizwa. Ikimaanisha hata mke naye.

Sasa, leo tuna wakina mama wachungaji wa ajabu sana, wanamkimbilia Daudi ili kumuongezea mashitaka ya kumuangamiza kabisa Nabali! Wakijua kuna kesi kwa mwangalizi au askofu inayomuhusu mume wake; wao moja kwa moja wanatafuta kuongeza mashitaka au kutoa ushahidi ili mume awe hatiani.


Laiti wangejitambua! Ndiposa wanakuja kushangaa katika pigo la mumewe, hadi ndoa na familia inayumba. Na yeye anakuwa ni sehemu ya maumivu hayo. Sifunzi kutetea maovu yamkini inaweza kuwa ni kweli yametendwa na mwenzako. Ila fahamu Abigaeli, hakutetea bali alikiri kosa, ndiposa anataja upumbavu husika kabisa; na kubwa zaidi aliomba msamaha. Nia yake haikuwa kuchochea, bali kumuombea msamaha. Uwe na akili na fikra za kunusuru jahazi lisizame. Uwe na nia ya kutuliza ghadhabu hasi dhidi yake.


Kitabu Kikitoka Kitafute:

Mawasiliano:

Tutembele ama Wasiliana Nasi 


http://www.ukombozigospel.blogspot.com


Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; 


https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h


Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD


Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk


Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv


Kwa Maombi +255759859287, Email: ukombozigospel@gmail.com


Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: 


https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbW


KwL


Tuandikie pia Maoni Yako; mwalimuoscarvitabu@gmail.com


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni