B Mwl Oscar Samba
Ni sehemu ya Kitabu chetu cha NAFASI YA MAMA MCHUNGAJI; KATIKA HUDUMA YA MUMEWE. Kitabu kipo katika hatua ya mwisho.
10. Mungu Amekupa Kiwango Fulani cha Busara au Hekima ama Akili. Nachelea kusema kuliko mwanaume: maana hili pia utaliona kwa wenza wakiume ambao wake zao ni wachungaji. Na wao (wachungaji wa kike) wanapaswa kujifunza sana kuwaheshimu, kwa kutanguliwa na utambuzi wa nafasi za waume zao katika hili eneo la utumishi wao. Unatakiwa uijue hiyo nafasi ya umakamo kuwa huwa inaambatana na hekima au busara au akili za namna hii; ili uzitumie kutatua migogoro.
Mama mchungaji epuka sana kuwa mtu wa kukoleza chumvi inapofika swala la tatizo au mzozo fulani. Epuka pia tabia ya kutaka kuwa upande wa mumeo ili tu kupata kibali kwake, angali unajua yeye ana makosa, au uamuzi wake sio sahihi.
Msuluishaji yeyote yule lazima awe na tabia na maarifa ya kuwa katika mizani ya haki na usawa. Usitafute kupata kibali, tafuta kutatua mgogoro. Mke wa Hamani inaonekana alijua ukweli, alifahamu mumewe hayupo sahihi, lakini hakumuonya. Hadi mambo yalipoelekea mrama au kwenda kombo, ndipo alipomueleza wazi wazi; ya kwamba huyu Modekai uliyeanza kuanguka mbele yake....., hili ni kosa.
Mke wa Hamani laiti kama angejua mapema ya kuwa, anguko la Hamani mumewe, ni anguko lake; basi angalichukuwa taadhari mapema. Hamani alipotundikwa, na mkewe na watoto nao waliuawa, wakapokonywa na nyumba yao.
Una neema ya ajabu sana, itambue na uitumie vizuri (msisitizo upo katika kuitambua na kuitumia vizuri). Mama mchungaji wangu aliyenilea Arusha, siku moja alichungulia dafutari la mchungaji la matangazo, akaona tangazo la kuivunja kwaya. Alitumia hekima kuinusuru, alimuomba kuwa atazungumza nao. Na kweli alifanikisha jambo lile. Unaonaje kama angekoleza chumvi?