Na Mwalimu Oscar Samba
Ujumbe hu ni Sehemu ya Kitabu chetu cha MUNGU ANAKUPENDA. Kitabu kinachonuia kukusaidia kuliona pendo lake hata kama upo wakati mgumu, ukifahamu kuwa haupitii kwa sababu Mungu amekuacha, hakupendi ama amekukatataa.
Yeremia 31:3-7
Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele,
ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.
Mara
ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili
utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi. Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya
Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake.
Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi
watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni, tukaende Sayuni, kwa Bwana, Mungu
wetu.
Maana Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa
furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana,
uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli.
Msatari wa 8 anazungumza kuhusu kurejeshwa kwao, anaongelea
habari za watu mbalimbali kurejea.
Hiki ni kipengele cha ajabu sana, ya kwamba Mungu
anazungumza na wana wa Israeli ya kuwa amewapenda kwa upendo wa milele, yaani
upendo usiokuwa na mwisho, upendo usio na mipaka, upendo usiofungwa na muda
wala umbali, upendo usiofungamana na misimu mbalimbali waliyokuwa wakiipitia.
Katikati ya utumwa na mateso ya watu waliokuwa wamewachukuwa mateka Mungu analidhiirisha pendo lake, na kuwapa tena ahadi ya kupanda mizabibu ama kurejea kwa uchumi na maisha ya neema kwenye maisha yao, anatanguliza neno kuwa upendo wake ni wa milele!
Sijui unapitia mahali pagumu kiasi gani ila ninachofahamu ni kwamba upendo ama pendo la Mungu juu yako ni la milele, halikuwahi kupunguka au kukuacha kwa sababu ya ugumu ulionao. Inawezekana marafiki wamekuacha, yamkini hata mume ama mke amekaa mbali nawe, ila fahamu kuwa Mungu hajakuacha.
Wakati Yusufu akiwa katika shimo huko nako pendo la Mungu
lilimfuata, alipoingia kwa Potifa na kuishi kama mtumwa huko nako lilikuwa
pamoja naye; Mwanzo 39: Bwana akawa
pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake,
yule Mmisri.
Ndugu zake walimuuza sawa, ila katikati ya machungu ya kuuzwa, na kufanywa mtumwa Bwana Mungu wetu hakumuacha, alikuwa pamoja naye, baba yake alimpenda sana ila hakuweza kuwa pamoja naye, alithania kuwa mwana wake amefariki.
Kama hapo haitoshi alisingiziwa na kutupwa jela, huko nako Bwana alikuwa pamoja naye!
Yamkini ninazungumza na mtu ambaye anasema moyoni mwake
lakini Mwalimu Oscar nimepakaziwa, wewe fahamu kuwa Bwana yu pamoja nawe,
alikuwa pamoja na kijana huyu wa Yakobo, uwe na hakika yu nawe pia, ni kweli
uko jela ya uchumi, uko jela ya ndoa yako, uko jela ya utumishi wako, na
ukitazama karibia kila mtu ni kama vile amekususa ama kukuwekea ukuta, wewe
usife moyo la muhimu fahamu kuwa Bwana yu pamoja nawe maana pendo lake
halifungamani na ubinadamu, halina umbali wala mipaka, linapenya hadi gerezani,
upendo wake u nawe hata katika wakati huo mgumu.
Haijalishi marafiki zako hawapokei simu, wapo mbali nawe
ila wewe fahamu kuwa Bwana yu pamoja nawe.
19-20 Ikawa bwana wake aliposikia maneno ya mkewe aliyomwambia, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka. Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo gerezani.
Inawezekana ni fika na bayana kuwa na wewe mwangalizi wako
amesikia maneno waliyokusingizia, askofu wako bila uchunguzi wa kina
amewasikiliza, ama ni mchungaji wako na umejikuta upo mahali pabaya kazini kutokana
na bosi ama mwajiri wako kuwasikiliza wafanyakazi wengine, na bila udadisi
ukajikuta unahukumiwa! Sauti yako ya kujitetea; ni kama vile umezibwa kinywa,
mimi ni kwambie tu ya kuwa Bwana yu Pamoja nawe!
2-23 Lakini Bwana akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.
Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu
watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye
aliyeyafanya.
Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno
lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa
Bwana alikuwa pamoja naye. Bwana akayafanikisha yote aliyoyafanya.
Usife moyo, wewe mtazame Yesu.
Maana wakati Yusufu anatupwa kwenye shimo, yupo utumwani,
na hatamae jela, ndugu zake waliendelea kusherekea na kufurahi, wakati yeye yu
mbali na wazazi wake, nduguze waliendelea kuishi maisha ya furaha pamoja nao.
Usife moyo, fahamu tu kuwa pendo la Mungu halina msimu,
maana wakati mafanikio yako yakiwa katika msimu wa maandalizi, na wengine
wakisherekea, uwe na hakika kuwa upendo wa Mungu ulipo juu ya wanaocheka ndio
ulipo ju yako wewe unayelia leo, maana unakuandaa kufurahi siku moja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni