Jumapili, 27 Septemba 2020

MUNGU ANAKUPENDA KWA SABABU AMEANDAA MPANGO WA KUKUTOA KWENYE HILO JARIBU AU PITO.

Basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu. 2 Petro 2:9.

Wakati wana wa Israeli wanalia, wanalalamika, wanaumia ama wanaonyesha hisia zao kutokana na ugumu wa mateso yale ya nchi ya utumwa wa Misri, Mungu kwa upande mwingine alikuwa akitekeleza mipango ya kuwaokoa kwenye ile nchi!

Hakuna mtu aliyekuwa akiona, kutambua, au kufahamu kuwa upande wa pili Mungu alikuwa akimpatia Musa maelekezo ya namna ya kuwatoa kwenye ile ncchi!

Na hata kabla ya hapo, Mungu alikuwa akimuandaa Musa kwa ajili ya swala hilo, sio kwamba tu alilifanya hilo wakati Musa akiwa Midiani, bali hata kabla ya Musa kukimbilia huko Mungu alishamuandaa, ndio maana yale mahubiri yake kwenye kitabu kile cha Matendo ya Mitume yanaelelezea vyema kuwa Mungu alimuandaa huyu, ila hakumuelewa mapema, na wana wa Isreali hawakulielewa lile ndio maana walimkataa kwa wakati ule!

 

Nataka hapa ujifunze kuona jinsi Mungu alivyokuwa akiona, na ufanye uhusianisho na maisha yako leo!

Kipindi hiki mateso kwao hayakua kama yalivyokuwa hapo mbeleni, ila Mungu alishaandaa njia na mpango kabla ya hayo yote!

 

Hii inatupa kufahamu nini! Ni kwamba hata kabla ya kupitia hapo, Mungu alishajua, na alishaanda njia au namna ya kutoka hapo!

Na cha ajabu ni hiki, hata kabla ya wao kuingia katika nchi hiyo ya mateso, au utumwa, Mungu alilijua hili, miaka mingi kabla yake, miaka mamia alishalifahamu hilo, na hapa anasema hivi;

 

Bwana akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne.Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. 
 Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado. Ni Mwanzo 15:13-16.

 

Kwa hiyo, kabla ya jaribu au pito hilo kukujia Mungu alilijua, akaliruhusu, na hata kama hajaliruhusu Yeye ni matoke tu ya hali iliyompa adui nafasi, au ni uonevu wake, ila fahamu kuwa mkono wake upo hapo ili kukusaidia maana bado angeweza kulizuia!

Ayubu aliteseka, alipitia mahali pa gumu sana, ila uwe na hakika kuwa Mungu alifahamu hayo, hata kama alionekana yu kimya kwake kwa muda mrefu, lakini la muhimu ni kujua kuwa ilifika wakati au majira akamtokea na kumpatia majibu yake! Na wewe wakati wako upo!

 

Mungu anasema wazi katika kile kitabu cha 2 Petro kuwa anajua namna ya kukutoa katika hayo majaribu, kama kwa Ayubu, na wengineo!

Ni nani angejua kuwa wakina Meshaki, Shedraki na Abernego wangeweza kutolewa katika ile hali kwa njia kama ile! Ni nani angezania kuwa Hamani angetundikwa kwa kuuawa kupitia mti aliouanda mwenyewe akinuia kumtundika Modekai!

 

Sasa mbona unaogopa! Mbona unafadhaika moyoni mwako kana kwamba mkono wa Mungu umeanza kupunguka, au kuishiwa uwezo?

Anasema katika Isaya kuwa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. 
Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. 
Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. 
Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.  Nin Isaya 41:10-13.

 

Usiogope, maana Yeye yupo ili akushike kwa mkono wake wa kuume ule wenye nguvu, yaani akuondowe kwenye hilo jaribu au pito kwa uweza wake, na anatoa ahadi nzuri sana na muhimu mno kuwa wale walioona hasira juu yako, ama adui zako atakutana nao, na utawatafuta wala hutawaona tena!

Ndicho kilichotokea kwa Hamani, aliwachongea Wayahudi, aliandaa mpango wa kuwaua na kuwaangamiza, alimchukia Modekao! Tena kwa hasira na chuki iliyo kuu!

 

Sasa wewe ni kwa nini unashangaa watu wapokuchukia bila sababu, au mkuu wako kazini, au mtumishi fulani, ama mtu fulani na yamkini hata ni jirani anapokuchukia bila sababu mbona moyo wako unaumia na kufadhaika!

Unajiuliza ulichomfanyia kibaya na hukioni! Kamulize Mudekai na Wayahudi kuwa walimfanyia nini Hamani hadi akawachukia! Utatambua kuwa kwa Modekai ni kwa sababu hakumsujudia, sasa na wewe ni kwa sababu hukuamua kupiga goti kwake, Kwa hiyo vita au chuki hiyo sio yako bali kwa ajili ya Mungu wako!

 

Sasa ni sawa Modekai hakumsujudia, sasa na Wayahudi waliingizwaje hapo! Utagundua kuwa ni mpango wa adui, maana aliwachukia Wayahudiu (Shetani) sasa ili kuwaangamiza akawasha chuki hiyo kwa Hamani!

 

Na wewe adui amekuchukia yaani Shetani, na ili kulifanikisha hilo au chuki yake inadhiirika kwa huyo aliyekubali kutumiwa naye!

 

Sasa cha kufanya ni wewe kuamua kushikana na Yesu kama Wayahudi ama wakina Modekai walivyofanya! Na hakika adui zako watakuwa sio kitu mbele zako!

 

Nakujuza haya kwa kina chake maana ni hatari sana kufika mahali na kumuona Mungu amekuacha kwa hiyo na wewe kuamua au kufikiri kumuacha, la! Anakupenda, na anakuwazia yaliyo mema, mpango wake kwako ni wa milele!

Kupitia hapo haina maana ya kuwa amekuacha, angekuacha ungekuwa umeshaangamia, maana adui ulionao wana nguvu na uwezo kuliko wewe, ila neema yake imekushikilia naye anataka kupitia wewe jina lake litukuzwe kama ilivyokuwa kwa Goliathi siku ile, kama ilivyokuwa kwa wakina Meshaki na wenzie, kama ilivyokuwa kwa Danieli, na Mungu wao kupata sifa kuu na watu hao kuinuliwa!

 

Kumbe ni kweli Mungu hajakuacha! Bali anakuwazia mema, ana mipango thabiti ya kukuokoa hapo, maana kama vile moto haukuwaangamiza wakina Meshaki, Shedraki na Abernego na kwako ndivyo ilivyo leo maana hilo jaribu haliwezi kukudhuru hata chembe!

 

Simba walifungwa vinywa, na Danieli kutoka salama katika lile jaribu na kwako ndivyo itakavyokuwa leo! La muhimu ni kujua katika yote hayo pendo lake Mungu halijapunguka kwako, ila anakupenda, ila anakuwazia mema, ni hatari kumuona kama aliyekuacha, hakuwahi kumuacha mtoto wake, maana katikati ya shimo aliingia, mfalme alimuona mtu wanne kwenye shimo, ambaye ni Yesu, maana hutajwa kama mwana wa miungu, na mfano wake huelezwa pale, uwe na hakika malaika aliyefunga vinywa vya simba au mkanywa yao na Danieli kuwa huru au salama, uwe na hakika na kwako yu nawe! Fahamu tu kuwa, anayajua mawazo anayokuwazia hapo, nayo ni ya ushindi, la umuhimu ni wewe kutulia katika mkono wake ulio hodari!

 

Danieli analihakikisha hili, ambalo ni ishara kubwa sana ya uwepo wa upendo wa Mungu kwake! Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. 
Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danielii katika lile tundu. Ndipo Danielii akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake
. Danieli 6:22-23.

 

Tunaona kuwa, “wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake,” ni kwa nini haya yotokee? “kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake,” sijui wewe ndugu yangu! Ila nawiwa kukutia moyo kuhakikisha kuwa unamtumaini Bwana Mungu wako, kaza katika hilo jambo ndugu yangu.

 

Ni nani angejua kuwa mflame yule yule aliyemtupa kwenye hilo tundu la simba ndiye ambaye angekuja kuagiza aokolewe! “,Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu”.

Huyu Mungu wa Danieli, hajahama, wala hajabadilika, maandiko husema kuwa Yeye; Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Peruzi katika Waebrania 13:8.

 

Aliyetenda kwa wakina Danieli, wakina Meshaki, na wengineo, aweza kukuokoa wewe leo na hayo mateso! Maana hata wewe usingeweza kujua kuwa ule moto ungenyamazishwa kiasi cha kushindwa kuwa na dhara lolote kwao!

 

Ila usiniulize ni kwa nini sasa unapitia hayo, au Mungu ameyachilia maana angeweza kuyazuia!

 

Fahamu sana kwua Mungu wetu hafurai kukuona unateseka maana nakupenda, kama anvyosema katika kitabu kile cha Maombolezo kuwa hafurai mateso ya anadamu! Kwa hiyo mapito hayo sio mateso kwako!

 

Ona kwa Danieli baada ya kuvuka hapo, utagundua kuwa kuna heshima aliipata, kuna kibali kipya kilitokea kwake, (kumbe baada ya dhiki kweli ni faraja!)

Ndivyo ilivyo mpendwa! Mungu akitaka kukuinua, ni kanuni yake kukupima kama kweli “unafiti” au unatoshea katika ngazi au viwango vipya vijavyo!

 

Ona hapa; Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu. 
 Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danielii; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. 
 Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danielii na nguvu za simba. 
 Basi Danielii huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi. Danieli 6:25-28.

 

Watu wote ilibidi watangaziwe kuhusu ukuu wa nafasi ambayo huyu mteule alipewa na Mungu, kwa hiyo baada ya hapo tarajia kuinuliwa na kutangazwa au kuenea kwa sifa na jina lako kila kona ya dunia yote!

Lakini sio hayo tu bali pia adu zake waliangamizwa kwa wakati ule wote! Kwa hiyo Mungu aliandaa njia ya kumuondolea usumbufu au upinzani katika ngazi mpaya au viwango vipya, ukianza mwanzoni mwa hiyo sura utawaona wakikaa kikao na kuandaa namna ya kumdhibiti maana kibali kilikuwa kikubwa kwake, sasa ili kuondoa hali hiyo Mungu akawategea mahali, na mahali hapo ndipo hapo, maana kilichokuja kuwapata ni hiki hapa; Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. (24).

 

Kwa hiyo Mungu anataka usiingie msimu wako mpya, au majira yako mapya na maadui ambao watakuzuia kula mema yako! Ndio maana unapitia hapo!

Utaliona hili pia kwa wale vijana mashujaa watatu waliotupwa kwenye tanuru la moto! Adui zao walilambwa na ule moto! Na wewe adui zako watakuwa sio kitu, utawatafuta wala hutawaona tena, maana punde Mungu akupendae mno anakwenda kudhiirika kwako, na kujifunua, nawe utauona mokono wake wa kuume wa haki yake, na uonapo neno haki yake moja kwa moja uwe na hakika

kuwa atakuhukumu kwa haki, wala hataacha haki yako iliyoonekana kudhulumiwa ianguke chini, kama alivorejesha vyote vya Ayubu tena mara dufu na kwako itakuwa hivyo.

 

Lakini jambo jingine muhimu ni hili hapa! Moto wa wakina Meshaki, ulifungua au ulikata kamba zilizokuwa zimewafunga!

 

Sijui na wewe ni kamba zipi zimekufunga? Lakini fahamu huo moto au hilo jaribu Mungu ameliachlia ili likate kamba zilizofunga uchumi wako, ndoa yako, moyo wako na kadhalika!

 

Wengine kuna tabia hatarishi kwao, kwa hilo jaribu linanuia kuzichonga, na kuwafanya wawe wazuri zaidi! Ila moto huo haukuwaunguza, na wewe hilo jaribu halitakuunguza ila litakata kamba! Maji hayatakugharikisha kama Isaya 43 isemavyo lakini yatakufundisha kuogelea!

 

Yamkini hujanisikia vizuri ila ukweli ni kwamba hayo maji hayatakugharikisha ila yatakufundisha kuogelea, na huo moto hautakuunguza ila utakupa joto maana yamkini baridi ni kali kwenye hilo shimo!

 

Moto huo utakupunguzia maadui hata kabla ya wewe kutolewa huko! Kwa vijana hawa maadui walipungzwa au kuondolewa kwa njia kuu mbili, kwanza walipotupwa tu ama waliowatupa walilambwa na huo moto!

Pili baada ya kutoka kwao, wale waliopanga mipango ilikuwa ni zamu yao kwa wao kuingia humo!

 

Ukitaka kuamini kuwa kulambwa kwa wale wa kwanza ni mpango wa Mungu, nenda kachunguze kama waliowatoa walidhuriwa kwa namna yoyote ile, maana hatuambiwi kuwa moto ulizimwa ndo wakatolewa.

 

USIFE MOYO MAANA MUDA WA KUTOKA WAKO UMEKARIBIA ILA MRUHUSU MUNGU AENDELEE KUKATA HIZO KAMBA, maana kama ulikuwa na kiburi kidogo, ukorofi kwa mbali, hasira ilikuwa ikikunyemelea, uwe na hakika baada ya hapa, utajikuta umekuwa mtu mpya, mpole na mnyenyekevu wa moyo! Walidhania wanakuangamiuza kumbe wanakusaidia kukata kamba!

 

Walidhania wanakumalizia kumbe ndo wanakufundisha kuogolea! Na watashangaa kuna siku unakuwa mwepesi wala sio kuogelea tu bali na kuelea unaelea! Huu ni ukuu wa Mungu wetu, kuna kitabu nimekuandikia faida ya majaribu, maana wengi hukosea na kuona majaribu ni mateso, ni taabu fulani, kumbe la! Ni shule, tena ni njia ya kukupunguzia maadui!

 

Mpendwa wangu ninakwambia kuwa, Mungu anakupenda, ninarudia tena kuwa anakupenda tena mno, anasema hivi, mawazo anayokuwazia ni mawazo ya amani, tena mno, ni mpango sahihi wa Yeye kukuinua, tazama wa wakina Meshaki utagundua kuwa badaada ya kupita pale waliinuliwa na kupewa heshima kubwa mnao!

 

Baada ya dhiki ni faraja, ikwa na maana kuwa ni lazima uandaliwe kwa ajili ya mema ya jayo, kwa mchumia juani hulia kivulini.

Usiniulize utatokaje hapo! Hata mimi sijui, ila ninachojua ni kwamba; basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu. Soa katika 2 Petro 2:9.

 

Sijajua kama unalifahamu hili jambo, maana wengine wasipoona upenyo wanadhania na Mungu huona hivyo, wengine akili zao zikifika mwisho na kuona hakuna namna yoyote hudhania na kwa Mungu ndivyo ilivyo, ila hajui kuwa; Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. Utalipata katika 1 Wakorintho 10:13.

 

Usipoona wewe haimaanisihi kuwa na Mungu naye hauoni! Maana mipango yake sio mipango yako, na kadhalika macho yake hayawezi kuwa kama yako! La muhimu ni wewe kuamini tu! Na la kwanza ni kuamini kuwa Anakupenda, na anakuwazia yaliyo mema, Yeye ni Mungu wa haki na muokoaji, atakuoke na kukutoa katika hiyo hali punde!

 

Hongera kwa kusoma ujumbe huu, nakutia moyo kuzidi kumtazama Mungu, na pia uwenda hujaokoka, yaani Yesu sio Bwana na mwokozi wa maisha yako! Nakutia moyo tena kuokoka sasa! Yamkini ni uchumi, fedha, hazipatikani, unazingirwa na nuksi na mikosi, kila unalofanya haliendi, unakabwa na mapepo, ! Wewe njoo kwa Yesu na hayo yote yatapita kabisa ! Sasa natumi u tayari!

 

Sema; MUNGU BABA, NINAKUPENDA, ASANTE KWA KUNIPENDA KWANZA, LEO NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NA NIPO TAYARI KUOKOKA, TAFADHALI INGIA NDANI YANGU, SAMEHE DHAMBI ZANGU, NA FUTA JINA LANGU KATIKA KITABU CHA HUKU, NA ULIANDIKE SASA KATIKA KITABU CHA UZIMA WA MILELE, Ameni.

 

Kwa kufanya hiyo umekwisha kuokoka sasa, na tafadhali tafuta kanisa la watu waliokoka lililopo karibu nawe ukasali, hapo, waambie kuwa umeokoa hivi karibuni, ili wakulee vyema kiroho.

 

Mawasiliano yetu, kwa M-Pesa au Simu: +255 759 859 287, barua pepe: ukombozigospel@gmail.com

pia temnbelea: www.ukombozigospel.blogspot.com . AU www.mwalimuoscarvitabu.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni