Jumatano, 3 Julai 2019

MUNGU ANAPOKAA KIMYA, WEWE FANYA YA FUATAYO, AMA TENDA HIVI:

Na Mwalimu Oscar Samba:

Wasomaji wa Biblia wanafahamu kuwa yapo maombi kadha wa kadha ambayo hayakuwahi kujibiwa, na mengine yalijibiwa lakini yalichukuwa muda mrefu tofauti na mtazamo wa wa husika ila Mungu alikuja kuyajibu.

Ibrahimu na mkewe ni kielelezo kikubwa katika hili, kwa hiyo, ikupe kufahamu kuwa wewe sio wa kwanza, sio hapo tu lakini twafahamu katika sura ya kutokujibiwa yapo hata maombi ya Yesu ambayo hayakujibiwa !
Alihitaji kikombe kimuepuke, na Mungu Baba kugoma kuyajibu ! Hadi alipobadili maombi, Musa na Yeremia nao wana orodha ya maombi ambayo hayakujibiwa !

Walijitetea kadri walivyoweza ili wasitumike lakini Mungu hakuzingatia hoja zao ! Kuna ndugu wa wiwili kipindi cha Yesu ambao ni wanafunzi wake, waliomba kuketi mkono wa kuume katika Ufalme wa Mbinguni ila maombi yao yalisogezwa
kando japo walijitahidi kujibu hoja kwa hoja !
Hii ikupe kujipa moyo kama una hakika maombi yako yamekataliwa ! Maana Mungu aliyekataa Ishmaili kukaa kwa Ibrahimu na kujiatia urithi hapo ndie huyo huyo aliyekuja kusikia kilio chake alipokuwa jangwani !

Na kama ni majibu kuchelewa basi usidhubutu kuona yamekataliwa,bali juwa foleni yako inakaribia, kwa hiyo usitoke kwenye mstari wa foleni bali endelea kungoja !

Nami kwa moyo mkunjufu nakupa dondoo kadhaa kama kichwa cha kipengele hiki kinavyotutaka kutenda pale tumuonapo Mungu yu kimya, huku ukiwa na hakika kuwa haijaaza kwako tu, maana hata Yesu pale msalabani alipitia kipindi hiki aliposema Baba au Mungu wangu mbona umeniacha ! Ila baada ya hapo ndipo alipokirimiwa jina lipitalo majina yote, kumbe mbele yako upo ushindi wala usiwe na shaka ! itabu chetu cha USIFIE JANGWANI, kimelidadavua hili kishujaa ! Karibu:

1. Mulize, Habakuki aliuliza, nawe uliza, kuuliza kwake kulikuja kuzaa majibu, ndipo akapewa njozi,nawe mulize Mungu sababu za ukimya wake; Habakuki 1:2 Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.

3 Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.

2. Fahamu Kanuni ya Mapenzi ya Mungu Makamifu Katika Kuomba, ni kweli tumepewa kanuni ya kuomba lolote kisha nasi tutapewa, lakini usisahau kuwa ipo na ile ya mapenzi yake, na hii ni muhimu sana kuizingatia; 1 Yohana 5:15 Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.


Kanuni hii ilimbana hata Yesu mwenyewe, alipokuwa akijaribu kukwepa mapenzi ya Babaye; Mathayo 26:42 Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe.
Uwe na hakika hata kwako yaweza kukubana !

Jambo lingine muhimu hapo ni kujiuliza ama kutazama kama hilo jambo litampa Mungu utukufu, maana hii nayoni kanuni au ni sababu moja wapo inayomsukuma Yesu kuhakikisha anakazania majibu yako yatukie;
Yohana 14:13 Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.

Jambo lingine tazama nia yako, kama ipo tamaa, au masilahi binafsi ama hila, uwe na hakika ni sababu moja wapo ya Mungu kuchelewa,au kugoma kukujibu; Yakobo 4:3 Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.

( Usisahau kuwa tuna kitabu cha NAMNA YA KUOMBA, chenye mbinu mbadala na kadhalika, pia kipo kitakachokuwezesha kufanya maombi ya vita ili kufanikiwa kufikia viwango fulani vya kimaisha na utumishi, kinaitwa, TEKA, MILIKI NA UTAWALE Ni muhimu kuvipata ili vikuwezeshe kufanikiwa katika uombaji.) Tuendelee !

Kuna swala linatajwa kama Kukaa Ndani ya Yesu, kisha na maneno yake yakae ndani yako, hapa ni Yeye ndani yako, na wewe ndani yake, alafu huambiwa,utapewa; Yohana 15:7 Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.

Kanuni hii imegawanyika katika nyanja au pande kuu mbili, mosi ni ile ya wewe kuokoka, na kuwa na imani katika kile au lile uliombalo, pili ni wewe kuhakikisha unachokiomba ni mapenzi makamilifu ya Mungu. ( Fahamu kuwa kuna muda unaweza kuomba maombi ya kulazimisha yaani ya nje ya mapenzi ya Mungu na Mungu kukupa, ambayo mimi nayaogopa sana, na kuna muda unaweza kuomba asikupe, na kutokupewa ni ishara ya kupendwa zaidi na Mungu, au Mungu kuupenda utumishi husika zaidi, ama neema yake kuwa juu yako zaidi, ni kweli "mtoto akililia wembe mpe umkate," ila kama unampenda zaidi, utajizuia kumpa, labla naye anganganie zaidi ! Hadi kuona kuliko kero za kungangania bora maumivu ya kujikata kwake ! )

Kuna kanuni nyingine inatajwa hapa kama Kuzaa Matunda; Yohana 15:16 Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.

Lakini sio kuzaa matunda, bali matunda yako pia yadumu, sio kuhubiria watu waokoke tu, bali wadumu pia, sio kuhubiri tu, bali na mafundisho husika yadumu maishani mwa wahusika, sasa kuna mambo mengine ili ujibiwe ni lazima uhakikishe unamtumikia Mungu, kanuni hii ndio iliyomnufaisha Zakaria, ni hatari ukaacha utumishi au ukalega kutumika, ukaacha kuimba, ukaacha kupiga ala za nyimbo kanisani na kwenye huduma, ukasusa ushemasi, ukaanza kutega maombi, kisa Mungu amekaa kimya, ama kwa sababu yoyote ile, uwe na hakika unajizibia mlango wa majibu au unajisogeza mbali na mtoa majibu !

3. Juwa Mungu Hujibu kwa Wakati Wake, hii ni kanuni muhimu sana japo ni ngumu karibia kuliko zote, maana kuna mambo mengine hupewi kwa sababu tu umeomba sana, ( japo maombi makubwa na yaliyo ya kina ni akiba na hukuwekea mazingira mazuri ya kujibiwa katika wakati husika, na huweza kukufupishia wakati pia,) ila ni muhimu kufahamu hujibiwa kwa wakati wa Bwana.

Anamwambia Habakuki kuwa njozi hiyo kuna wakati wake iliyopangiwa;  Habakuki 2:3 Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.

Swala la Yusufu kutoka gerezani lilikuwa la wakati, mbele yake kulikuwa na jukumu ambalo lilipaswa kutekelezwa kiwakati, majira ya kuingia Yoridani kwa wana wa Israeli yalikuwa ni ya kiwakati !

Ni kweli kunyenyekea ni kanuni ya kuinuliwa,ila kukwezwa huko bado kunategemea wakati wake ulioamriwa ! Kitu unyenyekevu unaotajwa katika andiko lijalo unafanya ni kuhakikisha kuwa wakati wa kuinuliwa ukifika, uweze kuinuliwa bila kikwazo, lakini usije ukafaulu mtihani wa unyenyekevu leo, na kulazimisha kuinuliwa kesho, ama na kuumia mbona bado hujainuliwa !

Bali fahamu, unapaswa kudumu katika unyenyekevu huo,ambao ndio njia ya neema ya kukuinua hupitia; 1 Petro 5:5 Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.

6 Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; ( Shika hilo neno kwa wakati wake,na sio wako !)

Kumbuka: 1 Yohana 5:14 Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. ( Sio yako ! Bali ni yake !)

4. Hakikisha Akili zako Zinakuwa, Kuna mambo Mungu hawezi kukupa kama huna uwezo wa kuyaimili, sasa unaomba upate kazi,wakati Mungu anajua huna nidhamu ya kazi, ni mvivu kuamka, ni mzito kujituma, hutaki kutumwa wala kugombezwa, au kukaripiwa, Mungu hawezi kukujibu,bali utashangaa unapitishwa katika mapito magumu, ukilalamika, utaoteshwa usiku upodarasani,ikiwa ni ishara ya kufundishwa nidhamu ya kazi.

Unaomba kipato kikuwe,au upate ajira nzuri, wakati huna nidhamu katika matumizi ya fedha ! Mungu anajua fika, ukipata fedha,wewe ni mavazi,ni kula ovyo, siku hiyo mshahara ukiingia tu hata nyumbani unachelewa kurudi, pato likiongezeka, ndo kwanza unabadilisha mlo, na badala ya kula nyumbani siku hiyo ni hotelini !

Sasa Mungu anajiuliza akiongeza pato ukiwa na akili hiyo, si-ndo kwanza utahamia hotelini kabisa ! Si-ndio chanzo cha magonjwa ya moyo na kisukari kutokana na hulaji ovyo !
Maana Mithali husema kufanikiwa kwa mpumbvu ni kwa hasara ya nafsi yake, sasa Mungu hataki akupoteze !

Akili nyingine ni ndogo kiasi kwamba mtu akiajiriwa tu, hata kanisani haendi tena, huduma hafanyi tena, akiulizwa jamani, kazi, kazi ! Sasa huyu Mungu kama anamtaka amtumikie, hataacha kuipiga hiyo kazi, au kuhakikisha haipati kabisa,maana kwa Mungu ni bora ufe maskini ila kazi yake iende ! Sasa kwa usalama wako ni wewe kujijengea nidhamu kiasi kwamba, vyote viwili viende maana sio furaha yake wewe uwe maskini maana husema katika Mithali kuwa huwarithisha mali wale wa mpendao !

Na hii ni kanuni ya kibiblia kabisa, kwamba kuna mambo huwezi pewa hadi akili au ufahamu wako kuhusu kuweza kuvimiliki au kuvitawala umeongezeka, ndiposa hufananishwa na mtoto, Mungu akimaanisha kuwa na akili za kitoto kiuchumi, kihuduma au kiroho na hata kindoa, maana wapo waombao waolewe au waowe lakini kwa kweli hata kuishi na kaka au dada, mama au rafiki hawezi, ni mjeuri wala hataki kuonywa, hataki kujituma maana ni mvivu kuliko maelezo, ni mtegevu hujawahi kuona, sasa nani atakae kubali kuja kulaumiwa na mwenzake kwa kupewa mwenzi mzigo !

Akilazimisha sana apewe wakufanani naye, yaani mzigo kwa mzigo,sasa Mungu kwa kuwa anampenda huyu mtu, ndiposa huanza kumpitisha, ili kuchonga tabia zake,humuinulia mafundisho ya kijamii na kimalezi, pamoja na yale ya kindoa, ili walau akili zake zikuwe, hekima ianze kuingia ndani yake, nje ya hapo, majibu yake huwa au husalia chini ya uangalizi maalumu !

Wagalatia 4:1 Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; 2 bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.

Kwa hiyo ukiona unaomba upate fedha au kazina hujibiwi,badili maombi, muombe Mungu akusaidie akili yako ikuwe kiuchumi, akupe hekima na nidhamu ya kazi, Kiasi kwamba kazi isiadhiri uhusiano wako na Mungu, na ndugu au ndoa,maana wapo ambao toka uchumi umekaa vizuri, ndoa zimevurugika !

Ukiona kuna uzito wa kukua kihuduma, ombea akili zako zikuwe kihuduma, maana yamkini Mungu anajua akikuongezea wakristo basi baada ya muda kidogo utaota mbawa maana sasa unanyenyekea kwa sababu huna fedha, huna gari,sasa huduma ikikuwa na kuwezesha hayo, kiburi kitakuwa,na kiburi ni matokeo ya kukosa akili au hekima,maana humea kwa mpumbavu na mjinga !

Wajanja wa kiroho huomba kwa uchache sana wapewe fedha,ila huomba kwa kina wapewe maarifa ya uchumi, na ukijizoeza kuomba hivyo, uwe na uhakika utaanza kufundishwa na Roho Mtakatifu kuhusu uchumi wa kibiblia, ambapo hata ukiwa tajiri bado kiroho chako kitasalia salama ! ( Hii ni siri kubwa sana, zaidi kuhusu uchumi na akili, au maarifa,tunavyo vitabu, pia kuhusu ndoa na nidhamu za kihuduma, pia vipo, na kipo kile cha Utumishi na Uchumi !)

Mpendwa , kama hujaokoka na unataka kufanya hivyo sasa tafadhli kwa imani kubwa nakuu kabisa fuatisha pamoja nami maneno haya, au sala hii ya toba ili uweze kuokoka, Sema;

BWANA YESU, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NATUBU MBELE ZAKO LEO, NISAMEHE NA NINAKUOMBA UFUTE JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, TAFADHALI LIANDDIKE KWENYE KITABU CHA UZIMA, NINAKUKIRII NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU, HAKIKA WEWE NI MUNGU NA ULIFUFUKA KATIKA WAFU, Amen.

Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, kwa maombi, sadaka kwa njia ya M-Pesa, kupiga simu au Wasats App, ni +25559859287. Tupo Arusha Tanzania.

Kwa undani wa Mafundisho au Habari zetu tembelea; www.ukombozigospel.blogspot.com .
#MwalimuOscarSamba #UgMinistry #UkomboziGospel #MwalimuOscarVitabu #Neno #Biblia #Zaburi #Pic #Picha #Tanzania #Afrika

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni