Na Mwl Oscar Samba
#FaidayaJaribu: #Usiogope
Ni Sehemu ya Kitabu Chetu Tarajiwa cha MAANA YA UZIMA, NA UZIMA WA MILELE. Pwenti ya Pumziko Kuu.
Kwenye Kipengele cha Taswira ya Uzima wa Milele
Pumziko Kuu; Yaani Sabato Kukuu. Watu wengi hawajui ya kuwa Sabato maana yake ni pumziko katika kilele cha uzima wa milele yaani wakati huu hapa ulimwenguni kwa kuokoka, (kupumzika katika Kristo Yesu kama mtua mizigo ya dhambi na kila mateso.) Na pili kama sehemu ya kupumzika kutoka katika dunia iliyopo chini ya umiliki wa Shetani kama mungu wa dunia hii, na pamoja na dunia yenye pigo la laana la kosa la Adamu na Hawa.
Unapookoka ni umeingia katika Sabato. Kwa hiyo, msabato halisi ni mtu aliyeokoka. Kama hujaokoka wewe sio Msabato, maana bado upo chini ya utumwa wa Shetani. Wokovu unakupa pumziko. Kanuni na sheria zile za Agano la Kale hususani sabato na taratibu zake zote, zilinuia kutufikisha hapa kwenye wokovu na hatimaye katika Sabato kamilifu ile ya Mbingu Mpya na Nchi Mpya.
Ndiposa Yesu alipokuja, mkazo wa sheria za kisabato ule wa Agano la Kale haukwepo tena. Maana amekuja Sabato Mwenyewe. Ndio maana alijibu hivi; Marko 2:27 Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. 28 Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia. ( Kwa hiyo kama utaendelea kusingizia kumsikiliza mjumbe wa Sabato Musa na kumuacha Bwana wa Sabato; basi utakuwa umekwama sana.
Mathayo 12:5 Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? 6 Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.
7 Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. 8 Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
Tuone kisa kingine:
Luka 6:2 Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? 3 Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? 4 Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao. 5 Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
Haikuishia hapo, bali mbele yake anaendelea kutupatia somo jingine. Na alifanya hivi kwa makusudi kwa nia ya kutaka kuwafundisha jambo muhimu hapo. Nje ya somo la ya kwamba Yeye ndiye Bwana wa Sabato; yaani ile ya sasa na ile ijayo: alinuia pia kumpatia sabato huyu mgonjwa! Na hii au na hizi zote ni miongoni mwa sababu kuu za Yesu kutenda miujiza mingi siku ya sabato. Yaani alinuia kujifunua kwa watu wote ya kwamba Yeye kwa jina lingine anaitwa Sabato.
Lakini pia alikusudia moja kwa moja kumpatia pumziko mgonjwa au mtu mwenye mateso. Sasa wale ambao hawakuokoka, hawakumuamini walibakia katika sheria. Wakaacha kumuona Bwana wa Sabato. Tujionee hapo mbele yake;
Luka 6:6 Ikawa siku ya sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. 7 Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia.
8 Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. 9 Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?
10 Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. 11 Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.
Ndio maana Paulo analieleza hili kwa upana sana tu. Akifafanua fika ya kwamba ilimbidi azaliwe katika sheria yaani zile za Musa, ili kutukomboa sisi ambao tupo chini ya hizo Sheria. Wanaompinga, maana yake wao bado ni watu wa sheria, ndio maana kwao Musa ni mkubwa kuliko Yesu. Hawajuia ya kuwa Musa alishawandikia akitaka wamuheshimu au kumtii Yesu; Matendo ya Mitume 7:37 Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye.
Ona Maneno ya Musa Mwenyewe; Kumbukumbu la Torati 18:15 Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye. 18 Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.
Kwa hiyo, huwezi kujiita wa Musa alafu ukamkana Yesu. Utakuwa ulishamkana na Yesu mwenyewe pia. Musa alikuwa ni mjumbe tu, na alibeba ujumbe wa Yesu, ambaye ndiye Bwana wa hiyo Sabato. Ukiona unashika sana alichoandika Musa, na unakibeza kile alichokisisitiza Yesu ama katika sura ya Agano Jipya, uwe na hakika kuna mahali umekwama. Adui Shetani amekupiga chenga. Na wewe siye wa kwanza, waone hawa; Yohana 9:28 Basi wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake yule; sisi tu wanafunzi wa Musa.
29 Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako. 30 Yule mtu akajibu, akawaambia, Hii ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho!
Lazima unue ya kuwa Musa ametoka kwa Yesu, na Musa alitumwa na Yesu. Sasa unamkataje Rais wa nchi na unamuheshimu mkuu wa wilaya aliyemteule wa Rais! Ukiishika Sabato nje ya alivyoelekeza Yesu alipojifunua katika Agano Jipya ni umepigwa chenga ya mwili na adui Shetani. Upo katika njia ya kumtumikia Shetani na kumsulubisha Yesu mara ya pili kama hao Mafarisayo walivyofanya wakimuona Yesu ni kama mvunja sheria za Musa!
Na ndivyo wasiyoyajua haya wanavyotuona tuliokoka kama ni wavunja sheria za Agano la Kale na maelekezo yake. Hawajui Waebrania 10 inasema ya kuwa Torati ni kivuli cha mema yajayo yaani Kristo. Sasa mwenye kivuli kilichotangua amekuja. Watu wengine wanatembea na picha au kivuli chake, na kumkataa mtu halisi! Hii nayo ni ajabu na mshangao! Waebrania 10:1 Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.
Ndio maana hata sasa, hatutoi dhabihu kama ilivyokuwa Agano la Kale. Maana dhabihu kuu imeshatolewa. Na Waebrania inafafanua vizuri kabisa. Uwe na hakika kama dhabihu zilivopata mbadala kwa Yesu kufa mara moja tu kama sadaka, na ndivyo sheria za kitorati zinavyopaswa kuchukuliwa. Nazo zilikuwa ni kivuli cha ujio wa Kristo, ikiwakilisha pumziko la sasa la dhambi na Sabato kuu ya Mbingu Mpya na Nchi Mpya. Tazama hapa kuhusu matoleo ya Agano la Kale na sasa ilivyobadilika; Waebrania 10:1 Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.
3 Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. 11 Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi.
12 Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; 14 Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. 15 Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema,
16 Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo.
Kwa hiyo, ukikataa mfumo huu mpya wa Sabato Kuu, ambao ndio wokovu, ni umeukataa na ushuhuda wa Roho Mtakatifu! Ndio maana watu hawa hata ujazo wa Roho Mtakatifu kwao ni jambo geni. Hapo tunaambia hili ni Agano Jipya ambalo Bwana amefanya nasi kumpitia Kristo. Ukiendelea kushikama na mfumo ule wa Agano la Kale kwa sura ambayo siyo sahihi, ni umekataa kuwa sehemu ya Agano Jipya yaani wokovu. Na wewe sio msabato Kiblia labla u msabato kidini. Ila waliookoka ndoo wenye pumziko la sasa na wakati ule ujao.
Ndio maana bado mizigo uliyoshikilia ni mingi, ikiwemo masharti ya vyakula na vinywaji. Vitu ambavyo hata Musa mwenyewe hakuwahi kuvikataza; sio Agano Jipya wala ka Kale. Mashariti ni mengi hata mengine kuyatimiza huwezi. Hii ni ishara ya kuwa bado huna pumzigo, bado upo chini ya kongwa la Sheria.
Paulo alilifafanua hili vyema sana tu! Wagalatia 4:4 Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, 5 kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. 6 Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. 7 Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.
Wengine wamekataa kuwa wana na wameendelea kubeba utumwa. Sisi wenzio tuna kula vyote maana Yesu ama Bwana wa Sabato alishaturuhusu; Marko 7:18 Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi;
19 kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. 20 Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.
21 Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, 22 wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. 23 Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
Hakuna haja ya kushinda hapa, bali kuna haja ya kulielewa hili andiko, hili lajitosheleza kila pahala; Yohana 1:17 Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. (Kitabu chetu cha YESU KAMA NEEMA NA KWELI kitakusaidia sana tena mno.)
SABATO KAMA WOKOVU: Unapotubu na kumuamini Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, moja kwa moja kinachotokea ni wewe kutuliwa mzigo wa dhambi. Agano Jipya pia kitu moja wapo kililofanya ni kututoa kwenye kongwa la sheria za Agano la Kale. Jipya limekuja kuliimarisha lile la kwanza. Na ndivyo Waebrania anavyosisitiza.
Yesu kwa kulijua hili aliachilia mwigo mkuu, nao ni wakuamua kumuendea Yeye ili kutufanya kuwa huru. Huu ni uhuru dhidi ya dhambi, na mzigo mkubwa wa kisheria ama sheria za Torati kwa lugha nyingine; Mathayo 11:28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; 30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Haya mambo hayawezekani nje ya kukaa ndani ya YESU. Yohana 8:31 Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; 32 tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.
33 Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? 34 Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. 36 Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.
Maana Yeye Yesu ndiye Bwana wa hii Sabato. Musa alituletea sheria ila kwa mkono wa Yesu tunayo neema na kweli. Neema kwa lugha nyingine ni sheria iliyokuja kwa mfumo wa Agano Jipya. Ni Sheria ya Musa kwa sura ya Agano Jipya. Na kweli maana yake ni kwamba ni udhiirisho au ufunuo wa Mungu katika sura dhairi tofauti na Agano la Kale. Hapo awali alijifunua kama kivuli, lakini sasa ni dhairi. Tulipewa patakatifu pa patakatifu penye mfano wa mbinguni kama Waebrania anavyotufunza, lakini sasa tunapo palipo halisi, ambapo hapajafanywa na mwandamu kama pale awali. Yesu kujaa kweli maana yake ama kumbuka ni kumfunua Mungu; Yohana 1:17 Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. 18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
Huwezi kumuona Baba bila Mwana, ukijiita ni wa Musa, na ukifahamu wazi kuwa Musa alitumwa na Mungu, kisha ukimkataa Yesu basi una bahati mbaya. Bora na heri ungezaliwa Agano la Kale, lakini kwa sasa Mwana ameshawekwa dhairi, ni fika huwezi kuhesabiwa haki kwa sheria, bali ni kwa neema maana hizo sheria sasa zii katika mfumo wa neema maana ndio ukamilifu wake. Na ukitaka kumuona Mungu kwa sasa, usimtafute kwenye sheria, mtafute kwenye Neema na Kweli vilivyoletwa na mkono wa Yesu. Maana Baba yu katika Mwana; Yohana 8:19 Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui; kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu.
23 Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. 24 Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.
25 Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia. 26 Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake, ndiyo ninenayo katika ulimwengu.
27 Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba. 28 Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo.
29 Naye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo. 42 Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.
Ukimuona Yeye ni umemuona Baba: Yohana 14:8 Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. 9 Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? 10 Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake.
Kwa lugha nyingine ni kwamba ukimkataa Yesu ni umemkataa Musa na Agano lote la Kale. Maana Musa alitumwa na Mungu, ambaye yu ndani ya Kristo, naye ni Mungu (Yohana 1:1 na kuendelea.)
NB: Wengi mnayachunguza maandiko na hamjui ya kuwa ndani yake ndimo alimo Yesu. Maana Yeye ni neno, ameandikiwa Yeye. Kosa hili walilifanya hawa ambapo na leo wengi wanalifanya; Yohana 5:39 Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.
Kama utasoma Agano Jipya na la Kale na humuoni Yesu kama Bwana wa Sabato; basi kuna shida kubwa sana! Unahitaji msaada, na msaada mmoja wapo ni kuzisalimisha fikra zako kwa Yesu. Ili uwe na moyo wa kujifunza. Kwenye kitabu chetu kile cha FIKRA SAHIHI KATIKA SHAMBA LA BWANA, kuna kipengele cha mtu mwenye moyo kama wa mtoto mchanga. Kisome kitakusaidia ili Mungu aweze kujifunua kwako.
Kamwe usikubali kuishi ulimwenguni kwa kufuatisha mkumbo wa kuamini kama wengine. Hata kama umezaliwa au kuolewa kwenye hiyo dini, bado unatakiwa kuhakikisha ya kwamba Biblia unaielewa kiubinafsi, ili uweze kumjua Mungu kipekee. Hutakufa na mtu, wala hutabeba hukumu yako na mtu mwingine. Kila mtu atasimama mbele za kiti cha hukumu mwenyewe.
Kuna dini ambazo zinasoma Biblia kwa sura za mtafisiri wao mkuu kama mwanzilishi wa dhehebu au imani yao! Wanataka kujua Helen White alitafsirije hilo andiko kisha ndiyo iwe tafsiri yao! Hilo ni kosa na usikubali kudanganyika.
Biblia inajiongoza yenyewe, kila tafsiiri lazima ibebwe na maandiko. Sio mtu anajitungia mambo yake huko na kutudanganya ya kuwa amefunuliwa. Hatupaswi kujenga misingi ya imani yetu kwa kutazama mtu fulani alifunuliwaje, bali ni kwa kutazama Biblia kwa ujumla inasemaje au inaaminije katika hilo.
Ndugu zangu zama hizi ni za uovu, manabii wengi na waalimu wengi wa uongo wameibuka. Na mtaji wao mkubwa ni uvivu wetu wa kumtafuta Mungu, uzito wa kuikubali hiyo kweli ya Mungu pamoja na kutaka wepesi wa kiimani. Hatutaki kuishi katika kanuni za Mungu zenye kupinga na kukemea dhambi, badala yake tunahitaji wepesi fulani kwa kupewa uhuru ya kwamba hata mtu akizini hawezi fukuzwa kanisani, hawezi kutengwa na ushirika kisa amekutwa kwa mganga wa kienyeji ama kwa sababu ya ulevi. Ni muuza baa lakini bado ni kiongozi kanisani. Ni mwenye nyumba ndogo lakini ni mzee wa kanisa. Na huu ndio mtaji mkubwa wa Shetani.
Ninalofahamu ni kwamba Yesu ni Neno kama ilivyo hiyo Yohana moja, moja na kuendelea, na alijifunua kwetu kwa kupitia Biblia Takatifu. Ni Biblia yenye vitabu 66, sio ile iliyozidishiwa vitabu, kitabu cha Danieli kina sura 12 na sio 14 kama kile cha dini fulani ilivyojiongezea.
Ndugu yangu ukitaka kumuona Mungu huna budi kuiishi Biblia, sio kuziishi ngonjera na hadithi za uongo za wakina Heleni White. Wapo na mitume na manabii waliokuja na mafundisho yao ya uongo. Mafuta na maji vimegeuka na kuwa ndio msingi mkubwa wa huduma za kitapeli siku hizi. Na kizazi cha leo chenye kupenda miujiza kuliko kumpenda Yesu ndiko kilikopotelea.
Ataenda aombewe lakini ni muuza baa, ni kahaba, ni mwizi, anafanya biashara za kishirikina. Lakini naye yupo kanisani. Huu ni msiba. Na hili ni tatizo na kikwazo kikubwa katika kumfikilia Yesu.
Ndugu yangu, mtu asikuyumbishe na mashariti ambayo ukurasa mpya wa Agano Jipya ulishafunguka, maana hayo yalikuwa ni kivuli cha yajayo. Kama zamani ilivyokuwa mwanamke aliyetoka kujifungua hakuruhusiwa kukaa na watu na hata mumewe hadi siku kadhaa na hata miezi ipite, na hata yule aliye katika tarehe zake za mwezi; na sasa wote Agano Jipya limetuondea huo unajisi kupitia msalaba wa Yesu Kristo! Uwe na hakika ndivyo ilivyo na katika vyakula na vinywaji. Haramu ni pombe tu maana huleta machafuko ya akili, matusi na ubaribifu moyoni. Ila chai ya majani ya chai, soda na vinginevyo ni ruksa. Na kila nyama pia; Wakolosai 2:15 akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.
16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; 17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. 18 Mtu asiwanyang'anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;
Kuna wengine wamenasa kwenye fikra kama hizi za Petro leo, lazima ujue hayo yalikuwa ni kivuli. Nguruwe na unajisi wa wanyama wengine waliwakilisha watu wa mataifa, leo mimi na wewe msalaba umetupandikiza katika mzabibu maana tulikuwa mzabibu mwitu ama zeituni. Tulikuwa najisi lakini damu ya msalaba imetusafisha. Imatufanya kuwa safi. Hili lazima ulielewe; Matendo ya Mitume 11:6 Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani.
7 Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. 8 Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu 9 Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. 10 Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.
Nikutie moyo kumuona Yesu kama alivyofunuliwa katika Biblia. Na ndivyo tunavyofunzwa; Waebrania 10:7 Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.
Maana yake amefunuliwa katika Neno, Biblia. Na neno viwe ndio msingi wako mkuu. Sio hadithi za mapokeo ya watu. Siku hizi hadi nguo nyeupe imekuwa ni ishara ya utakatifu, kwa hiyo kanisani wanavaa hivyo. Huu ni utapeli na upofu na upotoshaji wa kiroho wa dhairi kabisa. Dini yoyote inayokupa mashariti kama hayo, na yale ya kula na kutokula vyakula fulani, kutokunywa vinywaji fulani, itazame kwa sura ya upotoshaji.
Nakuonya kutokuwa na tabia kama za baadhi ya Wayahudi wa Thesalonike, bali uwe kama wale wa Beroya. Hawa waliya chunguza maandiko ili kutafuta ukweli, na walipodhibitisha basi walimuamini Mungu kupitia wakina Paulo.
Lakini wale wengine waliona wivu tu kwa sababu watu wengi wamewaamini, roho ya kutetea dini ikawaingia. Na ndivyo walivyo watu wengi leo, hususani viongozi wa kidini, wanaanzisha upinzani sio kwa sababu wanamtetea Yesu, bali ni kwa sababu mioyo ya watu inawaelekea wengine. Na hii ni hatari sana! Bali wewe chunguza, na kuchunguza haya nikufunzayo, ilijone kama ni mweli kama watu wa Beroya.
Matendo ya Mitume 17:1 Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2 Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu, 3 akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo.
4 Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache. 5 Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji;
11 Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. 12 Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache.13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawachafua na kuwafadhaisha makutano.
SABATO KAMA UZIMA WA MILELE:
Musa alikuwa na jukumu la kuwapa raha, jukumu ambalo alilikabidbi kwa Yoshua. Kanani ilikuwa ni kivuli cha Mbinguni Mpya na Nchi Mpya. Ikiwa ni baada ya kutoka katika utumwa wa Misri na mahangaiko ya jangwani, maana ndivyo ilivyo katika maisha yale yajayo.
Katika Waebrania tunajuzwa fika ya kuwa ipo Sabato nyingine iliyosalia. Ambayo ndio Mbingu Mpya na Nchi Mpya. Nami nikutie moyo tena na tena kutokuikosa kwa kuamua kuokoka, yaani kutu dhambi; Waebrania 4:7 aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo,kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu. 8 Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.
9 Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. 10 Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.
11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi. 14 Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. 16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Hapa tutapata raha, yaani pumziko la milele. Huu ndio ukamilifu wa Yesu kama Bwana wa Sabato.
Siku nikijaliwa kuja kukuandikia makala maalumu kuhusu Sabato, nitakupitisha kwenye kila andiko moja moja husani kwenye Agano la Kale kadri nitakavyojaliwa, ili kukupatia upana zaidi wa mada hii mubimu. Ila kwa mtaji huu, amua kuielewa Biblia katika uhalisia wake na sio kama wanavyoitafsiri wengine. Fahamu sana ya kwamba Yesu ndiye Bwana wa Sabato, sio Musa wala Heleni White.
Kitabu kikitoka Kitafute..hiki kitakuwa ni cha Bure kwa njia ya PDF au Soft Copy
http://www.ukombozigospel.blogspot.com
Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD
Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk
Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv
Kwa Maombi +255759859287
Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL
Nikutakie Siku Njema
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni