Namna
ya Kuishi Salama Maisha ya Uchumba hadi Ndoa.
Kusudio la
mada hii ni kukuwezesha kuishi vyema kiroho na kimwili, au kiushuhuda katika maisha
ya uchumba.
Swala la
ushuhuda ni muhimu sana katika hatua hii maana litawajengea heshima, kwa jamii,
jamaa wako wa karibu kiundugu na kanisa kiujumla, kwa hiyo ipo haja ya kuwa salama
kiroho na kimtazamo au machoni pa watu pia.
Maana ni
vizuri kuhesabiwa haki na Mungu lakini pia wanadamu wakuheshimu. Maana hali hii
itakupa haki kwao, lakini pia itaifanya huduma yako kukubalika, maana katika
ulimwengu huu tunamuhitaji Mungu kweli ili tufanikiwe, lakini pia tunawahitaji
wanadamu, na wanadamu hutazama kwa macho ya kimwili ili kuona, sio ya moyoni na
nje kama Mungu.
Maana yangu
hapa ni kukutaka kuepukana na mitazamo finyu ya vijana kadha kuwa anaishi kama
vile atakavyo yeye madamu hatendi dhambi kwake sio mbaya.
Na kujaribu
kutengeneza mazingira ya ushuhuda kwake ni unafiki, huku ni kukosa maarifa.
Hali ya
kupita kila kona, au kukaa ovyo na mwenzako ama kukutana katika mazingira
hatarishi kwa mujibu wa mboni za wanadamu, kwa madai kuwa nyie mpo vema kiroho
hata kama hamtendi kosa la kukutana kimwili, lakini pia kufanya hivyo ni
dhambi.
Inaweza
isiwe na madhara au matokeo kama vile ya kujamiiana, ila hali ya kuharibu ushuhuda
kwa makusudi ni kosa kiroho.
Paulo Mtume
anasema sisi ni barua, licha ya hivyo, anatuambia kama akila nyama itamkwaza
jirani yake, yupo tayari kutokuila, unaweza kujione uchaji wa mtumishi huyu
ulivyokuwa mkubwa.
Kwa hiyo
nawe unawajibika kujiwekea mazingira salama ili jina la Bwana lisitukanwe, hali
ya kusema kuwa Mungu anatizama moyo, au ya kuku mayai na ya watu maneno, eti
huwezi kuwazuilia kunena, unapaswa kuwa makini ili kumtetea Kristo.
“Madamu
sitazini, si dhambi mtumishi.” Acha ujinga, linda ushuhuda.
Huduma
nyingi za watu zimekufa, kwa kukosa hii hekima, zimeishilia kupakwa matope na
uvundo wa kila namna. Karibu:
(a) Jinsi ya Kutenda
Vyema.
(i) Zifahamu Sheria au kanuni za
Kanisani kwako,
makanisa mbalimbali yametofautia kivigezo, yapo ambayo ili ufunge ndoa au hata
uchumba kutangazwa ni lazima, muhusika awe anaudhuria ibada za Ushemasi, Seli,
au Jumuia, wenine huziita ibada za Nyumbani, au Kanisa la nyumbani.
Hususani
makanisa makubwa huwa na sera hii ili kuweza kuwa na taarifa sahihi za mtu anayenuia
kuchukuwa hatua hiyo, kwani kama kanisa lina watu wengi ni vigumu kwa uongozi
wa kanisa la mahali pamoja, kujua tabia zake, na kama kweli ana vigezo na sifa
za kufikia hatua hiyo, maana wengine huweza kuwa na ndoa nyingine au alishawai
kuolewa, na muda wake katika wokovu, na pia hali yake ya kiroho.
Kwa mantiki
hiyo, kikundi cha ibada za Jumuia, huweza kukufahamu vizuri zaidi.
Lakini pia
wengine, ni shariti uwe umelipa au kutoa Zaka ama fungu la kumi, kwa kipindi
kisicho pungua miezi 6.
Pia vigezo
vya muda wako wa wokovu au kuabudu hapo kanisani ni muhimu sana.
Kufahamu
kanuni na taratibu kama hizo, kutakusaidia kutokuingia katika malumbano ya
kihoja na wahusika, pia kutakuokolea muda, licha ya kukuokolea muda kutakufanya
kutenda vyema.
Maana
nimewaona watu walioabudu makanisani muda wa miaka mingi lakini kwa kuwa walipohamia
walihamia kienyeji, yaani bila barua ya utambulisho, walijikuta wakizuiliwa,
kuchuku hatua hizi za Uchumba hadi ndoa, na swala lipo sana kwenye huduma zenye
watu wengi.
Hatua za Kuchukuwa
mkishakubaliana:
(ii) Nendeni kwa Mchungaji, kama mna abudu katika makanisa
tofauti tofauti, ni vyema mkaanza katika kanisa la kijana wa kiume, au tumieni
utaratibu kwa kila muhusika kumuendea mchungaji wake, na mara baada ya hapo
ndipo muwaende walezi wate. Ila kibusara anzeni kwa wakiume.
Ili kulinda
ushuhuda mnaweza kuamua kukutana kanisani, ama kutumia utaratibu wa kuambatana
na washenga au mshenga.
(iii) Tafuta Mshenga na uambatane nae, ni muhimu kuanza kutafuta mtu huyu
maana atafanyika msaada mkubwa kwako, kama utatambua nafasi yake vyema.
Lakini mara
baada ya kumpa, huna budi kuhakikisha kuwa unambatana nae, ili kutimiza adhima
na dhima ya uwepo wake.
Sifa za Mshenga:
(1) Awe Mchamungu, sifa hii ni muhimu ili aweze
kukubeba rohoni, na kukushauri kiroho, lakini pia aweze kukulinda vyema kiroho,
pia asije kuhusika katika kukushawishi kuingia majaribuni, pia ili kumrahishia
Mungu pale atakapotaka kufikisha jambo fulani kwenu aidha kwa njia ya mashauri
na mahusia kutoka kwake.
(2) Awe na uelewa wa kutosha kuhusu
Mambo haya, Anapaswa
kuyafahamu kwa kiasi fulani maswala ya uchumba, ili aweze kukaa vyema kwenye
nafasi yake.
(3) Awe na Uwezo wa Kukushauri na
Ujasiri wa Kukukemea,
Ajawe na Hekima lakini pia Busara, ili kukusaidia katika kuchukuwa maamuzi
fulani, maana kuna majira mambo huweza kuwa magumu kiutatuzi, ila hekima yake
na Busara zake huweza kutumika katika kuleta utatuzi.
Lakini pia
ipo sifa ya ujasiri katika kukukemea au kukuonya, ni makosa kumtafuta mtu ambae
unajua utampiga chenga au kumkwepa ukiwa na nia ya hila moyoni mwako.
Lakini pia
mtu muoga hakufai, ni shariti awe na uwezo wakukukemea, na kukuzuilia kufanya
jambo fulani au kuziende njia fulani.
AKikuona unataka
kukata tamaa, au kutenda kinyume na maadili ya kiroho, kijamii ama kikanisa
aweze kukwambia waziwazi, kuwa hivi na vile sio sawa, na wakati mwingine
kuchukuwa hatua za kufikisha malalamiko yake katika ngazi husika ili kukulinda,
huku wewe nawe ukiwa mwepesi na mwenye moyo mnyofu katika kuonyeka, na kuwekewa
mipaka kiroho, kimwili, huku ukitambua ni kwa ajili yako, na kwa usalama wako,
na huyo anatimiza tu wajibu wake, tena kwako.
(4) Awe Rafiki yako wa Karibu, yaani anayekujua vizuri, kitabia,
kiimani, kiitikadi na hata kimaisha.
Licha ya mambo
hayo kumuwezesha yeye kukuelezea vyema ukweni ama popote itakapohitajika bila
kubabaika au kukurejelea mara kwa mara.
Pia itamsaidia
katika kuchukulina nawe, kiudhaifu, kiuchumi, na hata kiitikadi.
Na jambo
hili litamfanya kuwa mshauri, na mlinzi mzuri kwako, ukizingatia miongoni mwa
dhima yake ni kukulinda kimwili, na kiroho pia.
Lakini urafiki
huu usiwe wa kiundani kiasi cha yeye kukuonea haya katika kukulinda ama kukuzuilia
kitu fulani.
Majukumu na Taswira ya Mshenga :
(1) Kukushauri, (2)
Kukulinda kiroho ili msianguke dhambini,
ni wajibu wake, kuwa karibu nanyi, ili kuwasaidia msiwe na ukaribu ambao
unaweza kumpa Ibilisi au hisia zenu nafasi ya kuwatia majaribuni.
(3)
Kukusemea au kunena, ni msemaji badala
yako ukweni au kukuwakilisha punde atakapo hitajika kufanya hivyo, popote
kiuchumba.
(4) Kutatua
Migogoro, Ngazi muhimu ya kwanza, punde kunapo tokea tatizo ni kwa mshenga,
maana sio kila tatizo mtalipeleka kwa watumishi, walezi au wazazi ama wa
dhamini watarajiwa wa ndoa.
(5) Kukulinda
Kimwili, walioingia kwenye ndoa watakuwa wepesi wa kukubaliana nami, kuwa,
wiki au siku chache kabla ya kufunga arusi, muhusika huwa katika wakati mgumu
hususani katika usalama wa kimawazo.
Kwa hiyo
anahitaji mtu wakutembea naye, ili kumsaidia kuepukana na kadhia ya kupigiwa
honi kila wakati, na hata kumuepushia na kugongwa.
Lakini wapo
ambao huishilia kuwa na mawazo mengi yamkini kutokana na baathi ya mambo
kutoenenda sawa, kwa hiyo wanahitaji mfariji ili waweze kujipa moyo, lakini
wengine hushindwa kula chakula, kwa hiyo mshenga ana dhima ya kumsaidia ili ale
na wapo ambao hali hiyo hutokana na kuwa na mambo mengi.
(6) Ni Msaidizi kimajukumu, katika swala la kununua nguo au
kushona, ni mtu muhimu kuongozana nae, maana licha ya kukushauri, lakini pia
atakusaidia katika mambo mengi.
NB: Majukumu mengine hutokana na tamaduni na desturi za
mahali unapo owa au muelewaji anapotoka.
Makabila
mengine Mshenga huusika katika kumsaidia rafiki yake kutekeleza majukumu ya
kimahari, kama kuchinja, kupika, kumbebea chakula na kumpelekea wakati wa
sherehe za kimahari, na hata kubeba vitu vya mahari na kumpokelea zawadi. Kwa
hiyo ni muhimu kuzifahamu zilizo za kabila husika ili kurahisisha utekelezwaji
wake.
Tabia Madhubuti ama
Sifa nyingine na Maadili ya Mshenga Mzuri:
(1) Awe wa Jinsia yako, yaani kijana wa kiume, awe na
Mshenga wa kiume, na wa kike awe na Mshenga wa kike, hii ni sifa ya ulazima na
umuhimu kuliko zote, na ipo wazi natumia haihitaji maelezo mengi.
Itakusaidia
kuwa huru kwake, pili utakuwa katika mikono salama kihisia na kiroho pia.
(2) Awe anapatika kirahisi, Ni muhimu muda wake uwe haujambana
sana, ili kurahisisha ufanyaji wa majukumu yake, maana kuna mipango mingine
itamuhitaji kuwajibika usiku, mchana, na kila uchwao.
(3) Awe Tayari, jambo la utayari kwake ni muhimu
sana, maana kazi hii haina malipo, na huchukuwa muda, na huvuruga ratiba pia,
lakini pia, inahitaji kujitoa kiroho na hata kimwili, na kiucmi.
Maana kuna
mahali atalazimika kwenda na nauli zake au gharama zake kulingana na uwezo wa kiuchumi
wa muhusika.
Kwa hiyo sio
busara hata kidogo kumlazimisha mtu ama kumshawishi kupita kiasi angali unajua
hayupo tayari, kwani utakayeteseka au kukwama huko mbeleni ni wewe.
(4). Mwenye Lugha Nzuri, na Muongeji, “Msemaji.” Maneno yake ya kolee
munyu, maana ukweni ni mahali panapohitaji heshima.
Lakini pia
awe na uwezo wa kuongea hususani mshenga wa kijana wa kiume, maana ukweni
atahitajika kupanga hoja zenye nguvu hususani linapofika swala la mahari, maana
huyu hushirikiana na wazee katika kuhakikisha mahari inayopangwa utaimudu,
ndiposa ni shariti awe ni mtu ambae anakufahamu vyema, ili akuongele vizuri.
(5). Awe Muombaji, Huu ni mtu anaye wafahamu kiukaribu
mno, kwa hiyo ni rahisi kuwabeba kimaombi jambo ambalo litakuwa jema kwenu na kuwatulia
mzigo.
(6) Awe Mtu wa suluhu, sio mpenda shari, au
mshindani wa mambo. Jambo hili litakusaidia katika utatuzi wa matatizo, pamoja
na wakati wa kujenga hoja kama mwakilishi wako kwenye vikao, na kuzima mashauri
yenye chembe chembe za shari kwenye vikao.
(7) Asiwe mwenye Wivu, Wivu ulimfanya Sauli kutengeneza hila
dhidi ya Daudi, na kumpakazia yaliyo maovui ili amvurugie.
Kwa hiyo kuwa
makini na tabia hii kwa unayemchagua maana kwa nafasi yake, huweza kukuvurugia
au kutumiwa kuvuruga mipango yenu na Ibilisi.
Mwanzo 30
1 Naye
Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea ndugu yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama
sivyo, nitakufa mimi.
Hii ni tabia
ya wivu, tazama mtu anatishia kufa, au kufikia hatua ya kutamani kufa, shauri
ya wivu, na kwako huweza kufikia hatua ya kutamani kufanya lolote ili
akuvurugie, hata kuwawekea sumu. Kaini alimua nduguye shauri ya wivu.
Umakini ni
muhimu mno, Mithali 27: 4 Ghadhabu ni
kali, na hasira ni gharika; Lakini ni
nani awezaye kusimama mbele ya wivu.
Onyo kwa wenye Wivu: Ayubu 5: 2 Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao
wivu humwua mjinga.
(8) Asiwe Mtu ambaye Mlipishana
kimasilai, wakati wa
Kuchumbia, ama mwenye mahusiano ya kiundugu na wewe, au huyo mwenzako, lakini
pia asiwe mtu ambae aliwahi kuwa na mahusinano ya kiurafiki ama kimapenzi na
mchumba ako.
Akiwa ndugu
yako, anaweza kukuonea haya baathi ya nyakati, au asitekeleze vyema wajibu
wake, katika kukukaripia na hata kukushauri,
lakini pia akiwa ndugu wa mwenzako, ipo aibu itakayo mfunika wakati
wakutekeleza majukumu yake, lakini pia, kiujumla, hataweza kutenda vyema, aidha
kwakuegemea upande fulani, na kadhalika.
Lakini akiwa
ni mtu ambae alisawai kuwa na mahusiano ya kimapenzi, au aliwai kuchumbiana na
mwenzako, hakika hataweza kufanya majukumu yake kwa ufanisi na haijalishi amekuadia
kutende vyema au ni mwaminifu kwa kiasi gani, kwani kuna mambo mengine moyo na
nafsi ya mtu huwa na nguvu kuliko yeye.
(9) Asiwe ni wakuwaka Tamaa au Mwenye
Pepo hilo, sifa hii
ni muhimu ili kumzuilia kumtamani au kumpiga chenga rafiki yake. Yaani asije
akateta na shemeji yake. Vijana wanamuita mtu kama huyu, “Penda-penda.”
(10) Ajuwe Mipaka Yake na Kuiishi
Vyema, Ni muhimu
kujifahamu kuwa yeye ni msenga wala sio bwana au bibi arusi mtarajiwa.
Kufahamu
huku kutamfanya, kujua lugha za kunena na shemeji, uso wa kutazamana naye,
majibu ya kumpa, pia wakati wahusika wanaonge au kupanga mambo fulani,
atafahamu hatua za kukaa nao, au umbali na ukaribu, pia atahakikisha hawi kero,
kizuizi ama kipingamizi cha mahusiano yao na hata tenda nje ya majukumu, wajibu
na mwenendo wake.
Pia hata
weza kuwa msemaji, mapangaji au mzungumzaji wa kila jambo, bali kuna mengine ni
shariti aombe hizini ya muhusika au kumtaka kujinenea mwenyewe.
(11) Asijiweke au kujitegenezea mazingira
yakutiliwa mashaka,
Ewe mshenga, hakikisha unalinda ushuhuda wako, kama kuna umuhimu wa kukutana na
shemeji bila rafiki yako kuwepo, basi hakikisha ni katika mahali ambapo hapata
leta mashaka kifikra na kimtazamo, ikiwezekana iwe kanisani na rafiki yako
lazima ajuwe. Usidhubutu kumficha hata kama ikiwa ni shemeji amekutaka kufanya
hivyo, pia mshenga mwenza, yaani yule wa shemeji yako ni shariti afahamu na
awepo eneo la tukio hata kama hatasikiliza ila awe karibu mahali ambapo upeo wa
macho yake waweza fika bila kupapasa, kumbuka mazingira mazuri ni kanisani na maeneo
ya wazi.
Taadhari: We! Mshenga shemeji akikutaka,
usimlekezee macho, wala kutumia hata sekunde moja kumsikiliza, bali mkemee huku
ukitimua mbio kama Yusufu kwa mke wa Potifa.
Lakini pia,
hima vunja, Ushenga, ama jiuzulu haraka iwezekanavyo.
Mwisho
mwambie rafiki yako ubaya wa shemeji, mwambie ili ajuwe kuwa nazi aliyoichagua
ni korona.
Usi dhubutu
kumficha kwa kuhofia Uchumba kuvunjika, maana madhara ya mateso atakayokuja kuyapata
ni makubwa zaidi, nawe nafsi itakuhukumu pale utakapo yaona, na kumbwambia itamsadia
kuchukuwa maamuzi mapema, na kama hata chukua zigo la lawama halitakuwa juu
yako.
Wala usijiulize
kuwa atakuamini au la, wewe sema kuamini au kukataa ni juu yake, yeye mwenyewe.
(12) Mwenendo Mwema, Utauwa, hali ya kujitoa, na hata
nidhamu ya kimaisha ni miongoni mwa maadili muhimu sana kwake.
Pia swala la
uvaaji vizuri ni muhimu ili asije kukuabisha ukweni, na kwa marafiki wa
mwenzako na jamaa yake, maana rafiki wa mtu ni mtu, yaani jinsi watakavyomtazama
yeye, ndivyo watakavyokuona wewe. Kwa ujumla unapaswa kushirikiana na Roho
Mtakatifu, katika kumchagua Mshenga, maana dhima yake huweza kuendelea hata
baada ya maisha ya uchumba kuisha, wengi hufanyika marafiki wa kudumu wa ndoa,
na washauri, na walezi pia.
Hususani
ndoa inapokuwa changa inahitaji sana watu wa karibu wanao wafahamu vyema, ili
kuweza kushiriki mambo muhimu na nyeti vyema zaidi.
(13). Awe Mtunza siri, kwa makusudi kabisa nimeiweka sifa
hii kuwa ya mwisho kwani kikanuni za kiuandishi nilipaswa kumalizia na maelezo
yaliyopo kwenye pwenti iliyotangulia maana ina maudhui ya kihitimisho. Nami
nimeiweka hapa ili isalie vyema moyoni mwako.
Kutunza siri
ni muhimu sana, maana sio kila jambo lina wahitaji watu kujua, na utanzaji huu
utadumisha heshima yako na ya wahusika pia;
Mithali 25: 9 Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali
usiifunue siri ya mtu mwingine.
Kuna swali linakuja nafsini mwangu, Je Mwalimu naweza kuwa na washenga
zaidi ya mmoja, yamkini kwa sababu za kutofautiana kiuwezo, umri, na hata
kupatika, “nafasi katika muda”.
Jibu: Nimewai kuliona hili, ila kuna hitaji
umakini katika kupanga majukumu yao.
Kuna rafiki
yangu mmoja ambae hivi sasa ni Mchungaji, ilikuwa hivyo kwake.
Mahali
alipokuwa akiolewa, kulikuwa na tamaduni au desturi ngumu kwake, na wazazi wake
walikuwa mbali, kwa hiyo alimtumia mshenga mtu mzima na anayezifahamu zile mila
na taratibu vyema, maana hapa kijana, asingeweza kukamilisha jambo hili
kulingana na baathi ya makabila wazee wake kutokuwa radhi kunena au kuteta na
vijana mambo kama haya.
Lakini alikuwa
na kijana mwenzake, ambae aliketinae siku ya kugw kwa mkewe mtarajiwa, na natumai
pia katika maswala ya kukutana na mwenzake kuna utaratibu aliokuwa nao, maana
huyu aliyemuwakilisha ukweni, alikuwa ni mtu mzima kwa hiyo hawezi kumuhitaji
kila mara ili kumpa ushirikino anaoutaka anapokutana na mwenzake pia ukizingaia
alikuwa ni mtu mwenye majukumu mwengi.
Ila ni
muhimu kuwa na mshenga mmoja, na swala la mahari kuwe tu na wazee wa kanisa, au
wazazi na watu wazima wa kwenu wakuwakilishe wakisaidiana na mshenga wako.
Maana wakiwa
wengi wanaweza kukuvuruga, kiushauri na kadhalika.
(iv). Kapimeni Afya, Upimaji wa afya ni muhimu hususani
ugonjwa wa UKIMWI/VVU. Jambo hili linapaswa kifanyika mapema kabla ya uchumba
kutangazwa kanisani na utambulisho mwingine kwa jamaa zenu wa karibu.
Likichelewa
ni hatari, mfano kuna wachumba ambao walienda kupima ikiwa imebakia siku kama
3, ili wafunge arusi, na mmoja wao alikutwa ni mwadhirika.
Ilibidi
washindwe kuendelea, jaribu kuna jinsi lilivyo waathiri, maana jambo la arusi
kila mmoja analifahamu, kwa hiyo ni rahisi kujua sababu ya kutokuendelea kwao
na mchakato huo.
Lakini kwa kuwa
watu waikuwa wameshajianda mmoja wao alilazimika kuchumbia kwa haraka na
kufunga ndoa jambo ambalo pia ni hatari maana huweza kufanya hivyo bila
kumfahamu muhusika, kwani akili na fikra zanu na saikolojia hazina utulivu wa kutosha na kumuhusisha kwanu Mungu huwa ni
vigumu zaidi.
Kwa hiyo jambo
hili lifanyike hima au punde mara baada ya kutoka kwa Mchungaji.
(v). Katowe Posa na Kulipa Mahari, Kama upo kwenye kanisa makini na lenye utaratibu sawia, litakusaidia kukupa wazee, na wewe pamoja na mshenga wako na jamaa za kwenu mtaelekea ukweni kwa ajili ya posa na hatimae mahari.
Kitabu kikitoka, Usikubali kikupite maana yapo mengi zaidi ya hayo ikiwemo mbinu za kumpata huyu mwenzi, na kuhakikisha kama kweli katoka kwa Mungu.
Na Mwalimu Oscar Samba
#UgMinistry #SHARE #SAMBAZA Ili kueneza injili hii Zaidi.
Kama hujaokoka na unataka kuokoka ama ulirudi nyuma kiroho na unataka kutengeneza na BWANA kwa upya leo, tafadhali fuatisha nami maneno haya kwa Imani, Sema: BWANA YESU, NINAKUPENDA, NINAKIRI NA KUAMINI MOYONI MWANGU KUWA WEWE NI MUNGU, ULIKUFA NA KUFUFUKA KWA AJILI YANGU, INGIA NDANI YANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU LEO, AMENI.
Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo.