Jumatatu, 26 Januari 2026

Karibu Katika Mfululizo Wetu wa 10, katika Kitabu Chetu Hiki cha CHA #KUFANYA UNAPOKUWA NJIA PANDA. Pointi ya 8-10

Mwl. Oscar Samba

8. #Uwe na Utulivu Moyoni. Nimekujuza kuwa kama hujui cha
Kufanya usifanye chochote, ila na hapa nakutaka pa kuhakikisha ya
kuwa unakuwa na utulivu moyoni. Ukapata kibali cha kusoma kitabu
chetu kinacho uelezea nafasi ya mwili wa mwandamu au viungo vyake katika kumtumikia Mungu; kuna jambo muhimu sana utalipata
pale.

Jambo hilo lipo katika tukio la Nuhu akiwa katika Safina. Alimtuma
kunguru na kugundua kuwa muda bado wa kutoka safinani. Mara
baada ya muda kadhaa kupita, akamtuma njiwa: mara ya kwanza na
alirudi na jani la mti bichi. Napo kuna kitu aligundua ya kwamba bado
hakujakauka. Mara ya mwisho akamtuma na hakurudi tena; ndipo
alipogundua ya kuwa nchi imekauka!

Hakuwa na haraka, hakuchukua maamuzi hadi alipojiridhisha; sio


moyoni tu bali hata mwilini ya kwamba ni salama! Alikuwa na utulivu
wa kutosha kabisa moyoni. Sasa hapa sizungumzii tu maamuzi ila
ninazungumzia na utulivu moyoni.

Utulivu maana yake ni uwezo wa kustaimili vita vya ndani au nje,
vyenye kutumia uwanja wa mtu wa ndani wa kimawazo; yaani fikra. Na
ni lazima hali hii imkute mtu ambaye hajakata tamaa katika swala
husika. Aliyekata tamaa haiwezi kuhesabika kama ni utulivu kwa
sababu tayari alishatoka kwenye uwanja wa mapambano. Katulia sio
kwa sababu ana vita, ila ni kwa sababu kajitoa au katolewa kwenye
uwanja.

Kuna kipind fulani, (ambacho nimekielezea kwenye utangulizi pale
kwa kidogo) nilishindwa kuelewana na mchungaji wangu kiongozi;
jambo ambalo lilikuwa ni matokeo ya uongozi wa sehemu
kumshindikiza kuhusu maamuzi fulani juu yangu.

Niliagana naye hali iliyo ashiria mwisho wa mimi kuwa chini yake. Sio
kama mtumishi tu bali pia kama mshirika. Wakati nafika nyumbani na
kumshukuru Mungu kama maandiko yatutakavyo; kuwa tuwe watu wa
shukurani katika kila jambo. Roho Mtakatifu aliniambia kuwa; niwe na
Utulivu, sauti iliyokuwa na nia ya kunifanya kutokuwa na maamuzi
mabovu katika njia panda yangu.

Nami nilimjibu moja kwa moja kuwa, siwezi, nikimaanisha jinsi tukio
lile lilivyokuwa kubwa kwangu. Kwa hiyo kwa akili zangu siwezi kuwa
na utulivu. Ndipo nilipata ufahamu wa kugeuza udhaifu wangu wa
kutokuweza kuwa na utulivu; kama ajenda ya maombi mbele za Bwana.
Nikimtaka anipe utulivu. Baada ya muda, nilijisahau ama nilifikiria
kuwa sasa nimeshatulia vya kutosha. Kwa hiyo ninapaswa kufanya
maamuzi mengine. Nilijikuta napanga mipango ya kuhama katika
dhehebu langu na kuanzisha huduma! Mbele yangu kulikuwa na
maamuzi mawili makubwa, kufungua kanisa au kuhama dhehebu.

Nilipoingia kwenye maombi, nikimtaka Mungu sasa anipe kibali au
anipiganie, ndipo Roho wa Bwana aliponizuilia mambo yote mawili.
Hapo nikagundua kuwa kweli ninapaswa kuwa na utulivu!

Adui akitaka kukuyumbisha mahali, haachi kukufikisha njia panda.

Yaani kuhakikisha kunatokea tukio kubwa, ili uyumbe kifikra. Ama
anajua fika katika hali ngumu kama hiyo, yeye ni raisi kukuchomekea
mbegu fulani ya mawazo na kukuhamisha.

[Huwa ninasema, mbegu ya uwasi; mara nyingi hupandwa penye
uchungu na maumivu makubwa. Kuchoka ni mtaji mkubwa wa Adui
katika hili. Uasi wa Kora, Dasani na wengineo; ulikuja katika nyakati
kama hizi. Hata ule wa Hesabu 13/14; mara baada ya taarifa za uchungu
na za kuchosha za wale wapelelezi 10.]

#Tuendelee: Kuhama dhehebu sio vibaya, kufungua huduma sio vibaya
pia. Ila tatizo ni mpango wa Mungu~! Na unafanya hivyo kama
matokeo ya kutokuelewana na wenzako au kuna mpango wa Mungu
hapo! Hakikisha sana unakuwa na utulivu ili uweze kuisikia sauti ya
Mungu! Ukishindwa, basi kabla ya kutekeleza uamuzi unaonuia
kuuchukua; usogeze kwanza mbele za Mungu. (Na akiwa kimya,
nawe tulia “kiplefti”.) Uombee kwanza kwa muda, napo Mungu
hatakuacha atakupa majibu tu. Pia nawe hakikisha unamuomba
akuwezeshe kukubaliana na maamuzi yake. Maana madhara ya kupotea
au kuiendea njia nyingine ni makubwa sana. Sio wote wanaopotea
huwa wanarudi, wengine ndio wanatokomea kabisa.
9. #Dhibiti Kinywa Chako, Kitu kikubwa kilichowakamisha wana
wa Israeli ni manung’niko. Walijikuta wanaadhibiwa na Mungu na
wengi wao kuishilia jangwani, kwa sababu ya kushindwa kudhibiti
maneno ya vinywa vyao.

2 Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu
kama dhabihu ya jioni.
3 Ee Bwana, uweke *mlinzi* kinywani pangu, *Mngojezi* mlangoni pa
midomo yangu.
4 Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo
yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao
vya anasa.

Nimekupa na mistari kadhaa ili uweze kuona jinsi gani haya maombi ya
kudhibiti kinywa yanavyonenwa katika mazingira magumu! Kuna
mahali anapitia penye kashikashi na uzito fulani. Ndiposa maneno kama
yanatoka kinywani mwake. Ni muhimu kuhakikisha unayaomba haya
maombi. ili usije kumtenda Mungu dhambi.
Yakobo anazungumza kuhusu lijamu, msihi Mungu akufunge lijamu.

Lijamu ni aina ya kamba anayofungwa farasi mdomoni, nayo husaidia
sio tu kumzulia kupiga kelele anapokuwa katika magumu. Bali pia
hutumika kama kiongozi. Na wewe Roho wa Bwana, akifanikiwa
kudhibiti kinywa chako; uwe na hakika atakuwa amefanikiwa kitu
kikubwa sana kwenye moyo wako. Katikati ya magumu wewe imba
Zaburi na Nyimbo za Vitabuni.

10. #Tawala Hasira Yako: Napenda sana andiko hili; Mithali 16:
32 Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa; Na mtu
aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji.

Ni mwema kuliko shujaa. Na anayeweza kutawala au kudhibiti nyakati
mbalimbali zilizomzunguka; kwa kuifaya roho, moyo ama nafsi yake
kuweza kukabliana na mazingira kama hayo bila kutetereka: huyu ni
mwenye sifa njema. Na ni kuliko askari mwenye uwezo wa kuuteka
mji.

Mfano ni Yesu, alipokuwa katika hali ngumu, wakati Petro anamkata
mtu sikio. Yeye alilitwa na kulirejeshea sehemu yake! Huyu aliweza
kuitawala nafsi yake katika mazingira yale magumu. Hakurudisha
ngumi, wala kugombana. Kwa hiyo, ukipita mahali pagumu na wewe
kujipambania. kiasi cha kukosea; hapo uwe na hakika kuwa
umeshindwa kuitawala nafsi au moyo wako. Usije na kujitetea kuwa
lakini alinifanyia hivi na vile; ndio maana kama mwanadamu nilijikuta nafanya tukio hili na lile, uwe na hakika kuwa umeshindwa kujitawala
wewe!

Anayeitawala hasira ni kama shujaa na ni zaidi ya shujaa! Haya ni
maneno muhimu sana kuyaelewa, hasira ilimpoza Musa asiingie Kanani!

Imewafanya wengi kuingia katika hatia au makosa kadha wa kadha.
Hakikisha unamsihi Bwana akupe uwezo wa kudhibiti vitu au hali ama
hizi. Ili usije kumkosa Mungu na wanadamu pia. Njia panda nyingine
zina mtego wa hasira. ukikwama hapo ni umekwama sehemu ngumu
sana. Tuna kitabu cha IJUE NA UISHINDE HASIRA, kitakusaidia.

Kama Bado Hujaokoka na unaguswa kufanya hivyo, Fuatisha Pamoja Nami Sala Hii ya Toba.

*Sema* ; MUNGU BABA, NINAKUJA MBELE ZAKO, MIMI NI MWENYE DHAMBI, NAKUOMBA UNISAMEHE: AMENI.

Hakikisha unatafuta kanisa la Watu Waliokoka Ukaabudu Hapo.

Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Kwa Maombi: +255759859287
http://www.ukombozigospel.blogspot.com

Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD
Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk
Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv
Kwa Maombi +255759859287
Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL

UWE NA AMANI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni