KURASA

Jumamosi, 19 Julai 2025

ROHO MTAKATIFU KAMA MSAADA, KATIKA GHARAMA ZA KULIPA ILI KULETA UAMSHO

 Na Mwl Oscar Samba

Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. 

 Lengo la Somo: 

Kukuwezesha, au Kukujengea Fikra za Kuhitaji Msaada Wa Roho Mtakatifu; Ili Awe Mwezeshaji Wako Mkuu, Katika Kulipa Gharama kwa Ajili ya Uamsho.

Taswira ya Ujumbe: Imejikita katika kufahamu umuhimu wa kumpata Roho Mtakatifu kipindi cha maandalizi ya kiroho kwa ajili ya uamsho. Hapa nilipo nalenga aina ya upako unao hitajika, ili kulipa gharama ya kuleta Uamsho. Ni sawa na kipindi kile cha mwanafunzi kusoma kabla ya kazi. Uamsho ni kipindi cha kazi, lakini kabla ya kazi kilipita kipindi aidha cha chuo au shule. 

Askari kabla ya kuingia vitani, au kuwa askari kuna kipindi cha mafunzo au cha maandalizi ya vita. Sasa kipindi hiki katika swala la Uamsho, ndicho hukiita kipindi cha kulipa gharama kwa ajili ya Uamsho. 

Kati ya eneo kubwa na muhimu watu wengi hawalijui wala kulizingatia, ni lile la maandalizi au la kulipa gharama. Mfano, Uamsho wa huduma ya Yesu, ulilipwa gharama na watu wengi. Akiwemo Yohana Mbatizaji, aliyekaa nyikani akila asali ya mwitu na nzige. Akivaa mavazi kama ya Elia, yaliyo ya ngozi na kadhalika. Maana huyu alikuwa ni mtangulizi.

Yupo Simeoni, ambaye alilazimika kuishi miaka ya ziada, hadi pale atakapomuona Yesu. Na kwa kuwa alikuwa ni mtumishi; uwe na hakika alikuwa akibeba jambo hilo. Mtazame; Luka 2:25 Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26 Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. 

27 Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria.

Mtu Mwingine Aliyehusika ni Anna: Ukitazama maisha yake ya ujane, tena jinsi yalivyoanzia kipindi cha ujana wake, unapata picha ya wazi kabisa ya gharama iliyolipwa. Lakini pia, alikuwa ni mtu wa maombi. Tena maombi ya kulala hekaluni, alifanyika kuwa Mtawa. Aliyejitoa maisha yote kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni.

Pia, alikuwa ni nabii, na kama ndivyo; alikuwa akitabiri nini! Hapana shaka kabisa, alikuwa akiomba maombi ya kinabii. Ni unabii upi huo? Ni ule wa kutimizwa kwa kuzaliwa kwa Yesu. Yaani kama alivyotabiri nabii Isaya, Yeremia na kwingineko: ili unabii huo utimie. Hao ni baadhi tu ya walipa gharama kwa ajili ya huduma ya YESU.

Tumtazame mwana Mama huyu Shujaa; Luka 2:36 Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. 

37 Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. 

38 Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. 

Kama ndivyo, hii ikupe nidhamu kubwa sana, pale panapotokea Uamsho katika mikono yako. Unapaswa kufahamu kuwa, mlipuko unao uona au unao onekana katika mikono yako hivi leo; nyuma yake kuna gharama kubwa iliyolipwa na wengine. Sio swala la kujiona tu ya kuwa wewe ndiye yote katika yote. Bali ni swala la kutambua ya kwamba, wapo wengi waliochangia katika mafanikio hayo.

Hainalishi unawajua au huwajui, ila wapo. Mfano, kule nchini China, kuna muombaji mmoja aliwahi kuomba kwa ajili ya Uamsho kwa muda wa miaka 70. Akafa, haujatokea; na akamkabidhi mwanaye. Sasa, leo wewe Mungu aje akutumie, na Uamsho utokee! Uwe na hakika, unapaswa kufahamu na kuelewa ya kuwa, wapo waliolipa gharama kubwa kwa ajili ya jambo hilo.

Inawezekana kabisa, dhehebu fulani walipewa eneo la uombaji na Mungu kwa ajili ya swala hilo tu. Wengine wakapewa eneo la kusimamia imani au fundisho sahihi, (kuilinda Theolojia), na wengine wakapewa mifumo; na kisha kwako kukatokea huo mlipuko. 

Wewe unapaswa kujiona sii bora kuliko Yohana mbatizaji aliyetangulia mbele yako. Wala sii wa thamani kuliko wakina Simeoni, Isaya na Yeremia waliopitia nyakati za machozi kwa ajili yako; sanjari na wakina Ana Binti Fanueli waliolazimika kuishi maisha ya ujane na utawa kwa ajili ya jambo hilo.

 Nafasi ya Roho Mtakatifu Katika Kukuwezesha Kulipa Gharama ya Uamsho

1. Yesu Kabla ya Kuelekea Jangwani (Maombi ya Siku 40) Alijazwa Roho Mtakatifu Kwanza. Kuna swala muhimu la kufahamu hapa, ni kwamba nguvu ya maombi ya siku 40, tena bila kula wala kunywa, ilitoka kwa Roho Mtakatifu. Sio jambo jepesi kumudu maombi ya namna hii. Kwanza, utayari wake tu, ni ishara ya huu uwepo wa nguvu za Mungu.

Kwa hiyo, kabla ya kuanza huduma; ambayo ilijawa na Uamsho wa hali ya juu, Yesu alijazwa Roho Mtakatifu (wakati anabatizwa) lakini pia aliongozwa na huyu Roho au aliwezeshwa naye katika siku hizo 40, tena ilikuwa ni nyikani ama maporini.

Marko 1:9 Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. 10 Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; 11 na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. 

Hakikisha; 12 Mara Roho akamtoa aende nyikani.

13 Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.

Sasa, maandalizi hayo; au gharama hiyo ya hayo maombi; ndiyo iliyokuja kuzaa huu Uamsho tutakao uona hapa mbeleni. Fahamu sana ya kuwa, Yesu hakuanza huduma bila kujaa Roho, lakini pia bila maombi ya siku 40, ambayo ndiyo yaliyompatia hizo nguvu. (Msisitizo wangu katika kitabu hiki kidogo ama kama kitabu ndani ya kitabu kikubwa cha Uamsho, sii kukutaka kuomba maombi ya kuleta Uamsho bali ni kuomba au kuhitaji upako wa maandalizi au wakulipa gharama kwa ajili ya Uamsho). Kuomba kwa ajili ya uamsho katika ujumla wake ni jambo jema, ila hapa msisitizo wangu ni huo.

Maana wengi wanajikuta wakishawishika kuwekeza nguvu katika maombi ya sehemu ya pili, na kusahau umuhimu wa kwenda shule ndipo uanze kuandika barua za maombi ya kazi. 

Mtazame Yesu jinsi alivyochanua mara baada ya kufanya vyema katika kipindi cha upako wa maandalizi; Marko 1:16 Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. 

Upako wa kujipatia watendakazi pamoja naye, ama wanafunzi, ulitafutwa katika maombi yaliyowezeshwa na Roho Mtakatifu. Hili lifahamu daima, ili usije ukafanya huduma kwa akili zako mwenyewe. 

Tukio Jingine: Marko 1:23 Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti,

24 akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? 

26 Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. 

Tazama Upana Wake Zaidi: Marko 1:27 Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Elimu waliyokuwa wanaishangaa, ilitoka katika upako wa maandalizi. Ni sawa na mfanyakazi mwenye uwezo mzuri, hatengenezwi kazini tu; bali ubora wake unaanzia shuleni ama chuoni. Mafunzo yana nafasi kubwa sana. Kwa hiyo, ukitoroka siku 40 zako nyikani, au ukishindwa kutokana na kujaribiwa na Ibilisi hapo: uwe na hakika ni unajizuilia kunufaika na kilichokusudiwa. Ndiposa unahitaji upako huu, ili uvuke au utende vyema. Tuendelee:

Marko 1:28 Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. (Wengi wanataka habari zao zienee, lakini bado hawapo tayari kulipa ghrama.)

Marko 1:30 Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Marko 1:31 Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. 32 Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. 

33 Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. (Ukitaka mji wote ukukusanyikie, basi hunabudi kutenda vyema katika kipindi hiki cha upako wa maandalizi kwa ajili ya Uamsho.)

34 Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. 

37 nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Usitafute tu kutafutwa na watu wote; yaani kuwa na kibali kwa wote. Bali tafuta jambo moja muhimu la kuhakikisha unatenda vyema katika kipindi chako kama hiki.)

2. Mitume (Kanisa la Kwanza) Walipaswa Kupokea Nguvu Kwanza. Yesu kabla ya kuwataka waanze huduma, jambo la muhimu na lilillopewa kipaumbele cha kwanza, ni wao kupokea nguvu kwanza. Hilo ndilo lililopewa msisitizo zaidi. Na ili kupata nguvu, iliwalazimu kujazwa Roho Mtakatifu. Yesu anawaambia ya kuwa; wasiondoke, au wasianze lolote; mpaka wavikwe au wavalishwe (kama joho au koti) uweza utokao Mbinguni.

Tazama; Luka 24:49 Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. 

50 Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki. 51 Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa ju mbinguni. 

52 Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu.

53 Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu. 

Tazama Tena; Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. 

Yesu alifahamu kabisa ya kuwa, huduma iyokwepo mbele yao, iliwahitaji wao kuwa na uwezesho wa kipekee. Nafasi ya Roho Mtakatifu katika kuliwezesha hili ilihitajika kabisa. Tujione:

. Walishinda Vikwazo vya Baraza. Mara baada ya wakina Petro na Yohana kumuombea yule kiwete wa mlango mzuri (sura ya 3 ya Matendo ya Mitume) walijikuta wamekamatwa. Baraza la mji liliwainukia na kuwaweka ndani. Shitaka kuu lilitokana na aina ya mamlaka waliyoitumia kutenda muujiza ule.

Hukumu iliwataka kuhakikisha hawalitumi tena jina la Yesu. Katika hukumu ya namna hiyo, Petro kwa ujasiri anasimama na kuitetea imani. Maana nje ya hapo, Uamsho ungefia hapo; jitihada za kuhakikisha moto unawaka kila eneo duniani zingekwamia pale. 

Tazama; Matendo ya Mitume 4:3 Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. 

7 Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Tazama Huo Uweza: 8 Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli 9 kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, 

10 jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. 

11 Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. 

.Hata Zilipopungua Walihitaji Ujazo. Mara baada ya tukio hilo, kanisa likatambua ya kuwa, nguvu walizojaa siku ya Pentekoste zimepunguka. Kwa hiyo, chakufanya ni kuhakikisha wanarudi tena kwenye kituo cha mafuta, ilikuongeza nishati. Maana mapambano yanapaswa kuendelea. Upako wa namna hii ni muhimu sana kwa kila anayehitaji kuleta Uamsho. Kwani safari ya Uamsho imegubikwa na mambo mengi.

Matendo ya Mitume 4:29 Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, 

30 ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. 

31 Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. 

NB: Siku kumi walizopaswa kusubiri Gorofani, ndizo zilizokuja kuzaa huo uweza wa kuvumilia vikwazo na changamoto katika Uamsho. Matendo makuu yaliyoongozwa na wao ikiwemo kufufuka kwa Dorikasi na kadhalika; ni matokeo ya kutenda vyema kipindi kile cha siku kumi. Hii ikupe kutumia vyema nyakati zinazo nuia kukutaka kulipa gharama kwa ajili ya kuupata huu upako wa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Uamsho; Asante:

https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h

https://www.ukombozigospel.blogspot.com 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni