KURASA

Jumanne, 29 Julai 2025

AKILI ZILIZO MACHO KATIKA UFALME WA MBINGUNI Mathayo 24:45

Ujumbee huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya Cha: KILI ZILIZO MACHO KATIKA UFALME WA MBINGUNI

Mathayo 24:45

Na Mwalimu Oscar Samba 

Utangulizi
Kulala Usingizi, Kupoa kiroho, au Kifo cha Kiroho = Ni sawa sawa na:- (Hufananishwa na Hali ya Mtu Asiye na Akili ama Mwenye Tatizo hilo Katika Ulimwengu wa roho. 

Hiyo ni picha muhimu unayopaswa kuwa nayo, wakati huu unapoelekea kukisoma kitabu hiki. Ni muhimu sana kufahamu ya kuwa maana moja wapo ya Yesu ya kututaka tusilale usingizi yaani tuwe macho; ama tukeshe ililenga eneo la akili zetu.

Tazama mfano ule wa Wana Wali watano wenye Busara na watano Wapumbavu. Ndipo utakapotambua ya kuwa upumbavu unaotajwa pale, ni unaotokana na hali ya kutokujua ni nini cha kufanya katika nyakati kama hizi.

Malengo ya Kitabu:

1. Kuyafumbua Macho ya Aliyefumbwa, Kuziamsha Akili za Asinziaye ili Aweze Kuwa na Utayari wa Kutumika Kiusahihi (kama impasavyo), Katika Kulielekea Kusudi Aliloitiwa Kinyakati.

2. Kumpatia Ufahamu, Utakaotumika Vyema na Akili Zake, ili Kujua Ni Nini Kimpasacho Kukifanya Katika Majira Husika.

1 Mambo ya Nyakati 12:32 Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.

3. Kumjengea Fikra za Kumuwezesha Kuzitambua Hila za Adui Shetani; Katika Mpango wa Kumnyamazisha au Kutaka Kumpoozesha Kiroho na Kiutumishi, (au Kiutumishi/Kiroho.) 2 Wakorintho 2:11 Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikra zake.

4....


Lengo Kuu: Kukujengea Fikra za Kiuamsho, Ili Kuibua Hari na Kuamsha .... Kukuumbia Nia ya Kiuamsho Ndani Yako. (Penye Nia, Pana Utayari).

.....,....

1. Maonevu na Migogoro Katika Kanisa, Ama Baina ya Watumishi, au Washirika: Ni Ishara ya Kujisahau Kiroho. Watu waliopoteza kusudi, au kulisahau ama walioshindwa kujitambua ndio pekee huweza kuanza kuumana. Unapoona

watu wanagombania vyeo, wanapigania madaraka; ama wanafanyiana vigisu na visa sanjari na kuchimbiana mashimo; uwe na hakika kuna kujisahau mahali.

Tumewekwa kwenye shamba la Bwana ili tulitumikie Kusudi lake. Kusudi lake ni kuujenga mwili wa Kristo. Kwa hiyo, ukiona mtu mwenye kuubomoa huu mwili, uwe na hakika; aidha anatumikia kambi ya adui yaani ni msaliti miongoni mwetu; ama akili zake zimepofushwa. Kwa hiyo, hajui alifanyalo. Kashasahu kusudio la yeye kuajiriwa kwenye shamba hilo.
        Na badala ya kutumia jembe alilopewa ili apaliliye mazao; kageuka na kuanza kuyang'oa ama kukata mizizi yake kwa jembe! Mtu wa namna hii, kuna kuwa na shida katika fahamu zake.
Ukisoma Mathayo 24:42-51, utagundua kuwa imizo kubwa hapo ni kuhakikisha akili zetu zinakuwa macho. Ili nini? Ni ili tuweze kujua ni kipi chakufanya katika nyakati kama hizi. Ambapo mstari huo wa 42, anatutaka tuwe macho. Yaani tukeshe. Kisha katika 45, ndipo anaulizia ni nani aliye mtumishi mwenye akili. Hii inatupa kuunganisha kwa pamoja macho na akili. Ambapo hutambua ya kuwa, kuwa macho kiroho kuna maana ya akili zetu kuwa sawasawa.

Yesu katika muktadha wa maandika hayo hayo, anakuja na kutujuza kuhusu mtumwa yule ambaye hajakesha, na kwa mujibu sasa wa huo mstari wa 45, huyu ni yule ambaye akili zake hazijakaa sawa. Ni aliyekosa akili, maana hajawagaiya wajoli wake chakula kwa wakati. (Hajafanya aliyoagizwa na muajiri wake: ambaye ni Baba Yetu wa Mbinguni.) 

Tumuone ili sasa uweze kukubaliana nami vyema ya kuwa, pindi unapoona migogoro makanisani, ni hii ishara.
Ona; Mathayo 24:45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
Hakiki; 48 Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; 49 akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi;
50 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, 51 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Badala ya kumpiga Shetani, imegeuka na kuwa kupigana wenyewe kwa wenyewe. Yesu anawaweka watu wa namna hii katika kundi la wasio na akili, ama waliolala usingizi katika akili zao au kufa kiroho. Malumbano katika utumishi, kanisa la mahali pamoja, ama ngazi ya sehemu, jimbo na hata kitaifa: ni hii ishara. Kwa hiyo, ili kuwasaidia na kuleta suluhu la kudumu. Hakikisha unaombea akili zao, ombea macho yao ya ndani yaweze kuona sawasawa ili waweze kujitambua sawia.

2. Akili Zilizo Macho Kiroho, "Hufokasi" yaani Hujikita Katika Kusudi. Jembe au panga lililoshikwa na kichaa, ni tofauti sana vifaa hivyo vinapokuwa katika mikono ya mtu mwenye akili timamu.

       Sasa, mtu ambaye akili zake zipo macho, huwa na ufahamu na hali ya kulitambua na kulifanya kusudi la Uungu katika nafasi aliyopewa na Mungu. Tumuone mtumwa huyu mwenye akili anayetajwa na Yesu, ambaye amekidhi vigezo vya kukesha. Na fahamu ya kuwa, kielelezo moja wapo cha Yesu hapa, kinakaa katika eneo la kuwapa watu chakula kwa wakati. Muda ni miongoni mwa imizo kubwa sana.

Tazama; Mathayo 24:42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. 43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.(Kwa hiyo, kushindwa kujua ni nini cha kufanya; humfanya huyu mpendwa kushindwa kukesha. Kwa hiyo , akili zilizolala usingizi, ni matokeo ya kutofahamu neno la saa. Au neno la msimu au wakati husika. Huo msatari ukiusoma tena, utakutana na maneno..fahamuni neno hili...lipi la wakati ambao Bwana Yesu analijilia kanisa lake. Wakati wenye kusudi au maelekezo fulani ya nini chakufanya!)

44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. 45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. 47 Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote.

3. Taa Yake Huwa na Mafuta. (Hujuwa Wakati wa Kujaza Taa Zao Mafuta.) Kuna aina ya ujinga au upumbavu ambao ni matokeo ya kutokujua ni nini cha kufanya, katika wakati gani?) Fahamu kwamba, ujinga na upumbavu ni matokeo aidha ya akili kutokupata maarifa, ama kushindwa kugeuza elimu kuwa maarifa. Na pia ni matokeo ya kupumbazwa kiasi cha kusalia kujua cha kufanya, ila ukakosa busara ama hekima ya kulifanya kwa wakati husika.


Maandiko, yanauliza ya kuwa, ni nani mtumwa yule mwenye akili, ambaye atawekwa kwenye nafasi ili atimize majukumu yake kwa wakati? Imizo langu kubwa hapa ni huu wakati. Yule asiyejitambua, anaishilia kutenda mengineyo. Lakini chanzo ni kujisemea moyoni kuwa aliyemuajiri atakawia. Kukawia maana yake, ni kwamba hakuweza kusoma alama za nyakati za ujio wa mkuu wake.

Tazama; Mathayo 24:45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.  48 Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia.

Watumishi hawa wawili, wamepishana kwenye nyakati. Hali ya kutokujua ni nini chakufanya, inasalia kuwa changamoto.
Mfano wa Wana Wali 10, ni kielelezo kikubwa sana kwetu. Wenye hekima au wale wenye busara (akili), waliweza kutambua wakati ama majira ya kujaza taa mafuta. Kumbe, kuna majira muhimu kwa ajili ya maandalizi ya kila jambo! Na ukishindwa kuyatambua kamwe hutaweza kunufaika na harusi. Maana wote waliposikia kelele za ya kwamba bwana harusi anapita, na waamke; wote waliamka. Ila walionufaika na majira husika ni wale tu, wenye taa zenye mafuta!
Waliotambua muda au majira ya kuweka taa mafuta ndio walionufaika na jambo hilo. Na hizi ndizo akili zilizo macho. Ni maombi yangu kwa Mungu, uwe katika kundi la namna hii. Ili uweze kunufaika vilivyo na nyakati za kuburudishwa. Nyakati za "....haya ingia rahani mwangu...." Maana utumishi huu, una nyakati za namna hii.

 
Tazama: Mathayo 25:3 Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao;
8 Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
9 Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.


10 Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
11 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. 12 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
13 Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa. Tuna kundi la watumishi wanaoishi sasa, kana kwamba wanajua siku na saa anayokuja Yesu! Lakini nijuavyo mimi ni kwamba, tunapaswa kukesha maana hatuijui hiyo siku wala saa. 

Kuna maisha watu wanaishi, kana kwamba Yesu alishawapigia simu ya kuwa nitakuja miaka 1000 ijayo. Kwa hiyo, leo wamejisahau kabisa. Imizo la Yesu anakuja, Yesu yu karibu kulinyakuwa kanisa lake; linakupelekea moja kwa moja kwenye agizo kuu ambalo ndani yake limefungwa na hofu ya nyakati za mwisho. Ambazo msisitizo wake ni kwamba, Mwana wa Adamu yu karibu kurudi tena mara ya pili, ili alinyakuwe kanisa lake. Na kanisa hilo hupaswa kuwa safi, yaani bila mawaa. Kwa hiyo sasa, utakaso na toba ya ondoleo la dhambi huwa ni kipaumbele kikubwa.
Aina ya injili iliyohubiriwa na Yesu na kutanguliwa na Yohana Mbatizaji ni kwamba, Tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Hii ni dalili tosha ya kuwa, wahusika waliyaona majira ya kuja kwa Yesu mara ya pili ya kuwa; yamekaribia sana.

Kuna aina ya akili unapaswa kuwa nazo, ili uweze kutambua ni kipi kikupasacho kutenda, katika wakati uliopo. Kuna kosa ukilifanya, linaweza kukufanya kuwa msindikizaji asiye na faida katika utumishi au wokovu wako.

      Mfano ni wale wana wali 5, waliandaa taa bure, wakatoka barabarani kumlaki bure.   Wakaishilia kung'atwa na mbu, na baridi ya usiku bure.
Pamoja naa vumbi ama matope ya barabarani bure.
Wakajikuta wanapokea na adhabu nyingine ya kuzurura kwa nia ya kufuata mafuta; bure. 

Na fahamu sana kuwa, sio kwamba walikosa mafuta; la! Mafuta waliyapata kabisa. Ila walichelewa muda wa kuingia ukumbini. Kwa hiyo, kama ni gharama hawa wapumbavu walilipa zaidi. Maana kuna kamuda kaziada walikatumia (hapana shaka umbali uliongezeka) wa kwenda kujinunulia mafuta. Na kwa kuwa muda umeenda, huwenda yamkini kulikuwa na ziada nyingine pia. 

Mafuta wanayo, taa wanazo; lakini wanaishilia kukataliwa! Kuna gharama unaweza kuja kuzilipa, na ukasalia bila Uamsho maana kuna majira yalikupita.
Ndiposa ninasema ya kuwa; hili ni ombi langu kwa Mungu ya kwamba, majira kama haya yasikupite tafadha. Na mada ijayo, itakusaidia kujua ni kipi cha kufanya ili usipitwe nayo.

4. Wenye Akili/Busara Huwa na Uwezo wa Kuiandaa Kesho Tangia Leo. Niliporudia tena hivi sasa kusoma kifungu hiki cha Wana Wali 10, nimejikuta naondoka na ufunuo mpya kabisa ambao sijawahi kuwa nao.

Kumbe, taa zao wote au makundi yote mawili zilikuwa na mafuta, na zilikuwa zina waka! (Hili nalikuwa sijalijua.) Nilifikiri hawa watano waliondoka na taa zikiwa hazina mafuta kabisa. Kumbe sivyo.
Ila changamoto ya hawa wapumbavu, ilikuwa ni kukosa akili za kuweka akiba. Akili za kuinua au kutazama majira ya ziada. Maana wanasema, au wanaomba msaada kwa kusema TAA ZETU ZINAZIMIKA. Sio kwamba hazina mafuta, la! Hasha. Ni kwa sababu zinazimika. Kwa maana kwamba, ni dhairi wote walitoka na taa zenye mafuta. Ila changamoto ni kwamba, hawa wenye busara walibeba na mafuta ya ziada.

Tanki la taa zile zinafahamika uwezo wake wa kubeba mafuta, na hawa wenye busara walijiongeza katika kufikiri kwao. (Ingawaje inawezekana wale wapumbavu walitembelea mafuta yaliyosalia kwenye taa, kwa hiyo hawakuwa na ufahamu wa kuyaongeza. Lakini maandiko hutuonyesha kuwa, taa zao nazo zilikuwa na kiwango fulani cha mafuta bado).

Mathayo 25:4 bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.  8 Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Kumbuka; ni TAA ZINA ZIMIKA.
Inatupa kuona umuhimu wa kujipanga kwa ajili ya kesho. Hii ikuzuiliye kuridhika na hali ya sasa. Badala yake uwe mwepesi wa kufanyia kazi kila taarifa Roho Mtakatifu anayokupa kama taadhari kwa ajili ya mabaya au mema yajayo.

Na sifa hii ipo kwenye Busara; Mithali 22:3 Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.
Kwa mtaji huo ni kwamba, pia huweza kuyaona mema na kujipanga kwa ajili ya hayo mema. Huku ukichukuwa taadhri ya mabaya yajayo.
9 Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. Hawa katika busara zao, (kumbuka busara huhusisha sana uwezo wa kuamua kwa ufahamu mkubwa sasa, kwa ajili ya usalama au uhai ama ustawi wa baadae,) waliamua vizuri kabisa. Maana kama wangewapa, wote wangekosa kuingia ukumbini. 

Kabla ya kurusha lawama kwa kundi hili, lazima utazame kwa umakini. Maandiko husema ya kuwa, bwana harusi alikawia. Kwa hiyo, kikawaida kabisa tunapaswa kumlqumu bwana harusi au waliomsababisha kukawia. (Ingawaje Mungu hakawii wala hawai. Mambo yake ni kwa wakati wake. Ile amekawia, inatuonyesha ya kuwa kuna muda walikuwa nao kwenye fikra zao, ambao haukuwa wa Mungu.)

Tazama; Mathayo 25:5 Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. 
Bado, ninalazimika kuja katika eneo la Fikra au mtazamo. Kwa maana kwamba, busara ya Kiungu, itakuwezesha kung'amua au kukupatia fikra au mtazamo wa Kiungu dhidi ya swala husika. Hutatazama kibinadamu. Maana mwandishi hutumbia ya kuwa, bwana harusi alikawia. Alichelewa; lakini Habakuki 2:2, butujulisha ya kuwa Mungu hakawii wala hawai. Kwa hiyo, matarajio yetu !ambayo sasasigo yake) huweza kuwa kikwa.


Tunapoutarajia uamsho kesho, wakati ratiba ya Mungu ni kwamba huu ni muda wa maandalizi; usipokuja muda huo. Kuna hatqri ya mafuta yetu kutuishia njiani. Watakaoyatambua majira ya Mungu, watatumia muda wa maandalizi kuweka kiwango cha mafuta kitakachowafikisha mpaka mwisho. Mpaka wakati husika.
Ni muhimu sana kujifunza kuzivua fikra zako kila wakati, ili uweze kuvaa Fikra za Kiungu Katika Swala Husika. 

Maana watu wengi wanaokata tamaa katika kumngoja Bwana, ni matokeo ya wao kuandaa mafuta ya kilomita 4, kumbe safari ni kilomita 20! Bali wenye busara, hundaa mafuta ya mwendo husika.
Unajua, hawa wana wali 5 wapumbavu; wana vigezo vingi sana muhimu. Maana kama ni nianya kumlaki walikuwa nayo. Taa walikuwa nayo. Mafuta kiasi fulani walikuwa nayo. Kama ni kusinzia wote 10 walisinzia. Walipoamshwa na kelele, wote waliamshwa nankuamka. Wote wakandaa taa zao.

Na hata walipohitanika kulipa gharama ya ziada ya kwenda murudia mafuta au kununua; bado walilipa na wala hawajawalaumu wenzao kwa kuwanyima. Hawakupoteza muda katika kulalamika. Ila.tatizo sasa, lilikuja katika eneo la kutumia vyema muda wa kuweka taa mafuta, tena mafuta ya kutosha! Hilo litawafanya kuwa Wapumbavu.

5.


6.Hutumia Kipawa Chake Vizuri. Kamwe Hakiziki Mchangani ama Kukificha Kwenye Leso. Kutokujitambua, au kutambua hitajio ama kusudio au dhumuni la kuwekwa hapo shambni mwa Bwana Yesu; kunapelekea kutokutimiza wajibu. Wito ni kipawa, kama ilivyo karama ambapo ni sehemu ya talanta. Yesu ni kama mwekezaji, kwa lugha nyingine tungalimuita Kabaila. Ambapo anahitaji faida.


Injili ya Yohana 15, anaimiza sana kuhusu kumzalia Bwana Matunda. Alichoweka ndani yetu, anakihitaji kizae au kilete faida. Mungu sii Mungu wa hasara, bali ni faida. Sasa, adui akimkamata mtu fahamu zake, ndipo anapojikuta amejisahau na kuachana na maelekezo haya na kuanza kufanya kama atakavyo yeye.


Tazama kisha Nitakupatia Kielelezo Kingine cha Wazi Kabisa; Mathayo 25:18 Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.
20 Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.
21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.

 
24 Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; 25 basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. 

Watumishi hawa walijisahau sana. Badala ya kufanya Mapenzi ya Baba, wakajifanyia ya kwao. Walisahau kuwa shamba hilo sio lao. Kuna mwenye shamba, ambaye ndiye Mmiliki. Ndiye anayewalipa ujira au mshahara wafanyakazi hao wote.
Kama kuna jambo huwa ninajaribu kujitahidi, ni kutamani kuyafanya mapenzi ya Mungu aliyeniajiri katika shamba lake. Hii imejikuta ikiwa ni haja yangu kubwa kabisa katika wito au utumishi huu. Ni mfano wa mtu aliyeamua kumuajiri mfanyakazi katika duka au kampuni yake, ama yule wa nyumbani kwake. Mfanyakazi huyo hupaswa kufanya au kufuata maelekezo ya muajiri wake. Asije akajiundia ya kwake; maana hivyo haifai kabisa. Kwani hitajio la kazi au wajibu ama jukumu husika, ndilo lililompa hiyo ajira. Hakuajiriwa ilimradi tu, bali aliajiriwa kwa malengo na makusudio maalumu.

*Tuwatazame* ; Marko 12:1 Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri.
2 Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu.
4 Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha za kichwa, wakamfanyia jeuri.

6 Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu.
7 Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu.

8 Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. 9 basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine.
10 Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni.
11 Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?
12 Nao wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao.

     Kitabu hiki kikupe sana wewe kujiuliza; je, wewe upo kundi lipi? Maana hivi leo: tuna maaskofu na waangalizi ambao wamegeukia kuuwa na kukandamiza huduma za watu. Tuna wachungaji ambao wamekuwa ni mabingwa wa kukanyagia huduma na karama za wengine. Wamegeuka wakina Sauli wa siku za leo. Wana wawinda wale ambao wanafanya vizuri, wivu umegeuka kuwa chanzo cha kuharibika kwa mioyo yao.

7.
8.
9.
. Mabishano, Malumbano, Matabaka na Kujiona Bora Zaidi ya Wengine; Ni Dalili Aidha ya Akili Changa (Macho Yenye Uono Hafifu) ama Kukosa Hizi Akili Kabisa.

Kitabu Kikitoka Kitafute:

*Na Mwl OSCAR SAMBA*

( #NasahazaMwlOscar )
#FaidayaJaribu: #Usiogope

HAKIKA MUNGU ANAJUA UHITAJI WAKO

Mathayo 6:8 Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba.

Kwa Miaka Mingi Andiko Hili Limefanyika Faraja Kubwa Sana Kwangu; Nami Ninatamani Uione Siri Iliyopo Hapo Ili Likuvushe Unapopitia.

http://www.ukombozigospel.blogspot.com
Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD

Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk
Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv
Kwa Maombi +255759859287
Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL

Nikutakie Siku Njema

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni