Bwana Yesu asifiwe sana!
Masomo ya wiki mbili mfululizo zilizopita, juu ya Sera ya ufalme wa Mungu kuhusu ujenzi wa nyumba za kuishi, yamezaa maswali kadha kutoka kwa wasomaji.
Maswali hayo yalihusu kupata ufahamu zaidi, juu ya sera hii ya ufalme wa Mungu. Tumeyapokea hayo maswali, ingawa si rahisi tukayajibu yote, kwa sababu ya “ufinyu” wa nafasi ya kufanya hivyo.
Lakini kwa leo tunataka tujibu swali moja, kati ya maswali mengi yaliyoulizwa, – na tunaamini majibu hayo yataongeza ufahamu zaidi juu ya utekelezaji wa sera hii.
Swali lenyewe lenyewe liliulizwa hivi: “Je, unatushauri kuweka wakfu au kuitakasa ardhi kabla ya sijajenga?”
Majibu yake ni haya:
Kuna tofauti kati ya kutakasa kitu,
na kule kukiweka wakfu hicho kitu. Unaweza kutakasa kitu bila kukiweka wakfu. Lakini huwezi kukiweka wakfu hicho kitu bila ya kwanza kukitakasa!“Kutakasa” kitu ni kukitenga kitu hicho ili kisafishwe ili kiweze kutumiwa! “Kuweka wakfu” kitu ni kukabidhi uhalali wa kumiliki kitu hicho kwa mwingine, ili akitenge na kukisafisha ili akitumie kama mali yake!
Kwa mfano: Kwaya ya Kanisani inaweza kwenda mahali kuazima vyombo vya muziki, ili wavitumie kuimbia nyimbo za Mungu, na wakiisha kuvitumia wavirudishe kule kule walikoazima!
Vyombo vya kuazima hawawezi kuviweka wakfu, bali watavitakasa kwa lengo la kuvitumia. Lakini ikiwa watavinunua vyombo hivyo ili viwe vyao, hawataishia kuvitakasa tu – bali wataviweka wakfu, ili Mungu wao avitumie kama “mali” yake!
Unaposoma kwa haraka matumizi ya maneno haya katika biblia, utaona ni kama vile yametumika kwa kuonyesha ya kuwa “kutakasa” na “kuweka wakfu” kunafanana! Lakini ukiyafuatilia kwa makini unaona ya kuwa matumizi ya maneno hayo yanatofautiana!
Hebu tusome maneno haya ya biblia: “Bwana akasema na Musa, akamwambia, nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote, kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo” (Kutoka 13:1,2).
Mungu angetumia neno hili “nitakasie” bila kuongeza maneno haya “ni wangu huyo” angekuwa anataka – tujue ya kuwa anataka “kumtenga na kumsafisha mzaliwa wa kwanza na kumtumia – bila kummiliki kama mali yake!”
Lakini aliposema neno hili “nitakasie”, na akaongeza kusema “ni wangu huyo” alitaka tujue ya kuwa anataka “kumtenga huyo mzaliwa wa kwanza, na kumsafisha ili amtumie huku akimmiliki kama mali yake!”
Kwa hiyo, katika kuombea kiwanja chako cha kujenga nyumba yako, usiishie kukitakasa tu – bali kiweke wakfu ili Mungu akimiliki kama chake! Hii ni kwa sababu ndani ya maombi ya kukiweka wakfu kuna kukitakasa pia!
Maombi ya jinsi hii ni vyema yakafanyika kabla ujenzi haujaanza. Lakini kama umeanza kujenga au umejenga nyumba bila kukiweka wakfu kiwanja – bado unaweza ukafanya maombi haya ya kukiweka wakfu!
Hatua muhimu katika kuomba maombi ya kukiweka wakfu kiwanja ni kama zifuatazo:
Hatua ya 1: Unaweza ukaomba maombi haya ukiwa kwenye kiwanja husika; au ukiwa mbali na kiwanja hicho, lakini huku ukiwa umeshika kiwakilishi chake – kama vile hati ya kiwanja hicho, au udongo, au jiwe kutoka kwenye kiwanja hicho (Soma Yoshua 1:3 na Yoshua 5:15).
Hatua ya 2: Mshukuru Mungu kwa kukuwezesha kupata kiwanja hicho au shamba hilo (Soma Wakolosai 3:17).
Hatua ya 3: Omba toba kwa jambo lo lote lililo kinyume na mapenzi ya Mungu lililowahi kufanyika hapo. Toba hiyo itengeneze njia ya ujio wa umiliki wa Mungu kwenye kiwanja hicho (Soma Mathayo 4:17).
Hatua ya 4: Mwaga damu ya Yesu – kwa njia ya kusema kwa kinywa chako – juu ya kiwanja hicho ili damu hiyo ya Yesu itumike:
(i) Kuondoa alama za kiroho za uasi (dhambi) kama vile: madhabahu za miungu mingine, mapepo, kumbukumbu mbaya, ukiwa, nakadhalika (Soma Luka 22:30).
(ii) Kukitakasa kiwanja ili kiwe katika hali ya kutumiwa na Mungu
Hatua ya 5: Kiweke wakfu kiwanja hicho; au kikabidhi kiwanja hicho kwa njia ya maombi ili kiwe “mali” ya Mungu, na kwa njia hiyo kiingizwe rasmi kwenye orodha ya viwanja vilivyo “mali” ya Mungu kiumiliki (Soma Ezekieli 45:1 – 4).
Kwa Mfululizo Mwingine au Sehemu Tangulizi Tafadhali Fuatana Nasi Ktk Channeli Yetu ( Bonyeza Link)
Follow the Mwalimu Oscar Samba Mafundisho Ya Neno La Mungu channel on WhatsApp:
https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni